Mheshimu sana mke wako, usimdharau

Void ab initio

JF-Expert Member
Mar 1, 2015
5,703
5,635
Mr. Nevian alikua bize kuchat katika simu yake, hakuwa akimsikiliza mkewe ambaye alikuwa akimuambia kuwa kapata kazi na kesho yake ndiyo alikuwa anaenda kuripoti. “Ofisini kuna yule Bosi wangu kaondoka, kesho wanaweza kunifanya Mkurugenzi wa fedha maana pale mimi ndiyo pekee nina CPA, kesho ndiyo wanatangaza na kwa kuwa hawakutangaza nafasi za kazi na kufanya usahili ni zamu yangu”.

Nevian aliongea huku akitabasamu, mkewe alimpongeza na kutaka kumuambia kuhusu kazi yake lakini hakutaka kumsikiliza. “Wewe na wewe hiyo kazi kila siku kazi! kazi! Kwani kufua Nepi kumekuchosha kama unaona watoto wamekua wakubwa nikuzalishe mtoto mwingine maana nimechoka na hiyo mipango yako ya kazi kila siku mibarua kuandika hata usahili huitwi…”

Mkewe alinyamaza huku akitetemekwa kwa hasira alitamani aondoke pale lakini alijua angeambulia makofi kama angemuacha mumewe anaongea. “Wewe kaa hapa, mumeo naenda kuwa Bosi nitakuwa bize zaidi kazini unafkiri nani atakaa na watoto humu nyumbani! Hizo kazi zenyewe kwani watakulipa mshahara bei gani?” Aliuliza lakini mkewe hakuwa na jibu. “Hatujaongea kuhusu mshahara bado…”

“Sasa kama hamjaongea kuhusu mshahara unaenda kufanya nini? Hivi unafikiri kazi zilivyo za shida hivi watakupa mshahara gani? Chuo chenyewe umemaliza miaka saba sasa zaidi ya kupangusa watoto mavi huna uzoefu mwingine! Unafikiri ni kazi gani ya maana watakupa! Hebu niondokee huko!!!” Aliongea kwa hasira na kunyanyuka, alimuacha mkewe kaduwaa.

Usiku alimuambia mkewe kumuandalia nguo za kuvaa na asubuhi mapema kabisa alimka na kujiandaa kwenda kazini, hata kunywa chai hakutaka, alimuacha mkewe akiwa kimya ambaye alipanda daladala kwenda kuanza kazi yake mpya. Kazini kila mtu alikuwa akimpongeza Nevian kwani walijua kabisa ndiyo alikuwa anapandishwa cheo, yeye ndiyo pekee alikuwa na CPA na utendaji wake ulikuwa si wakutilia shaka.

Waliitwa kwenye kikao, walikaa kumsubiri Mkurugenzi. Hatimaye aliingia na kuanza kuwasifia kwa juhudi zao za kazi akiwataka kuendelea na moyo huohuo, aliwaambia kuhusu nafasi iliyowazi na kuwaambia ni wakati wakupata Mkurugenzi mpya wa fedha ambaye ataonyesha utofauti na kuleta mawazo mapya katika kampuni.

“Juzi wakati nikiwaza ni wapi nitampata mtu wa kuchukua nafasi hii kwa bahati tu nilikutana na rafiki yangu mmoja, huyu alikuwa mtu muhimu sana wakati tukiwa Chuo, mawazo yake na akili zake nilijua atakuwa mtu mkubwa sana. Wakati tunaongea aliniambia anatafuta kazi na mmi sikuwa na hiyana.

Sikutaka kuipoteza ile nafasi, ilikuwa kama bahati kuwa kuna nafasi hapa ofisini na hata kama isingekuwepo nisingeruhusu akili kama hiyo kupotea mtaani, naomba sasa tusimame tumkaribishe Marry Jackob Massawe, Mkurugenzi mpya wa Fedha na Utawala.”

Mkurugenzi alimaliza kuongea, ukumbi mzima kila mmoja akiwa ameduwaa walisimama, Nevian nikama alipigwa na ganzi, alisimama bila kujijua, alichanganyikiwa zaidi kuona mkewe akiingia mule ndani. Mpaka mkewe anasimama mbele ya ukumbi alikuwa haamini kilichokuwa kimetokea.

“Samahani kwa kuchelewa si unajua usafiri wa Dar…” Mkewe alitania huku akikaa. “Usiwe na wasiwasi Bosi kuanzia sasa utakuwa na Gari yako na dereva wako, sema kwaheri Daladala..” Wote walicheka. Mkurugenzi aliendelea kumsifia, akimuita mchapakazi, mtu ambaye walikuwa wote chuoni na anajua umakini wake utaipeleka Kampuni yake sehemu aliyokuwa anaitaka.

Alimpa nafasi ya kuongea, Marry alianza kwa kuwashukuru, bila kuongea maneno mengi aliwaomba ushirikiano wao na kukaa. Watu walimpigia makofi, kama Mkurugenzi wa Fedha na Utawala alimaanisha kila mfanyakazi alikuwa chini yake hivyo walilazimika kumheshimu wapende wasipende.

Mumewe bado alikuwa haamini kilichotokea, watu walitoka lakini yeye alibaki palepale ukumbini akiwa hajui cha kufanya. Baadaye alitoka na kwenda ofisini kwa Mkurugenzi, alimuambia Mkurugenzi kuwa yule ni mkewe na hawawezi kufanya kazi pamoja, yeye ana uzoefu na hawezi kukubali awe Bosi wake.

Mkurugenzi alitabasamu na kumuambia, sikujua kama ni mkeo, una bahati sana kuoa mwanamke mwenye akili kama yule, alikuwa anatukimbiza sana Darasani, muda mrefu nimemtafuta kufanya kazi naye sijui ulikuwa umemficha wapi ana kipaji kikubwa sana nina uhakika ataihuisha kampuni yetu. Lakini kama huwezi kufanya kazi chini yake basi usijali nakuelewa.

Unaweza kuandika barua ya kuacha kazi ndani ya masaa 24 na kumkabidhi Bosi wako ambaye ni mkeo.” Bosi aliongea kwa kumaanisha, Nevian alinywea na kunyamaza. “Itakuwa shida kufanya kazi na mkeo kama Bosi wako?” Mkurugenzi alimuuliza. “Hapana Mkuu, hapana Bosi, mke wangu ni mtu mzuri tutafanya kazi bila tatizo lolote.” Alimaliza na kutoka huku kanywea kama Kondoo aliyemwagiwa Maji.

***MWISHO

Kuna wanaume wengi huwadharau wake zao na kuona kama vile hawana akili lakini ukichunguza ni kuwa hawajapata tu fursa za kusoma au wamesoma lakini wamechagua familia na si kazi. Mheshimu sana mkeo, wewe kufanya kazi na yeye kubaki nyumbani hakukufanyi kuwa na akili zaidi yake, ni mgawanyo tu wa majukumu.
 
Daaah patamu hapo nahisi huko nyumbani Nyumba ilikuwa ya moto na Mr akawa mdogo km piriton.
 
Hii stori ina mafumbo sana hivi umekusudia kumpiga fumbo Lowassa(mume) na huyo mke ndio Magu na mkurugenzi akiwa Mzee wa Pipa??
 
Back
Top Bottom