Botswana yafuzu, Kenya, Uganda, Sauzi, Senegal safi Send to a friend Sunday, 27 March 2011 21:21
JO'BURG, Afrika Kusini
BOTSWANA imefuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali za Mataifa ya Afrika huku vigogo Afrika Kusini na Senegal nazo zimejiweka kwenye mazingira mazuri ya kuungana naye.
Jerome Ramatlhakwane, ambaye hana namba ya kudumu kwenye kikosi chake cha Vasco da Gama inayoshiriki Ligi Kuuu ya Afrika Kusini, alifunga bao la mapema mwanzoni mwa kipindi cha pili na kuipa Botswana ushindi mzuri wa bao1-0 dhidi ya Chad.
Pamoja na Pundamilia hao wanaotoka nchi yenye utajiri wa almasi na ikiwa na watu milioni mbili wanaweza kupoteza kiti cha uongozi wa Kundi K, lakini wamejihakikishia kufuzu kati ya timu mbili za juu na kuelekea Gabon na Equatorial Guinea.
Mshambuliaji Ramatlhakwane alifunga bao hilo dakika ya 50, nyota huyo amefunga mabao matano kati ya saba yaliyowafanya kufikisha pointi16 katika mechi sita waliwazocheza, pamoja na ule wa ushindi wa nyumbani na ugenini dhidi ya mabingwa wa Afrika wa mwaka 2004, Tunisia.
Mabao yote aliyoyafunga yaliamua mechi na shujaa mwingine ni kocha Stanley Tshosane, ambaye amekuwa na mafanikio makubwa tangu alipotua Botswana.
Botswana haijawa kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika tangu yalipoanzishwa mwaka 1957.
Mchezaji Moses Chavula alifunga bao kwa mpira wa adhabu dakika ya 18 na kuipa ushindi Malawi 1-0 nyumbani dhidi ya Togo na sasa wanasubili mchezo wao dhidi ya Tunisia jijini Blantyre mechi itakayoamua nani ataungana na Botswana.
Uzuni ilibadilika kuwa furaha dakika za mwishoni wakati Katlego Mphela na Demba Ba walipofunga mabao ya ushindi na kuzipa pointi tatu muhimu kwa Afrika Kusini na Senegal na kuwaweka matatani mabingwa wa zamani Misri na Cameroon.
Misri iliyotwaa ubingwa wa Afrika mara tatu mfululizo na kuweka rekodi ya kutwaa taji hilo mara saba, walitegeneza nafasi nyingi za kufunga kabla ya Mphela kufunga bao la ushindi zikiwa zimebaki dakika tatu mpira kumalizika na kuamsha shangwe jijini Johannesburg.
Senegal iliyofunga mabao 11, katika mechi mbili zilizopita, lakini walijikuta kwenye wakati mgumu mbele ya Cameroon na kuwalazimu wasubili hadi dakika ya 92, wakati mshambuliaji wa West Ham, Ba alipoamsha cheleko jijini Dakar.
Matokeo hayo yanaifanya Misri kuwa nyuma kwa pointi sita kwa Afrika Kusini katika Kundi G, nao mabingwa mara nne Cameroon wamebaki nyuma kwa pointi tano kwa vinara Senegal katika Kundi E zikiwa zimebaki mechi tatu kumalizika kwa mzunguko huo.
Uganda, ambayo haijafuzu kwa fainali za Afrika tangu ilipotinga fainali na kukosa ubingwa mbele ya Ghana miaka 33 iliyopita, inaonekana ipo kwenye kiwango chini ya kocha wao Mscotland, Bobby Williamson na shujaa wao David Obua kutoka kwa Edinburgh club Hearts.
Mshambuliaji huyo mrefu alifunga bao katika kipindi cha kwanza nchini Guinea Bissau na kuipa Uganda ushindi wa bao 1-0 na kuendelea kuongoza kwa pointi saba, tatu zaidi ya Kenya, na mechi zake mbili zilizobakia kati ya tatu atacheza jijini Kampala.
Kenya iliamka na kuichapa Angola 2-1 jijini Nairobi japokuwa mfungaji wa bao la ushindi kiungo wa Inter Milan, Macdonald Mariga alipokea kadi mbili za njano hivyo hatazikosa mechi ya marudiano hapo mwezi Juni.
Miamba mingine ya Afrika Mashariki, Tanzania walitumia vizuri uwanja wake wa nyumbani shukrani kwa bao la kichwa la Mbwana Samata akiunganisha kona dakika za majeruhi kuipa Taifa Stars ushindi wa mabao 2-1dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati katika Kundi D.