Kuna hii tahariri ya leo ya Tanzania Daima nimeona tushee namna huyu mama Buriani alivyojikanyanga jana kutetea utumbo wa matumizi mabaya ya walipa kodi walalahoi eti kisa kueleza uzuri wa bageti mbaya.
JANA Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Dk. Batilda Burian, alitangaza bungeni kuwa serikali ilitumia sh milioni 142.96 kugharamia safari za mawaziri na wasaidizi wao mwaka jana, wakati wa ziara za mikoani, kwa kile kilichoelezwa kutoa ufafanuzi kuhusu bajeti ya serikali ya mwaka 2007/08.
Dk. Burian alieleza hayo alipokuwa akijibu swali bungeni na kueleza kuwa ziara hizo zilikuwa muhimu licha ya kuwapo wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi kuweza kuifanya kazi hiyo.
Alieleza kuwa wabunge kama wawakilishi wa wananchi wana wajibu wao na serikali nayo kwa upande wake inayo majukumu yake. Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhonga Said Ruhwanya (CHADEMA).
Kiasi hiki cha fedha kilichotumika kwa ziara hizi ni matumizi mabaya ya fedha kwa sababu fedha zilizotumika ni za walipa kodi wengi wao wakiwa walalahoi.
Pamoja na serikali kutumia kiasi hicho kikubwa cha fedha, hakuna mafanikio ya moja kwa moja yaliyoonekana kutokana na ziara hizo zilizowagharimu wananchi.
Fedha hizi zilizokwenda kuteketezwa katika ziara ambazo hazikuwa na manufaa yoyote kwa umma zingeweza kutumika kufanyiwa shughuli mbalimbali za maendeleo kama kuboresha sekta ya elimu na nyinginezo muhimu au kushughulikia kero mbalimbali za wananchi.
Hakika jambo hilo na mengineyo ambayo yamekuwa kero kwa wanannchi kwa kiasi kikubwa, yameshusha umaarufu wa serikali hiyo iliyokuja na falsafa ya Ari mpya, Nguvu mpya na Kasi mpya.
Kushuka kwa umaarufu wa serikali kulidhihirishwa na utafiti wa REDET uliofanywa mwisoni mwa mwaka jana.
Tangu awali wananchi walionekana kuzipinga ziara hizo za mawaziri, lakini kama kawaida yake serikali ililazimisha na kupuuza mawazo ya wananchi walio wengi.
Matokeo yake katika ziara hizo, baadhi ya mawaziri walizomewa na wananchi. Kuna ushahidi wa wazi kabisa, ingawa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikipinga kuwapo kwa vitendo hivyo.
Kama kweli ziara hizo zilikuwa na lengo la kueleza uzuri na ubaya wa bajeti, wananchi walikwishafahamu tangu ilipopitishwa bungeni Julai, mwaka jana, kwani baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo gharama za maisha zilipanda na hali ya maisha kuwa ya juu.
Hata kama kulikuwapo na ulazima wa kufanya ziara hizo, jukumu hilo wangeachiwa wabunge ambao wana nafasi nzuri ya kuwafikia wananchi na hapo ndipo unapoonekana umuhimu wa mgawanyiko wa madaraka.
Ufujaji wa aina hiyo wa fedha za walipa kodi kwa kiasi kikubwa unawaumiza wananchi na kuwafanya wasiwe na imani na serikali yao.
Haijawahi kutokea katika historia ya Tanzania serikali ikatuma mawaziri na manaibu wake kwenda mikoani kwa wananchi kuelezea uzuri wa bajeti. Kibaya zaidi, hakuna mafanikio yaliyoonekana kutokana na ziara hizo. Hili ni funzo kubwa kwa Serikali ya Awamu ya Nne.
Serikali ikitaka iendelee kuaminiwa na kuheshimiwa na wananchi, ni lazima itimize ahadi zake kwa vitendo na si maneno, kwani hayawasaidii kuleta maendeleo kwa wananchi waliokwishaanza kuonyesha kukata tamaa na serikali yao.