Miaka 12 Ya Kifo Cha Nyerere: Hata Tumbili Hung'amuka! ( Makala, Raia Mwema)

mkatofa

Member
May 6, 2010
38
7
Na Maggid Mjengwa,KESHO kutwa WaTanzania tutaadhimisha Siku ya Kumbukumbu ya Kifo cha Mwalimu Nyerere. Ni miaka kumi na miwili iliyopita tangu Mwalimu atutoke. Hakika, siku hii sasa imekuwa muhimu kwa sana kwetu Watanzania .Maana, WaTanzania wanazidi kutambua, kuwa Mwalimu Nyerere, pamoja na mapungufu yake ya kibinadamu, katika uhai wake, siku zote alisimama upande wa wanyonge walio wengi. Mwalimu aliitazama zaidi Tanzania kuliko Chama alichokiongoza. Na kuna wakati, kwa maneno yake mwenyewe, Nyerere alitamka; CCM si baba wala mama yangu. Mwalimu alikuwa tayari kuikana CCM lakini si kuikana Tanzania. Mwalimu alidhamiria kuwakomboa Watanzania kifikra ili waondokane na unyonge na umasikini wao. Hakika Nyerere alikuwa kiongozi wa kanuni, kilichokufa ni kiwiliwili, fikra zake ziko hai na atabaki milele katika mioyo ya Watanzania wengi.Naam. Mwalimu aliwataka Watanzania waamke. Na hapa nilipata kusimulia visa viwili vinavyotukumbusha wajibu wetu wa kuamka sasa kutoka usingizi wa pono. Katika kuadhimisha miaka kumi na miwili ya kifo cha Mwalimu, naamini, visa hivi vinapaswa kusimuliwa tena ili viifikie jamii pana. Hapo zamani palipata kutokea bwana aliyefanya biashara ya kuuza kofia. Alizipanga kofia zake kichwani. Alivaa moja na nyingine zikapangana juu yake. Zikawa kama kichuguu. Siku moja wakati akivuka pori akitembeza kofia zake, akajiwa na uchovu. Akaamua kukaa chini ya mti kivulini. Usingizi ukamjia.Alipoamka akashangaa kuona tumbili wametapakaa juu mitini wakiwa wamevaa kofia. Walimwachia kofia moja tu kichwani mwake. Bwana yule akajaribu kutoa ishara zote kuwataka tumbili wale wamrudishie kofia zake. Tumbiri waliigiza ishara zile, lakini hawakwenda kumrudishia kofia zake. Mwishowe bwana yule akajiwa na busara. Akavua kofia yake na kuibwaga chini ardhini. Tumbili nao, wakiwa juu ya miti, wakafanya hivyo hivyo. Wakazibwaga kofia zile chini. Hivyo basi, bwana yule alifanikiwa kuziokota kofia zake zote.Miaka ikapita, bwana yule hakuweza tena kuendelea na biashara ile. Aliaga dunia, lakini kabla hajafa alimrithisha mwanawe ambaye pia alimwadithia kisa kile cha tumbili na kofia. Ikatokea siku moja mwanawe, katika biashara yake ya kuuza kofia, ikamkuta hali kama iliyomtokea marehemu baba yake. Akafanya kama alivyofanya marehemu baba yake. Ilipofika hatua ya yeye kubwaga kofia yake chini ardhini, tumbili wale walizikamata kofia zao kichwani kwa mikono yao. Tumbili wale walihakikisha hazianguki ardhini. Naam. Wakati ulikuwa umebadilika, tumbili walibadilika pia, lakini mtoto wa mwanadamu hakubadilika. Maana, hata tumbili wale nao waliadithiwa na babu zao kisa cha kuhadaiwa na kufanywa wajinga na binadamu. Walijiandaa kutofanya makosa yale yale waliyofanya babu zao. Na hiki hapa ni kisa kingine; palitokea watu watatu. Watu hao walikuwa na ujinga wa kutokujua kusoma na kuandika. Akatokea bwana mmoja akawakabidhi mikungu mitatu ya ndizi.Akawapa pia bahasha yenye barua ndani yake. Akawaagiza; "pelekeni mikungu hiyo ya ndizi nyumbani kwa rafiki yangu". Njiani watu wale wakajisikia njaa kali. Wakautafuna mkungu mzima wa ndizi. Walipofika mwisho wa safari, wakaikabidhi mikungu ya ndizi na barua ile kwa mwenyeji wao. Mwenyeji aliisoma kwanza barua ile, akawashukuru. Kisha akasema; "Naiona mikungu miwili. Je, uko wapi mkungu wa tatu wa ndizi? Watu wale walitahayari. Walishangaa sana, kuwa bwana yule amebaini, kuwa njiani wamekula mkungu mzima wa ndizi! Walirudi nyumbani wakiamini, kuwa bahasha ile waliyopewa ilikuwa na macho. Iliwaona mara ile waliposimama njiani na kula ndizi zile. Ikatokea tena, wanaume wale wakatumwa na bwana yule yule. Waende mji ule ule na kwa rafiki yake yule yule. Wapeleke tena mikungu mitatu ya ndizi. Njiani wakajisikia tena njaa kali. Wakaambizana; tusimame na tuule mkungu mzima wa ndizi. Lakini, tuhakikishe, kuwa mmoja wetu ameichukua bahasha tuliyobeba. Aiweke ardhini, kisha aifukie kidogo na mchanga. Halafu aikalie kwa ******, bahasha isiweze kabisa kuona wakati tunatafuna mkungu wa ndizi! Wakamaliza kuutafuna mkungu wa ndizi. Wakahakikisha wametupa maganda porini. Wakafika kwa mwenyeji wao. Wakakabidhi mikungu miwili ya ndizi na bahasha. Wakashangaa sana, kuwa hata safari hii, mwenyeji wao amewauliza tena ulipo mkungu wa tatu wa ndizi. Wakabaini, kuwa humu duniani kuna maarifa ya kusoma na kuandika. Na hata sasa, miaka kumi na mwili baada ya kifo cha Mwalimu, jamii yetu imo katika vuguvugu la mjadala juu ya kero ya ufisadi. Wananchi wamebaini, kuwa kuna "mikungu yao ya ndizi" inaliwa njiani na watu waliotakiwa kuifikisha kwa wananchi. Wananchi wameanza kuguna na hata kuwazomea mafisadi. Naam, wakati umebadilika.Wananchi sasa wanawahoji viongozi waliowapa dhamana ya kuwatumikia. Wanawatuhumu kwa ufisadi. Wananchi wana haki ya kuhoji na kudadisi. Wana haki ya kupewa majibu ya ufafanuzi, si majibu ya kubezwa. Inahusu rasilmali zao. Inahusu haki zao. Hapa tunauona mgogoro kati ya baadhi ya waliokabidhiwa dhamana na wale wanaowaongoza. Ni hali yenye kufanana kwa kiasi fulani na visa nilivyosimulia hapo juu. Ni kweli, kuwa baadhi ya viongozi na watendaji wetu ni mafisadi wa kutupwa. Kuukana ukweli huo si tu ni kuwadharau wananchi, bali ni kuwatukana. Kero ya kukithiri kwa vitendo vya kifisadi ni tatizo la kitaifa. Linahusu mustakabali wetu kama taifa. Si suala la kambi ya upinzani na chama tawala pekee, linatuhusu sote. Kinachotokea sasa ni dalili za Watanzania kuanza kumuenzi Baba Wa Taifa kwa vitendo. Watanzania wameanza kukemea kwa sauti na bila woga, yale ambayo Baba wa Taifa alikemea wakati wa uhai wake. Watanzania wameanza kuwaandama wale wenye kutafuna mikungu yao ya ndizi mchana wa jua kali huku wakidhani, kuwa Watanzania ni wajinga, ni vipofu wasioona. Tunajua, kuwa maafisadi wachache wamo ndani ya CCM, wamo ndani ya kambi ya upinzani, wamo nje ya vyama vya siasa. Ni wajibu wa Wana-CCM wenye kukitakia mema chama chao na nchi yao , kupambana na mafisadi hao ndani ya chama chao. Ni wajibu wa wanachama wa vyama vya upinzani wenye kuvitakia mema vyama vyao na nchi yao, kupambana na mafisadi ndani ya vyama vyao. Ni wajibu wa hata tulio nje ya siasa za vyama, kushiriki mapambano hayo. Mapambano haya ni ya lazima, maana, tunashuhudia wachache wenye kuhujumu rasilmali za taifa kwa ufisadi wao wanavyoonyesha pia dharau kwa umma. Wanaamini, kuwa fedha zao zitanunua haki mahakamani. Kuwa zitawafunga pia midomo baadhi ya wanahabari. Hata pale inapotokea wakasikia wananchi kwa uwingi wao wanalalamikia jambo, au hata kuwazomea, basi, mafisadi hawa, kama ilivyokuwa kwa watu wale waliotumwa mikungu ya ndizi, nao hushangaa na kujiuliza; hivi wananchi hawa wamejuaje kuwa tunafuna rasilimali zao wakati wenye macho ya kuona na kutetea tumewakalia? Marehemu Bob Marley ni mmoja wa wasanii mahiri waliopata kutokea humu duniani. Msanii huyu alipata kuimba; Unaweza kuwapumbaza watu wachache kwa kipindi fulani, lakini huwezi kuwapumbaza watu wote kwa wakati wote! Nahitimisha.
 
Back
Top Bottom