‘Mizigo inayosafirishwa nje haitozwi kodi’

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
KODI ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika huduma ndogo ndogo inayolenga bidhaa zinazosafirishwa nje imeibua mjadala miongoni mwa wadau, hususani watumiaji wa bandari ya Dar es Salaam wanaosafirisha mizigo kwenda nchi jirani.

Miongoni mwa malalamiko ni kwamba, VAT katika mizigo inayosafirishwa nje imekuwa ikiongeza gharama wanapopitisha mizigo katika bandari ya Dar es Salaam ikilinganishwa na bandari ya Mombasa hivyo kusababisha wateja wengi kukimbilia bandari hiyo ya nchi jirani. Wadau hao wanakwenda mbali zaidi kwa kubainisha kuwa mbali na VAT, kwenye huduma ndogondogo zinatotolewa kwenye mizigo inayosafirishwa nje, pia kodi imekuwa ikitozwa sambamba na kwenye usafirishaji wa mizigo hiyo.

Kodi hiyo inatozwa kutokana na sheria ya kodi ya mwaka 2014 ambayo ilianza kutumika mwaka wa fedha uliopita. Hata hivyo, Mamlaka ya Mapato (TRA) inafafanua kwa kuweka bayana ukweli juu ya utaratibu wa utozaji wa kodi husika. Mtafiti wa TRA, Beldon Chaula anasema chini ya mfumo wa VAT, sheria inaelekeza kutozwa kwenye bidhaa, huduma, vinapotumika ndani ya nchi. Pia nyumba mpya inapouzwa hutozwa kodi. Hutozwa asilimia 18.

“Vitu hivyo vikienda nje hutozwa kodi kwa asilimia sifuri. Kwa sababu kodi ya VAT ni kodi ambayo inamhusu mlaji, hivyo kama mizigo imefika bandarini na haijalipiwa hapa, mizigo hiyo haina kodi kwa sababu havijaliwa au kutumika ndani bali hutozwa nchi ambayo mzigo huo unakwenda kutumika,” anasema. Anaongeza, “ Lakini kuna ambavyo vimesamehewa kodi kutokana na umuhimu w ake na mahitaji hata kama vinatumika au kuliwa ndani ya nchi ambavyo kutokana na umuhimu wake wa kiuchumi, jamii, mahitaji na kiusalama mfano wake ni vifaa vya kijeshi, chakula na dawa.”

Kwa mujibu wa sheria, mizigo inayosafirishwa nje na usafirishaji wa mizigo hiyo inatozwa asilimia sifuri lakini huduma ndogondogo kwenye mizigo iendayo nje ndiyo inayotozwa kodi ya VAT ili mradi hizo huduma zimetolewa ndani ya nchi. Huduma hizo ni pamoja na gharama za kupakua au kupakia ndani ya meli na kwenye magari, usalama, ukaguzi wa mizigo, maandalizi ya nyaraka, gharama za kuhifadhi na huduma zingine.

Kushuka kwa mizigo Kamishna wa Mapato ya Ndani wa TRA, Elijah Mwandumbya anafafanua zaidi akisema, hakuna uhusiano wa kodi hiyo na kushuka kwa kiwango cha mizigo katika bandari ya Dar es Salaam. Mwandumbya anasema pamoja na kuwapo kwa sheria hiyo, bado gharama za bandari ya Dar es Salaam ni nafuu ikilinganishwa na bandari pinzani ya Mombasa, nchini Kenya.

Takwimu za ulinganifu wa gharama za kutumia bandari hizo mbili kwa mizigo ya kwenda Rwanda, zinaonesha mteja atakayetumia Bandari ya Dar es Salaam kwa kontena lenye urefu wa futi 20 linalokwenda Rwanda atatumia dola za Marekani 4,169 (takribani Sh milioni 8), ikiwa ni pamoja na gharama za bandari na VAT ya huduma ndogo ndogo. Wakati kontena kama hilo kwa bandari ya Mombasa, ambayo haina sheria inayotaka huduma hizo kutozwa VAT itamgharimu dola za Marekani 4,465 (zaidi ya Sh milioni 9) kwa Bandari ya Mombasa.

Kwa upande wa kontena lenye urefu wa futi 40 ambalo linakwenda Rwanda, mteja atatumia dola za Marekani 4,123 kwa bandari ya Dar es Salaam, na kontena la kiwango hicho hicho litatozwa dola za Marekani 4,341 kwa bandari ya Mombasa. “ Tatizo hapa si VAT pekee bali ni mchakato wa utoaji mizigo bandarini ambao unacheleweshwa kutokana na wadau wote wanaohusika katika utoaji wa mizigo kuwajibika na kuwa na ufanisi,” anasema.

Chaula anafafanua zaidi kuwa VAT haihusiki na kushuka kwa mizigo inayopitishwa bandari ya Dar es Salaam. Anasema utafiti uliofanywa kuanzia Aprili mwaka jana hadi Aprili mwaka huu, unaonesha kuwa mizigo imeshuka kwa asilimia 15 wakati bandari ya Mombasa ambayo haina kodi ya VAT imeshuka kwa asilimia 25. Anaweka wazi sababu za kushuka kwa mizigo ni kutokana na kuyumba kwa biashara China jambo ambalo halijaiathiri Tanzania pekee bali dunia kwa ujumla. Takwimu zinaonesha biashara nchini humo imeshuka.

Februari mwaka huu ilishuka kwa asilimia 20.6 kutoka dola za Marekani bilioni 126. Lakini Chaula anasema pamoja na mizigo kushuka, ukusanyaji wa mapato umeongezeka baada ya kuziba mianya ambayo wafanyabiashara wasio waaminifu walikuwa wakiitumia kukwepa kodi. Taarifa zinaonesha, siku zote kodi iliyokuwa ikikusanywa ilikuwa ni kati ya Sh bilioni 200 hadi 300 kwa mwaka katika makusanyo ya miaka iliyopita bandarini hapo.

Lakini kati ya Aprili hadi Juni mwaka huu, TRA imekusanya kati ya Sh bilioni 458 na Sh bilioni 517. “Wafanyabiashara na wasafirishaji ambao wanalalamikia VAT inayotozwa kwenye huduma ndogondogo ndio watu ambao walikuwa wakiingiza mizigo bila kulipa kodi,” alisema na kusisitiza kuwa mpango wa kudhibiti wakwepa kodi umethibitisha ongezeko la ukusanyaji wa mapato pamoja na kushuka kwa mizigo.

Anaongeza: “Kwa sasa mfanyabiashara ambaye ni mbabaishaji hawezi kuendelea kutumia bandari ya Dar es Salaam. Tuache wafanyabiashara wa kweli watumie bandari na mapato yataongezeka. Chakula anashangazwa na suala la namna VAT ya huduma ndogo kwa wanaosafirisha mizigo nje ya nchi lilivyopamba moto wakati huu wakati sheria imeanza kutumika tangu mwaka 2015 kabla ya Rais Magufuli kupewa madaraka ya kuongeza nchi “ Ingekuwa na mantiki na uzalendo, kama wafanyabiashra kwa sasa wamengukuwa wanajadilj njia nzuri ya kutekeleza sheria hiyo.”

Hata hivyo, jibu kuhusu sababu za mjadala kuibuka sasa linajibiwa na ukweli kuhusu msimamo na mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli wa kuweka mkazo katika ukusanyaji mapato, kudhibiti makusanyo ya fedha katika lango kuu la uchumi; kwa maana ya bandari.

Chini ya mkakati huo, mpango wa serikali ni kukusanya fedha nyingine kupitia TRA kutoka kwenye vyanzo mbalimbali zitumike kwa maendeleo mbalimbali nchini. Katika mwaka huu wa fedha, makadirio ya fedha na matumizi ya serikali ni Sh trilioni 29.5. Asilimia 40 ya mapato hayo inalengwa kutokana kwenye mapato yasiyo ya kodi na yale yatokanayo na kodi.
 
Back
Top Bottom