Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
MBIVU na mbichi kuhusu ukweli wa mkataba kati ya Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enterprises Limited wa ufungaji wa vifaa vya kuchukulia alama za vidole katika vituo vya polisi nchini, kujulikana leo.
Jeshi la Polisi linatarajiwa kuwasilisha mkataba huo, unaosaidikiwa kuwa tata, uliotiwa saini mwaka 2011 na kampuni hiyo, mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Katika mkataba huo wenye thamani ya Sh. bilioni 37, unawahusisha baadhi ya vigogo wa serikali, wabunge na wakuu wa jeshi la polisi wastaafu, ambao baadhi yao wamesikika katika vyombo vya habari wakikanusha kuhusika na kashfa hiyo.
Akizungumza na Nipashe jana, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Hilary Aeshi, alisema leo watakutana na viongozi wa jeshi la polisi na kupokea mkataba waliouomba wiki iliyopita.
Alisema baada ya Kamati kupokea mkataba huo, wataupitia na kuujadili na kutoa maagizo kadhaa kwa jeshi la polisi.
“Kesho (leo) ndiyo tarehe 11 hivyo tutapokea huo mkataba kama tulivyowaomba watuletee. Wakituletea tutausoma na kuujadili na tutawapa maelekezo,” alisema Aeshi.
Aliongeza kuwa kuna uwezekano wa kuundwa kwa kamati ya kuchunguza suala hilo endapo maelezo watakayoyapokea hayataeleweka.
Alisema kuundwa kwa kamati hiyo ya uchunguzi kutatokana na madai ya jeshi la polisi linadai kuwa vifaa hivyo vimefungwa katika vituo vyote nchini.
“Kama vifaa vimefungwa katika vituo vyote nchini, ni matumaini yetu kuwa vitakuwa vinafanya kazi. Huwezi kufunga vifaa ambavyo ni vibovu, hivyo kama maelezo tutakayoyapokea hayataridhisha kuna uwezekano wa kuundwa kwa kamati ya uchunguzi,” alisema Aeshi.
Hivi karibuni PAC ilibaini kuwapo kwa viashiria vya ufisadi katika jeshi la polisi, kutokana na Lugumi kulipwa Sh. bilioni 34 kati ya Sh. bilioni 37 za mkataba mzima.
Katika utekelezaji wa mkataba huo, inadaiwa kuwa Lugumi imelipwa kiasi hicho cha fedha ilhali imefunga mitambo katika vituo 14 kati ya 138 nchini kote.
Chanzo: Nipashe