Justine_Dannie
JF-Expert Member
- Dec 1, 2014
- 1,963
- 1,617
Nasaha za Mihangwa
ABEID KARUME: Aliuawa kulipiza kisasi au kumpindua? II
Joseph Mihangwa
Toleo la 127
31 Mar 2010
KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya wiki iliyopita, tuliona juu ya utata uliozunguka kifo cha Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Abeid Amani Karume, Aprili 7, 1972. Tulihoji iwapo mauaji yake yalitokana na chuki binafsi dhidi yake au kama lilikuwa jaribio la mapinduzi lililoshindwa.
Tuliona pia kuhusu taarifa za kukanganya juu ya wauaji, kama nao waliuawa papo hapo au waliuawa baadaye, au kama walisalimika.
Nilieleza pia kwamba taarifa zisizothibitishwa zilionyesha kwamba, akiwa kwenye mafunzo ya kijeshi huko Tashkenti (Urusi ya zamani), mmoja wa wauaji wa Karume, Luteni Hamud Mohamed Hamud, aliweka wazi dhamira yake ya kumuua Mzee Karume, na taarifa hizo zilimfikia Karume, lakini hakuchukua hatua.
Niliuliza; je, kwa nini Karume hakuchukua tahadhari/hatua yoyote? Je, taarifa hizo zilikuwa za uongo?
Niliendeleze suala hilo katika sehemu hii ya pili ya makala kwa kusisitiza kwamba; haijafahamika bado kama Luteni Hamud na wenzake waliuawa hapo hapo na walinzi wa Rais Karume au kama waliweza kutoroka, kama tulivyoeleza mwanzo. Hata baadhi ya watu waliokuwapo siku hiyo kwenye eneo la tukio wanashindwa kutoa maelezo ya kueleweka.
Mmoja wao, Hayati Thabiti Kombo Jecha, ambaye pia alikuwa Katibu Mkuu wa ASP na mmoja wa waliojeruhiwa vibaya katika rabsha hiyo, amenukuliwa na Minael Hossana Mdundo katika kitabu chake Masimulizi ya Sheikh Thabit Kombo Jecha (Uk. 157/8) akieleza: “Mara ikapigwa risasi kutoka mlangoni, ikampiga Mheshimiwa Sheikh Karume shingoni. Hapo hapo akaanguka akisema “Hamad”… bahati mbaya risasi zote alizopigwa zilimpiga sehemu mbaya”.
Kisha anaendelea: “Kusema kweli mimi sikumwona huyo mtu aliyekuwa akitupiga risasi, wala sikumwona alikuwa amesimama wapi. Lakini baadaye nilipata kusimuliwa na wengineo, (kwamba) kijana aliyetupiga risasi alikuwa anaitwa Hamud. Alikuwa anatumiminia risasi sisi na kurudi kinyume-nyume. Wala hakuwa peke yake, alikuwa na wenzake”.
Juu ya kuuawa kwa Hamud, Mzee Kombo anasema: “…mmoja wa walinzi wa Rais, hali amejeruhiwa vibaya, akajitahidi mpaka akampiga Hamud risasi ya bastola, Hamud akafa papo hapo”.
Inaonekana ukweli ni kwamba, Luteni Hamud ndiye aliyefyatua risasi ya mauaji, na wenzake wakiwa nje ya ukumbi alimokuwamo Karume na wenzake. Wala hakuna ubishi kwamba Hamud alikufa kwenye eneo la tukio; iwe kwamba alipigwa risasi na mlinzi wa Rais Karume au alipigwa risasi na Kapteni Ahmada au alijiua, ni suala lingine.
Je, Luteni Hamud, Kapteni Ahmada na Ali Chwaya walikuwa na watu wengine nyuma ya mauaji haya? Kama walikuwa na watu wengine nyuma, basi hayawezi kuhusishwa na Hamud pekee katika kulipa kisasi. Na isitoshe, Ali Chwaya na Kapteni Ahmada walikuwa na chuki gani dhidi ya Karume?
Kama kulikuwa na watu wengi zaidi nyuma, basi mauaji haya lazima yaguse mambo ya kisiasa kwa upana zaidi ambapo Hamud na wenzake walikuwa mawakala tu. Hebu tuangalie dhana hii ya pili, tofauti na ile ya kulipa kisasi.
Kama nilivyosema mwanzo, kwamba kwa kuongoza Zanzibar kwa mkono wa chuma na ukatili uliovuka mipaka, Rais Karume alikuwa amejiandalia mwenyewe mazingira hatarishi yaliyoongoza kwenye kifo chake.
Kulikuwa na majaribio ya hapa na pale ya kutaka kuiangusha Serikali ya Karume kuanzia mwaka 1964. Thabit Kombo Jecha katika “Simulizi” anayataja baadhi, likiwamo lile la Desemba 1964 lililoongozwa na Amour Zahor wa Unguja; la 1967 likiongozwa na Suleiman Hamad Suleiman wa Pemba; la 1967 tena, likiongozwa na Saleh Ali Nassor wa Unguja; na la 1968 likiongozwa na Salim Mohamed Abdullah wa Pemba.
Mzee Kombo anasema: “Majaribio yote hayo yalikuwa mepesi, maana walikamatwa kwa urahisi kila walipopanga. Lakini usaliti uliotisha sana ulitoka kwa viongozi wenzetu ndani ya ASP na ndani ya Serikali ya Mapinduzi… Katika njama hizo alikuwapo Abdullah Kassim Hanga, Suleh Saadallah Akida na Abdul-aziz Twalha, wote mawaziri”.
Wote hawa, wenye siasa za mrengo wa Ki-Karl Marx na maswahiba wa kundi la Babu (Umma Party), waliuawa kikatili na katika mazingira ya kutatanisha.
Ukweli ni kwamba, wanaharakati hawa, kwa umoja wao wa chini kwa chini na wale wa Umma Party, walimnyima Karume usingizi kwa tishio la kumpindua; na hii ni moja ya sababu zilizomfanya atafute haraka Muungano na Tanganyika ili kujiponya; vinginevyo asingeepuka kupinduliwa.
Kufuatia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Karume alishinikiza uhamisho wa wanaharakati wote hatari Visiwani kwenda kwenye Serikali ya Muungano ili waweze kumezwa wasiweze kufurukuta.
Waliokumbwa na shinikizo la Karume ni pamoja na Abdullah Kassim Hanga, aliyefanywa Waziri katika Ofisi ya Rais wa Muungano, akishughulikia mambo ya Muungano, Abdulrahman Babu (Mipango na Uchumi), Salim Ahmed Salim (Balozi wa Muungano, Cairo).
Wengine ni Othman Sharrif (Afisa Mifugo, Mbeya) na Kanali Ali Mahfoudh (Mkurugenzi wa Operesheni, Jeshi la Ulinzi -JWTZ).
Kwa wale waliobakia Visiwani ghadhabu ya Karume iliwashukia mara kwa mara kwa kukamatwa na kutiwa kizuizini, na hata kuuawa. Mmoja wa waliotiwa kizuizini na hatimaye kuuawa ni Mzee Mohamed Hamud, baba yake Luteni Hamud Mohamed Hamud, muuaji wa Karume.
Kufikia mwaka 1967, licha ya kujificha ndani ya mbawa za Muungano, hofu ya Karume ya kupinduliwa ilikuwa imezidi kipimo kiasi cha kuogopa kivuli chake mwenyewe.
Na katika kuzima hoja kwa vitisho na ukatili, mwaka 1967/68 watu 14 walitungiwa tuhuma za uongo za kutaka kuipindua Serikali ya Karume, zikiwalenga wanaharakati wa mrengo wa Kikomunisti.
Mmoja wa mashahidi wa uongo walioandaliwa dhidi ya watuhumiwa alikuwa Kapteni Ahmada, ambaye kwa uongo wake “watuhumiwa” wanne walinyongwa mwaka 1969, akiwamo Hanga, Abdul-aziz Twalha, Saleh Sadallah Akida na Othman Sharrif. Kwa uongo huo, Ahmada alizawadiwa cheo cha Kapteni.
Hapa, yafaa tuangalie kidogo mfumo wa Sheria na utendaji haki ulivyokuwa Visiwani. Oktoba 1966, Rais Karume alijipa mamlaka ya kuanzisha “Mahakama” maalum yenye wajumbe wasiozidi 14 wenye mamlaka ya kusikiliza na kutoa hukumu kwenye kesi za makosa ya kisiasa kama vile, uhaini, uhujumu au wizi wa mali za umma.
“Mahakama” hiyo hakufungwa wala kubanwa na Kanuni za kimahakama za kawaida, na watuhumiwa hawakuruhusiwa utetezi wa kisheria wala mawakili.
“Mahakama” hiyo ilikuwa na uwezo wa kutoa hukumu ya kifo ambapo rufaa ilikuwa kwa Karume mwenyewe.
Mwaka huo huo (1966), Serikali ya Mapinduzi ilitangaza kufutwa kwa haki ya kukata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki.
Mwaka 1970 ilipitishwa Sheria mpya ya kuanzisha muundo wa mahakama za kienyeji zenye “mahakimu” watatu maarufu kwa jina la “Mahakama za Wananchi”. Mahakimu hao wapya walioteuliwa na Rais Karume, kwa kawaida walikuwa makada wa ASP wasio na elimu hata ya Msingi.
Hukumu ya kifo ilitolewa kwa makosa mengi, kama vile utoroshaji wa karafuu nje ya mipaka ya nchi, uhaini, na kwa mujibu wa Anthony Clayton katika kitabu chake “The Zanzibar Revolution and its Aftermath”, hata makosa kama vile kutoa mimba na matumizi ya vidonge vya kupanga uzazi(contraceptives), yalikaribisha adhabu ya kifo.
Wengi wanaamini kwamba Karume, kwa kuulea ukatili wa “mahakimu” hawa wa mahakama zisizo rasmi(Kangaroo Courts), na wa lile kundi la Mahakimu 14, maarufu kwa jina la “The Gang of Fourteen”, ilikuwa ni moja ya mambo yaliyosababisha awe shabaha ya mauaji.
Kufikia mwaka 1972, upinzani kwa Serikali ya Karume ulichukua sura ya maasi ya umma ya chini kwa chini kwa mara ya kwanza tangu kunyongwa kwa Hanga na wenzake mwaka 1969.
Katika hali ya kuonyesha kwamba Karume alikosa usingizi na amani kutokana na hali tete ya kisiasa iliyokuwa ikimwandama, mapema mwezi Januari 1972, alimfukuza kazi Waziri wake mmoja, Ahmed Badawi Qualletin na maafisa wengine wa Serikali, Ali Sultan Issa na Khamis Ameir, kwa tuhuma za kuvuruga utulivu wa kisiasa, wengi wa hawa wakiwa wanachama wa zamani wa Chama cha Umma Party cha Babu.
Kisha, Februari 1972, ujumbe mzito wa watu sita, ulitumwa Dar es Salaam kwa Mwalimu Nyerere, kumwomba amrejeshe Babu na wenzake waweze kuhojiwa kwa tuhuma ya kula njama kutaka kuipindua Serikali.
Hata hivyo, Mwalimu, kwa kukumbuka jinsi alivyoombwa hivyo hivyo kumrejesha Hanga na wenzake kwa misingi hiyo hiyo mwaka 1967, naye akakubali na watu hao wakauawa kikatili bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, alikataa kurudia kosa hilo; lakini akakubali shinikizo la Karume la kumvua Babu uwaziri katika Serikali ya Muungano.
Hatua hiyo ya Karume iliyojaa hofu na kutojiamini, ilitokana na umaarufu pamoja na ushawishi mkubwa wa Babu kwa jamii ya Kizanzibari, licha ya yeye kuishi Bara.
Ni harakishe hapa kutamka mapema, lakini bila ya kuathiri hitimisho langu baadaye juu ya ushiriki wa Luteni Hamud na Kapteni Ahmada, kwamba, Ahmada alijiingiza katika mpango wa mauaji ya Karume kama hatua ya kujutia ushahidi wake wa uongo aliotoa dhidi ya Hanga na wenzake wakanyongwa mwaka 1969 na yeye wakati huo akaanza kujihisi kuwa ni “adui wa umma”. Kwa hiyo, hatua hiyo ilikuwa ni kama njia fulani ya kujisafisha jina machoni mwa jamii ya Kizanzibari.
Upo ushahidi wa Ahmad wa kukiri mbele ya rafiki zake kwamba, alishurutishwa kutunga ushahidi wa uongo; na kwamba, ingawa alizawadiwa cheo cha Kapteni wa Jeshi, nafsi yake iliendelea kumsuta na kujutia tukio hilo ambalo Wazanzibari wengi walifahamu fika kwamba, tuhuma dhidi ya watu hao walionyongwa za kupanga kuipindua Serikali ya Karume, zilikuwa za uongo.
Ahmada alikerwa pia na jinsi demokrasia ilivyozidi kudorora/kuyoyoma na kukithiri kwa ukatili Visiwani baada ya wanamapinduzi wengine 15 kuuawa kikatili na kwa mazingira ya kutatanisha.
Imeelezwa pia kwamba, Ahmada alichukizwa na hali ngumu ya maisha kwa Wazanzibari iliyosababishwa na Serikali ya Karume, licha ya Serikali hiyo kuwa na akiba kubwa ya fedha za kigeni kutokana na bei nzuri ya karafuu katika soko la dunia.
Kwa upande wa Luteni Hamud, jarida moja la kila mwezi - “Africa Events” la Agosti 1992 (Uk. 27) linadai kuwa, alichukua uamuzi wa kumuua Karume kulipa kisasi cha kuuawa kikatili kwa Baba yake, Mzee Mohamed Hamud na Karume akiwa kizuizini, kama nilivyosimulia hapo mwanzo.
Mpaka sasa hakuna sababu zinazotolewa juu ya kushiriki kwa raia Ali Khatibu Chwaya na Koplo mmoja wa JWTZ katika mpango huu wa mauaji.
Hata hivyo, itoshe kusema tu kwamba, kushiriki kwao kunaelekea kutetea na kuimarisha dhana ya pili, kwamba kwa sababu Serikali ya Karume ilishindwa kukidhi matarajio ya Wazanzibari wengi kufuatia Mapinduzi ya Januari 12, 1964, hivyo hapakuwa na njia ya kuleta mabadiliko isipokuwa kwa njia ya mapinduzi ya kutumia nguvu.
Lakini hapa panazuka swali tena: kwamba, kama lengo la Hamud lilikuwa ni kulipa kisasi; na lile la Ahmada lilikuwa kujutia ushahidi wa uongo uliosababisha watu wasio na hatia kunyongwa, na pia kama njia ya kusafisha jina lake; kwa nini tukio hilo lilihusisha watu zaidi ya wawili hao? Si hivyo tu, kwa nini watu zaidi ya 1000 walikamatwa kufuatia mauaji, kama haukuwa mpango mpana wa mapinduzi?
Kufikia hapo ni dhahiri kwamba kero za kisiasa na kiuchumi zilikuwa chanzo cha hali ya mparanganyiko Visiwani uliojenga mazingira ya kuuawa kwa Karume.
Na kadri kalamu ya upanga ya Karume ilivyozidi kuandika historia ya ukatili na udikteta Zanzibar kwa wino wa damu, kwenye kurasa ngumu za hasira na chuki, kushuhudia uvunjaji wa haki za binadamu, ukatili na kutia watu kizuizini; mauaji ya kisiasa ya kutisha na uchumi ulioshindwa; ndivyo siku ya kiama kwa Karume ilivyozidi kujongea hima.
Mpango wa kuipindua Serikali ya Karume ulibuniwa mwaka 1968 na wanaharakati wa Mapinduzi ya 1964, wakiwamo raia na wanajeshi wachache. Kikao cha mwisho cha mpango huo kilifanyika Aprili 2, 1972 nyumbani kwa Luteni Hamud, ambapo ilikubaliwa kwamba mapinduzi hayo yafanyike Aprili 7, 1972 kwa kutumia mbinu zile zile zilizotumika wakati wa Mapinduzi ya Januari 12, 1964. Nani alikuwa kiongozi wa mpango huo?