Milima, mabonde kurejesha CCM ya Nyerere, Karume

Milima, mabonde kurejesha CCM ya Nyerere, Karume

kalulukalunde

JF-Expert Member
Joined
May 27, 2016
Posts
1,056
Reaction score
1,086
MACHO na masikio ya Watanzania na dunia kwa ujumla yanaelekezwa katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaofanyika mjini Dodoma leo, ambao unatazamiwa kumchagua Rais John Magufuli kuwa Mwenyekiti wa Taifa mpya wa chama hicho kikongwe barani Afrika.

Rais Magufuli anapokea kijiti hicho kutoka kwa mtangulizi wake Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ikiwa umesalia takribani mwaka mmoja kabla ya muda halali unaotajwa na Katiba ya CCM katika kuwasimika viongozi wapya kufika.

Pamoja na matakwa hayo ya Katiba, CCM imejiwekea utamaduni ambao sasa umegeuka kuwa utaratibu kwa mwanachama wake anapochaguliwa kuwa Rais, kukabidhiwa pia kofia ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho kabla ya muda ili kumwezesha kutekeleza majukumu yake kwa tija na ufanisi zaidi na hivyo kuharakisha utekelezaji wa Ilani yake.

Tofauti na miaka iliyotangulia, Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM wa leo unaonekana kuvuta hisia za watu wengi zaidi, kutokana na ukweli kwamba chama hicho kipo katika harakati za kujibadili, safari inayoaminika kuasisiwa na uongozi unaoondoka madarakani wa Kikwete, jukumu ambalo lilitekelezwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana.

Mwezi Machi mwaka 2011, CCM ilijikuta ikiingia katika shinikizo kubwa la mabadiliko ya uongozi, taarifa zikibainisha kuwa msukumo huo ulitoka miongoni mwa wana-CCM na hata nje na hasa upepo mbaya wa kisiasa uliokuwa unaovuma ukichochewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati huo. Taarifa za ndani ya CCM wakati huo zilieleza bayana kuwepo na uwezekano mkubwa wa mabadiliko ya uongozi wa juu wa chama hicho kikongwe nchini, wakati wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM walipokutana mjini Dodoma mwezi Machi, 2011.

Mkutano huo wa NEC-CCM ulikuwa mkutano wa pili uliozongwa na shinikizo la mabadiliko ya uongozi wa juu, ukitanguliwa na mkutano kama huo uliofanyika Butiama, mkoani Mara, Machi mwaka 2008. Mkutano wa wakati huo wa Butiama uligubikwa pia na shinikizo la kutaka kufukuzwa baadhi ya viongozi wa CCM hasa waliokuwa wakituhumiwa kwa kashfa mbalimbali za kitaifa.

Hata hivyo, katika mkutano huo ambao haukuhudhuriwa na marais na wenyeviti wastaafu wa CCM, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, vigogo waliolengwa kufukuzwa walibaki, tena wakisifiwa kwa umahiri wao katika uongozi hali iliyowakatisha tamaa waliokuwa na kiu ya kuona mabadiliko ya uongozi. Inaelezwa pia ya kuwa kati ya mambo yaliyozidi kuwapa nguvu upinzani na hasa Chadema ilikuwa ni hatua ya CCM kushindwa kuwajibishana katika makosa yaliyo wazi mbele ya jamii.

Taarifa zilisema kuwa kutokana na mwenendo usioridhisha wa uendeshaji wa chama hicho hakukuwa na namna ya kufanya zaidi ya kuwaondoa katika uongozi sekretariati nzima iliyokuwa inaongozwa na Katibu Mkuu wa wakati huo, Yusuf Makamba.

Kama ilivyotarajiwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais mstaafu Kikwete aliwasilisha katika mkutano huo wa NEC mapendekezo ya kuifanyia mabadiliko makubwa sekretarieti ya chama hicho kwa kumuondoa Katibu Mkuu Makamba na kuingia Wilson Mkama ambaye kazi yake kubwa inaaminika ilikuwa ni kutengeneza mazingira ya uongozi ambao baadaye ulishikwa na Kinana.

Naam,Katibu Mkuu Kinana aliposhika nafasi hiyo alianza harakati za kukibadili chama hicho ili kukirejesha katika misingi ya awali, ya chama kinachopigania wakulina na wafanyakazi wa Tanzania. Wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Miaka 34 ya CCM, Rais mstaafu Kikwete alisema CCM inalazimika kuachana na wanachama na viongozi wanaokuwa mzigo kwa chama hicho na kujifananisha na nyoka ambaye huwa anajivua gamba linapochakaa.

Kauli hiyo ya Kikwete ilikuwa chanzo cha kuibuka kwa falsafa mpya ndani ya chama hicho ya kujivua magamba iliyotumika kama kichocheo cha chama hicho kuanza kujisafisha. Mkutano Mkuu 2012 Kimsingi, maazimio katika mkutano mkuu wa 2012 yalikuwa mengi, lakini Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais mstaafu Kikwete alisema kulikuwa na maazimio matatu kwa ujumla wake.

Alisema mambo hayo ni kuimarisha CCM kama taasisi, viongozi wa CCM kufanya kazi ya chama kwa kuwa karibu na wananchi na pia kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi 2010-2015. Ni kutokana na kauli hiyo, Katibu Mkuu wa CCM akiongozana na baadhi ya maofisa wa juu wa CCM akiwemo Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye (sasa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo), aliamua kufanya ziara katika mikoa yote nchini ili kuanza kazi ya kuirejesha CCM mikononi mwa wananchi wanyonge.

Kinana akiwa kwenye ziara zake hizo alitangaza waziwazi kwamba yeye anataka CCM ya waanzilishi, yaani ya Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Amaan Karume irudi. Alisema CCM lazima ipinge unyonyaji, ukabaila uzembe na ufisadi kwa nguvu zote. Alisisitiza kuwa viongozi wa CCM lazima waitishe vikao vyote vya kikatiba kuanzia mashina, matawi, kata, wilaya na mikoa kama ilivyo kwa vikao vya kitaifa.

Viongozi hao wa CCM, Kinana anasema, lazima watoke ndani ya CCM na kusisitiza kwamba makatibu wa mikoa wawe na utaratibu wa kuwapendekeza wanaofanya vizuri kupanda vyeo kuwa makatibu wa wilaya, hali kadhalika wa wilaya lazima wawapendekeze wale wa kata ili wapande vyeo wanaofanya vizuri. Pamoja na kusema ukweli kuhusu hali halisi ya uongozi ndani ya CCM, Kinana alianza kutamka wazi kwamba hivi sasa mambo mengine ndani ya CCM ni ya ‘hovyo kabisa’ na yanahitaji marekebisho ya haraka.

Katibu Mkuu huyo alisisitiza kuwa kuimarisha CCM ni pamoja na kufanya kazi ya chama ndani ya umma na kwamba viongozi wa chama lazima watoke kwenda kuwatembelea wananchi, kuzungumza nao, kuona au hata kushiriki katika shughuli zao hususani kilimo na ufugaji.

Katika kudhihirisha hayo kwa vitendo Kinana akiwa katika ziara zake alionekana akishiriki katika kazi mbalimbali za kijamii na uzalishaji mali kama ilivyokuwa kwa Nyerere na Karume, ikiwemo kushiriki shughuli za kilimo, ujenzi wa shule, zahanati, barabara na miundombinu mingine muhimu, hatua iliyochangia kwa kiwango cha juu wananchi kurejesha imani na mapenzi kwa chama hicho.

Sambamba na kushiriki, Kinana aliwataka viongozi wa CCM hususani wenyeviti na makatibu wa wilaya na mikoa washiriki kazi za maendeleo pamoja na wananchi. Alisema kwa sasa lazima kazi za kujitolea zifufuliwe zikiwamo za kujenga shule, kulima barabara za mitaa, na hata kujenga nyumba za wanakijiji.

Aliwahamasisha viongozi wa CCM wawahamasishe wanachama wake kushiriki kazi za maendeleo kwa hiari kwa kutumia muda wa saa moja na hata mbili huku akisema; “CCM tuliyoachiwa na waasisi wetu ilikuwa ni ya kutetea wanyonge, kuwatetea wazee, watoto, yatima na wajane. Hivyo, CCM ya sasa lazima iwatetee wakulima, wafanyakazi na hata wafanyabiashara wanaoonewa.” Aina ya utendaji ya Kinana ndani ya CCM ilianza kuwavutia wananchi na viongozi wengi.

Akizungumzia ziara hizo, Mwenyekiti wa CCM anayeondoka madarakani leo, Kikwete alikiri wazi kwamba Kinana amekuwa akishiriki katika kutafuta majawabu ya matatizo yanayowakabili Watanzania na kwamba amekuwa msaada mkubwa kwa chama hicho.

Ni katika ziara hiyo iliyoanzia Mtwara Desemba 2012 na kumalizikia Kisiwani Ukerewe, Mwanza Julai, 2015, sauti za Watanzania zilianza kusikika zikikiri wazi kuwa CCM ya wakati wa Nyerere na Karume imeanza kurejea na bila shaka hilo ni moja ya mafanikio makubwa ya CCM katika kushinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015.

Hata hivyo, CCM inafanya Mkutano Mkuu Maalumu leo huku Watanzania wakiwa na imani kwamba safari iliyotekelezwa kwa mafanikio na Sekretarieti ya Kinana, sasa itapata kasi zaidi mara baada ya Rais Magufuli kukabidhiwa rasmi uenyekiti wa Taifa wa CCM. Imani yao inatokana na dhamira ya dhati inayoendelea kuoneshwa na Rais Magufuli katika kuirejesha Tanzania mikononi mwa wananchi wanyonge, huku akiapa kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi, ambavyo mizizi yake pia ilisababisha athari kubwa ndani ya chama hicho kikongwe duniani.
 
Back
Top Bottom