Mheshimiwa Spika naomba tena mwongozo wako | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mheshimiwa Spika naomba tena mwongozo wako

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Sep 18, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Sep 18, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,641
  Likes Received: 82,270
  Trophy Points: 280
  Mheshimiwa Spika naomba tena mwongozo wako

  Padri Privatus Karugendo Septemba 17, 2008
  Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

  MHESHIMIWA Spika Samuel Sitta ninasimama tena kwenye jukwaa hili kuomba mwongozo wako. Hata kama sintapata jibu, sintachoka kusimama na kuomba mwongozo wako. Ni haki yangu kikatiba kutoa maoni yangu.

  Mwezi uliopita, niliomba mwongozo wako kuhusu utoro wa waheshimiwa wabunge. Wakati nikiomba mwongozo wako, viti vya wabunge zaidi ya 100 vilikuwa wazi. Na hili halikutokea siku moja ile ya kufungua maonyesho ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam, siku Wizara ya Afrika ya Mashariki ilipowasilisha Bajeti yake, bali karibia siku zote za Bunge la Bajeti, viti vingi bungeni vilikuwa wazi.

  Nilitaka kufahamu kutoka kwako ni kazi ipi ya wabunge wanafanya zaidi ya kukalia viti vyao bungeni na kuwakilisha sauti za majimbo yao. Wanachaguliwa kwenda bungeni, wanachaguliwa kuwakilishi majimbo yao bungeni na Bunge liko Dodoma na wala si Dar es Salaam. Wengi wa wabunge wanaonekana kwenye mitaa ya Jiji la Dar es Salaam wakati Bunge likiendelea kule Dodoma.

  Kuna maoni yanayozagaa mitaani kwamba kati ya vigezo vya kumchagua mbunge, kiwepo cha kumtaka anayegombea awe anaishi jimboni mwake. Kinyume na sasa hivi ambapo wabunge walio wengi wanaishi Dar es Salaam. Wanatoroka vikao vya Bunge kwenda Dar es Salaam, kuagalia familia zao na miradi yao. Wabunge walio wengi wanakwenda kwenda majimbo yao ya uchaguzi wakati wa kampeni za uchaguzi. Hivyo wako mbali na majimbo yao, wako mbali na matatizo ya majimbo yao. Kama Wabunge wangekuwa wanatoroka bungeni, kurudi majimboni kwao kuzungumza na wapiga kura wao, lingekuwa ni kosa lenye heri.

  Wakati nikiomba mwongozo wako, nilitaka kujua, hawa watoro wanachukuliwa hatua gani. Je, mshahara wao unabaki palepale? Je, wanapokea posho bila kuvikalia viti vyao bungeni? Nilitaka pia kufahamu kutoka kwako ni kazi ipi ya Spika zaidi ya kukalia kiti chake cha Uspika na kuendesha mijadala bungeni. Mara nyingi kiti chako kinakaliwa na Naibu Spika na Wenyeviti. Wewe unakuwa wapi? Wakati mwingine unaonekana umekalia kiti cha Mbunge wa Urambo Mashariki. Ni kweli wewe ni mbunge wa jimbo hilo, lakini nafikiri kazi yako kubwa ni kuliongoza Bunge na si kukikalia kiti cha jimbo lako.


  Maboresho unayotaka kuleta bungeni, ni pamoja na hili la Spika kupoteza kiti chake cha jimbo na kupoteza uanachama wa chama chake cha siasa. Vinginevyo Spika, anakuwa na maslahi binafsi. Spika ambaye kichwani mwake anafikiri kiti cha jimbo lake la uchaguzi, anafikiria chama chake, hawezi kuliongoza Bunge bila ya upendeleo. Ndiyo maana nilishawishika kukuomba mwongozo wako. Hadi leo hii sijapata mwongozo huo!

  Wakati wa kufunga Bunge la Bajeti mwaka huu ulisikika ukiwaonya Wabunge watoro. Ulitishia kuwataja kwa majina na hukusita kuwataja na kuwasifia wabunge na mawaziri wanaovikalia viti vyao bungeni bila kuchoka. Sina uhakika kama onyo hilo ni sehemu ya jibu lako kwangu? Furaha yangu ni kwamba, onyo hilo lilionyesha kwamba ombi langu la mwongozo haukuwa uzushi. Ni kweli wabunge wanatoroka bungeni.

  Leo ninapokuomba mwongozo wa pili, ninaomba nikukumbushe ule wa kwanza. Bado ninasubiri majibu. Ni lazima tufike mahali tujenge utamaduni wa viongozi wa kitaifa, kujishusha na kuingia moja kwa moja kwenye majadiliano na wananchi. Njia ya kutumia vyombo vya habari, kama redio, luninga na magazeti ni muhimu na bora kwa majadiliano mapana ya kuwafikia wananchi wengi. Viongozi wetu, wanawekwa madarakani na wananchi, bila wananchi hakuna kiongozi atakayesimama.

  Hivyo ni muhimu kujua wanayoyasema wananchi, ni muhimu kujadiliana nao na kujenga mahusiano na mawasiliano ya karibu. Spika akijibu hoja iliyoandikwa gazetini hapotezi cheo wala heshima ya Uspika, bali anajijengea mahusiano bora na wananchi, anajenga daraja badala ya kutengeneza ufa kati yake na wananchi.

  Yanaandikwa mengi juu ya viongozi wetu, yanaulizwa maswali mengi juu ya viongozi wetu, yanaandikwa mengi yanayokwenda ndivyo sivyo kwenye utawala, lakini hakuna majibu yanayotolewa. Ikitokea yakatolewa majibu, yanakuja kwa njia ambayo haina nafasi ya majadiliano, yanakuja kama vile “dogma”, amri au sheria.

  Wakati mwingine majibu yanakuja kwa njia ya vijembe, vitisho na majivuno hali inayotoa picha ya “nchi hii ina wenyewe”. Hatuwezi kuacha kuandika maana nchi hii ni yetu sote, tunaandika yale tunayoyaona, tunayoyasikia, tunayoyaishi na yale yanayotugusa katika maisha ya kila siku. Ninasita kusema kwamba viongozi wetu hawasomi magazeti, maana hata kama hawasomi wao, wasaidizi wao wanasoma na ni lazima watawaeleza tu.

  Hata kama wewe Mheshimiwa Spika, hukusoma hoja yangu ya kukuomba mwongozo, nina uhakika wasaidizi wako walisoma na kukuelezea. Lakini unazingatia utamaduni ule ule wa kutojibizana na watu wa chini.


  Kuna rafiki yangu ambaye ni kiongozi. Aliposoma niliyoyaandika, (si haya ya kuomba mwongozo wa spika ni matatizo mengine ya wananachi wa vijijini) yakamgusa, alitaka kujibu – lakini eti alishauriwa kutoka juu, kwamba asipoteze muda wake kujibizana na waandishi. Hekima na busara ni kukaa kimya na kupuuza. Niliyokuwa nimeyaandika ni mambo ambayo hata ukiyafunika leo kwa kuamua kukaa kimya; yatajitokeza kesho na keshokutwa. Kukaa kimya si jibu. Huwezi kukaa kimya katikati ya watu wanaozungumza, huwezi kukaa kimya kitikati ya watu wanaoandika, huwezi kukaa kimya katikati ya watu wanaoimba na kucheza na huwezi kukaa kimya katikati ya watu wanaolia na kuomboleza. Ni lazima utazungumza, na ukikataa, unalazimishwa!

  Nchi zilizoendelea, viongozi hawapuuzi yale yanayoaandikwa kwenye magazeti. Kila linaloandikwa linafuatiliwa na kama kunahitajika jibu linatolewa. Viongozi hawa wanafahamu kwamba yanayoandikwa kwenye magazeti na kwenye vyombo vingine vya habari ni maoni ya wananchi; kuyapuuza ni sawa na kujiweka kitanzi. Na kusema kweli, kuwasikiliza wananchi na kukubali kufanya nao majadiliano, ni kati ya vitu vilivyosaidia maendeleo makubwa tunayoyashuhudia katika nchi hizi. Tukitaka kuendelea, ni lazima tuige wanayofanya wenzetu.

  Mwongozo ninaouomba leo kutoka kwako, Mheshimiwa Spika, ni juu ya Kipindi cha Maswali na Majibu. Nimekuwa nikifuatilia kipindi hiki kwa muda mrefu. Yanaulizwa maswali mengi na yanatolewa majibu mengi vilevile.

  Swali langu ni je, Bunge lina mfumo gani au chombo gani cha kufuatilia utekelezwaji wa majibu yanayotolewa bungeni wakati wa kipindi cha maswali na majibu? Na je, wabunge wetu wanafuatilia kwenye wizara husika kuhakikisha ahadi zinazotolewa kwenye majibu zinatekelezwa?

  Swali jingine dogo la nyongeza, je, Bunge lina madaraka ya kuziwajibisha wizara zinazoshindwa kutekeleza ahadi zinazotolewa bungeni? Ni chombo gani chenye mamlaka ya kuhakikisha yale yote yanayojibiwa kwenye kipindi yanatekelezwa?

  Na swali dogo kabisa la nyongeza, je, mbona wabunge wanapojadili maslahi yao binafsi, kama vile kuongezewa posho, kupewa dreva, walinzi na mengine, ufuatiliaji wao unakuwa mkubwa na wenye kasi kuliko wanavyofuatilia utekelezwaji wa majibu ya maswali yao? Wao ni muhimu, wao ni waheshimiwa zaidi ya watu wanaowawakilisha?

  Mawaziri wote ni wabunge. Ubunge wao ni sawa na wa wale wanaowauliza maswali. Wako ngazi mmoja – ni marafiki ni ndugu na wana mshikamano. Hata wanapojibu maswali, hakuna dalili za kuonyesha kuogopa kuwajibishwa. Wanajibu kwa “raha zao”, wanajibu kwa utani na mizaha. Wakati mwingine wanajibu bila kuwa na umakini wa kutosha. Wanajua wanawajibu wenzao. Ndiyo maana kunazuka maoni kwamba mawaziri, wasiwe wabunge. Ili wabunge wawe na “meno” wakati wa kuuliza maswali na kuwa na nguvu za kuwawajibisha mawaziri.


  Nimeamua kuomba mwongozo wako, maana kuna maswali yanayoulizwa kila kikao cha Bunge, na majibu yanayotolewa ni yale yale. Nafikiri hata wizarani hawajishughulishi kuandaa majibu, wakiliona swali wanarudisha majibu yale yale.

  Naogopa kulidhalilisha Bunge maana mimi ni mzalendo, lakini Kipindi cha Maswali na Majibu kinafana fanana na mchezo wa kuigiza. Haiwezekani kwa watu makini swali liulizwe zaidi ya mara tatu na kupatiwa jibu lilelile bila kuwapo mipango na mikakati ya ufumbuzi.

  Kinachosikika ni kilio cha wabunge, kwamba maswali yao yasipopatiwa ufumbuzi hawatachaguliwa tena. Muhimu kwao ni kuchaguliwa kuingia bungeni na wala si kushinikiza kwa kila njia kupata ufumbuzi wa matatizo ya wananchi. Kwanini mambo mengine yanakwenda polepole, lakini maslahi ya waheshimiwa wabunge yanashughulikiwa kwa kasi kubwa?

  Maswali yote yanayoulizwa bungeni ni ya msingi, ukitoa yale ya kipuuzi na utani. Mengi ni juu ya barabara, maji, hospitali, shule, bei za mazao, usalama wa raia na mali zao na usalama na amani katika mipaka. Mara nyingi majibu ni kwamba Serikali haina fedha na nchi yetu ni masikini.

  Majibu haya hayana ukweli wowote. Serikali yenye matumizi makubwa, yenye mashangingi kila wizara, kila idara, kila mkoa na kila wilaya, yenye kuendesha semina kwenye hoteli za kitalii, yenye kulipia matibabu ya viongozi nchi za nje, haiwezi kuwa haina fedha. Na nchi yenye madini, ardhi yenye rutuba, maziwa yenye samaki wengi, mbuga za wanyama na vivutio vingi vya kitalilii haiwezi kuwa masikini. Inawezekana ni nchi yenye watu wenye umasikini wa kufikiri na kupanga, lakini nchi yenyewe si masikini. Nchi yetu ni tajiri. Tukiendelea kuimba umasikini ndani ya utajiri, tutasutwa na vizazi vijavyo.

  Nitashukuru kupata mwongozo wako Mheshimiwa Spika. Lakini hata nisipopata mwongozo wako, nikapata jibu kwa matendo nitashukuru. Maswali yaliyoulizwa kwenye Bunge lililopita, yasipoulizwa tena ni dalili kwamba kuna utekelezaji.

  Lakini pia kuna miradi iliyotolewa ahadi ya kutekelezwa katika kipindi hiki cha Bajeti. Mfano ujezi wa barabara katika majimbo fulani fulani, miradi ya maji, miradi ya umeme, hospitali na mingine mingi ikitekelezwa, mwongozo wako utakuwa umepokelewa. Naomba kutoa hoja!

  Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa S. L. P. 114 Magu, Mwanza. Simu: 0754 633122
   
 2. Msongoru

  Msongoru JF-Expert Member

  #2
  Sep 18, 2008
  Joined: Apr 16, 2008
  Messages: 306
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 35
  Tatizo ni katiba mzeee!!!
   
 3. Lambardi

  Lambardi JF-Expert Member

  #3
  Sep 18, 2008
  Joined: Feb 7, 2008
  Messages: 10,313
  Likes Received: 5,605
  Trophy Points: 280
  Pamoja na Katiba tatizo ni Mtazamo..na lengo halisi la wabunge wetu kule Bungeni................................
   
 4. M

  Masatu JF-Expert Member

  #4
  Sep 18, 2008
  Joined: Jan 29, 2007
  Messages: 3,285
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 135
  Of all people huyu Samwel Sitta ndio anataka tumuamini yeye msafi na mpinga ufisadi. He is stuck in in the middle ni fisadi hata hivyo anataka jamii umuone ni mpinga ufisadi na kuna watu wanataka kumuua au kumvua kiti chake cha ubunge!
   
 5. Shakazulu

  Shakazulu JF-Expert Member

  #5
  Sep 18, 2008
  Joined: Feb 23, 2007
  Messages: 940
  Likes Received: 10
  Trophy Points: 35
  Where is this coming from? Umesoma habari yenyewe au unakurupuka tu kujibu?
   
 6. K

  Kipanga JF-Expert Member

  #6
  Sep 18, 2008
  Joined: Apr 24, 2008
  Messages: 679
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 0
  ....Karibu wabunge wote ni wajasiriamali wale na ndio maana hawatulii wakati wa vikao akili iko kwenye vi-project.....Njaa mingi wajameni
   
 7. Pundit

  Pundit JF-Expert Member

  #7
  Sep 18, 2008
  Joined: Feb 4, 2007
  Messages: 3,741
  Likes Received: 25
  Trophy Points: 135
  Katika kupenda uwazi, kuwepo na kitabu cha wazi cha hasibu za mahudhurio ya wabunge bungeni, muda waliotumia bungeni na muda ambao hawakuwepo.Miswada waliyochangia na miswada waliyokosa.

  Halafu kitabu hiki kichapishwe wananchi waweze kukipata. Ikishafanywa hivyo Spika asitakiwe kukurupushana na wabunge kama mwalimu mkuu na wanafunzi, wananchi wenyewe waachiwe kuchagua cha kufanya, kusuka au kunyoa.
   
 8. M

  Masatu JF-Expert Member

  #8
  Sep 18, 2008
  Joined: Jan 29, 2007
  Messages: 3,285
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 135
  Btw me and u wewe ndie mkurupukaji unaehitajiwa kuisoma makala ( btw the lines)
   
Loading...