Simba vs. Mazembe leo: Ni tambo tupu
• TP: Tumekuja na kikosi cha maangamizi
na Dina Ismail
WAKATI leo zinashuka kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam kukwaana katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, timu za Simba na TP Mazembe kila moja imejitapa kutoka kifua mbele.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana, viongozi wa timu hizo, kila mmoja aliahidi timu yake kuibuka na ushindi katika mechi ya leo.
Kocha Mkuu wa Simba, Mzambia Patrick Phiri, alisema kwamba amekiandaa vema kikosi chake na hasa kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika mechi ya awali, hivyo ana uhakika watatoka kifua mbele.
Alisema, anajisikia fahari kucheza na vinara wa soka mara mbili mfululizo barani Afrika, lakini hilo haliwatii hofu wachezaji wake kucheza vema na hatimaye kushinda mechi hiyo.
"Mazembe ni kama walimu wa soka Afrika, wamekuja kutufunza soka...lakini hiyo si sababu ya kutufanya tupoteze mechi yetu, naamini tutashinda na kuweka historia," alisema Phiri.
Kocha huyo aliongeza kuwa wachezaji wake wako katika hali nzuri ya mchezo huo, ambao kwa namna moja au nyingine ni lazima washinde ili kusonga mbele.
Naye Meneja wa TP Mazembe, Tzediric Kitenge alisema kuwa wamekuja na kikosi cha maangamizi, hivyo ni lazima waibuke na ushindi.
Alisema bao pekee walilolipata Simba katika mechi yao ya awali iliyochezwa katika Jiji la Lubumbashi si kigezo kuwa wataweza kuwafunga mabao zaidi na kuwatoa katika michuano hiyo.
Katika hatua nyingine, Kitenge alikana tuhuma dhidi ya timu yao kudaiwa kutaka kutoa rushwa kwa waamuzi katika mechi yao ya awali na Simba na kudai kuwa zina lengo la kuwaharibia.
"Kama kuna kitu hicho, mtu aje na kuthibitisha, timu yetu ni nzuri na imewahi kuzifunga mabao mengi timu kubwa ikiwemo Esperance (Tunisia), na nyinginezo, hiyo ni katika kupakana matope," alisema.
Naye mshambuliaji wa Simba, Mussa Hassan Mgosi, alisema wako vizuri kimchezo na leo lazima historia ya mwaka 2003 ijirudie.
Ili kusonga mbele, Simba inahitaji kushinda mabao 2-0, kwani katika mechi ya awali ugenini walilala 3-1.
Iwapo Simba itashinda mechi ya leo, itaweka historia ya mwaka 2003 walipoivua ubingwa Zamalek ya Misri.