Mgogoro wa kikatiba Tanzania: Chanzo ni nini? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mgogoro wa kikatiba Tanzania: Chanzo ni nini?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by mosquito, Jan 24, 2011.

 1. m

  mosquito Member

  #1
  Jan 24, 2011
  Joined: Nov 5, 2010
  Messages: 15
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Mgogoro wa kikatiba Tanzania: Chanzo ni nini?
  Makala ya Kiongozi wa Upinzani kwenye Baraza la Wawakilishi, Mhe. Abubakar Khamis Bakari
  Wah. Wazanzibari Wenzangu, Wake kwa Waume,
  Wah. Wageni Waalikwa,
  Wah. Salaam na Amani Ziwe Juu Yenu.

  Utangulizi
  Wahe. Wazanzibari;
  Mada mulionipa kuiongelea ni “Mgogoro Wa Katiba”Tanzania. Ni mada refu na pana. Huwezi kuzungumzia mgogoro wa Katiba bila kwanza kugusia, ingawa kwa kidogo tu mambo matano muhimu, nayo ni–
  1. Zanzibar kama nchi na Mamlaka yake.
  2. Tanganyika kama nchi ilivyokuwa wakati huo na mamlaka yake
  3. Muungano na Makubaliano ya Muungano.
  4. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  5. Katiba ya Zanzibar,
  na kuona zaidi vipi maeneo haya matano yanahusiana pamoja au kutofautiana na hivyo kuleta migongano isiyokuwa na maana yeyote ile.
  Lengo langu basi ni kufafanua maudhui hizo ili kongamano letu hili mwisho kabisa liweze kujadili na kuona nini cha kufanya katika kuondokana na matatizo hayo.

  Zanzibar na mamlaka yake
  Zanzibar ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Wakoloni tarehe 10 Dec. 1963. Uhuru huu wa bandia haukuwaridhisha walio wengi, na ilipofika January 12, 1964, Serikali ya Zanzibar ilipinduliwa na kuwa “Jamhuri ya Watu wa Zanzibar”, iliyokuwa na mamlaka yake kamili ya kufanya shughuli zake zote, za nje na ndani. Hii ndio maana katika Sheria ( Decree) No. 5/64 ya Zanzibar katika kif. nam. 2 na nam.3 vilisisitiza kuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ni nchi ya kidemokrasia inayoendeshwa na utawala wa sheria …”. Sheria hii hadi leo bado haijafutwa. Katika kuihakikisha Zanzibar kama ni nchi, Katiba ya Zanzibar kif. Cha 9(1) kinasema waziwazi kuwa:
  “Zanzibar itakuwa ni nchi ya kidemokrasia na haki za kijamii”

  Na katika kif 9(2), Katiba hiyo imeendelea kuelezea mamlaka ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na mamlaka ya kuendesha nchi.
  Nyerere anasadikiwa vile vile akisema kwa undani wa roho yake kwamba:

  “Ikiwa watu wa Zanzibar, bila ya kuingiliwa na watu wa nje na ikiwa wana sababu zao, wakaamua kuwa Muungano umekuwa kero kwa maisha yao, na kwamba hauna maslahi na wao sitowalazimisha kubakia na Muungano huo. Muungano huu utasita pale tu nchi shiriki itapoamua kujitenga.”
  (Tizama gazeti la London Observer la tarehe 20 Aprili, 1968)
  Hii inaongeza ladha zaidi ya kuonesha kuwa hata muasisi wa Muungano wetu anaamini kuwa Zanzibar ni mamlaka huru na pekee na kwamba haitowezekana hata kidogo kuifanya mamlaka hiyo isitambuliwe kua ni nchi. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia inathibitisha kuwa Zanzibar ni nchi, ina serikali yake na pia ina mamlaka yake kwa mambo yote yasiokuwa ya Muungano (Vif. 102,103,104 vya Katiba hiyo vinahusika).

  Tanganyika – Kifo Cha Makusudi
  Tanganyika nayo ilipata uhuru wake tarehe 9 Desemba 1961 na mwaka mmoja baadae (1962) ikawa ni Jamhuri ya Watu wa Tanganyika. Mara tu baada ya kuangushwa kwa Serikali ya Zanzibart tarehe 12 January 1964, ni miezi mitatu tu baadae, Jamhuri ya Watu wa Tanganyika waliungana na Jamhuri ya watu wa Zanzibar kufanya Muungano wa Jamhuri ya Watu wa Tanganyika na Jamhuri ya Watu Zanzibar.
  Wadau hawa wa Muungano (nchi ya Tanganyika na nchi ya Zanzibar) walibadilishwa kabisa majina yao baada ya kutungwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977. Ibara ya 94(1) ya Katiba hiyo inaweka majina ya Tanzania Bara ikimaanisha iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Tanganyika na Tanzania Visiwani ikiwa ni ile iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
  Mnamo mwaka 1984 kulikuwa na mabadiliko mengine ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mabadiliko hayo (The 5th Constitutional Amendment) yaliyofanywa kwa mujibu wa Sheria No. 15/84 ibara ya 53 ilibadilisha maneno Tanzania Visiwani “Kuwa Tanzania Zanzibar”kwa kumaanisha ile iliokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Pengine hii illifanywa makusudi ili kuondoa “makelele” ya aliekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Wolfgang Dornado pale aliposema kuwa kuiita Tanzania visiwani sio sahihi kwa sababu “Mafia na visiwa vyengine vidogo vidogo ambavyo navyo vilikuwa katika mamlaka ya Jamhuri wa Watu wa Tanganyika havihusani na Zanzibar.
  Kutoka na mabadiliko hayo, neno “Tanzania Bara bado lilibakia kwa ajili ya “Tanganyika”, wakati Zanzibar ilitafsiriwa kuwa ni “Tanzania Zanzibar” Kwa maana hiyo Zanzibar ilibakisha jina lake wakati jina la Tanganyika liliuliwa kwa mukusudi.

  Makubaliano ya Muungano na Uhalali wake: Katiba Mama ya Jamhuri ya Muungano inakiukwa
  Sheria mama inayohalalisha Muungano wa zilizokuwa nchi mbili huru za Tanganyika na Zanzibar ni “Makubaliano ya Muungano ya Mwaka 1964”. Makubaliano haya ndio KATIBA MAMA ya Muungano wetu, na ndio Katiba Kuu ya nchi kuliko hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Katiba ya Zanzibar.
  Kisheria pale ambapo Katiba ya Jamhuri na ile ya Zanibar zinatofautiana na Katiba Mama, basi Katima Mama (yaani Makubaliano ya Muungano) ndio yatayosimama na Katiba hizo mbili, kwa kadiri ya pale zinapotofoutiana, basi huwa ni batili.

  Makubalino kama haya ya England na Scotland ya mwaka 1707 ambayo yalianzishwa mwaka 1603 na kujadiliwa tena mwaka 1705 yalithibitishwa na Mahkana Kuu ya Scotland katika kesi ya Mac Cormak Vs.The Lord Advocate (1953) Scotish Law Times (SLT) 255,261,262 kuwa hata Bunge la Uingereza halina uwezo kuingilia vifungu vya Makubaliano ya Muungano huo . Hii ni kwa sababu huo ndio mkaaba mama ambapo kuna utaratibu wake wa kuubadilisha.
  Makubaliano haya basi ni sawa sawa Mkataba Maalum (Treaty) uliotiwa saini na Viongozi wa nchi mbili husika. Mkataba maalum, “Treaty” unapotiwa saini na nchi husika basi huwa kwa mujibu wa Sheria ya Kimataifa ni lazima kupata ridhaa za nchi hizo. ( kama kesi ya R.V.H.M. Treasury and the Bank of England exp. Centro Com. Times Law Report Oct 7, 1993 ilivyoamuliwa ). Mkataba huu wa Muungano wenyewe, katika Ibara ya viii ya Mkataba huu ulizungumzia dhahiri kuhusu ulazima wa kupata ridhaa toka kwa nchi husika yaani Tanganyika na Zanzibar. Kitendo hichi cha ridhaa kilipatikana kutoka Serikali ya Tanganyika kama ilivyoelezewa katika Tanganyika Legal Notice No. 243 ya 1964. Lakini kwa Zanzibar, ridhaa hii haikufanywa na Baraza la Mapinduzi ambalo kwa wakati huo ndilo llilokuwa chombo cha kutunga sheria na pia chombo cha utawala (Executive cum Legislature). Kwa maana pana basi mkataba huo haukupata msingi madhubuti wa kisheria,kwa sababu Zanzibar haikuridhia Mkataba huo.
  Hata hivyo, kwa sababu watu wa Tanganyika na wale wa Zanzibar wamekuwa wakikaa nao Mkataba huo kwa miaka mingi bila malalamiko katika vyombo vya kisheria nchini, basi pengine watu wa Jamhuri ya Tanganyika na wale wa Jamhuri ya Zanzibar wameridhika na makubaliano hayo na hivyo kukubali maamuzi haya bila wasiwasi wowote. Na kwa msingi huu, tunaweza kabisa kusema kuwa Muungano huo ni halali kwa sababu ya ridhaa (acquiescence) ya watu wenyewe.
  Katiba ni nini na vipi inavyotakiwa iwe

  “Katiba………..ni maandiko maalum yanyoweka utaratibu wa namna gani utawala, bunge na mahakama zitafanya shughuli zao. Katiba vile vile inaweka namna
  haki za wananchi zitavyoshughulikiwa na Serikali….._
  (Tizama Kitabu cha B.R.Atre Legislative Drafting 2nd Edn, pg 200)

  Kwa maana fupi kabisa, Katiba ni makubaliano maalum ya kanuni, utaratibu na mazoea ya chombo fulani yaliyowekwa pamoja na ambayo yanatoa mfumo, muundo na kazi ya chombo hicho. Pale tunapozungumia katiba ya nchi, basi tunakusudia uhusiano maalum baina ya mtu na taifa wenyewe katika misingi hiyo ya kutekeleza yale yote yaliyowekwa katika katiba hiyo (kanuni). Katiba, kwa maana nyengine ni ramani inayoonesha nguvu fulani ambazo zinahalalishwa na utumiwaji wa nguvu hizo katika mikondo mitatu ya taifa – Utawala, Bunge na Mahkama.
  Katiba ni sheria kuu au kwa lugha ya siku hizi ni sheria mama katika nchi. Kwa mfano, Kifungu cha 4 cha Katiba ya Zanzibar kinasema hivi:
  “Katiba hii…………itakuwa na nguvu za kisheria nchini kote, na …….ikiwa sheria yoyote itatofautiana na Katiba hii, basi Katiba hii ndiyo itayokuwa na nguvu na sheria hiyo itakuwa batili
  kwa kiwango kila ambacho kinahitilafiana”.
  (Tizama vile vile Katiba ya Kenya, Afrika ya Kusini, Namibia ,Barbados n.k.)
  Hii inaonesha wazi kuwa Katiba ndio msingi mkuu wa sheria zote, na hakuna chombo kinachoweza kuichezea kwa kuibadilisha ovyo ovyo ila kwa utaratbu maalum uliowekwa. Na ndio maana huko Marekani kesi muhimu ya Marbury vs. Madison ikaamuliwa ya kuwa:

  “…..kwa sababu Katiba ndio sheria kuu ya nchi (kama ilivyo ibara ya VI ya Katiba ya Marekani) na kwa sababu ni mamlaka ya Mahkama kutekelza sheria hizo kwa vitendo, inamaanisha kwamba sheria nyengine za nchi, na hata sheria zinazopitishwa na Baraza la Wawakilishi (congress) zinaopotofautinana na kifungu chochote cha Katiba, basi sheria hizo zinatoa nafasi kwa Katiba, na sheria hizo lazima ziainishwe na Mahkama zetu kuwa ni batili”.
  Katiba pia inatoa mfumo au utaratibu wa kisheria kwa nchi husika juu ya muundao wa Serikali yake, vyombo vyake vya kisiasa na mahusiano baina ya wananchi na serikali na pia mahusiano baina ya wananchi wenyewe.

  Katiba ya nchi vile vile ni kama mkataba ambapo wananchi wenyewe na taifa hilo wamekubali kuwa mkataba huo utumike katika kuwaongoza wao na Serikali yao, pamoja na kukubaliana ni namna gani vyombo vya dola vitafanya kazi. Katiba ni lazima iwepo katika nchi ili kukinga matatizo yanayoweza kujitokeza ikiwa kila mwananchi atafuata utaratibu wake, au kila mkondo wa Serikali utafanya wanachokitaka. Katiba ni kanuni maalum ambazo zina lengo la kuiweka jamii pamoja, jamii ambayo itaishi katika mazingira ya amani na utulivu bila ya kuwa na migongano kwa lengo la kuleta maendeleo katika nchi hiyo.
  VIPI KATIBA INATAKIWA IWE?
  Aliyekuwa Jaji Mkuu wa Marekani Sir. John Marshall, alisema katika kesi maarufu ya Mc. Culloch Vs. Maryland – 4 wheat 316 (US 1819) kwamba Katiba yao ni Katiba ambayo:
  “…………ina lengo la kushi miaka kadhaa ijayo, na kwa hivyo iwe inaweza kuhimili misukosuko kadhaa ya binaadamu”.
  Lakini ili nisipotoshe maana halisi aliyoielezea Bw. Johm Marshall, yeye alisema kwa lugha ya Kiingereza kuwa:
  “Our constitution ………….is a Constitution intended to endure for ages to come, and consequently to be adapted to the various crises of human affair”

  Sasa basi Katiba yetu ya Tanzania na kwa maana pana Katiba ya nchi nyengine yoyote, ambayo ni sheria mama ya nchi,lazima ilenge huko alikokuona Bw. Jonh Marshall. Inatakiwa iwe inakidhi haja ya mabadiliko ya nchi kisiasa na kiuchumi. Inatakiwa iwe ni nyumbufu (flexible) kukubaliana na ukuwaji wa mabadiliko kadhaa ya taifa husika, na wakati huo huo misingi yake mikuu iwe bado inaongoza taifa hilo na watu wake bila ya kutetereka.
  Katiba nzuri ya nchi, na ambavyo ndivyo inavyotakiwa iwe, ni kama ile aliyoielezea Jaji Sower katika kesi ya Tuffuor v. A. of Ghana – (1980) A.G. 637, 674 kwamba Katiba ya nchi ni chombo ambacho kinakidhi matakwa ya wananchi na kwamba vile vile inaonesha historia yao. Hivyo basi katiba yoyote ile nilazima itizamwE kuwa ni dira, na ni:

  “…………..alama muhimu (land mark) katika kuwaoneshea watu njia ya maendeleo. Ndani yake mna tama na malengo (hopeS and aspirations) kwa kupata maisha mazuri. Katiba ina misingi yake ya sheria (its letter of the law) na ina malengo yake (its spirit). Katiba ndio kichwa cha mikondo mitatu ya utawala ambapo kila mkondo unafanya wajibu wake ………..na uwezo wao unatokana na Katiba hiyo, Katiba inaelezea pia namna ya kuibadilisha……..kwa maana hiyo lugha inayotumika katika Katiba ni lazima iwe ina fikiriwa kama ni kitu kinachoishi (living organism) ambacho kinakua na kuendelea……..(capable of growth and development”).
  Jee Katiba zetu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar zinakidhi yote hayo tuliyelezea, ambayo ni muhimu kuwemo katika Katiba?,
  Jee!, wakati wa kuandikwa Katiba hizi zilipata idhini ya watu wenyewe?. Jee! Katiba hizi zinalinda maslahi ya watu na mfumo wa vyama vingi, au kulinda haki za binaadamu au utawala wa sheria? Yote hayo ni mambo ya kujiuluiza; na ikiwa jibu halioneshi kuwa ni ndio, basi Katiba hizi zitakuwa hazikidhi ule msemo maarufu wa kidemokrasia uliomo ndani ya Katiba wa kwamba ni watu wenyewe ambao wameiandika Katiba yao. Hivyo basi kukosekana kwa mambo hayo kunaonyesha wazi umuhimu wa kuwa na Katiba mpya itayoingiza angalau kwa kiasi kikubwa mambo tuliyoyaelezea hapo juu.

  Sasa natuangalie yote tuliyosema, kama yamo ndani ya Katiba zetu za Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar na baadae ndio tutaamua kama kuna haja au la ya kuwa na Katiba Mpya kwa maslahi ya wa-Zanzibari na wa-Tanzania kwa ujmla.
  KUNA HAJA YA KUWA NA MABADILIKO YA KATIBA?
  Kitu cha mwanzo cha kutizama katika utaratibu wa mabadiliko ya Katiba ni kujuwa maeneo ya mabadiliko ya Katiba pamoja na umuhimu wake ili mabadiliko hayo yafanyike vizuri. Malengo yanayotaka kufikiwa lazima yaonekane na yakubalike. Wananchi hawatokubali mabadiliko yoyote ikiwa malengo hayo hayakuainishwa ipasavyo. Kwa hivyo ni lazima kuwe na makubaliano ya Kitaifa katika mabadiliko yoyote yale ya Katiba. Hapa tunasisitiza umuhimu wa kushirikishwa wananchi walio wengi. Suala hapa ni wananchi na si vyama au itikadi za vyama.
  Ulazima wa mabadiliko ni lazima uwe unalazimisha haja hiyo, uwe halali na ukubalike. Wakati wa mabadiliko hayo lazima uwe muafaka na wananchi lazima wakubali kwamba wakati sasa umefika kuwa na mabadiliko. Shauku ya mabadiliko inaweza kuanzishwa na viongozi lakini ni lazima baadae ichanuwe kutoka kwa watu wenyewe kwa nyakati maalum ambazo ni nzuri kwa mabadiliko ya Katiba. Nyakati hizo muafaka ni pamoja na nyakati zinazokuwa zimeiva kwa mambo hayo, ambapo ni mara:

  • baada ya vita
  • baada ya mapinduzi
  • baada ya muungano wa nchi mbili au zaidi
  • baada ya mabadiliko ya kisiasa katika nchi
  • baada ya mabadiliko ya mfumo wa kisiasa kutoka chama kimoja kwenda vyama vingi au
  • baada ya kutoka mfumo wa kijeshi uliopo katika nchi kwenda katika utawala wa kidemokrasia.
  Haya ni miongoni mwa mambo ambayo yanapalilia kwa nguvu kubwa sana sababu za kuwepo au kutungwa kwa Katiba mpya ya nchi kutokana na Katiba iliorithiwa. Nchini Uganda kwa mfano, matayarisho ya Katiba mpya ambayo ingeweza kusahihisha makosa yaliyopita kama walivyodai wanachi ilikuwa ni suala la mwanzo katika ajenda za NRM (National Resistance Movement. Kenya vile vile mabadiliko ya Katiba yalikuwa ni ajenda kubwa wakati wa vyama vingi hadi kufikia kuandikwa kwa rasimu ya Katiba ya Kenya iliojuilikana kwa jina maarufu la Katiba ya Bomas. Afrika ya Kusni nayo walilazimisha kuwa na Katiba mpya baada ya mabadiliko makuhwa ya kisiasa yaliyotokea. Mabadiliko yote hayo yana lengo moja tu, la kuiweka nchi iwe na Katiba ya Kidemokrasia ili vyombo vitavyofanya kazi kwa mujibu wa Katiba hiyo view na ufanisi mzuri wa shughuli za uendeshaji pamoja na kuleta maendeleo ya nchi kwa faida ya watu na nchi husika. Lengo hapa ni lile lile alilolielezea Jaji Sawyer la kuwa na utaratibu mzuri wa utawala wa nchi kwa faida ya nchi na wananchi.
  Ni muhimu kujuwa lengo la mabadiliko hayo ya Katiba pa moja na kujuwa mipaka yake kwa madhumuni ya kuwa na mkakati halisi na njia nzuri za kufanya mabadiliko hayo. Wakati mwengine inaweza ikawa ni muhimu kuifuta Katiba yote na kuiandika upya, lakini wakati mwengine Katiba ya zamani inaweza ikafanyiwa baadhi ya marekebisho na kubakia ile ile. Hata hivyo pale unapokuwa na Katiba ambayo imeshajaa viraka vya mabadiliko basi lazima sasa katiba hiyo ifanyiwe marekebisho kwa kuiandika upya. Hata hivyo katika msingi ya nchi ambazo zimeungana na baadaye kuwa nchi yenye mfumo wa vyama vingi, basi ni vyema Katiba yote ikabadilishwa, kwa maana ya kuzingatia muungano huo pamoja na matakwa ya siasa ya vyama vingi. Hapo tunaweza tukaweka maudhui yetu wenyewe ndani ya Katiba hiyo kwa mujibu wa siasa zetu, utaratibu wetu na mipango yetu tunayohisi yatafaa na kusaidia. Tukifanya hivi tunaweza kujisifia kusema kwamba Katiba yetu ni Katiba yenye mizizi yake nyumbani kwetu (home grown). Wenzetu wa Guyana walifanikiwa kuwa na Katba waliotayarisha wao wenyewe bila ya kutegemea sana kutoka katika Katiba za nchi nyengine. Na Katiba hiyo ilisaidia sana kuijenga Guyana mpya kwa misingi ya ujamaa waliyokuwa wamejiwekea.
  KATIBA YA TANZANIA NA KASORO ZAKE
  Katiba hii inatokana na Katiba iliyotayrishwa mwaka 1965 mara tuu baada ya Tanganyika kuungana na Zanzibar. Katiba hiyo ilikuwa ni ya muda na baadae katika mwaka 1977 ikafanywa Katiba ya kudumu. Hapa tunaona kwamba Katiba hii inatokana na chama kimoja cha TANU, baadae ikawa ni Katiba inayotokana na Chama cha ASP na TANU halafu Katiba hiyo hiyo ikawa inatokana na Chama cha Mapinduzi – CCM. Marekebisho mengi yamefanywa baina ya 1965 hadi leo, yote yakiwa na lengo la kukipa madaraka na uwezo zaidi Chama Tawala. Lakini kwa vyovyote vile Katiba hiyo ilikuwa haina mabadiliko makubwa, ila ni kukiimarisha chama tawala. Na hata baada ya kuunganisha vyama na baadae kuwa na mfumo wa vyama vingi, basi hakuna mabadiliko makubwa yaliyofanywa. Kwa maana hio demokrasia ya Kikatiba katika mfumo wa vyama vingi ndani ya Tanzania ilikuwa, na inaendelea kuwa haipo. Chama cha Wanasheria, Chama cha Haki za Binaadamu na Chama cha Majaji wa Kenya kwa pamoja walisema katika mapendekezo yao ya kudai Katiba mpya kwamba:
  “…………..mambo yote ya Kikatiba, Kiutawala na Sheria kutoka karne ya chama kimoja hayajabadilika”(Nairobi Law Monthly No. 51 January 1955)

  Hakuna maelezo mengine mazuri na matamu yanayoisemea Katiba ya Tanzania tulionayo hivi sasa kama maelezo ya wa Kenya hao. Katiba yetu ya Tanzania ina mabaki tele ya utawala wa chama kimoja, haiendani na wakati huu wa mfumo wa vyama vingi, haitowi demokrasia ya kweli kweli na zaidi haichanganui hasa yale mambo yanayopaswa kushughulikiwa na Zanzibar, Tanganyika na Tanzania. Vile vile Katiba iliopo hivi sasa inalenga tu maslahi ya waliowachache na mara zote haitilii maanani makundi mengine ya jamii. Katiba ya aina hii inawawekea ngumu wananchi na ndio maana ikaitwa “ instrumental”. Zaidi ya hayo Katiba iliyopo hivi sasa imetowa nguvu nyingi kwa utawala ambazo zikitumika vibaya zinaweza kumfanya hata kiongozi wa nchi kuwa dikteta. Mwalim Nyerere mwenyewe alisikikana akisema kuwa ana nguvu za kutosha katika Katiba za kumfanya awe muimla (dikteta). Kwa kiongozi kama mwalimu Nyerere tusingetia wasi wasi sana, lakini jee akija akipatina Rais mwengine yeyote ambae hana busara kama za mwalim Nyerere?.
  Mbali na hayo, ifuatavyo ni mfano tosha ya kuona kuwa Katiba ina migogoro mingi ambayo lazima majibu yake yapatikane.

  1. Orodha ya kwanza ya nyongeza ya pili chini ya ibara 98(1)(b) ni kwa nini mabadiliko ya kuthibitisha mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lazima yaungwe mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote na sio theluthi mbili ya Wabunge wote toka Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge wote tokea Zanzibar? Kwa sababu wabunge kutoka Bara ni wengi hii inaonesha kuwa wanaweza kubadilisha lile wanalolitaka wao tu kwa maslahi yao na sio kwa maslahi ya pande mbili za Muungano.
  2. Orodha ya pili ya nyongeza ya kwanza chini ya Ibara ya 98(1)(b)ina matatizo katika kifungu cha (5) na (6). Ni kwanini mambo haya, yaani madaraka ya serikali ya Zanzibar na Mahkama Kuu ya Zanzibar pale yanapofanyiwa mabadiliko yaungwe mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Zanzibar? Hivyo mamlaka ya Serikali ya Zanzibar na Mahkama Kuu ya Zanzibar ni lazima zipate idhini kutoka kwa Wabunge wa Tanzania Bara? Haielekei na wala si sahihi kabisa.
  3. Mabadiliko yote yaliyofanywa katika orodha ya mabo ya Muungano kutoka 11 ya mwanzo mpaka 16 baina ya mwaka 1965 na 1976, na baada ya hapo mambo ya Muungano yakafanywa hadi kufikia 22 yote hayo ni batili na ni mgogoro wa Kikatiba (Constitation Issue) ambapo ni lazima utafutiwe ufumbuzi. Ni mgogoro wa kikatiba kwa sababu Katiba mama ni Makubaliano ya Muungano. Hivyo si Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo ingebadilisha orodha ya mambo ya Muungano.Ilivyo ni Mkataba wa Muungano wenyewe ndio ufanyiwe marekebisho kwa utaratibu maalum waliojiwekea, ingawa kosa jengine ni kuwa utaratibu huo haukuwekwa kisheria.
  4. Ibara ya 111(b) ya Makubaliano ya Muungano imevunjwa vibaya sana na ni kinyume na Katiba mama. Ibara hii ilianzisha ofisi ya Makamo wa Rais kuwa na nafasi mbili, Makamo wa Rais mmoja awe ni Rais wa Zanzibar ambae ndie atakae msaidia Rais kwa shughuli zake huko Zanzibar. Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 47(2),(3) imeanzisha mgogoro mkubwa katika kufuta Ibara ya (iii) (b) ya Mkataba wa Muungano katika 11th Constitutional Amendement, mamlaka ambayo Katiba ya Jamhuri haina. Kisheria tunaweza kabisa kufunguwa daawa Mahakama Kuu ili kutafuta uhalali wa Makamo wa Rais anaechaguliwa kwa utaratibu wa hivi sasa.
  5. Ibara ya 59(1) ya Katiba ya Muungano nayo ina mgogoro. Mambo ya Sheria si suala la Muungano., lakini Idara hii inaanzisha Afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano. Nionavyo mimi, ni lengo la makusudi lililofanywa ili eti Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano awe na hadhi zaidi kuliko wa Zanzibar. Ni kwenda kinyume na makubaliano ya Muungano, na kwa maana hiyo kuleta mgogoro usio na sababu yeyote ile.
  6. Ikiwa Serikali ya Muungano ina bajeti ya Muungano. Jee ni kwa nini zile Wizara ambazo si za Muungano zina kasimiwa matumizi yake na Serikali ya Muungano ?. Jee hatuoni kuwa Ibara ya 133 mpaka 144 zinazozungumzia masuala ya Fedha kwa Jamhuri ya Muungano zinaonesha tuu kuwepo kwa Serikali ya Zanzibar na ile ya Muungano. Jee!, hili nalo si tatizo la Kikatiba ?
  7. Hata sheria zinazopitishwa kuhusiana na Joint Finance Committee zinapaswa ziungwe mkono kwa wingi wa kura tu ya wabunge wote Sina uhakika kama njia hii inaweza ikawasaidia wa -Zanizbari katika kutetea maslahi yao na ya nchi yao.
  8. Kwa utaratibu wa mfuno wa Muungano ulivyo, Serikali ya “Tanganyika” inatumia mwamvuli wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kujinufaisha wenyewe kwa gharama za Serikali ya Zanzbar, na hasa katika mambo ya misaada kutoka nje pamoja na suala la gesi. Gesi ambayo ni suala la Muungano na ambayo imeshaanza kuvunwa kwa karibu miaka 5 sasa na kupata mabilioni ya fedha. Fedha hizi zinatumiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa shughuli za kuiendeleza Tanzania Bara kiuchumi na kimaendeleo. Zanzibar haijapewa hata shillingi moja inayohusiana na mapato ya gesi asilia.
  9. Ripoti ya Nyalali ( Nyalali Commision ,ukarasa wa 140) pia inaelezea matatizo ya Zanzibar kuhusu gharama za kuendeshea serikali kwa mambo yasiyo ya Muungano. Hii inatokana na sababu kuwa serikali ya Jamhuri wa Muungano ndio hiyo hiyo serikali ya “Tanganyika”, na hivyo matumizi ya Serikali ya Tanganyika au kwa maana nyengine matumizi ya manbo yasio ya muungano pia yanatokana na Serikali ya Muungano ambapo wachangiaji wake ni pamoja na Zanzibar.
  10. Mashirika ya Muungano nayo yanaleta migogoro ya Kikatiba kwa sababu Zanzibar haipati haki yake kamili. Mifano ipo mingi lakini tutaje michache tuu.

  1. Suala la 4.5% iliotolewa na Zanzibar kwa uimarishaji wa Benk Kuu hapo mwaka 1967, hadi leo hakuna faida au gawio ( interests and or dividends) zinazojuilikana na ambazo zinagawiwa kwa Zanzibar kama ni kutokana na mchango wao.
  2. Hakuna mgano wowote unaotolewa kwa Zanzibar kwa mashirika kama vile ya Air Tanzania, Posa , Simu, Bandari na kadhalika. Mambo haya ndio yanayozua migogoro katika Muungano wetu.
  (tizama pia ritoti ya Nyalali ukurasa 140 ambayo pia imeelezea kwa kirefu udhaifu huu).
  11. Kwa mujibu wa orodha ya Mambo ya Muungano, sasa kuna mambo “22” ndani ya orodha huo. Lakini tatizo linalojitokeza kila unapoongezwa orodha huo wa Muungano, basi Zanzibar inapoteza uhuru wake. Lakini hua ni kosa kubwa mtu anapodai kuwa jambo Fulani litolewe katika orodha huo. Huyo ni haini. Orodha huu sasa umefanywa kama mfano wa “ Caspian Sea” ambapo bahari hii ina mdomo wa kuingilia maji tuu lakini haina mdomo wa kutolea maji hayo ( inlet but no outlet) Jussa kaika Kitabu chake cha “Research” ya kumalizia shahada yake – Treating the Disease Not the Symptoms – The Case for Zanzibar’s Opt Out from the United Republic of Tanzania, ukurasa wa 18, alisema kwamba unapoongeza mambo ya Muungano, basi hii inadhoofisha uhuru -sovereignty wa Zanzibar. Kwa kweli ukitazama kwa upana mambo haya ya Muungano ni karibu 36 ambapo yamechanganywa changanywa na kuwa 22 !.
  12. Suala la Mambo ya Nje ni la Muungano. Kuna Mabalozi karibu 23 wa Tanzania nchi za nje. Mabalozi watatu tuu ndio wa Zanzibari. Uwakilishi huu pia unaathari, katika bodi za mashirika ya Muungano. Shirika la ndege la Tanzania, Posta , Simu na Bandari ni miongoni mwa mifano mizuri.Shirika la ndege kwa mfanoau Posta hakuna hata m-Zanzibari mmoja katika menejimenti hizo za mashirika ya Muungano, wakati mashirika hayo hayo yana wawakilishi wa bodi zao kwa shirika la ndege mmoja na kwa posta wawili tu!
  Mifano ya aina hii inayoleta migogoro ndani ya Katiba ni mingi na inataka majibu ambayo yatawatosheleza wa- Zanzibari na wa- Tanganyika. Lakini kwa hapa hiyo tulioielezea inatosheleza. Hebu sasa tujaribu kutazama migogoro mengine ya Kikatiba ambayo nayo ni matatizo makubwa ya Muungano wetu.

  KOSA JENGINE LA KIKATIBA.
  Kama tunlivyosema hapo awali kuwa Mkataba wa Muungano ndio Sheria Mama, na si Katiba ya Jamhuri ya Muungano au ya Zanzibar ambayo inaweza kuwa juu ya Mkataba huo. Mnano tarehe 26/03/1965 Nyerere aliikubali (assent) Sheria iliotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ya kupeleka mbele muda uliowekwa na Mkataba wa Muunganio wa kuliita Bunge la Katiba ( Summoning of Constitutent Assembly). Sheria hiyo No 18/65 inayojuilikana kuwa ni An Act to extend the time for the Summoning of a Constituent Assembly, ilitamka wazi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano hatolazimika kuunda Kamisheni kwa ajili ya kutoa mapendekezo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano au kwa kuuita mkutanol wa kikatiba kwa kutafakari mapendekezo hayo, na kuikubali katiba katika kipindi cha mwaka mmoja tokea kuanzishwa kwa Muungano. Lakini Rais, kwa kushaurina na Makamo wa Rais ambae ni Rais wa Zanzibar ( kwa wakati huo) wanaweza kuunda kamisheni hiyo, wakati ataoona unafaa .(mkazo ni wangu)
  Kitendo cha kutungwa kwa sheria hii na Bunge la Jamuhuri linathibitisha kuwa Bunge hilo limeweza kurekebisha Mkataba wa Muungano, mkataba ambao ni makubaliano ya Kimataifa (International Treaty). Hii si sawa hata kidogo na ni kosa kubwa kisheria.
  Pili, Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika ibara 102 mpaka 106 zinaanzisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (102,103,104) Baraza la Mapinduzi (105) na Baraza la Wawakilishi (106). Hali hii mbaya ya kikatba pengine imefanywa makusudi ili kudhoofisha uwezo na nguvu za Zanzibar
  na hii pia ni uvunjaji wa Makubaliano ya Muuungano kwa sababu Zanzibar ni nchi iliokuwepo pamoja na Katiba yake kabla ya muungano. Hapa mtu anaweza kujiuliza ni chombo gani kikubwa au ambacho kinakuwa juu kuliko mwenzake; Katiba ya awali ya Muungano au Mkataba wa Muungano? Kwa hapa inaonesha ni Katiba ya Jamhuri ambayo ni kubwa kuliko Makubaliano ya Muungano na hata katiba ya Zanzibar. Hii si kweli hata kidogo. Makubaliano ya Muungano yako juu kuliko Katiba ya Muungano; na Katiba ya Muungano ni sawa sawa na Katiba ya Zanzibar. Kwa maana hiyo basi, na hapa panafukuta mgogoro wa kikatiba.

  MKATABA WA MUUNGANO NA KATIBA–ZILIKUSUDIA KUWE NA SERIKALI NGAPI-MOJA, MBILI AU TATU?
  Mkataba wa Muungano kama tulivyosema hapo awali ndio Sheria Kuu, na iko juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanziba.r Ibara ya
  iii(a) ya makubaliano hayo ina ainisha na kuweka chombo tofauti cha utungaji wa sheria (legislatire) na utawala(executive) kwa Zanzibar kwa mambo ambayo hayamo kaaika mamlaka ya Bunge na utawala wa Jamhuri ya Muungano.Wakati huo huo, Bunge hilo (Parliamnt) na utawala huo, (Executive) wa Jamhuri ya Muungano umepewa mamlaka aina mbili chini ya Ibara ya (iv) ya Mkataba wa Muungano kama ilivyo hapa chini:

  1. mambo yote ya Muungano yaliyomo na yanayohusiana na Jamhuri ya Muungano na
  2. kwa mambo mengine yote yasiokuwa ya Muungano kwa Tanganyika.
  Kwa uchanganuwo usio na wasiwasi na kwa ufafanuzi mzuri uliomo katika ibara ya iii (a) na ya iya Mkataba wa Muungano; basi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina mamlaka tatu kama ifuatavyo:
  1. Mamlaka ya Zanzibar kwa mambo ya Zanzibar amabyo hayamo katika orodha wa Muungano na ambayo yanashughulikiwa na Zanzibar wenyewe.
  2. Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano kwa mambo ya Tanzania Bara ambayo hayamo katika orodha wa Muungano na
  3. Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano kwa Mambo yote ya Muungano.
  Hizi kisheria ni mamlaka (jurisadictions) TATU, ingawa mamlaka mbili zimewekwa katika mfumo mmoja – yaani katika Katiba moja na ile ya tatu
  Katika Katiba nyengine. Kwa maana hii, hapa hapana suala la serikali moja kama wale wasioona wanavyofikiria. Serikali moja hutokea mara nyingi, ikikwa nchi moja imeilazimisha nchi nyengine kuwemo ndani ya mamlaka hio ambapo nguvu zote za mamlaka huwepo katika serikali iliyolazimisha. Mkataba wa Muungano kamwe hausemi hivyo na wala haujaulazimisha Serikali ya Zanzibar au ile ya Tanganyika.

  Pia hapa suala la serikali za majimbo halipo kwani Muungano wa aina hii huzifanya nchini wanachma kuwa na nguvu zaidi nchini mwao kuliko Muungano wenyewe kama unayoonekana Muungano wa “European Union”.
  Lakini Zanzibar na Tanganyika zimeanzisha Muungano wa kisiasa na kila nchi kubakia na utawala wake wenyewe isipokuwa mambo maalum yaliyoainishwa katika mkataba wao kama alivyoelezea Aboud Jumbe katika kitabu chake “The Partner-ship” Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Miaka 30 ya Dhoruba, (ukarasa wa 22-24).
  Uzito wa namna ya serikali ulivyokusudiwa pia umeelezewa na Nyerere mwenyewe katika maeneo tofauti. Mfano mzuri ni kama huo tulioutoa hapo juu kwa Nyerere aliponukuliwa na gazeti la London Observer hapo tarehe 20 Aprili 1968 kwa kusema kwamba hatomlazimisha mtu yeyote katika kuukubali Muungano huo na kwamba muungano huo utasita pale tu nchi shiriki zitapoamua kujiengua.
  (Tizama kitabu cha “Zanzibar and the Union Question, Sura ya 3 ilioandikwa na Wolf Dourado uk. 84.)
  Ni dhahiri basi Mkataba wa Muungano umeweka wazi kuwepo kwa serikali tatu, ya Muungano, ya Tanganyka na ya Zanzibar. Kwa maana hiyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara 64(1),(2) na (5) nayo inaweka mwega mzito ya kuwepo kwa mamlaka (jusisadiction) hizo tatu. Labda watekelezaji wa sehemu hii ndio wenye matatizo. Ni kweli tuna Katiba mbili lakini ni kweli zaidi kuwa tuna serikali tatu. Vile vile Mkataba wa Muungano kamwa haukuifuta serikali ya Tanganyika wala Katiba ya Tanganyika na hivyo kuonesha wazi kuwa wakati wa Muungano kuliwepo na serikali za nchi ya Tanganyika , nchi ya Zanzibar na seikali ya Muungano wenyewe. Kosa kubwa lililofanywa kikatiba ni kwa sheria Na. 22 ya 1964 ya Bunge la Tanganyika (Sheria ya kurekebisha Makubaliano ya Muungano) na kuitwa “The Union of Tanganyika and Zanzibar Act”, ilipoiondoa Katiba ya Tanganyika kwa kutumia madaraka yasiokuwa yao na ambapo ni kinyume na utaratibu wa kikatiba.( tazama vifungu 5(2),(3),8.) Hapa watekelezaji wa Katiba pia walikosea sana.

  MGOGORO MWENGINE WA KATIBA KATIKA MAHAKAM YA KATIBA YA JAMHURI WA MUUNGANO
  Suala la Mahakama ya Katiba nalo ni tatizo linalokwaza Muungano wetu. Uanzishwaji wa Mahakama hio umepwe umuhimu wake katika Katiba zote, kama inavyoelezewa katika ibara 125-128 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ibara 124(2)(a) ya Katia ya Zanzibar ya 1984. Lakini haijuilikani kama Mahakama hii ni ya Muungano au la maana haikuelezewa katia nyongeza za kwanza ya Ibara ya 4 inayohusu mambo ya Muungano.
  Mamlaka ya Mahkama hii ni kusikiliza na baadae kutoa maamuzi ya upatanishi (reconciliatory decisions) kwa yale mambo yanahusu tafsiri ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serkali ya Mapinduzi za Zanzibar (Ibara ya 126(i) ya Kaiba ya Jamhuri ya Muungano). Kwa maana hiyo, kifungu hiki kinaondoa malalamiko mengine yeyote yanayohusu mambo mengine ya Muungano. Hii nayo ni dosari na kasoro kubwa. Pia hamna maelezo yeyote yanayohusu “ugomvi” au maatizo yatayotokea baina ya Tanzania Bara (Tanganyika) na Zanzibar, na pindi yakitokea yatasawazishwa na chombo gani. Au hii imefanywa makusudi kuonesha kuwa Tanganyika haipo? Yeyote aliefanya hivi basi alikwenda kinyume na matakwa ya Katiba na hakuwa na uhalali wowote ule.
  Mahkama itakuwa na wajumbe wataoteuliwa na Serikali ya Zanzibar na wajumbe kama hao wataoteuliwa na Serikali yaJamhuri ya Muuungano. (ibara ya 127(1). Zanzibar inaweza kumteua mtu kutoka Bara na Tanzania Bara inaweza kumteua mtu kutoka Zanzibar, kama inavyofanywa mara kwa mara katika baadhi ya taasisi. Sasa ikiwa suala lililoletwa mbele ya Mahkama hii linahusu mambo ya Muungano. Jee, Tanzania Bara ndio itatetea maslahi ya Zanzibar katika suala hili?
  Suala la aikidi (quorum) ni wajumbe waote, na pale anapopungua mmoja basi lazima ajazwe na upande uliopungua . Uamuzi, ambao unachukuliwa kwa angalau kila upande utapokubali kwa theluthi mbili ya wajumbe wake nao unaleta mashaka ya kupata uamuzi wa kihali ; maana kila upande utapendelea sehemu yake unakotoka (Tizama kitabu cha Zanzibar and the Union Question, sura ya 2 ilioandikwa na Abubakar Khamis Bakary, uk 13-14).Kutokana na migongano hii ni dhahiri kuwa Mahkama hii haiwezi kufanya kazi vilivyo. Prof. Shivji hakukosea pale aliposema ndani ya Kitabu chake – Pan Africanism or Pragmatism – lessons of Tanganyika – Zanzibar Union, kuwa:
  “………Haiwezekani kuwa na Mahkama maalum ambayo akidi (composition) yake si sawa sawa baina ya wa- Bara na wa anzibar. Kwa kifupi, Mahakama haiwezi kufanya kazi. Pengine haikutakiwa kamwe ifanye kazi”
  (cap. 5 p. 180).
  Huu ni ukweli usiopingika.
  ZANZIBAR NA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI
  Kila mmoja wetu, na katika nchi zetu, sote tunauhitaji umoja huu.Wadau wote wangalipenda kwanza tuanze na misingi ilio bora zaidi na yenye uhakika wa kuhimili vishindo. Ni hapo tu, ambapo watu wa nchi hizi wangaliweza kufurahia uhuru ulio mpana zaidi kwa kuwa na uendeshaji wa kidemokrasia wa chombo hiki. Bila shaka hatimae kingetoa fursa sawa kwa wananchi wa nchi zote tatu wakiwemo na wananchi wa Zanzibar ambao nao kuna mambo mengi wanayopaswa kuyashughulikia wao wenyewe kama nchi na ambayo hayamo katika orodha ya mambo ya Muungano na hivyo basi kutokushughulikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.Umadhubuti wa aina hii ndio utaofanya hata nchi jirani kutuonea wivu na wao kushawishika kutaka kujiunga na umoja huu.
  Kwa maana hiyo basi ninahisi kwanza tungelitazama matatizo yetu yaliopo na kuyatatua na baadae kufanya shirikisho lililo madhubuti zaidi . Baadhi ya mambo muhimu ya kuangaliwa ni pamoja na:-
  a) Kuweka bayana mambo ambayo Zanzibar, kama nchi inayoshughulikia mambo yake yasiokuwa ya Muungano, watayashughulikia wenyewe.
  b) Vipi ikiwa mambo hayo yatashughulikiwa na Jamhuri ya Muungano pale ambapo masuala hayo sasa yamewekwa kuwa miongoni mwa shughuli za umoja huo.
  c) Mgao wa faida na hasara kwa nchi hizi tatu katika Jumuiya na vipi Zanzibar itafaidika au itahasirika kutokana na faida au hasara hiyo.
  d) Vipi mambo kama yale ya Bunge la Afrika Mashariki, au Mahkama ya Afrika Mashariki zitakuwa na uwakilishi unaokubalika kwa Zanzibar hasa ukitilia maanani kuwa masuala ya Bunge na sheria si mambo hasa ya Muungano na hivyo basi uwakilishi huo wa Zanzibar usifanywe na chombo cha Muungano kama vile Bunge.Utaratibu huu wa Bunge la Jamhuri kuchaguwa wabunge kutoka Zanzibar kuiwakilisha katika Bunge la Afrika ya Mashariki ndio unaofuatwa hivi sasa, utaratibu ambao ni maonevu matupu kwa Zanzibar.
  Kwa maana hiyo basi kutakuwapo na migongano ya wazi baina ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa mambo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika yale mambo ambayo si ya Muungano.Ni maoni na mapendekezo yangu kwamba ni vyema kuyasawazisha mambo haya ambayo ni makubwa na mazito ili hatimae yasije yakaleta tofauti zisizokuwa za lazima.

  KATIBA NA MKATABA WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI – NAYO NI MIGONGANO MITUPU
  Kila mtu anaielewa vyema Ibara ya 4(3) na Nyongeza ya Kwanza ya Ibara hio inayoelezea mambo ya Muungano na yale yasiyokuwa ya Muungano. Orodha hiyo ya mambo 22(!) ambayo kwayo ina utata inayatoa mambo mengi kuwa si ya Muungano.
  Mambo hayo ambayo si ya Muungano, sasa yamewekwa chini ya mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwa maana hiyo kwamba yatashughulikiwa na Serikali ya Muungano. Kwa maana nyengine pana, kubwa na ya wazi ni kuwa , Zanzibar yenye mamlaka ya kushughulikia mambo hayo yasiyokuwa ya Muungano kwa maslahi ya Zanzibar na watu wake, sasa imepokonywa mamlaka hayo na kuambiwa kwamba sasa mambo hayo ingawa si ya muungano lakini yanashughulikiwa na Serikali ya Muungano kwa niaba ya Zanzibar. Hatuoni kwamba sasa tunakwenda kwenye hadithi ya mchungaji na ngamia wake alipomkaribisha ngamia huyo kuficha baridi yake sehemu ndogo ya kichwa na mwili wake? Lakini sasa inaonesha wazi kuwa mambo hayo yameshaingizwa ndani ya kundi la mambo yanayoshughulikiwa na Jamhuri ya Muungano,yaani sasa ni Mambo ya Muungano kwa mkono mwengine! Cheche hii ilioanguka kwenye majani makavu inaweza wakati wowote kushika moto.Tutahadharini.
  Kwa kifupi mambo aina hiyo ni pamoja na yafuatayo:-
  Ø Ibara ya 24 ya Mahkama ya Jumuiya ambayo inahusiana na uteuzi wa Majaji wa Mahkama ya Afrika ya Mashariki. Zanzibar tunasubiri furaha ya Rais wa Jamhuri (at the pleasure of the president) tu ndio tuweze kuteuliwa.
  Ibara ya 48 ya
  Ø Mkataba ambapo haitoi uwakilishi wa wabunge wa Jumuia kwa Zanzibar na kwamba hata Bunge la Muungano suala hili halikuona haja angalau na nafasi tatu kupelekwa Zanzibar kwa kupatikana wajumbe wataochaguliwa na Baraza la Waakilishi.
  Mfumo wa sasa wa Bunge ni kuwachagua Wazanzibari watakaowakilisha Zanzibar katika Bunge hilo la Afrika Mashariki.

  • Ibara ya 76 ya uanzishaji wa soko la pamoja (common market)
  • Ibara ya 79 kuhusu uendelezaji wa viwanda
  • Masuala ya uendelezaji wa miundo mbinu kama ulivyoelezewa katika Sura ya 15 ya Mkataba huo wa Afrika ya Mashariki.
  • Elimu na Mafunzo (Ibara ya 102)
  • Ibara ya 105 inayohusu chakula na usalama wake, mifugo (107) udhibiti wa maradhi ya miti na mifugo (108). Umwagiliaji maji (109)
  • Mazingira (177)
  • Utalii na wanyama pori (ibara ya115), Afya (118), Mila na utamaduni (119 na 120) na mengi mengineyo.
  Mambo ambayo nimeorodhesha hapo juu yanahitaji uangalifu mkubwa jinsi ya kuyashughulikia. Hii ni kwa sababu Zanzibar inayotakiwa iwashughulikie wananchi wake katika masuala haya wamenyanganywa madaraka hayo na hivyo kuwa yanashughulikiwa na chombo chengine (Jamhuri Muungano) ambacho hakihusiki. Suala hili ni kwa nini? Utata huu hautoifanya Zanzibar kukosa haki zake za Jumuiya? Kwa maana hiyo hapatokuwa na mgogoro wa Jumuiya ndani ya Tanzania na hivyo kukuza matatizo au kwa jina maarufu kero za muungano ambazo hadi hii leo hazijapatiwa ufumbuzi? Kwa maana hii, Katiba ya Jamhuri na Mkataba wa Jumuiya imesaidia sana kuendeleza migongano iliopo ya kikaiba na kuikosesha Zanzibar haki yake ya kuwatumikia wananchi wake (wa-Zanzibari ) kwa yale mambo ambayo si ya Muungano na kila upande wa Muungano kutakiwa kikatiba kuyashughulikia wenyewe. Mifano ndio hio ya barabara, kilimo, elimu, uvuvi, afya mifugo, mila na utamaduni, utalii na kadhalika.
  SASA WAZANZIBARI TUFANYEJE?
  “Ngome intuumiza………………. Naswi tumumo ngomeni………..”
  (Na Abdilatif Abdulla katika kitabu chake “Sauti ya Dhiki)

  Migogoro tulioielezea katika makala hii, ingawa sio yote, inaelezea mambo mawili makubwa. Kwanza ni kuwa Katiba zetu, pamoja na Makubaliano ya Muungano zina mapungufu mengi ambayo yanatokana na uandishi wenyewe wa Katiba hizo pamoja na sheria zake zinazohusiana na hayo.
  Pili, tumeona kuwa baadhi ya watekelezaji wenyewe nao wanahusika na wamechangia pakubwa katika kukoroga mambo.
  Kwa maana hiyo basi, mimi binafsi ninaamini kuwa mgogoro wa Kikatiba, Tanzania ni matunda yanayotokana na mchanganyiko wa uandishi wa baadhi ya vifungu na ibara zenye matatizo (ambiguous clauses) na vilevile kwa na baadhi ya watekelezaji wa Katiba hizo kutokuwa na moyo wa uzalendo wa utekelezaji mzuri wa matakwa ya Katiba hizo.
  Kwa hiyo, Katiba zetu zenye utata sisi wa – Zanzibari zinatuumiza, na kama alivyosemaAbdillatifa Abdulla, bado na sisi tumo na tunaendelea kuzitumia Katiba hizo zilizojaa mazonge!. Hili ni tatizo, na sasa jee tufanye nini? Tubakie tukiumia au tutafute ufumbuzi?

  UFUMBUZI GANI ?
  Abraham Lincoln aliekuwa Rais wa Marekani alisema kwamba “Nyumba iliogawika ndani yake haiwezi kusimama……”.
  (Abraham Lincolln – springfiled llinois 17-6-1851 An outline of an American History pg. 76)

  Kutokana na wasia huo. “Wazanzibari waliogawika hawawezi kabisa kuijenga Zanzibar yao” Ni lazima tuwe kitu kimoja, tuwache ushabiki wa vyama na wakisiasa na sote kwa pamoja tushabikie Zanzibar yetu. Ni lazima tuwe wazalendo kwa Zanzibar yetu.
  Dhana hii ya uzalendo (patriotism) ndio itakayo tuokoa. “Patriotism” ni neno linalotokana na neno la Kilatin (baba) ambalo ni “pater”. Hili limezaa (patriotism) (kwa Kiingereza) – yaani uzalendo. Uzalendo ni mapenzi ya nchi ya baba, kuitumikia kwa dhati nchi ya baba. Maana yake basi ndio kuipenda nchi yetu Zanzibar kwa hali na mali; na kuwa tayari kufa kwa ajili ya kuitetea nchi yetu. Hivyo ni lazima kwa wa-Zanzibari wote ndani ya Zanzibar na nje ya Zanzibar wawe na mtazamo huo wa umoja na upendo katika kujenga nchi ( Zanzibar ) yao. Na hili ndilo linalohitajika.

  Baada ya kuwa na uzalendo jambo muhimu hapa ni makubaliano ya pamoja (consensus). Suala hili ni muhimu katika kutatua matatizo (conflicts) na katika kuimarisha demokrasia na usalama wanchi. Vile vile uzalendo mkubwa unahitajika kwa lengo la kuweka ushabiki wa vyama upande, na wakati wote ule nchi yetu Zanzibar iwe ya mwanzo. Makubaliano ya pamoja inamaanisha fikra zilizo sawa na zinazolingana, inamaanisha vile vile mwelekeo wa pamoja wenye lengo la kuleta mafanikio hapo baadae. Silazima makubaliano haya yawe asilimia mia moja (100%), lakini inatosheleza kabisa ikiwa angalau idadi kubwa ya wa- Zanzibari wanakubaliana na mawazo hayo. Hivyo moja ya kazi kubwa tulionayo ni ya kuwaelimisha wananchi wetu kuhusu umuhimu huu wa kubadilisha Katiba na kwa hili ni lazima tuungwe mkono na walio wengi.
  Katika kufanya hivyo ammbo yafuatayo ni lazima kuyatekeleza.
  • Kuuhamasisha umma kwa mazungumzo ya wazi kuhusu mambo ya Katiba
  • Kuwe na chombo cha pamoja kuhusu uhamasishaji huo
  • Kuwe na uhakika kwa wananchi kuwa Katiba hio itakuwa ni Katiba ya watu
  • Kuwe na uhakika kuwa matakwa yao yatazingatiwa katika Katiba, na
  • Kuwe na mabadiliko ya kikweli kweli katika Katiba hizo, mabadiliko ambayo yatatatua kwa kiasi kikubwa vile vilio vya wa- Zanzibari vinavyohusiana na maonevu yanayofanwa kwa nchi yao na vizazi vyao.
  Ni lazima ieleweka vile vile kua kazi hii si rahisi. Inahitaji muda mwingi na pia fedha nyingi ili kutayarisha mikakati nilioielezea hapo juu. Shughuli hii ni lazima iwe na nguvu za umma na si za wanasiasa tu. Ni lazima wengi wetu wapatiwe nafasi ya kutoa maoni yao ambayo yatakidhi ile haja ya kuwa na Katiba ya watu kwa ajili ya watu, Katiba ambayio itakuwa na mwelekeo wa kudumu kwa faida pia ya vizazi vyetu.
  Zaidi ya hayo ni lazima basi Katiba hii iwe na mizizi yake kutoka hapa hapa nyumbani kama zilivyo Kaiba za Guyana na Papua Guinea.
  Hapo tena ndio kutakuwa na haja ya kuandikwa kwa Katiba mpya ya Tanzania kwa lengo la kuyatatua matatizo hayo tuliyoyaona hapo juu, au na matatizo mengine yote yatayojitokeza hapo baadae.Vile vile tuchukueni nafasi hii hii kwa ajili ya kutoa mapendekezo ya mabadiliko au ya marekebisho ya Makubaliano yetu ya Muungano kwa ajili ya kuuimarisha zaidi muungano wetu.
  Kazi ya kutayarisha Katiba mpya ni ngumu, njia yake ni refu na gharama zake ni kubwa. Kazi hii inataka juhudi kubwa za wana siasa pamoja na makubaliano ya wananchi wenyewe. Lazima pia pawe na elimu ya kutosha kwa walengwa wote ili waelewe hasa ni nini kinachotakiwa. Katiba hio inatakiwa ibebe misingi na mawazo ya hapa hapa nyumbani (home grown), ingawa ni vyema pia kuchota kidogo (to distill) yale mema yanayotokana na Katiba za wenzetu. Si vibaya hapa kama tutazitaja Katiba chache ambazo ingepaswa kuangaliwa kwa makini ili tuweze kufaidika na demokrasia iliomo ndani ya Katiba hizo. Katiba hizo ni pamoja na Katiba ya Afrika ya Kusini, Namibia, Rasimu ya Katiba ya The Bomas ya Kenya, Katiba ya Maccao ,Finnland, Papua New Giuinea, Katiba za visiwa vya West Indies kama vile Barbados, Jamaica na Trinidad na Tobago, Katiba ya India, Australia, Marekani na nyingi nyenginezo ambazo kwa kweli zimeweka bayana matarajiao ya watu wanchi zao. Katiba nyengine pia zinaweza kutufunza mambo mabli mbali ambayo nayo tunaweza kuyapima ikiwa nayo yanafaa kuwemo katika Katiba yetu au laa. Kwa mfano:-

  1. Katiba Canada na vifungu vyake vya kulinda haki ya matumizi ya lugha
  2. Katiba ya Japan yenye vinfungu vilivyopiga marufuku matumizi ya majeshi kwa njia isio halali
  3. .Katiba ya Fiji ambayo nayo inawalinda watawala wa kijadi (traditional chiefs)
  4. Katiba ya Uswiss ambayo imeelezea kwa vizuri mfumo wa “federation” na vipi mabunge yake mawili yanalinda mfumo huo
  Kwa kumalizia, nawaombeni nyote mnaohusika kwamba msivunjike moyo. Kazi ya kushawishi watu kukubali kufanya mabadiliko au kuandika upya Katiba ya nchi ni kazi mgumu sana. Ni sawa sawa na kufanya mapenzi na tembo (ndovu). Kazi hii inakaribia kuwa haiwezekani, na hata kama mtu atafulu, basi hakuna chochote kiwacho kwa muda wa miaka miwili! Na baada ya hapo ndio pengine utaona mambo yanaanza kujionesha!. Lakini tuifanyeni kazi hio angalau kwa manufaa ya vizazi vyetu vya kesho.
  Nimejaribu kuchokoza kidogo kuhusu mada hii. Lakini sina uhakika kama nyote mmechokozeka. Hata hivyo ninawashukuru sana sana kwa kunisikiliza. Ninawaombeni tuyajadili matatizo haya na tumalizie mjadala wetu huu kwa kuwa na mikakati madhubuti ya kujikwamua na kuondoka ndani ya ngome hii inayotuumiza. Nina hakika tunaweza – tujaribuni !

   
 2. K

  Kipre tchetche JF-Expert Member

  #2
  Jan 24, 2011
  Joined: Dec 13, 2010
  Messages: 238
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Ni viongozi wa vyama tawala kutumia
  madaraka Yao kuiba ,kuharibu,kutomtetea
  mwananchi
  wa kawaida na kuruhusu kundi dogo
  liwatawale walio wengi kimabavu na
  kuwanyima uhuru wao wa kujieleza
  pamoja na kutumia muda mwingi wawapo
  madrakani kujilimbikizia Mali wakiwanyanganya
  wajane na yatima.
   
Loading...