Mabondia waliogoma watoswa timu ya taifa
• Yumo Nahodha Joseph Martin, Nasser Mafuru
na Samia Mussa
KATIKA kile kinachoonekana Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), kuwashughulikia mabondia wa timu ya taifa walioshiriki mgomo wa mashindano ya Mabingwa wa Mabingwa Ukanda wa Afrika Mashariki mwishoni mwa mwaka jana, limetangaza kikosi kipya huku mabondia mahiri na wa siku nyingi wakitemwa.
Katika tukio ambalo liliacha historia chafu katika medani ya michezo hapa nchini, ni pale mabondia hao chini ya Nahodha wao Joseph Martin, waligomea mashindano hayo ya mabingwa wa mabingwa yaliyokuwa yanafanyika ukumbi wa DDC Mlimani Park, Mwenge jijini Dar es Salaam huku wao wakiwa wenyeji kwa madai ya kunyimwa kifungua kinywa huku timu ngeni kutoka Uganda, Kenya na Mauritius zenyewe zikipata huduma hizo.
Akitangaza jijini Dar es Salaam jana, kikosi hicho kipya cha taifa ambacho kinatarajiwa kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwamo ya majiji huko Kampala, Uganda na All Africa Games, Maputo Msumbiji, Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga, alisema uteuzi huo umezingatia mambo mengi, likiwamo suala la umri, kiwango kizuri alichokionyesha bondia katika mashindano ya taifa na nidhamu, ambapo kamati ya utendaji ya BFT, imepitia majina ya mabondia wote na kujiridhisha kuwa wanastahili kuitwa timu ya taifa ambayo itakuwa chini ya kocha mkuu, Mcuba Hurtado Primenter.
"Tunawaomba mabondia ambao nitawatangaza muda mchache ujao, watangulize uzalendo pamoja na nidhamu wanapokuwa katika na wanapochaguliwa kushiriki mashindano ya kimataifa," alisema Mashaga, kauli inayoonyesha wazi kukemea tukio lililofanywa na mabondia wa timu ya taifa mwaka jana la kugomea mashindano na kuitia aibu nchi kimataifa.
Alisema, pamoja na kutangaza kikosi hicho, hadi hivi sasa hakuna vifaa vinavyoweza kutumiwa na mabondia wala fedha za kuiweka kambini, lakini uongozi wa BFT, bado unaendelea kufanya jitihada ili kikosi hicho kiweze kuingia kambini haraka iwezekanavyo.
Katika kikosi hicho kipya, mabondi wa muda mrefu katika timu ya taifa akiwamo nahodha, Joseph Martin wa JKT, Leonard Machichi wa Ngome, Nasser Mafuru wa Magereza na wengineo wametemwa.
Mashaga alitaja majina ya wanaounda kikosi hicho kipya kuwa ni John Christian (Kinondoni), Yahaya Maliki (Polisi), Dogo Mussa (Ilala), Abdallah Kassim, Boniface Mlingwa, Omary Mrisho (Ngome), Nassoro Ally, Ismail Isack (Pwani), Godfrey Timothy (Morogoro) na Wambura Amiry (Temeke).
Wengine ni Bosco Bakari (Mwanza), Elius Nkome (Rukwa), Idd Pialali (Kinondoni), Victor Njaiti (Magereza), Godfrey James Ngome), na Museven Gasper (Polisi).
Pia wamo Mohamed Chimbulimbuli (Polisi), Method Choga (Pwani), Suleimani Kidunda (Ngome), Abdallah Rashid, Abdallah Shabani (Kinondoni), Juma Ally, Juma Farahani (Tabora), Issa Kimanga (Ruvuma), Shabani Yusuph (Temeke), Amosi Godwin (Magereza), na Maxmilian Patrick (JKT).
Mashaga alisema kuwa kocha mkuu wa timu hiyo atakuwa Mcuba, Hurtado akisaidiwa na kocha mkuu mzawa, Benjamin Mwangata, Makoye Isangula na Edward Emmanuel, kutoka Klabu ya Sifa, huku aliyekuwa kocha msaidizi, Remmy Ngabo akiachwa.
Wakati huo huo, kamati ya utendaji ya BFT, imempa adhabu bondia Renatus Mpandangazi wa Polisi, kutocheza mashindano mawili yanayoandaliwa na BFT, baada ya kuomba radhi kwa barua na kukiri kosa ili asamehewe, baada ya kuonyesha utovu wa nidhamu wakati wa mashindano ya taifa.
Aliongeza kuwa BFT inaendelea kupitia taarifa za baadhi ya mabondia na makocha ambao walionyesha utovu wa nidhamu katika mashindano hayo, ili kujiridhisha kama wanastahili kuadhibiwa, ambapo uchunguzi ukikamilika, watatoa taarifa.