MIAKA 34 YA CCM: Itambue Roma ilianguka siku moja

mzambia

JF-Expert Member
Dec 31, 2010
885
60

KABLA sijaanza kuandika makala hii niliyoitafakari kwa kina nilifarijika na jinsi Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilivyohenyeshwa na kubwagwa kwenye baadhi ya majimbo nchini katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.
Nafarijika na kauli za baadhi ya waandamizi wa chama na serikali pamoja na wastaafu wanazozitoa kuwa kuna mpasuko na makundi yanayohasimiana ndani chama hicho ambayo yamefikia katika hatua mbaya ya kukimega.
Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere, aliwahi kusema upinzani wa kweli utatoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi CCM, nami napenda iwe hivyo kwa sababu tumechoshwa na hali ya mambo inavyoendelea hivi sasa ambapo rasilimali za taifa zimefanywa kuwa ni za kundi Fulani.
Kuibuka kwa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kumpinga kauli za baadhi ya viongozi wanaotaka kuilipa Kampuni ya Dowans pamoja na kuiamuru serikali kuivunja bodi ya mikopo ni ishara ya wazi kuwa sasa chama hicho mambo ni hobela hobela.
Kwa muda mrefu tuliiona CCM na jumuiya zake zikiwa na msimamo imara kwenye masuala yanayogusa masilahi ya wananchi lakini hivi sasa ni tofauti kabisa kwani kila mmoja hujiangalia namna atakavyonufaika kama akiliunga mkono kundi Fulani.
Ndoto walizokuwa nazo viongozi wake kwa muda mrefu kuwa chama hicho kitaendelea kutawala milele hivi sasa zinaaanza kuonekana kuota mbawa kwa sababu upinzani umekuwa imara zaidi huku CCM ikiendelea kunyong’onyea licha ya kufanya hila kwenye chaguzi mbalimbali.
Inawezekana walikuwa wakisema hayo kwa kulinganisha na kile walichokiita nguvu iliyonayo chama hicho na udhaifu wa upinzani. Naheshimu misimamo yao, lakini napata picha kwamba wanachama hao walikuwa wanazungumza kitu wasichokijua.
Watu wenye mawazo kuwa CCM itatawala milele, naweza kuwafananisha na ‘watoto’ wasio na upeo mkubwa wa kufikiri ambao wakikua watang’amua hicho wanachokisema au kukifikiri si sahihi bali walikuwa wakifuata historia au kuzungumza maneno matamu midomoni.
Wanakariri vibwagizo vya zamani bila kusoma alama za nyakati, rejea kauli ya Katibu Mkuu wa chama hicho kuwa CCM ni baba na itaendelea kutawala milele na kamwe haitonyimwa na kelele zinazopigwa na wapangaji (wapinzani)?
Naomba leo nitoe mifano michache, wasomi watakumbuka vyema jinsi dola ya Roma ilivyotawala dunia kwa kipindi kirefu kabla ya Kristo na baada (miaka 500). Hata mmoja wa watawala wake, Augustus Caesar, alishiba ujeuri na utukufu wa madaraka akajipachika cheo cha mwana wa mungu!
Niseme wazi leo duniani hakuna dola iliyowika kama ya Roma, ilidumu kwa karne nyingi na iliwahi kutoa hata unabii na utabiri wa kinabii na maandiko matakatifu lakini haikudumu milele, ilifikia mahali dola hiyo kwa jeuri, mbwembwe na ufisadi kama huu wa CCM ilisambaratika na kutoweka.
Ndiyo maana katika makala hii nimeanza kwa kusema Roma ilianguka siku moja itakuwa CCM? Angalia leo Afrika kusini makaburu walivyokuwa wametawala na kuwakandamiza Waafrika weusi na kujiapiza kwamba kamwe mtu mweusi hatajitawala wao wakiwa hai.
Makaburu hao na mashabiki wao walikuwa wakiimba nyimbo kama hizi zinazoimbwa na viongozi, wanachama wa CCM, lakini mwisho wa siku hiyo milele waliyokuwa wakiisema iliwatokea puani kwa kushuhudia Waafrika weusi wakitwaa madaraka chini ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Nelson Mandela
Mei 10,1994 ni siku ambayo makaburu hawatoisahau kwani ndiyo siku aliyoapishwa Mandela, tena baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa kidemokrasia ambao ulikuwa mwanzo na mwisho wa utawala wa makaburu.
Hapo ANC kikakoma kuwa chama cha upinzani, kikawa chama tawala. Makaburu hawakuona tena mbele wala nyuma, ile milele yao ikawa haina maana tena. Yakawa maneno matupu kama haya ya kina Yusufu Makamba, John Chilligati, Tambwe Hiza na wana CCM wengine.
Kifupi ni kwamba hakuna chama kilichopewa dhamana ya kutawala watu milele. Nachopenda kusema ni kwamba CCM inapotimiza miaka 34 inapaswa irejee historia , ijifunze, iache jeuri (kutumia majeshi/dola) kitimize wajibu wake.
Kitambue kwamba kuwa chama tawala leo, hata kama kingekaa madarakani kwa miaka 2000 (elfu mbili) hiyo si milele si leseni wala si sababu ya wao kushindwa kuondolewa madarakani.
Rejea kumbukumbu zinaonyesha miaka ya 1964 kilichokuwa chama cha upinzani cha UNIP chini ya aliyekuwa Rais Kenneth Kaunda kiliwahi kushika madaraka ya Zambia, zamani ikiitwa (Southern Rhodesia) kilikomesha kabisa zilizokuwa tambo (majivuno) ya watawala weupe (makaburu) ambao nao waliapa kumtawala mtu mweusi milele.
Lakini UNIP nayo baada ya kukaa madarakani kwa muda mrefu ikalewa madaraka na kuwapuuza wananchi ambao waliamua kikiadhibu kwa kukiondoa madarakani mwaka 1991 na kukichagua chama cha upinzani cha MMD, chini ya uongozi wa Frederick Chiluba.
Uongozi wa Chiluba ambaye alikuwa mlokole haukuwa wa kilokole kama wananchi walivyoaminishwa, ulitumbukia katika wizi, rushwa, ufisadi wa kupindukia ambao ulipozidi wananchi hawakusita kuonyesha hasira zao.
Rais aliyefuata baada ya Chiluba, alikuwa ni hayati Levy Mwanawasa ambaye alipoingia madarakani alianza kuwachukulia hatua kali wala rushwa na mafisadi wakubwa, akiwemo Chiluba na washirika wenzake waliokuwa wakituhumiwa kujinufaisha wakiwa madarakani.
Mifano ipo mingi sana, Malawi, nao waliwahi kutoa adhabu kwa watawala wao, Kamuzu Banda kiongozi aliyeongoza Malawi kupata uhuru mwaka 1964, naye baada ya kukaa madarakani muda mrefu alilewa madaraka, aliondolewa kwa nguvu ya umma (wananchi) wakiongozwa na Bakili Muluzi mwaka 1964,.
Mvinyo wa madaraka nao ulimkolea Muluzi, na akajikuta akianza kufanya biashara akiwa ikulu huku wananchi wake wakiendelea kulia njaa bila ya yeye kujali, hasira za wananchi kupitia kwa rais aliyechaguliwa baadae Bingu wa Mutharika zikambana Muluzi ambaye inadaiwa alifanya biashara akiwa ikulu.
Mfano mwingine ni mwaka 2002, Wakenya hawakutaka mchezo, walimwondoa madarakani Rais Daniel Arap Moi ambaye alikaa madarakani muda mrefu –miaka 24, waliamua kukitosa chama cha KANU kilichoongoza nchi hiyo tangu uhuru.
Tukumbuke ni Moi huyu huyu kipindi fulani aliwahi kusikika akiwaambia baadhi ya viongozi wetu, tena kwa jeuri kwamba, ‘Haiwezekani na ni fedheha isiyokubalika eti chama tawala kushindwa wakati kikiwa madarakani’, yu wapi leo?
Moi aliwahi kuwatangazia Wakenya, kama ilivyo CCM leo kwamba KANU itatawala milele, lakini milele yake iliota mbawa pale alipokiona chama hicho kikuwa ni cha upinzani licha ya kufanyika kwa hila za kutaka kukibakisha madarakani. KANU kilikuwa ni chama kilichotikisa na kuogopwa kama CCM lakini mwisho wake kilikuwa cha upinzani, somo tunalolipata hapa ni kuwa kumbe nguvu za vyama tawala si yao pekee, bali inasaidiwa na vyombo ya dola ikiwepo polisi, jeshi na vinginevyo
Siku vikinyang’anywa serikali huo ndio mwisho wao, vinakuwa kama samaki uliyemtoa kwenye maji. Namalizia kwa kusema CCM ingeondolewa leo, nchi ikaongozwa na chama chochote cha upinzani kama ilivyo kwa Kenya, Zambia na kwingineko. Watanzania wa leo si wa mwaka 47 wanajua kutofautisha baadhi ya kauli na matendo ya watawala wao, CCM imeadhimisha miaka 34 tangu ilipozaliwa na kama isipobadilika huko tuendako itakuwa chama cha upinzani

SOSI: TZ DAIMA
 
Back
Top Bottom