Miaka 41 ya CCM na dhana ya siasa ni "Uongo"

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,899
Rai kwa wasomaji: Tujadili hoja na si kutukana.
-----------------------------------
KATIKA dunia ya leo kuna mitazamo kinzani juu ya siasa, Kuna baadhi ya watu ambao, kwao siasa inatafsiriwa kuwa ni uongo unaotumiwa na kundi dogo la watu wenye nia chafu ya kutaka kutumia madaraka kujinufaisha binafsi. Mtazamo mwingine ni ule wa wale wanaoamini kuwa SIASA ni Uongozi mwema.

Tunapojenga uongozi wa kifisadi bila Shaka unawavutia sana watu wenye tamaa ya mali kuingia katika siasa ili wakaibe na kupewa rushwa kuanzia ngazi mbalimbali hususan ya mtaa hadi taifa. Ndiyo sura halisi ya siasa nchini. Kupitia nadharia hii wengi ndipo wanakuja na usemi wa siasa imekuwa “sihasa.”

Nchi ikikosa viongozi makini, wabunifu, waaminifu, waadilifu na wazalendo wa kweli, maana yake ni kwamba Uongozi mbaya umetengeneza ombwe la uongozi na kuwa kikwazo kikuu cha maendeleo ya taifa.

Maneno “siasa na uongozi” naweza kuyatumia kama ni yenye maana sawa kwa maudhui ya andiko hili. Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alipohutubia kilele cha maadhimisho ya miaka kumi ya CCM na miaka 20 ya Azimio la Arusha mwaka 1987. Alitamka maneno yafuatayo, akizungumzia dhana ya uongozi, Mwalimu Nyerere alisema, “Uongozi ni Kuonyesha Njia.”

Kwa maana hiyo, viongozi sharti wafahamu vema matokeo ya uongozi wao. Wasome imani za wanaowaongoza na nyakati zilizopo ili kutambua matumaini ya umma kimaisha. Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli ameshatamka kuirudisha CCM Katika misingi yake kama ilivyokuwa kwa waasisi wake. Kiongozi huyu anaamini kuwa CCM itaweza kujitakasa, itaweza kuwa Chama cha Wakulima na Wafanyakazi, Chama cha Wanyonge! Lakini nayaona haya yanaongelewa mdomoni huku utekelezaji wake ukiwa wa kiini macho.

Binafsi, naliona hili ni jambo jema kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli kuona kuwa umri wa CCM sasa umeondoka kwenye "Ujana" unaingia kwenye "Utu-Uzima" Kwa Mujibu wa Sera ya Vijana ya Taifa, kwa nchi yetu Kijana ukomo wake ni miaka 35. CCM inatimiza miaka 41 hapo Februari 5 , 2018! CCM si Kijana tena,Huu ni umri wa Urais kwa Mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bila shaka inahitajika busara mpya kwa CCM. Changamoto iliyopo ni kwa Mwenyekiti wake Rais John Pombe Magufuli ni kwa Jinsi gani DOZI atakayoipatia CCM itakifanya Chama hicho kiondokane na busara ya kitoto kwa sababu sasa ujana umeisha!! Bado kuna pahala napaona JPM anayumba na hasa kushughulikia rushwa ya makundi, kuna double standards, bado hapaswi kufifisha demokrasia kwa kuzuia mikutano ya siasa, hii ni hofu isiyo na faida.

Ni vema Rais Magufuli angetimiza dhamira yake ya kuisuka upya CCM ambayo kwa muda mwingi ilishaanza kama si kupoteza kabisa mvuto machoni pa watu wengi bali pia kuwekwa katika moja ya vyama vyenye kutojali kabisa misingi yake kwa kuacha mifumo ya kisiasa iwe huru na ifanye kazi yake bila kuingiliwa.

Kila mtu anajua kuwa, Siasa haikamiliki bila itikadi. Kama viongozi hawaijui siasa na itikadi ya chama chao na ile ya taifa lao, labda kwa makusudi au kwa kutojua na hasa kwa sababu ya kulinda maslahi binafsi, wajue wanalipeleka ovyo taifa.

Viongozi wa namna hiyo wajue wanalirudisha nyuma taifa ambalo limetarajia watu wake wafaidi matunda ya maendeleo kuliko kushuhudia maendeleo ya vitu. Hii ndiyo ilikuwa imani ya Mwalimu Nyerere.

Lakini adui mkubwa wa Siasa ni Uongo na uzandiki vinapofanywa kuwa ndio siasa na itikadi, kila kitu kinachohusu maendeleo ya watu kinakufa. Hakutakuwa na tiba bora, elimu bora, maji safi na salama, tija katika uzalishaji wala ajira.

Badala yake, katika safari isiyo na mwelekeo wa kujenga taifa, watu watabaini umaskini, ujinga naw maradhi, maadui wakuu wa binadamu, vikishamiri.Hayo ndio matokeo ya uongozi ulioshindwa kutambua umuhimu wa kutumia raslimali watu kuwaendeleza watu – wananchi.

Kitu kibaya tunachokibaini na kukiona hapa ni kwamba taifa limekosa viongozi wanaojali kuwa watu wana haki ya kupata chakula bora, mavazi bora, malazi bora – maisha bora kwa jumla. Watazalishaje mali wakiwa dhaifu? Na cha zaidi ni jamii pia kutotambua kuwa si jukumu la serikali tu au chama kinachotawala kufanya kila jambo bila wao (wananchi) kuwajibika ipasavyo kwa kila shughuli halali iwaleteayo kipato.

Nao “wanasihasa” wanapoulizwa kulikoni, hutoa majibu yaliyojaa kiburi. Utasikia, “vijana warudi vijijini wakajiajiri, wale nyasi, wavivu wa kufikiri, shauri yao hawapendi shule au wanadharau kazi”.Ni majibu yanayovunja moyo wananchi. Wanajisikia vibaya kwamba hawathaminiwi. Kwa upande mwingine, huu ni ukweli mchungu. Lazima mizani iweze "kubalansi" Wananchi kama nilivyosema hapo juu ni lazima wawajibike.

Hata hivyo, yawapasa viongozi watambue kuwa siasa njema hutatua matatizo na shida za wananchi zikiwemo zinazokwamisha maendeleo ya uchumi wa nchi na wa familia mojamoja. Siasa mbaya huangusha huduma za jamii.

Kwa kuwa siasa ni uongozi, basi viongozi lazima waongoze kiadilifu, kizalendo na kwa kuzingatia hali halisi ya mambo. Wanapaswa pia kuwa wenye huruma na imani kwa wananchi. Kazi ya wanasiasa na hasa Afrika ni kuongoza harakati za kukomboa watu kutoka kwenye makucha ya unyonyaji, umasikini na ukoloni mamboleo.

Madhila hayo hayajaondoka Tanzania. Lazima yaondolewe ili kuwapa matumaini wananchi. Kumbe siasa ya nchi haitakiwi kuwa iliyolala au inayojengwa na kucheza mchiriku na bongo fleva. Na hapa ndipo miaka 41 ya CCM inapaswa kubeba hii kama changamoto yake kuu.Siasa iliyolala hukwamisha maendeleo na huchangia umasikini na udhalilishaji wananchi.

Mwanasiasa yeyote katika nchi masikini kama Tanzania, anapochaguliwa kuongoza popote, ajuwe anabeba jukumu la kubadilisha hali za watu kuwa nzuri. Atumie stadi za uongozi mwema kuonyesha njia.

Tabia ya viongozi kuongoza kwa kufikiria zaidi maslahi binafsi iwe mwiko. Viongozi wa nchi hizi masikini waangalie maisha ya Manabii ambao waliongoza karne za mwanzo za ulimwengu.Manabii hawa, walitumia stadi za uongozi kusimamia haki za waliowaongoza; wanyonge na hata waliokuwa na uwezo. Walitumwa na utashi na imani ya kutumikia Mwenyezi Mungu aliyewaumba.Walijua kuwa kupewa uongozi ni kuchukua ahadi ya kutenda kwa haki.

Lakini wanaoifanya kazi ya siasa kwa kuigeuza ni pango la wizi, rushwa, uonevu, unyonyaji na hata kuua raia, wajiandae kupokea adhabu ya muumba. Yeye anaona kila tendo linalotendwa na viumbe wake wakati wote.

Tunajifunza kutoka kwa wanafalsafa wa Kiyunani – Plato na Aristotle pamoja na upungufu wake, ni mwongozo wa kisiasa katika nchi zinazoongozwa kwa misingi ya kidemokrasia. Wanafalsafa hawa wanasisitiza siasa ni msingi bora wa mambo yote.

Wanasisitiza viongozi lazima wawe waadilifu na umma uwe na uwezo wa kuwajibisha viongozi wao wanapotenda kinyume na taratibu na sheria zilizowekwa.

Ni wapi pa kuanzia kufanya mabadiliko ya kisiasa na kuwaondoa “WANASIHASA”? Ni watu wenyewe. Muhimu waamke na kutambua wajibu wao katika kuwaweka viongozi wao kwenye mstari ulionyooka.

Mwalimu Nyerere aliandika miongozo mizuri katika Azimio la Arusha akisema kwamba ili tuendelee tunahitaji mambo matatu: Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora. Alitambua mchango wa mambo hayo katika maendeleo ya mwanadamu.

Kupitia siasa safi kila kitu cha kunufaisha wananchi hupatikana. Bali ni muhimu viongozi wanaotarajiwa kufanikisha ustawi wa wanadamu, wapatikane kwa njia ya haki. Watokane na ridhaa ya watu wenyewe wanaotaka kuongozwa.

Hata kwenye vyama vya siasa au vikundi vingine vya kiraia, viongozi lazima wapatikane kwa njia ya haki siyo vurugu na upindishaji wa sheria na taratibu.

Kuhakikisha hayo yanatokea, zile taasisi za kidola zilizokabidhiwa wajibu wa kuchunga nidhamu ya mambo – kama vile vikosi vya ulinzi na usalama, vyombo vya uchunguzi na mahakama, zapasa kutenda kwa dhamira ya kujenga taifa.

Utamaduni wa ubabaishaji na ubaguzi mbele ya sheria usipewe nafasi maana taasisi hizi zina jukumu zito na muhimu la kusimamia haki kutendeka.

Taasisi hizi zikiendesha mambo kwa chuki na ubaguzi unaoelekea kuhifadhi maslahi ya viongozi tu, zitambuwe zenyewe zitakuwa zimetengeneza mazingira ya kuleta vurugu na kuhatarisha utulivu katika nchi.

Uongozi ukishajua unalindwa na taasisi hizi, unazidi kujisahau na kujinufaisha binafsi huku wakibeza haki za raia.

Hapo raia watakuwa wamefikishwa pabaya. Watakataa kustahamili maudhi ya viongozi wao kwa kujua kuwa kuwaendekeza, ni kujimaliza wenyewe na nchi yao. Watachagua kubaki na nchi yao viongozi waondoke.

Je, dhamira ya RAIS Magufuli ya Kuitakasa CCM itafanikiwa? Bado naona kuna ombwe kubwa ndani ya Chama cha Mapinduzi, Bado rushwa na ufisadi umekuwa mfumo wa maisha ya uongozi ndani ya CCM, bado Kansa aliyoiongelea Mwalimu Nyerere kuwa CCM haiwezi kupona inaendelea kuitafuna, Bado ile Pumzi kuisha aliyoiongelea Kingunge and Ngombale Mwiru inazidi kuisha kabisa, Bado ile kauli ya Horace Kolimba ya " CCM imepoteza dira" inaishi hadi leo. Mungu awapumzishe kwa amani Magwiji hawa!

Je, tunahitaji kumuombea Rais na Mwenyekiti wa CCM John Pombe Magufuli?!

Nawatakia maadhimisho mema ya miaka 41 ya Chama chenu, lakini haitoshi kila mara kuwaombea mema ilhali mmefunika Mask kwenye SURA na UBONGO wenu, hamtaki kubadilika, wakati fulani tutachoka itabidi tuwaombee mabaya ili mpumzike muwe chama cha upinzani!

Tutafakari kwa hoja kwa pamoja!
 
Halafu miaka 26 ya vyama vingi upinzani umeshindwa kushawishi watu kuwa wenyewe ndiyo mbadala wa walioshindwa.
 
Back
Top Bottom