Rooney afungiwa mechi mbili Send to a friend Tuesday, 05 April 2011 20:01
LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa Manchester United, Wayne Rooney amefungiwa kucheza mechi mbili za Ligi Kuu ya England baada ya kushangilia bao kwa kutukana katika kamera za televisheni zilizokuwa zikirekodi pambano hilo.
Rooney ambaye ni mshambuliaji wa kimataifa wa England baada ya kufunga penati ambalo lilikuwa ni bao lake la tatu katika mechi alizifuata kamera zilizokuwa zikirekodi pambano hilo na kutukana mbele ya kamera hizo.
Katika mechi hiyo Manchester United iliichapa West Ham mabao 4-0.
Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka la England FA ilisema," FA leo imemfungia mchezaji wa Manchester United, Wayne Rooney kwa sababu ya kutukana."
Kama Rooney akikubali tuhuma hizo atafungiwa kucheza mechi mbili ambazo ni dhidi ya Fulham ambayo ni mechi ya Ligi Kuu ya England na ile ya nusu fainali ya kombe la FA dhidi ya Manchester City iliyopangwa kufanyika Aprili 16.
Kama Rooney akipinga tuhuma hizo, kesi yake hiyo itasikilizwa na tume maalum ya FA ambayo inaweza kutoa adhabu kubwa.
Hata hivyo baada ya mechi hiyo ya Manchester united dhidi ya West Ham Kumalizika, Rooney alisikitikia kitendo chake cha aina ya ushangiliaji aliouonyesha na pia televisheni ya Sky Sports iliyoonyesha mechi hiyo iliwaomba msamaha watazamaji wake kwa kitendo hicho kilichoonyeshwa na Rooney.
Rooney ambaye ni mchezaji bora wa mwaka wa England msimu uliopita amekuwa na wakati mgumu msimu huu kwa sababu ya matatizo yake binafsi, kuwa majeruhi na kiwango chake kupungua.
Lakini katika wiki za hivi karibuni aameanza kuonyesha kiwango kizuri huku akifunga mabao tisa katika mashindano yote aliyocheza tangu mwezi Februari.