Kanungila Karim
JF-Expert Member
- Apr 29, 2016
- 20,744
- 25,446
Mtunzi:Abyas Mzigua
Sehemu ya kwanza.
"AANH ewe Mungu! Hivi nina mkosi gani mimi? Mbona watoto wa wenzangu wanafanya kazi na kuwalisha wazazi wao? Wa kwangu ana nini? Eti Zakayo, una nini wewe? Au unataka kuja kuolewa?"
"Daah...hapana mama!"
"Ndiyo. Maana kazi kufanya hutaki. Unategemea nini sasa?"
"Si kwamba sitaki , hali imebadilika mama yangu, hali ngumu mno!"
" Hali..nguu...muuu..!"aliigiza kwa kubana pua, kisha akaendelea kufoka,"yani mwanaume mzima, midevu mpaka kwenye viganja vya mikono,unasema kabisa hali ngumu? vijana wa mjini sijui mko vipi!"
Alimaliza na kuusukuma mlango kwa hasira, akatoka nje.
Kwa majina, naitwa Zakayo Mdaki. Ni mtoto wa pekee, wa Marehemu mzee Mdaki Zakayo, aliyefariki miaka kumi iliyopita, kwa ajali ya kugongwa na gari akiwa anaendesha baiskeli yake, jioni...akitokea kibaruani.
Kifo cha mzee wangu kilituacha wawili tu, mimi na mama yangu.
Ambaye alikosa uwezo wa kunipeleka sekondari, baada ya kumaliza darasa la saba. Na badala yake, niligeuka msaidizi katika kajimgahawa chake kidogo cha chakula, kilichokuwepo pembezoni mwa barabara, mitaa ya Magomeni, Mwembechai.
Nilifanya kazi kwa bidii mno, kwa kuwa mgongo wa ndoto zangu, ulishaegemea mgahawa ule.
Nilitamani siku moja ndoto yangu itimie:nipate pesa na kurejea tena shuleni.
Walakini, tamaa hubaki tamaa ikiwa Mungu hakupanga. Hata ukafanya jitihada za kuvuja jasho la damu!
Ndivyo kwangu ilivyokuwa...
Siku wagambo walipoamua kutuvunjia, wakaharibu kila kilicho ndani.
Pesa, vyakula na vyombo vya thamani-walivibeba wakaondoka navyo.
Tulijaribu kufungua mashitaka.
Bila kukumbuka kuwa, 'kila mbuzi hula kwa urefu wa kambaye'.
Hakuna tulichoambulia. Zaidi, tuliuvaa usumbufu wa 'nenda-rudi'.
Mwishowe, tulikata shauri, tukaachana nao.
Kuanzia hapo, mama hakuwa na shughuli nyingine yo yote.
Nikajitwika utoto, ukaka na ubaba...kutafuta vibarua mitaani, walau tupate cha kutupia kinywani.
Mambo yakawa yanasonga.
Tofauti na siku zilizopita!
Maisha ya hivi karibuni, yamegeuka kichwa chini, miguu juu.
Kila ninapojaribu kupapasa-hola!
Na mama ndiyo hivyo,'Ananiona m'bwetekaji tu'.
JIONI moja, nikiwa katika randaranda zangu, nilikutana na rafiki, rafiki wa kitambo sana! Tangu shule ya msingi. Haikuwa rahisi kwangu kumkumbuka.
Alibadilika sana!
Mavazi, muonekano na gari aliyokuwa anaendesha, iliakisi ubora na hadhi yake.
Mwenzangu alinikumbuka vema kabisa.
Labda kutokana na kutobadilika.
Yumkini umasikini ulinidumaza. Nikashindwa kuonesha utofauti;kati ya utoto, ujana na uzee.
Aliniomba tutafute sehemu, tukae ili tuzungumze kidogo. Maana ni muda mrefu hatukutiana machoni.
Hakuna masikini anayekaidi wito wa tajiri.Hakuna!
Au yupo asiyefahamu kuwa,'Mfuata nyuki hurejea na kibuyu chenye asali'?
Natumai hayupo!
Nilipanda garini mwake, tukaianza safari.
Si mbali kihivyo tulipoelekea.
Ilikuwa ni katika baa iliyopo mtaa wa tatu, tokea pale tulipoonana.
Soga za wakati huo, zilichukua nafasi kubwa baina yetu.
Tulicheka na kunywa pamoja.
Lakini, kooni mwangu nilikabwa na kifundo cha uchungu.
Hali ilivyozidi kunishika, niliamua nikifungue tu...
"Daah! jamaa yangu Mkojera, hivi umetobolea wapi yani?" niliuliza.
"Kivipi Zakayo?"
"Nazungumzia maisha, naona unang'aa sana siku hizi! Au umepata lishangazi linakulea?" nilijaribu kumchombeza kwa swali la kipuuzi.
"Hahahhhah, hamna bwana rafiki yangu. Kumbe hujaacha tu mambo yako!"
"Aaa'nh, tuambiane bwana ndugu yangu. Unaona wenzako tunavyopigika?"
"Hamna. Haya mambo mazito! Lazima uwe mwanaume ili upate vitu hivi ndugu yangu?"
"Dooh, sasa hayo matusi ya nguoni. Ina maana sie tusiokuwa navyo, ni wanawake au?"
"Simaanishi hivyo Zakayo, yapasa kujikaza sana ili uvipate!"
"Mradi hufi, mimi niko tayari Mkojera. kwa lolote!"
"Unamaanisha unachozungumza?", Mkojera aliongea kwa kunikazia macho, kuonesha kutaka uhakika kutoka kwangu.
"Ndiyo ndugu, hakuna anayetaka umasikini bwana!"nilijibu.
"Basi sawa,"aliafiki, akashusha pumzi na kuendelea,"Kesho tukutane saa kumi na mbili asubuhi. Palepale nilipokukuta leo. Kuna sehemu nitakupeleka!"
Nilimshukuru sana Mkojera. Sana!
Si tu kwa kuahidi kunisaidia. Bali pia, kuonesha dalili ya ukunjufu wa mtima wake, kwa kuniachia Shilingi elfu kumi mfukoni.
Niliipeka pesa ile, kama ilivyo nyumbani. Nikamkabidhi mama yangu.
Nampenda sana aisee!
Saa 10:15,
Ndivyo kulivyosomeka. Baada ya mboni zangu kugota ukutani, kulipo na mishale miwili: mrefu na mfupi, yenye kuzizunguka namba kwa zamu.
Tayari kulishakaribia kukucha.
Shauku ya safari na woga wa kuchelewa kuamka, ukanifanya nisilale mpaka ilipoingia alfajiri.
Nilijiandaa harakaharaka.
Sikutaka kumsumbua mama yangu, nilitoka nikiwa nimemuacha bado yu-ndotoni.
Njiani, kila hatua niliyopiga, ilijenga taswira mpya ya maisha yangu.
Nilianza kujiona nami ni mmojawapo ya wapanga foleni, huku wameshika sukani za magari yao, wakisubiri muwako wa taa ya kijani.
Mara, nikavuta picha nyingine. Kuwa nasugua kadi kwenye mashine ya benki, pesa zikichomoka kama uchafu.
Kila kitu, nilihisi kinaenda kubadilika chini ya pambazuko la siku hii.
Nilipuuzia kabisa waswahili, na kudai kwao kuwa,'Mafanikio hayana njia ya mkato.'
Sikutaka hata kidogo, kulifikiria hili!
......
Tukutane kesho.