kbm
JF-Expert Member
- Oct 5, 2012
- 5,224
- 1,676
Rais John Magufuli.
Siku moja tangu Rais John Magufuli, kuonyesha kukerwa na umeme utokanao na mitambo ya kukodi kutokana na gharama kubwa ya tozo ya uwekezaji ‘capacity charge' zinazotozwa na kampuni zinazozalisha umeme, Nipashe imebaini tayari Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limeshatumia Sh trilioni 4.6 kwa ajili ya gharama hiyo ikiwa ni mbali na ile ya kununua umeme wa kampuni hizo.
Jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba, aliliambia gazeti hili kwamba, mpaka sasa wameshamaliza mikataba na kampuni moja ya kufua umeme na nyingine moja mkataba wake utaisha mwezi huu na kwamba kutokana na agizo la Rais Magufuli, hawataingia tena mkataba wa umeme na wazalishaji wa nishati hiyo.
Juzi akiweka jiwe la msingi kwenye mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi II, Rais Magufuli alisema: “Ni lazima nchi yetu tuachane na umeme usio na uhakika, umeme wa kukodishakodisha, umeme wa kutumia watu na ndiyo maana kumekuwa na matatizo mengi mara IPTL, mara nini, ni kwa sababu tulizoea maumeme ya kukodisha kodisha, ya wafanyabiashara, kwa hiyo hatua hii ya umeme wetu, ambao tutaumiliki sisi wenyewe tutafanikiwa katika maendeleo.
“Tuachane na mitambo ya kukodi, tumechoka kufanyishwa biashara na wawekezaji, tunalipia `capacity charge' za ajabu ajabu halafu tunalipia bei ya ajabu.
“Tunawapa shida Watanzania wa hali ya chini, kila mmoja anahitaji umeme, lakini wengine wanashindwa kuuvuta kwa sababu umeme ni wa juu.”
HALI HALISI
Moja ya taarifa ya serikali ambayo gazeti hili imeiona, inaonyesha kwamba kampuni ya kufua umeme ya IPTL ambayo inauzia Tanesco kila uniti ya umeme kwa Dola za Marekani senti, 23.1 kila mwezi inalipwa Capacity Charge ya Dola za Marekani 2,655,786.
Ukikokotoa kiasi hicho kwa wastani wa kila Dola moja kwa Sh. 2190.15, inafanya kila mwezi IPTL kulipwa Sh. bilioni 5.816 ambayo kwa mwaka inakuwa wastani wa Sh. bilioni 69.792.
Kutokana na hesabu hizo, tangu IPTL kuanza uzalishaji mwaka 2002 mpaka sasa wamelipwa takribani Sh. trilioni 1.046 na mpaka mkataba wao wa miaka 20 uishe mwaka 2022, watakuwa wamelipwa wastani wa Sh. trilioni 1.395.
Kwa upande wa Aggreko, ambao taarifa hiyo inaonyesha wanauzia Tanesco uniti moja ya umeme kwa Dola za Marekani senti 35.8, kila mwezi wanalipwa Capacity Charge ya Dola za Marekani 2,084,998.43 ambazo ni wastani wa Sh. bilioni 4.566.
Kiasi hicho kinaamanisha kwamba, kila mwaka Tanesco hulipa kampuni hiyo Sh. bilioni 54.792 na mpaka Desemba, 2014 walipopunguza uzalishaji kutoka megawati 100 mpaka 50, walikuwa wamelipwa wastani wa Sh. bilioni 164.376.
Kuanzia muda huo ambao walianza kuzalisha megawati 50 mpaka mkataba wao utakavyofika kikomo mwishoni mwa Machi, mwaka huu, watakuwa wamelipwa Sh. bilioni 68.49 na kufanya kwa muda waliokaa Tanzania kuvuna Sh. bilioni 232.866.
Kwa upande wa Symbion Arusha ambao taarifa hiyo ya serikali inaonyesha kwamba walikuwa wakiuzia Tanesco uniti moja ya umeme kwa Dola za Marekani senti 44.4, kila mwezi walikuwa wakilipwa Capacity Charge ya Dola za Marekani 1,866,760 ambazo ni wastani wa Sh. bilioni 4.088 kwa mwezi.
Fedha hizo ni wastani wa Sh. bilioni 49.056 kwa mwaka na hivyo tangu 2012 mpaka 2014, mkataba wao ulivyoisha walikuwa wamelipwa wastani wa Sh. bilioni 147.168.
Symbion Dodoma ambao wanauzia umeme Tanesco kwa senti za Marekani 42.4 kwa uniti, walikuwa wakilipwa Capacity Charge ya dola za Marekani Dola 2,252,145 kila mwezi ambazo ni wastani wa Sh. bilioni 4.932.
Kutokana na hali hiyo, kwa mwaka walikuwa wakilipwa Sh. 59.184 na kwa miaka mitatu waliyokaa walikusanya Sh. bilioni 177.552.
Symbion Dar es Salaam, ambao wanauzia Tanesco uniti moja kwa senti za Marekani 3.2 , wanalipwa kila mwezi Dola za Marekani 2,694,600 sawa na wastani wa Sh. bilioni 5.901.
Kutokana na hesabu hizo, kwa mwaka wanalipwa Sh. bilioni 70.812 na kwa miaka mitatu walikuwa wamelipwa Sh. bilioni 212.436.
Kwa upande wa Songas ambao taarifa hiyo ya serikali inaonyesha kuwa wanauzia umeme Tanesco kwa senti za 2.4 za Marekani kwa uniti, wanalipwa Capacity Charge ya Dola za Marekani 5,209,911.94 kwa mwezi ambazo ni sawa na wastani wa Sh. bilioni 11.410.
Kulingana na hesabu hizo, kila mwaka kampuni hiyo inalipwa Sh. 136.92 tangu 2001 walivyoingia mkataba na Tanesco.
Kwa kipindi hicho cha miaka 15, kampuni hiyo imelipwa wastani Sh. trilioni 2.053.
TANESCO WANENA
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Tanesco Mhandisi Mramba, alisema: “Kwa sasa hivi tumebaki na mkataba mmoja tu wa Aggreko ambaye awali alikuwa akizalisha megawati 100 tukapunguza ikabaki megawati 50.
AGGREKO TULIANZA NAO 2012
“Mkataba wake (Aggreko) unaisha mwisho wa mwezi huu, kwa maagizo ya Rais utakapoisha huo hatutauendeleza, IPTL siyo wa uzalishaji wa dharura kwa hiyo ni tofauti na hao wengine, ile dharura ndiyo tumeshamalizana nayo na hatutaendeleza,” alisema Mramba.
Alisema tangu Desemba, 2014 walipunguza uzalishaji wa umeme wa Aggreko kutoka megawati 100 mpaka 50 hali iliyofanya pia capacity charge ipungue kwa karibu nusu.
Kuhusu mkataba wa IPTL, alisema utaisha mwaka 2022 na kwamba, pia hawataingia mkataba mpya.
Kuhusu Songas alisema: “Hatuwezi kuachana nao, hii ni ya kudumu.”
Kwa upande wa ile ua Symbion, alisema: “Tulishaachana nayo 2014, Dodoma na Arusha iliisha Juni, 2014 na Dar es Salaam iliisha Septemba, 2014 tangu 2012, tulipoanza nao.”
SOURCE: NIPASHE