Mjue muuza matunda gengeni anayeingiza bilioni 20 kwa mwaka

Mjue muuza matunda gengeni anayeingiza bilioni 20 kwa mwaka

Interest

JF-Expert Member
Joined
Apr 11, 2015
Posts
3,434
Reaction score
7,096
attachment.php


UKWELI ambao pengine una kushangaza ni kuwa matajiri wengi hupenda kusimulia nyakati zao za giza. Kipindi ambacho maisha yalikuwa magumu, yenye mateso, manyanyaso na taadhira.


Upande wa pili, maskini wengi hujitahidi kwa kila namna kuficha aibu zao. Watu wakiwa kwenye utafutaji huwa hawataki wajulikane kama ni wajaa dhiki wakubwa. Wapo hudanganya hata mahali walipotoka ili kukwepesha ramani.

Ni kwa nini matajiri wengi hupenda umaskini wao wa zamani ujulikane wakati maskini hupambana kuficha hali halisi ya maisha yao hususan ukweli wa dhiki ndani ya familia zao?

Heshima; Neno hili moja tu linajibu swali hilo katika pande zote mbili. Tajiri hutaka asemwe kuwa alikuwa maskini kwa sababu ya heshima. Maskini hukataa asijulikane kwa sababu ya heshima.

TAJIRI NA HESHIMA

Siyo uongo kuwa unaposema mtu fulani alikuwa maskini wa kutupwa katika kipindi ambacho anakuwa ameshabadili kibao cha maisha ni heshima. Yaani ule umaskini wake unakuwa unazungumzwa kama historia, hapo unamuongezea thamani.

Kuna tofauti kubwa kati ya utajiri wa kurithi (Inherited wealth) na ule wa kuuvujia jasho (self made wealth). Kwa maana ule wa kuupigania kwa njia halali mpaka kuupata ni kielelezo cha ushujaa wa mtu.

Mohamed Dewji ‘Mo' ndiye tajiri namba moja nchini kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za fedha na uwekezaji. Amefanya kazi kubwa mno kuanzia nyakati za mwisho wa miaka ya 1990 mpaka sasa.

Mo ni mrithi bora, maana alichukua mikoba kutoka kwa baba yake, Gulam Dewji na kuunda Mohamed Enterprises, kisha kuleta matokeo makubwa kupindukia, akiwazidi mpaka wababe wa kibiashara nchini akina Reginald Mengi, Said Salim Bakhresa, Rostam Aziz na wengine.

Hivi sasa Mo ndiye mfanyabishara za halali anayeongoza kifedha, kwa maana kupitia ule uwekezaji unaoonekana. Utajiri wake ni mkubwa, unaokuwa kwa kasi. Anafanya kazi kisasa, kiuchapakazi na kiteknolojia.

Hata hivyo, pamoja na hatua ambazo Mo anapiga na heshima ambayo anastahili kwa namna alivyozipaisha mali alizorithi kutoka kwa baba yake, lakini anabaki tu kuwa mtoto wa tajiri mwenye akili.

Mengi, Bakhresa na Rostam, heshima kubwa ambayo wanakuwa nayo ni kwamba wao hawajarithi. Utajiri wanaomiliki umetokana na kuanzia sifuri, wakavuja jasho, wakatokwa machozi mpaka kuufikia ‘ubabe' wa kifedha walionao.

Hivyo basi, ukikutana na Mengi anakueleza kuwa alilala na ng'ombe pamoja na mifugo mingine ni kwa sababu anataka ushike adabu zako unapomuona amekaa pazuri, kwa maana maisha ya nyuma yalikuwa magumu hasa.

Bakhresa akikwambia alikuwa anauza maandazi, maana yake anataka unavyoona miliki kubwa alizonazo sasa, ujue kuwa zimetokana na ushujaa wake binafsi, siyo kitu kingine.

Rostam akisema alikuwa anabana sehemu ya ada mpaka akapata mtaji wa kuanzia kabla ya kuvuja jasho kwa malengo, anataka ukisikia anamiliki Vodacom Tanzania na uwekezaji mwingine ndani na nje ya nchi, umpigie saluti.

Kwa manti hiyo, matajiri wengi hupenda wajulikane walipotoka kama kielelezo cha kutambulika kwa ushujaa wao. Kutoka kuchangia malazi na ng'ombe mpaka ubilione wa mfano Tanzania kwa nini usimpe utukufu wake Mengi?

Na ndiyo maana Mo ni tajiri mkubwa ambaye historia yake haina mvuto sana kwa sababu alikuta baba yake alishafanya kazi kubwa, kisha yeye akapokea kijiti. Akina Rostam na Bakhresa hawakuanzishiwa mwendo na mtu.

MASKINI NA HESHIMA

Maskini anayeendelea kuuishi umaskini wake anakuwa hana ushujaa wowote, hivyo anaona hali halisi ya maisha yenye asili yake yakijulikana, yatamvunjia heshima na pengine kumharibia fursa mbalimbali.

Na ndiyo maana maskini wengi huishi maisha ya urembo yenye ubandia (synthetic life), hasa nyakati wanapokuwa wanatafuta. Wapo wengi tu wanaotafuta maisha wakijitahidi kuficha hali halisi za umaskini wao lakini wanapofanikiwa hujaa ushujaa wa kusimulia walipotoka.

Tajiri akisema "nilikuwa na chawa au funza", kwake ni ufahari kwa mageuzi aliyofanya. Maskini hufikiria akisema atadharaulika na kupuuzwa moja kwa moja.

Tajiri husema nyumbani kwao kulikuwa na nyumba ya tembo (full suit), yaani udongo kila upande au iliyoezekwa nyasi kwa sababu ukirudi nyumbani kwao hukuti tena suti, unakuta mjengo wenye thamani kubwa na wa kisasa alioujenga.

UMASKINI NI MAPITO


Hata wewe hapo ulipo unaweza kusimama kifua mbele, pamoja na umaskini wako, simama useme kuwa nyumbani kwenu ni shida lakini hayo ni mapito tu ya maisha.

Sema: "Sisi ni maskini, nyumbani kwetu paa ni nyasi, mvua ikinyesha tunaogelea, maana nyumba inageuka bwawa nje, ndani mpaka vyumbani, ila yatakwisha. Mungu yupo."

Usiache kumtanguliza Mungu mbele kwa maana yeye ndiye mfanikishaji wa kila jambo. Nia jumlisha juhudi kisha ukamuomba Maulana akufanyie wepesi, hakuna kinachoshindikana.

Jiulize, wao wamepata kwa nini, kisha ukose kwa upungufu gani ulionao? Mungu ni wa kila mtu. Huhitaji mtu wa kati kumfikia Muumba wako, sema naye usiku na mchana huku ukipambana.

Nikuhakikishie; Kwa hali yoyote uliyonayo Mungu anao mpango wake mzuri tu na wewe. Usikate tamaa, ni dhambi. Yeye aliyekuumba anajua fungu lako lipo na anatambua utalifikia kwa kujituma kwako huku ukimuomba yeye. Unapokuwa hai, elewa kuwa Mungu amekubakiza kwa sababu zaidi ya milioni, kwa hiyo tabasamu.

NATALIA VODIANOVA ALIKUWA WAPI?


Mwana Hip Hop, Joseph Osmond Mbilinyi ‘Sugu' ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini kwa sasa, katika wimbo wake Sugu anaimba: "Nayajua matatizo zaidi yako, na hata kama ni msoto nimepata zaidi yako, usinione brother-men kwa kuwa nipo na mkoko..."

Hapa Sugu alikuwa anafikisha ujumbe kuwa unaweza kumuona mtu kwenye hali fulani bora, ukadhani ni legelege, hujui ni kwa kiasi gani alivyopambana kufika mahali ambako unamuona yupo.

Unaweza kudhani wewe una maisha magumu kumbe hujafikia hata nusu ya huyo ambaye unamuona anaendesha gari la kifahari au kuishi kwenye nyumba kama hekalu. Jitambue, pambana kwelikweli. Unaweza kumzidi huyo ambaye hivi sasa unamuona malaika japo uhai wake unategemea nishati ya jua linalomulika dunia.

Kama alivyosema Sugu, mtu akimuona Natalia Vodianova kwa haraka kwa sababu anaishi maisha yenye gharama kubwa, atadhani ni wa kutoka familia bora.

Vile alivyo mrembo na kwa sababu maeneo anayotembelea, sehemu anazofanya manunuzi ni zile za wenye nao, moja kwa moja hisia zinakuja kuwa Natalia ni mrembo wa kishua, kutoka ushuani kwa washua!

Tema mate chini; Natalia ni kati ya watu ambao wanaona fahari kubwa sasa hivi kuusema umaskini wa nyumbani kwao, maana alishafanya mabadiliko makubwa.

Alitoka kwenye familia yenye hali ngumu mno. Maisha yakumtegemea mama tu, akiwa na ndugu zake wengine wawili, ni nyakati ngumu ambazo Natalia hutoa machozi kila anapozikumbuka.

Natalia alizaliwa Februari 28, 1982 kwenye Jiji la Gorky (sasa linaitwa Nizhny Novgorod), Urusi, wakati wa Umoja wa Jumuiya za Kisovieti (USSR). Akakulia kwenye eneo la kimaskini sana ndani ya Jiji la Avtozavod.

Akiwa na dada zake, Kristina na Oksana, maisha yalikuwa magumu na kila siku iliyopita kwenda kwa Mungu, walihesabu maumivu makali kupindukia. Zaidi walimuonea huruma mama yao aliyekuwa anapambana kutafuta japo mkate wa siku.

Kutokana na ugumu wa kimaisha, Natali hakwenda shule, badala yake aliishia kumsaidia mama yake kutembea mitaani kuuza matunda, angalau jioni wanapokutana nyumbani, waangalie mahesabu ya kilichopatikana ili moto uwashwe, sufuria liungue jikoni na chakula kipatikane.

Hayakuwa maisha yenye uhakika, na yalimtesa mno Natalia ambaye pamoja na umaskini wake, vilevile kukosa elimu, lakini bado alikuwa anawaza kuwa na maisha bora zaidi.

Alipokuwa anapita barabarani kutembeza matunda, alijionea watu wenye maisha mazuri wanavyoishi, naye alitamani kuona familia yake inakuwa na hali bora zaidi. Vilevile alitamani sana kumsaidia mama yake.

Katika kupigana huku na huko hasa baada ya kuzurura mno mitaani na biashara ya matunda, Natalia alishirikiana na rafiki yake, wakaanzisha kibanda kidogo cha kuuza matunda. Alikuwa na malengo makubwa ya kumsaidia mama yake hasa kumpunguzia mzigo wa kuwahudumia yeye na dada zake.

MUNGU NA SHANI YAKE


Huwezi kupata picha nzuri ya Natalia kama huwafikirii wauza ndizi, matango na biashara nyingine ndogondogo ambao wanazunguka mitaani kila siku na kukutana na kila aina ya masimango na manyanyaso.

Mfikirie dada anayepita mitaani akiwa mchafumchafu na kumwambia kuwa huwezi kununua ndizi zake kwa sababu ni mchafu. Unampa maneno makali kuwa huwezi kula maembe yake kuwa atakusababishia kipindupindu.

Ukiwa na picha hiyohiyo ambayo unaipata kutokana na binti mhangaikaji wa biashara ndogondogo mitaani, waza sasa kuwa nyakati zijazo anakuwa bilionea mwenye kutazamwa duniani kote, wewe ukibaki na dharau zako.

Chukua hii; Mheshimu kila unayekutana naye, maana hakuna mwenye kuijua kesho ya mwenzake. Unayemuona leo na kumfananisha na kibaka kwa kumuonea, si ajabu kesho ndiye akawa rais wako.

Akiendelea na biashara ya matunda lakini umri nao ukawa unasogea. Natalia akawa anahama kutoka kwenye utoto mpaka usichana.

Kama ujuavyo Mungu anapotaka kumnyanyua mja wake, pamoja na uchakavu wa kimaisha na nguo chafuchafu zenye kuchanika alizokuwa anavaa, bado uzuri wa Natalia uliweza kupenya na kuonekana waziwazi.

Kazi ya Mungu inaendelea kujidhirisha, kwani Natalia alipofikisha umri wa miaka 14, alionwa na mawakala wa masuala ya mitindo na alipokuwa na umri wa miaka 15, tayari alishapata mwanga wa kufanikiwa baada ya kuibuliwa.

Kwa vile alitokea kwenye maisha ya dhiki na hakuwa na msingi wowote, mawakala wa masuala ya mitindo baada ya kumuibua, ili watengeneze fedha nyingi ilibidi kwanza wamuandae na kumpeleka shule kidogo angalau kumuondoa tongotongo.

Natalia alipofikisha umri wa miaka 17, alisafirishwa na mawakala kutoka Urusi mpaka Ufaransa ambako alisaini mkataba na kampuni kubwa ya mitindo duniani, Viva Models.

Kuanzia hapo kila kitu kilibadilika. Alianza kufuatwa na fedha kila anapokwenda. Mikataba ikawa inanona kwa sababu aliwavutia wengi kufanya naye kazi. Natalia akawa siye yule tena.

Ghafla akageuka balozi wa kujitegemea aliyeing'arisha Urusi. Waliokuwa wanamsimanga kipindi akiuza matunda barabarani wakawa na mshangao.

Wanaulizana: "Kile kibinti kichafu-kichafu?" Halafu wanapeana majibu: "Ndiye huyohuyo!"

Natalia akawa anahitajika kwenye majukwaa ya Ulaya na Marekani. Kila onesho kubwa la mitindo, waandaaji walihakikisha wanamlipa fedha nyingi ili asikose, Maana kukosekana kwake, kungepunguza ladha.

Wataalam wa fasheni pia waliamini mno kwa huduma ya Natalia, kila mmoja akiamini kwamba anapotokeza na vazi lake, ni turufu kwake kufanya biashara.

AKINA BABA MSIKIMBIE FAMILIA


Baba, shikamana na familia yako kwa ugumu wowote ule ambao unakutana nao. Hujui Mungu amekubariki kiasi gani kukupa mke na watoto ambao unawakimbia.

Baba wa Natalia, Mikhailovna Vodianova, baada ya kuona maisha ni magumu, akaiona familia yake ni mzigo, akakimbia. Akaacha mkewe anawalea mabinti zake kwa dhiki kubwa.

Mikhailovna akiwa hana hili wala lile, tena pengine akihisi wanaye wanaendelea kupigika na mama yao, mara akapata taarifa kuwa familia aliyoitelekeza kwa dhiki, siyo maskini tena.

Akapata taarifa kuwa familia aliyoikimbia, inaishi kwenye jumba la kifahari na maisha ni yenye uhakika. Wanaendesha magari mazuri utadhani wanatokea ukoo wa familia ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin au bilionea Roman Abramovich.

Labda mabadiliko hayo yametokana na binti yake mmoja kupata mume mwenye fedha! Anakuja kugundua kuwa hakuna nguvu ya mwanaume, bali ni mwanaye Natalia ambaye anakula sahani moja na matajiri wenye umaarufu mkubwa duniani.

Mikhailovna nafsi ilimsuta, ikabidi aitafute familia yake na kuomba msamaha kwa kosa alilofanya la kuwatelekeza wakiwa wadogo. Nao wakamjibu: "Kumbe bado upo, karibu, sisi ndiyo wanao uliotukimbia na huyu ni mkeo uliyemuona hana maana na ukamwacha solemba."

Natalia hakuwahi kumuona baba yake tangu alipowatelekeza akiwa mdogo, alikuja kuonana naye akiwa anaelea kwenye ulimwengu wa umaarufu na utajiri juu.

Chukua hii; Umaskini ni wako na mtoto ni wako. Hujazungumza na Mungu ni kwa namna gani atayabadili maisha yako. Pengine mwanao ndiye utajiri wako, unapotelekeza familia, maana yake unatelekeza utajiri.

NATALIA NA MAFANIKIO


Mwaka 2012, Jarida la Forbes ambalo linaongoza kwa heshima duniani kutokana na kutoa takwimu zenye uhakika, liliripoti kuwa Natalia anaingiza dola milioni 8.6, sawa na shilingi bilioni 18 kwa mwaka. Hata hivyo zipo taarifa kuwa Natalia amekuwa kwenye wakati mzuri kuingia kati shilingi bilioni 20 mpaka 25 kwa mwaka.

Natalia pia ni muigizaji, ameshafanya vizuri Hollywood kupitia filamu za CQ akiwa na Billy Zane, iliyotayarishwa na Kampuni ya Roman Coppola, Clash of the Titans ya Medusa, Belle du Seigneur, iliyotayarishwa na Glenio Bonder ambayo alicheza kama mhusika mkuu. Filamu hiyo ilitoka mwaka juzi (2013).

Natalia hasahau alipotoka, amekuwa akianzisha na kushiriki hatua mbalimbali kusaidia wenye uhitaji. Anayo Taasisi ya Moyo Mweupe (Naked Heart Foundation) ambayo inafanya kazi ya kusaidia kila mtoto wa Urusi kupata elimu na masuala mbalimbali ya kijamii.

HAKIKA MAISHA HUBADILIKA


Mwaka 2001, Natalia akiwa na umri wa miaka 19, huku maisha yakimuendea vizuri upande wa mitindo, alikutana na Justin Portman ambaye ni mdogo wa Viscount wa 10 wa Uingereza, Christopher Portman.

Viscount ni cheo cha heshima nchini Uingereza. Viscount ndiye anakuwa msimamizi na mwendelezaji wa mali za umma.
Natalia alifunga ndoa na Justin, kwa hiyo aliolewa kwenye ukoo wenye heshima na uwezo mkubwa nchini Uingereza. Angefikaje huko? Mungu hunyoosha njia.

Natalia na Justin walifanikiwa kupata watoto wanne lakini mwaka 2011 walitengana baada ya uhusiano wao kudumu kwa miaka 10.

Chukua hii; Ikae kichwani kwako kuwa safari ya maisha ya binadamu duniani ina mengi yenye kona kona. Dhiki unazo leo, kesho utajiri ni wako. Mpende mwenzako, msaidie unayemuona, mheshimu kila unayekutana naye. Mungu ana siri kubwa kwa waja wake.

By Luqman Maloto
 

Attachments

  • 1982263_1220288017986214_1371026743315630727_n.jpg
    1982263_1220288017986214_1371026743315630727_n.jpg
    51.8 KB · Views: 8,426
Maisha mzunguko! Namfahamu jamaa alikuwa anapanga nguo chini mtaa wa kongo,kila siku wanakimbizwa na askari wajiji, leo hii jamaa ana tzs bilioni kadhaa hapo hapo kariakoo.
 
Maisha mzunguko! Namfahamu jamaa alikuwa anapanga nguo chini mtaa wa kongo,kila siku wanakimbizwa na askari wajiji, leo hii jamaa ana tzs bilioni kadhaa hapo hapo kariakoo.

hajapitia kwa waganga kweli? siku hizi utajiri mwingi ni wa manyoka
 
Mafanikio aliyopata huyu dada si kwa kuuza matunda ila kwa sababu ya umbo lake
la ulimbwende. Heading yako inapotosha, irekebishe kwani nshaanza kujisikia vizuri
maana mke wangu ana kakibanda ka matunda hapa Naibili!
 
  • Thanks
Reactions: amu
Biashara ya matunda iko wapi mbona sijaiona au nimeiruka maana ni ndefu sana! Ungeenda direct kwenye topic mkuu inachosha kidogo.
 
Heading haina makosa inasadifu ujumbe aliotaka kuutoa na inaonyesha biashara yake ya matunda ndio iliyosababisha akapata connection ya mitindo
 
Kwa ufupi sana:Maskini wa leo ndio tajiri wa kesho na tajiri wa leo huenda akawa ndio maskini ama tajiri zaidi kesho,kubwa tuheshimiane kwa tofauti zetu za mali,afya,elimu,mavazi na hata jamaa zetu.
 
Back
Top Bottom