Mgomo wasababisha walimu kushushwa vyeo | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mgomo wasababisha walimu kushushwa vyeo

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, Nov 23, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Nov 23, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,688
  Likes Received: 82,553
  Trophy Points: 280
  Date::11/22/2008
  Mgomo wasababisha walimu kushushwa vyeo
  Gedius Rwiza
  Mwananchi

  KESI ya mgomo wa walimu jana haikuweza kuendelea kama ilivyopangwa baada ya Chama cha Walimu (CWT), kuwasilisha madai mapya kikieleza kuwa kuna walimu wananyanyaswa, kushushwa vyeo na kukamatwa kutokana na kushiriki mgomo ulioanza Novemba 17, lakini ukazuiwa na Mahakama ya Kazi.

  Naibu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch aliweka bayana hayo wakati akitoa maelezo kwa Msajili wa Mahakama ya Kazi ambako walienda kusikiliza hatima ya pingamizi la serikali la kuzuia mgomo lililotolewa usiku wa Novemba 17 na Jaji Ernest Mwipopo, ambaye alisema mgomo ungefanyika ungeathiri sekta nzima ya elimu na wanafunzi kwa ujumla na serikali ingeweza kupata hasara.

  Kutokana na madai hayo mapya ya CWT, hakuna shauri lililosikilizwa jana.

  Katika madai hauo, CWT inadai kuwa imepata taarifa kutoka mikoa mbalimbali kuwa wanachama wake ambao ni walimu wakuu wanashushwa vyeo, wengine wanakamatwa na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya kwa madai kuwa wanachochea mgomo.

  Oluoch alionyesha watu waliofanyiwa vitendo hivyo na kuongeza kuwa, baadhi ya walimu waliokuwa wanaishi katika nyumba za serikali, wamefukuzwa na hivyo kuishi kama watumwa hali ambayo alisema ni ukiukwaji wa sheria.

  Oluoch aliwataja walimu waliofanyiwa vitendo hivyo kuwa ni Mwalimu Gabriel Gyoze na Stephen Makulila wa Shule ya Sekondari Italie iliyo wilaya mpya ya Chato Biharamulo mkoani Kagera na mwalimu wa Shule ya Msingi Balili iliyo Bunda ambaye inadaiwa ameshushwa cheo na mkurugenzi wa wilaya hiyo.

  Alisema kuwa baadhi ya walimu waliotuhumiwa kuhamasisha mgomo wametimuliwa kutoka katika nyumba za serikali.

  Msajili huyo, Samwel Karua alikubali kupokea hoja hizo na kuamua kuwa suala hilo lianze kusikilizwa Desemba 5.

  Katika maelezo yake, Oluoch alisema si kweli kwamba serikali imewalipa walimu na kwamba wanashangazwa na kuona walimu wa sekondari, vyuo vya ualimu na watumishi wanaofanya katika taasisi mbalimbali za wizara ya elimu bado hawajaguswa wala kuongelewa, wakati wanastahili kulipwa.

  Aliongeza kuwa kama serikali ina nia ya kujadiliana na CWT, lazima kwanza ilipe madai ya walimu bila kubakiza hata senti moja na kwamba malipo hayo yahusu walimu wote na si wa shule za msingi tu. Alisema hali ya baadhi ya walimu kutolipwa, inaweza kusababisha matatizo ya walimu kukosa suluhisho.

  "Lazima ilipe madai yote kwanza bila kubakiza hata senti tano vinginevyo mvutano utaendelea kuwa mkubwa. Tunataka kuona hata walimu wa sekondari na vyuo wamepata haki zao," alisema Oluoch.

  Alisema kuwa katika uhakiki uliofanyika walibaini kuwa walimu wa sekondari na vyuo wanaidai serikali Sh 4.2 bilioni, lakini hadi sasa hawana taarifa za malipo hayo na badala yake wanaambiwa kuwa uhakiki unafanyika. Alisema uhakiki huo hauhusishi viongozi wa CWT, hali ambayo alisema inawatia wasiwasi.

  Mwananchi imepata taarifa kutoka Chuo cha Ualimu cha Msasani, Tukuyu kinachotoa daraja la tatu (A) na diploma kwamba walimu hawajalipwa wala kuhusishwa katika zoezi hilo. Mmoja wa walimu wa chuo hicho aliiambia Mwananchi kuwa, hadi sasa hakuna kilichofanyika na kwamba ameanza kukata tamaa.

  Naye, Ummy Muya anaripoti kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jana ilianza kulipa madai mbalimbali ya walimu wake zaidi ya 3,000 baada ya kupewa Sh612 milioni kwa ajili ya zoezi hilo.

  Mwenyekiti wa CWT wa Ilala, Zubeda Aziz alisema walimu watalipwa kwa makundi na kwamba waliolipwa jana mchana ni madai ya walimu 610 ya likizo ya mwezi Juni mwaka huu.

  Mwenyekiti huyo alisema Jumatatu jumla ya walimu 836 watalipwa malipo ya matibabu, likizo, masomo na posho ya kujikimu, wakati Jumanne watalipwa walimu ambao wanadai malimbikizo ya fedha zao za likizo tangu mwaka 1991 hadi 1999.

  Alieleza kuwa, kutokana na zoezi kufanywa kwa shinikizo na kwa haraka halikosi mapungufu hivyo aliwataka walimu wote ambao waliandika madai yao na kuyawasilisha lakini majina yao hayapo, wasubiri zoezi la uhakiki baada ya malipo ya sasa kumalizika.

  "Sisi tumeunga mkono kauli ya rais wetu wa CWT ya kuhakiki kwa kupita shule hadi shule mwalimu kwa mwalimu," alisema Aziz na kuongeza:

  "Kulikuwa na malimbikizo ya madeni ya muda mrefu yenye thamani ya Sh290 milioni na mwaka 2004 walilipa Sh 91 milioni kwa baadhi ya walimu."

  Pia, kuna wastaafu 32 ambao wanatakiwa kulipwa jumla ya Sh10 milioni.

  "Wapo walimu waliokufa fedha zao tutazilipa kwa wasimamizi wa mirathi walioteuliwa kifamilia wakiwa na vielelezo," alisema.

  Katika hatua nyingine walimu wawili ambao majina yao haya kuwepo katika orodha ya walimu wanaolipwa sasa walisema kutokana na kuelezwa kuwa mchanganuo huo wa uhakiki utapita shule hadi shule na kwa mwalimu mmoja mmoja, wanaamini watalipwa.

  "Imani ya kulipwa inaonekana kutokana na walimu waliolimbikiziwa madai yao tangu mwaka 1991 wanalipwa leo hii (jana) hivyo tunasubiri," alisema mmoja wao.

  Naye Saa Mohammed anaripoti kuwa mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni amemtaka katibu CWT wilayani Kinondoni kuhakiki malipo ya walimu mapema na kuyafanyia marekebisho ili waweze kulipwa madai yao.

  Kwenye ofisi za CWT za wilaya hiyo, walimu walikuwa wengi kufuatilia uhakiki huo. Walimu wanadai Sh1.9 bilioni wilayani humo, lakini kiasi kilichotengwa hadi sasa ni Sh582 milioni tu.
   
Loading...