0digg
Ramadhan Semtawa
KATIKA hali ambayo si ya kawaida, Zainab Kaswaka aliyekuwa anasafiri kwa ndege kutoka jijini Dar es Salaam kwenda London, amekutwa na bastola kwenye ndege ya Shirika la Emirates na kuzua tafrani kubwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Viwanja vya Ndege nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ulrich Matei, zimeeleza kuwa tukio hilo lilisababisha ndege hiyo iliyokuwa tayari imeanza kuruka, kutua tena kwa ajili ya kuitoa bastola hiyo na kuikabidhi kwa walinzi uwanjani hapo kabla ya kuendelea na safari.
Kwa mujibu wa habari hizo, tukio hilo ambalo limekuwa likiumiza vichwa vigogo wa usalama wa viwanja vya ndege nchini, limetokea Desemba 2 saa 11:45 na tayari Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Insepekta Jenerali (IGP) Said Mwema ametaka maelezo ya tukio hilo.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na Mwananchi umebaini kwamba, Kaswaka alipanda na kukutwa na bastola hiyo aina ya Bareta yenye namba BAA197059 ikiwa na risasi nne na magazini moja ambayo alilazimika kuikabidhi kwa wahudumu wa ndege hiyo.
Abiria huyo alikuwa na hati ya kusafiria namba AB00828, alipita na kukaguliwa katika mashine mbili za usalama (X-ray machines), lakini walinzi hao ambao wanatajwa walichukuliwa kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kikosi cha Anga Ukonga (Air wing), hawakuweza kubaini kama katika mizigo ya abiria huyo kulikuwa na pochi yenye bastola hiyo.
Sehemu ya uchunguzi huo ilibaini zaidi kwamba, wakati abiria huyo akiwa tayari amekwishapanda ndege hiyo, ndipo mumewe alimwarifu kwa simu kuwa ndani ya mkoba wake mdogo uliokuwa katika begi kubwa, mlikuwa na bastola.
Mwananchi ilibaini zaidi kwamba baada ya kuarifiwa bastola hiyo ingemsumbua mbele ya safari, abiria huyo aliangalia mfuko huo na kuikuta, kisha kuikabidhi kwa mmoja wa wahudumu wa ndege ambaye naye aliikabdihi kwa rubani.
"Baada ya rubani kukabidhiwa bastola hiyo, alifanya mawasiliano na mamlaka za usalama uwanjani kisha akageuza ndege hiyo hadi uwanjani hapo, takribani dakika kumi tangu ilipoanza kuruka kuelekea nchini Dubai,"alisema.
Hata hivyo, uchunguzi huo ulibaini kuwa badala ya abiria huyo kuwekwa chini ya ulinzi kwa ajili ya kuchukuliwa maelezo maalumu, aliruhusiwa kuendelea na safari hiyo na sasa anasubiriwa arejee nchini ndipo atoe maelezo.
Kufuatia tukio hilo la abiria kupenya na bastola, tayari kumeibuka mvutano miongoni mwa mamlaka za usalama uwanjani hapo huku polisi wakianza kutuhumiwa kwa kushindwa kumpekua abiria huyo na kubaini bastola hiyo.
Lakini, polisi nao wamekuwa wakirusha mpira huo kwa walinzi waliokuwa wakifanya ukaguzi kwa kutumia mashine hizo maalumu za kubaini mizigo isiyostahili kupita na abiria kuingia nayo ndani ya ndege.
IGP awaka
Vyanzo vilivyo karibu na IGP Mwema, vimesema tayari mkuu huyo wa jeshi la polisi lenye ametaka maelezo ya tukio hilo kutoka kwa Kamanda wa Viwanja vya Ndege Nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ulrich Matei.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo karibu na IGP, tukio hilo limemstua na kuacha maswali mengi kutokana na kwamba kama abiria huyo angekuwa ni mhalifu angeweza kuitumia bastola hiyo kufanya mauaji na hata kujeruhi watu ndani ya ndege.Hata hivyo, IGP Mwema alilishauri gazeti hili limwulize msemaji wa jeshi hilo, Adivera Senso ambaye baada ya kuulizwa, naye akataka kamanda Matei.
Kauli ya kamanda Matei
Kamanda wa Viwanja vya Ndege Nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ulrich Matei alithibitisha tukio hilo na kusema tayari hatua kadhaa zimechukuliwa kwa watu waliokuwa kwenye mashine hizo za ukaguzi.
Kwa mujibu wa kamanda Matei, wanajeshi wote waliokuwapo zamu kwenye mashine hizo siku ya tukio, wamerejeshwa kambini kwa ajili ya hatua zaidi za kinidhamu.
Kamanda Matei alisema, baada ya tukio hilo na ndege kurejea tena uwanjani hapo, vyombo vya ulinzi na usalama vikiwamo polisi na usalama wa taifa, walikutana na kujadili hilo ikiwamo kuangalia picha za abiria walivyokuwa wakipita kwenye mashine hizo.
Alifafanua kwamba baada ya kuangalia picha hizo, ilibainika tukio zima lilitawaliwa na uzembe kwa walinzi hao kutoka JWTZ ambao walikuwa katika mashine hizo, kwani hawakuwa makini kuona namna abiria huyo alivyokuwa akipita na bastola iliyokuwa katika pochi hiyo.
Matei ambaye alifafanua tukio zima kwa uwazi, alisema ndege hiyo ilipaa katika njia maalumu iitwayo 'runway five' na kuongeza kwamba hadi sasa tayari kumechukuliwa hatua mbalimbali za maboresho ya udhibiti wa mfumo wa ukaguzi na usalama unaofahamika kama 'quality control.'
Kwa mujibu wa Kamanda Matei, baada ya tukio hilo, pia wameamua walinzi wanaofanya ukaguzi kwenye mashine hizo, wasiwe na simu za mkononi kwani imebainika kuwa simu ni moja ya sababu zinazowafanya kukosa umakini katika kazi uwajibikaji wao.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu hatma ya abiria huyo, alisema imebainika hakuwa na kosa lolote kwani alipita tu na bastola yake pasipokufahamu wala hakuwa na nia mbaya. Silaha hiyo inashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege.
Kamanda Matei alieleza kuwa abiria huyo ni mkazi wa jiji la Dar es Salaam eneo la Jangwani Mtaa wa Swahili na alikuwa akisafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea London, kwa shughuli zake binafsi. |