Miwani ya urembo yatajwa kuharibu macho

Miwani ya urembo yatajwa kuharibu macho

esther mashiker

JF-Expert Member
Joined
May 29, 2018
Posts
616
Reaction score
555
1078474


WATANZANIA wametahadharishwa kuhusu matatizo ya macho na wametakiwa kujiepusha na mambo yanayosababisha ubovu wa viungo hivyo muhimu. Wito huo umetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Alibainisha hayo mwishoni mwa wiki katika kambi ya macho ya siku nne iliyoandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Wanawake ya mkoani Tanga (Tawode) kwa kushirikiana na taasisi ya Kiislamu ya Bilal Muslim Mission ya Tanzania, chini ya udhamini wa taasisi ya Better Charity ya Uingereza. Ummy ametaja mambo yanayosababisha ubovu wa macho kuwa ni uvaaji wa miwani ya urembo, matumizi ya dawa za macho bila ushauri wa daktari na ulaji wa vyakula ambavyo havina vitamin A.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, katika kila Watanzania 100, wanne kati yao wanasumbuliwa na ubovu wa macho, mmoja anakabiliwa na upofu na watatu kati yao wanasumbuliwa na uoni hafu na wa kati. “Ukiona una tatizo la macho nenda kwenye vituo vya afya ukafanyiwe uchunguzi ili upate matibabu haraka, watanzania hakikisheni mnachunguza afya ya macho na afya ya kinywa mara moja kila mwaka,” alisema.

Aliongeza, “Katika watu 100 wanaokwenda kutibiwa magonjwa ya macho 80 kati yao wanapona, hivyo inapotokea fursa kama hii ichangamkieni”. Mwenyekiti wa Taasisi ya Bilal Muslim Mission Africa, Mohsin Abdallah Sheni alisema kuwa taasisi hiyo inakwenda kutoa huduma pale penye matatizo na mahitaji .

Alisema katika kambi hiyo ya siku nne mkoani Tanga, watu 2,000 wamepatiwa matibabu ya macho ikiwemo kufanyiwa uchunguzi, kufanyiwa upasuaji, kupewa dawa za macho, miwani ya kusomea, kuonea mbali, kuonea karibu na miwani ya jua.

Mbali na matatizo ya macho, pia waliwafanyia uchunguzi wa kinywa na meno wakazi wa Tanga na wale waliogundulika na matatizo ya meno, walipatiwa matibabu.

Alisema tangu taasisi hiyo ianze kutoa huduma za matibabu ya macho, watu 5,000 wamepatiwa matibabu ya macho na 500,000 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya macho. Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Clemence Marcell aliishukuru taasisi hiyo kwa kufanya huduma ya matibabu kwa wakazi wa mkoa wa Tanga bure.
 
Back
Top Bottom