"Mimi ni gamba, tena nene"

"Mimi ni gamba, tena nene"

EMT

Platinum Member
Joined
Jan 13, 2010
Posts
14,477
Reaction score
15,347
Chama nambari wani kilipokuja na sanaa za kujivua magamba niliogopa. Magamba yalipokipiga mkwara kikanywea. Badala ya kuyashughulikia, yalikishughulikia na yakaendelea kufanya vitu vyake. Nami naona heri nijigeuze gamba, lau nifaidi wafaidicho magamba.

Siku hizi kuwa gamba ni ‘dili’ bab-kubwa. Unageuka gamba na kukomba ili uzidi kutuna. Katika ugamba wangu, nitaanzisha biashara ya kusafirisha dawa za kulevya, pembe za ndovu na nyara za taifa.

Kwa vile nitakuwa na gamba nene, hata uwanja wa ndege hawatanikamata. Simpo. Kama nitaona wale `dogi’ wa polisi wanaanza kunisumbua, nitaongea na jamaa zangu wa zima ‘faya’, waniingizie `kago’ yangu.

Watashindwa nini iwapo nitawapa dau kubwa? Tuache utani, taarifa kuwa watu wa zima ‘faya’ wanatumia `migari’ yao kuvusha bidhaa za wizi pale Mwalimu Mchonga International Airport, zilinifungua akili. Nilizibuka na kugundua ni kwanini `mibwimbwi’ inajaa kwenye kaya. Kumbe jamaa ndiyo wanakula `dili’!

Badala ya kuzima moto wanahangaika na wizi siyo? Ipo siku wataungua motoni waangalie. Ila `waliniboa’ niliposikia kuwa wanachana mizigo ya abiria, tena waliotoka `majuu’ na kuiba `vijisimu’ na `vipapakatishi’ vyao. Wajua vipakatishi ni nini? Laptop au kompyuta lapa. Hayo tuyaache. Leo siwafundishi Kiswahili sanifu.

Nataka niwe gamba, tena lile la nguvu. Najua nikishaunyaka ugamba, nitapata `mshiko’ wa nguvu kiasi cha kuficha sehemu yake kule Jersey na uswazi ya Uswizi, kabla ya kugeuka mfadhili wa miradi mbalimbali ya kiroho na uroho kama magamba.

Nitakuwa nikiabudiwa kama magamba mengine. Nitatisha kama ukoma, achilia mbali miwaya. Lazima niwe gamba nifaidi bwana. Unadhani kuwa gamba mchezo? Kuanzia leo naitwa mlevi Nkwazi Gamba nene na la haja. Raha ya kuwa gamba ni kwamba unageuka mtakatifu.

Dhambi zako zote zinasafishwa na unakuwa mweupe kama theluji. Nani hapendi kuwa kama theluji? Niongeleapo gamba hapa simaanishi lile jeusi la kobe na kasa. Ni gamba jeupe la `utakatifu’ lililojaa utakavitu. Gamba la kitu si la kinyama mwitu kama kobe. Gamba na neema na `zali’ na si gamba la konokono au kakakuona.

Gamba langu lina nguvu kuliko hata magamba ya vyuo au shahada ambazo nimejaza nyumbani kwangu. Lazima nivae gamba. Ukiwa na gamba wenye gwanda na magwanda hawakutishi. Badala ya kukutia adabu, wanaishia kukujadili huku wewe ukijinoma na `maulaji’ yanayotokana na kuwa gamba. Gamba bwana!

Ujanja kupata gamba na si vinginevyo. Raha ya kuwa gamba ni kwamba unalinda kokwa ambalo mara nyingi ndilo linamhifadhi mdudu. Unahifadhi kokwa na kokwa linakuhifadhi. Mnahifadhiana. Maana ukibanduliwa, ujue ndiyo mwisho wa kokwa.

Na gamba haliwezi kuota bila kuwapo kokwa. Kokwa haliwezi kuishi bila gamba. Hivyo, tunatumiana na kutumiana hadi tunaishi. Uzuri wa kuhifadhi na kuhifadhiwa na kokwa si kama ule wa malkia wa mchwa ambaye huwaruhusu `walume’ wampe `urodazi’ halafu akawaua ili wasijishaue kuwa walishiriki kikombe na bi-mkubwa.

Uzuri wa kuvaa gamba au kuwa gamba ni kupata ulinzi kutoka kwa watukufu wenye magamba mazito. Mara hii, mmesahau jinsi gamba lilivyomuokoa Eddie Ewassa na Andy Change baada ya wapingaji kuwashupalia?

Risasi za wapingaji hazikuwapata kwa vile zisingepenya kwenye magamba yao mazito. Hakuna kitu hunifanya ninywe na kucheka kama sanaa za jamaa yangu Njaa Kaya. Wajua? Akiwa ameuchapa `ulabu’ si alijisahau akapayuka kuwa lazima genge lao lijivue gamba, asijue anahusika katika hilo!

Baada ya magamba mengine kuinyaka, yakapanga mikakati ya kumvua nguo ili kila mtu aone gamba lake lilivyo nene kama yao. Akiwa amemtuma Mapepe Napepea Ninaye, kuwashambulia magamba wenzake bila kujua na yake wanayajua, Njaa Kaya aliishia kuuchomoa na kunywea.

Huku Mapepe naye akizodolewa kwa kimuhe muhe na unywanywa wake. Mapepe alinywea, kadhalika akakosa hata la kuwaambia waandishi wa umbea. Aliona aibu kuongea utadhani alikuwa na kiseyeye. Magamba yaliendelea kundunda hadi kutishia hata ulaji wa mweyewe.

Asingestuka na kuufyata, angeishia kuvuliwa gamba lake na kuadhirika huku wao wakiendelea `kupeta’, kutesa na `kusepa’. Kimsingi, rafiki yangu wa kaya huwa na ka-ugonjwa ambako kitaalamu huitwa payukayosis mental marasmus.

Huu ni ungonjwa hatari ambao ukimpata mtu huadhirika mchana kweupe. Nakumbuka ugonjwa huu uligunduliwa mara ya kwanza nchini kutoka kwa mgonjwa aliyeitwa Yusifu Makambae Ngosi.

Huyu bwana alikuwa ana kaugonjwa haka. Alikuwa akipayuka huku kinywa na ubongo vikikosa mawasiliano. Hata Mapepe Musa Nnaye naye ana ka-ugonjwa haka, ingawa hakajafikia kiwango cha wagonjwa wawili wa kwanza. Gamba ni kinga kuliko hata tunguli. Ukiwa na gamba hata `ndata’ hawakuoni na wakikuona wanapumbaa, wakikuacha ukifanya vitu vyako.

Kama si gamba, rafiki yangu Andaraman Kinamna angekuwa akikunyea `mtondoo’ lupango. Baada ya `zali’ lake la kusafirisha vipusa Mbali ya Mashariki kufichuka, `ndata’ walitaka wamtie mikononi. Walipogundua kuwa kumbe naye gamba wakanywea. Kuwazodoa zaidi Njaa Kaya alimpa `ulaji’ kwenye genge na kutuacha wengine vinywa wazi.

Jamaa anazidi kutanua hata kwenda kutembelea miradi yake huko alikouza nyara za umma. Wajua? Nyara za umma hata ukiziteka nyara hakuna wa kukuuma, maana huwa nyara za umma, sawa na mali ya umma, haziumi. Unaziuma na hakuna chombo cha dolari cha kukuuma, angalau ukakoma.

Kayani kwetu lazima uwe gamba ndiyo uishi, vinginevyo utajiishia sawa na walalanjaa. Nani alijua kuwa Roast Tamu La Aziz angeweza kufanya yote aliyofanya kuanzia Kagodamn, Downs, Richmonduli na uchafu mwingine na akaendelea kuula bila kuliwa?

Gamba bwana! Ukiwa na gamba una kinga ya uhakika. Ndiyo maana nami napanga kuwa gamba ili wenye magwanda wakinilenga wanoe kama walivyonoa kwa magamba tajwa hapo juu.

Mwandishi wa makala haya ni msomaji wa NIPASHE anayeishi nchini Canada. Anapatikana kupitia barua pepe: nkwazigatsha@yahoo.com

Chanzo:
Home
 
Mi siyo gamba

Sent from my BlackBerry 8520 using JamiiForums
 
Huwezi kuwa unaishi kanada halafu uwe na akili mgando namna hii
 
Ha haaa, nimeipenda ya Mapepe Napepea Ninaye....

Jamaa ashukuru yuko Kanada vinginevyo tungemtuma Ramadhani Ighondu amtie adabu kwenye kucha, meno na macho yake bila ganzi
 
Endelea kuwa gamba mkuu
Kiukweli, mimi mwenyewe nataka niwe gamba,
Huku kitaa mambo hayaendi, sina kabisa pesa kwa sasa, nikiwa gamba tena la ukweli nikaanza kuwatukana akina Slaa na Mbowe, walah nakwambia mambo yangu yatakuwa supa muda sio mrefu.

Mimi sitategemea hizi buku saba za kupost kwenye mitando, nitaanzisha dili mbalimbali, haramu na halali, kama ni kwenye gari muda wote inapepea bendera ya magamba na picha za mkulu za wakati wa kampeni, mfukoni na kadi ya magamba, nimeweka wimbo wa sisiem nambari wani, hakuna askari atakayenisumbua kwenye dili zangu.

Niwe gamba halafu niwe hata mjumbe tu wa mkutano mkuu, haki ya nani ukata itakuwa bye bye.
 
Hamna kitu hapounajipendekeza kwa slaa tu
Mkuu, hebu ni PM na mimi namna ya kuwa mshirika ili tuungame pamoja katika chama chetu kilichotulea, CHADEMA wanataka kuleta vurugu tu hawana lolote.

Ni PM basi mkuu, tayari nimeshaonyesha adivataizi, namna ntakavyokuwa nawatoa nishai.
 
Mkuu nimeikubali luga yako fasihi.
We ni mkali wa luga, lakini hata mantiki imo.
 
Watanzania, kuwa gamba nene gamba jembamba yote ni gamba tu.

Hii dhana ya kujivua gamba naona watanzania wengi hawana imani nayo, lakini ni dhana ya kukirudishia chama heshima kwa jamii, na kwa kiasi fulani imefanikiwa.

Lakini mleta mada naona kwenye uandishi wake amejaza kebehi za kutosha as if on earth everything is perfect except CCM and its government.

Hapa duniani kila kada kwa namna moja hama nyingine ina mapungufu, mambo ya kubanwa na mishipa ya shingo kusema ya wenzako kama wewe tu ndiye uliyepewa macho, sio uungwana.

Dhana ya watanzania kujiuliza tumeifanyia nini nchi yetu ndio inakuja hapa, je, mleta mada kama haya ya wizi unayajua, umechukua hatua gani madhubuti mbali na hii ya kuja kulia lia humu JF?

Kama una vielelezo vyote vya kubaini wahusika wa matukio uliyo yaeleza, kwanini hamtaki kuviwasilisha mahala stahiki? Na sio pengine, ni polisi.

Wote humu jamvini tuna imani na mahakama zetu kama vyombo vya kusimamia na kutetea haki na usawa, nenda na ushahidi wako kama wewe ni mzalendo kweli instead ya kuja na shutuma humu JF ya kwamba ukiwa 'gamba' ndio mambo ya kiuhalifu ruksa kufanya na hakuna atakae hoji.

"KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI, KIDUMU CHAMA TAWALA."
 
Mkuu si mzima wewe ,jipange tena urudi tena hii hoja haijahiti.
 
Gamba kinga tosha dhidi ya maradhi ya kiuchumi na kisiasa bongo!
 
Aisee huyu bwana nimtaalamu wanao sema nimgonjwa ndio wagonjwa anaeleweka vizuri tu, anafaa kuwa mwana mashairi
 
Mkuu,

Umeifanya siku yangu kuwa nzuri sana kwa simulizi hii...
 
Back
Top Bottom