Millya na wenzake kuhojiwa tena | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Millya na wenzake kuhojiwa tena

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Oct 31, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Oct 31, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  Mvutano UVCCM Arusha

  Paul Sarwatt

  Arusha

  [​IMG]


  Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James ole Millya

  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha kinakabiliwa na wiki ngumu ya kufanya uamuzi wa kuwajadili wanachama wake wa Umoja wa Vijana wanaodaiwa "kuasi" kwa kufanya maandamano haramu pamoja na kufungua mashina mawili ya wakereketwa, Oktoba 10, mwaka huu, kinyume cha taratibu.


  Hatua hiyo iliibua upya mgogoro mkubwa baina ya uongozi wa Wilaya ya Arusha Mjini na ule wa Mkoa wa Arusha ambao kwa muda mrefu umekuwa haupikiki chungu kimoja kutokana na tofauti za kisiasa.


  Mgogoro ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoani hapa unadaiwa kuungwa mkono na pande mbili zinazowapigia debe watu wanaotajwa kuweza kuwania nafasi ya urais, mwaka 2015, kwa tiketi ya chama hicho tawala.


  Maandamano hayo ambayo yaliongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM ngazi ya Taifa, Beno Malisa, yalipigwa marufuku na sekretarieti ya CCM Mkoa iliyoketi Oktoba 8, baada ya kupokea malalamiko ya kamati ya utekelezaji ya Wilaya ya Arusha Mjini.


  Maandamano hayo pia yalizuiwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha lakini vijana hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa umoja huo Mkoa wa Arusha, James ole Millya, walikaidi maagizo hayo na baadaye jeshi hilo lilisalimu amri.


  Awali, uongozi wa Wilaya ya Arusha chini ya Mwenyekiti wake, Goddy Mwalusamba, ulipinga vikali hatua ya Malisa kufungua mashina ya wakereketwa kwa maelezo kuwa uongozi wa wilaya ambao ndiyo wenye majukumu ya kuandaa shughuli hiyo, haukushirikishwa.


  Mwenyekiti huyo na kamati yake ya utekelezaji walilamika kwa uongozi wa CCM Mkoa wa Arusha ambao haraka ulichukua hatua ya kuwataka Millya na wenzake kusitisha shughuli hiyo kwa kuwaandikia barua lakini walipuuza maagizo hayo.


  Pamoja na kupuuza, Millya anadaiwa kutoa kauli zenye utata akiwatuhumu baadhi ya viongozi wenzake ndani ya UVCCM ngazi ya Taifa, kuingilia masula ya umoja huo mkoani Arusha.


  Mwenyekiti huyo pia anadaiwa kulishambulia Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha lililojaribu kuzima maandamano yao kwa kushawishiwa na mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwan, ambaye hata hivyo, hakumtaja kwa jina kwa wakati huo.

  Ndani ya UVCCM, Ridhiwan ni mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM-Taifa.


  Lakini licha ya Millya kutomtaja Ridhiwan katika mkutano wa hadhara, anadaiwa kumtaja katika kikao kati yake na waandishi wa habari, kilichofanyika katika Hoteli ya Lush Garden, alipozungumzia mtafaruku uliokuwa umejitokeza.


  "Ingawa polisi wanadai kutunyima kibali cha maandamano ya kufungua mashina ya Umoja wa Vijana na mkutano wa hadhara kwa kile wanachodai taarifa za kiintelijensia kugundua kutatokea uvunjifu wa amani, tumepata habari kuwa Ridhiwan ndiye kapiga simu kuelekeza tunyimwe. Sisi tutaendelea na shughuli yetu liwalo na liwe, wacha watupige mabomu kama CHADEMA," alikaririwa akisema Millya.


  Millya pia alimshambulia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye na kumtaja kuwa ni kama ugonjwa wa saratani kwa chama hicho na kuonya kama hataadhibitiwa, atasababisha anguko la chama.


  Kutokana na kauli hiyo, Jeshi la Polisi lilitangaza kumsaka Millya ambaye alijisalimisha wiki iliyopita na kuhojiwa kwa saa kadhaa na jeshi hilo kupitia kwa Kaimu Kamanda wa Mkoa, Akili Mpwapwa, lilidai kuwa kauli ya Millya ililenga kulipaka matope jeshi hilo.


  Hata hivyo, baada ya mahojiano hayo Polisi mkoani Arusha hawakutangaza iwapo watachukua hatua zozote za kisheria dhidi ya Millya. Lakini wakati ikionekana kuwa Mwenyekiti huyo ameruka kiunzi cha polisi, bado giza limetanda kuhusu hatima yake ndani ya chama hicho, hasa ikizingatiwa kuwa uongozi wa mkoa umeitisha vikao vya kimaadili kwa lengo la kumjadili.


  Taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo mbalimbali ndani ya CCM mkoa wa Arusha na Umoja wa Vijana zinaeleza kuwa kikao cha Kamati ya Maadili kilitarajiwa kufanyika siku yoyote kuanzia wiki hii, pamoja na kile cha kamati ya siasa ya mkoa na lengo la vikao hivyo ni kumjadili Millya na wenzake.


  Taarifa hizo zinabainisha kuwa baada ya vikao hivyo mapendekezo yake yote yatapelekwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ngazi ya Mkoa, kinachotarajiwa kufanyika wiki ya mwanzo ya Novemba. Awali, kikao hicho kilipangwa kufanyika Oktoba 29, lakini kilisogezwa mbele.


  Wengine watakaongukiwa na "rungu" la Kamati ya Maadili na siasa kwa kujadiliwa ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu kupitia UVCCM, Catherine Magige, ambaye anadaiwa kushirikiana na Millya na wafuasi wake, kutoa kauli chafu dhidi ya viongozi wa CCM.


  Katika orodha hiyo pia yupo Katibu wa Mkoa wa UVCCM, Abadalh Mpokwa na wajumbe kadhaa wa kamati ya utekelezaji ya mkoa na wanachama wengine wa UVCCM, ambao wanadaiwa kuwa vinara wa kuendekeza makundi na migogoro kwa kutumiwa na baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wanawalipa fedha wanachama hao.


  Aidha, hali pia si shwari kwa Kaimu Mwenyekiti Benno Malisa ambaye inaelezwa kuwa na anaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu na vikao vya juu vya chama kwa hatua yake ya kushinikiza mashina hayo yafunguliwe wakati haikuwa katika ratiba ya chama.


  Taarifa zinaeleza kuwa Benno alikuwa mjini Babati mkoani Manyara kuhudhuria sherehe za harusi ya Katibu wa UVCCM wa mkoa huo na ndipo katika sherehe hizo, wakapanga kufungua mashina mjini Arusha hatua ambayo ilikuja kupingwa na vijana wa Wilaya ya Arusha Mjini, kutokana na taratibu kudaiwa kukiukwa.


  "Ni kweli tunajiandaa kufanya vikao vya kuwajadili viongozi wa Jumuiya ya Vijana (Millya) na wenzake kuanzia leo (Jumatatu) na kutakuwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa, itakayofanyika wiki ijayo," alidokeza kiongozi mwandamizi wa chama hicho mkoani Arusha, aliyeomba jina lake lihifadhiwe.


  Kiongozi huyo aliongeza kuwa tofauti na vikao vya Juni, mwaka huu, ambapo Millya alipewa onyo kali, vikao vya sasa vitafanyika kwa tahadhari kubwa kwani baadhi ya wajumbe wamechoshwa na migogoro isiyoisha ndani ya CCM ngazi ya mkoa, ambayo inaelezwa kuwa chanzo chake ni kauli tata za Mwenyekiti huyo wa UVCCM.


  "Zamu hii wajumbe wamejipanga sana kuhakikisha kuwa hawatetereki katika kufikia maamuzi magumu na maamuzi ya vikao hivyo yanaweza kuleta maumivu makali kwa wahusika bila kujali nyadhifa zao," alijigamba kiongozi huyo bila kufafanua ni maamuzi gani.


  Kiongozi huyo alisema miongoni mwa tuhuma zinazowakabili Millya na wenzake ni pamoja na kukaidi maagizo ya sekretarieti ya CCM Mkoa, kufanya maandamano haramu na kutoa kauli zenye lengo la kuwachafua viongozi wa chama wa ngazi juu mbele ya umma.


  "Millya amevumiliwa sana kwa kauli zake za kudhalilisha viongozi wa ngazi za juu wa chama na wengine ambao ni wakubwa kwake kiumri, kwa hiyo sasa wengi wanasema lazima achukuliwe hatua kali za kinidhamu, CCM si genge la wahuni hata kidogo," aliongeza kada huyo.


  Akizungumza Raia Mwema kuhusu taarifa za vikao hivyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, hakuwa tayari kukubali wala kukanusha kuwepo kwa vikao vya kuwajadili Millya na wenzake.


  "Naomba muwe wavumilivu muda ukifika tutawaarifu kwa sasa bado hatuna cha kuwaambia na pia mkumbuke kuwa CCM inafanya kazi kwa kanuni na taratibu zake, hivyo muda muafaka wa kuwapa taarifa ukiwadia tutawaambia," alisema Chatanda.


  Kwa upande wake, Millya hakupatikana juzi kwa simu yake ya mkononi kwani kila alipopigiwa hakuipokea lakini Mbunge wa Vitimaalumu, Catherine Magige, alieleza kuwa hadi juzi hakuwa na taarifa zozote rasmi za kuitwa kwa ajili ya mahojiano na kamati hizo za chama.


  "Sina taarifa za kuitwa kwenye mahojiano yoyote ya chama ndiyo kwanza nazisikia kwako kama yapo nitayasubiri kwa hamu," alisema Magige na kukata simu.


  Katika hatua nyingine isiyotarajiwa, Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond na ambaye ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, alivunja ukimya kwa kuitisha mkutano na waandishi wa habari nyumbani kwake na kuwakana Millya na wenzake hao.


  Kwa mujibu wa Lowassa, hahusiki na kundi hilo la akina Millya na wenzake licha ya kuhusishwa nao kwa muda mrefu sasa, ikidaiwa kuwa vijana hao wakiongozwa na Millya wamekuwa wakipigania maslahi yake binafsi na si ya CCM.


  Lowassa alieleza kuwa wakati vijana hao wakifanya maandamano yao yeye alikuwa nje ya nchi kwa matibabu hivyo asingeweza kuwasiliana nao na kupanga mipango ya maandamano hayo haramu.


  Mbunge huyo wa Monduli pia alitumia fursa hiyo kukanusha kuhusika kumhujumu Rais Jakaya Kikwete, akisisitiza kuwa ni jambo lisiloingia akilini kumhusisha yeye na mkakati huo.


  Alitumia madaraka aliyonayo kwa sasa kuwa ni sababu kubwa za kutofanya hujuma. Madaraka hayo ni ubunge kwa tiketi ya CCM na uenyeiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.


  Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Millya kukumbwa na sekeseke baada ya Juni 11, mwaka huu, Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Arusha, kumpa onyo kali, baada ya kubainika kwamba alimtukana, kumkashifu na kutumia lugha ya udhalilishaji dhidi ya Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda.


  Katika kikao hicho cha Halmashauri Kuu, Millya aliokolewa na wajumbe ambao hata hivyo, kulikuwa na madai mazito kuwa baadhi walihongwa fedha ili kumpigania asinyang'anywe kadi yake ya chama. Je, historia itajirudia tena ndani ya miezi mitatu? Vikao vya CCM vitatoa majibu sahihi.


   
 2. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #2
  Oct 31, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  Ridhwan ni kiongozi Umoja wa Vijana, ni kiongozi wa Usuluhishi Yanga

  Kote huko hawampendi na bado anajipeleka; ni mtoto wa pekee wa rais wa nchi ya bTanzania mwenye Udaki zaidi ya wote naona zaidi ya Mwinyi

  Naona Kikwete kaingia sio kuongoza kwa miaka 10 ni kwa Karne
   
Loading...