Mkopo si hisani, ukikopa rejesha

Mkopo si hisani, ukikopa rejesha

Mawele

JF-Expert Member
Joined
Jul 25, 2023
Posts
403
Reaction score
1,185
Umoja wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha Tanzania (TAMIU) umeiomba Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu ya fedha kwa wakopaji, hatua inayolenga kupunguza changamoto zinazokabili sekta hiyo pamoja na kuboresha urejeshaji wa mikopo.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa TAMIU, mwenyekiti wa umoja huo, Juma Mnaka, amesema ukosefu wa elimu sahihi kwa wakopaji ni chanzo kikuu cha matatizo yanayojitokeza katika marejesho ya mikopo.

Amesema Wananchi wengi bado wana uelewa mdogo kuhusu dhana ya ukopaji, huku baadhi yao wakichukulia mikopo kama fedha za msaada badala ya mkopo unaopaswa kurejeshwa.

Aidha, Mnaka amewataka wakopaji kuhakikisha wanakopa kwa malengo maalum na yenye tija ili kuwawezesha kurejesha mikopo yao kwa wakati, akisisitiza kuwa ukopaji si hisani.

Katika hatua nyingine, amewashauri Wananchi kukopa kupitia taasisi zilizosajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania ili kuepuka malalamiko ya kuonewa na baadhi ya watoa huduma wasiofuata taratibu, ikiwemo kunyang’anywa mali kinyume cha sheria.

Sambamba na hilo, mwenyekiti huyo ametoa wito kwa watoa huduma ndogo za fedha kujiunga na TAMIU na kujisajili rasmi BOT ili kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo.

Kwa upande wao, baadhi ya wajumbe wa mkutano huo, Abisai Owuocha na Happy Mzave wametaja changamoto nyingine zinazoikabili sekta hiyo kuwa ni pamoja na ongezeko la matapeli na ukosefu wa mifumo inayounganisha taarifa za taasisi za fedha. Wameeleza kuwa hali hiyo inachangia wakopaji kukopa katika taasisi zaidi ya moja bila udhibiti, hivyo kusababisha ugumu katika marejesho.

Naye afisa kutoka Idara ya Usimamizi wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa BOT, Potamia Mamsey ameonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu au taasisi yoyote itakayobainika kutoa huduma hizo bila kufuata sheria na kanuni zilizowekwa
 
Back
Top Bottom