Mgogoro wa ccm aibu kwa taifa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mgogoro wa ccm aibu kwa taifa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Pdidy, Nov 14, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Nov 14, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,151
  Likes Received: 5,585
  Trophy Points: 280
  Mgogoro CCM aibu ya Taifa

  [​IMG]
  Lula wa Ndali-Mwananzela​
  Novemba 11, 2009[​IMG]

  WAPO wanaofurahia na kuchekelea mgogoro unaoendelea ndani ya CCM. Wapo ambao wanaombea kuwa mgogoro huo uendelee ili hatimaye CCM imeguke na labda vyama vya upinzani vitapata nafasi ya kukubalika; wapo ambao wamekaa pembeni na popcorn zao wakiangalia onyesho la maigizo na filamu isiyoisha ambao nyota wake ni viongozi wakubwa tu wa CCM!
  Na tupo sisi wengine ambao tunajua kuwa ni vizuri CCM kumeguka ili Taifa lipone na tunajitahidi kuharakisha kumeguka huko. Hata hivyo, tusipoangalia sisi sote tutakuwa kama fisi anayenyemelea mkono wa mtu udondoke ili ajipatie kitoweo.
  Hayo yote tisa; kumi ni kuwa kinachoendelea sasa hivi ndani ya Chama cha Mapinduzi na Serikali yake ni aibu, na tena ni aibu mara nne kwa taifa letu.

  Ni aibu ya wanaolumbana na kupeana mipasho, ni aibu ya uongozi wa juu wa CCM na wana CCM, ni aibu ya familia zao na ni aibu ya Rais Kikwete. Kwa kila kipimo hatuwezi kuendelea kuchekelea aibu hii na kudhania kuwa kwa kufanya hivyo tunaita baraka kwetu. Lakini kama msemo wa Kiingereza usemao kuwa “the chickens have come home to roost” yaani “kuku wamekuja nyumbani kutamia” yaani kuvuna kile mtu alichopanda.
  CCM ilipulizia migogoro kwenye upinzani
  Tangu kurudi kwa mfumo wa vyama vingi na hasa uwepo wa vyama vya UMD na NCCR MAGEUZI, tunakumbuka vizuri sana jinsi gani vigogo wa CCM walivyokuwa kifua mbele kuvibeza vyama hivyo na pale migogoro ilipokuwa inatokea ndani ya vyama hivyo CCM haikuchelewa kupiga panda la kutangaza kwanini vyama hivyo havifai! “Wana migogoro ya viongozi hawa” walikuwa wanatuimbia kila kukicha.
  Wale walioamini wakaendelea kuichagua CCM kwa sababu CCM ilionekana imetulia, sera zake murua na ni yenye umoja wa ajabu. Waliovaa magwanda ya njano na kijani wakichezacheza na kofia zao zenye alama ya jembe na nyundo waliimba kwa furaha “CCM nambari wani”. Leo hii hakuna anayethubutu kufanya hivyo tena.
  Hata wale waliokuwa na kimbelembele cha kuandamana kila Kamati Kuu ikifanya jambo, Rais akikoa au Mwenyekiti akisema kitu cha kusisimua, leo wamejificha katika aibu yao kwani hawaamini kile chama cha Mwalimu kimefikia kilipofikia. Kumbe ukipanda migogoro kwa wenzako na wewe utavuna migogoro!
  Ndiyo maana nasema yanayoendelea leo ni aibu. Si kuku waliwaachilia wenyewe, na sasa wanatamia!? Turudi kwenye zile aibu nne.
  Aibu ya wanaolumbana
  Mambo tuliyoyasikia na kauli tulizozisikia na kuzisoma zinatufanya tuinamishe vichwa vyetu kwa masikitiko. Yale ambayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayesimamia Utawala Bora, Bi. Sofia Simba anadaiwa kusema kama ndivyo alivyoyasema na kama mashambulizi dhidi ya viongozi wenzake ndivyo yalivyokuwa, basi ni aibu!
  Wengine tumebakia kujiuliza inakuwaje huyu bado yuko serikalini na kwenye chama akiendelea kupeta kama mbingu na nchi ni vyake!?
  Maneno ya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu ambaye naye aliwahi kukutana na songombingo Dodoma kwenye sakata la Tanganyika kuwa Bi. Simba anahitaji kupimwa akili yake kwa wengine yanachekesha; lakini kwa sisi wengine yanasikitisha.
  Ina maana Mzee Malecela alikuwa ana maana kwenye Baraza la Mawaziri kuna kichaa? Kwamba mmoja wa mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wetu ana matatizo? Sasa kama anajua hilo, kwanini asimuambie Rais wake kwa heshima zote badala ya kumpaka mama huyo hadharani jinsi hiyo?
  Au anataka kutuma ujumbe kwa Kikwete kuwa amechagua vichaa? Aibu! Lakini itakuwaje kama ilimbidi aseme hivyo kwa sababu ndivyo anavyoona mambo yanayoendelea?
  Ukisoma majibu ya Mzee Mengi kwa Bi. Simba ni kitu kile kile. Nilijiuliza kulikuwa na ulazima gani kwa mzee Mengi kumjibu Bi. Simba na pasipo huruma kutoa shutma kuwa yanayosemwa juu yake ni uongo na kumpa maelekezo Bi. Simba ya nini cha kufanya? Na yeye alikuwa anamtumia ujumbe Rais Kikwete kuwa waziri wake wa Usalama wa Taifa anatumia madaraka yake vibaya kunyanyasa raia? Kwanini na yeye asiamue kutumia njia za moja kwa moja kutuma ujumbe huo? Ni aibu tu ndugu zangu.
  Ni aibu ya uongozi wa juu wa CCM na wana CCM
  Pamoja na yote ambayo tunazungumzia leo hii, upuuzi (ninamaanisha hilo) unaoendelea CCM leo hii usingeweza kabisa kutokea wakati wa uongozi wa Mwalimu. Leo hii uongozi wa juu wa CCM umegawanyika, Mwenyekiti hana ubavu na walio chini yake; Kamati Kuu imegawanyika, Halmashauri Kuu imegawanyika, matokeo yake hata wanachama nao wamegawanyika.
  Watu wako chama kimoja kwenye Bunge moja lakini hata kuzungumza hawazungumzi. Mwenyekiti wao ameshadai kuwa imefika mahali watu hawaachiani gilasi za maji kwa kuogopa kuwekeana sumu! Hii ni aibu ya uongozi wa juu wa CCM!
  Ina maana ndani ya CCM hakuna tena chombo chenye uwezo wa kulazimisha nidhamu na mijadala ya kiutu uzima kuliko vituko tunavyoshuhudia leo hii? Ni aibu!
  Ndiyo, ni aibu kwa wanachama wa CCM ambao leo wanajibaraguza kwa kudai kuwa ya kwao ni demokrasia lakini ikitokea CHADEMA, TLP, CUF ni mgogoro!
  Leo wanachama wa CCM hawana pa kuficha nyuso zao kwani yale “matatizo ya uongozi” yaliyokuwa yanaimbwa na kuhubiriwa sasa yanatokea ndani ya chama chao; na wao wanaaibika! Wenyewe wanataka tuamini ati ni “demokrasia ya chama”! Hiyo demokrasia ya migogoro inaruhusiwa ndani ya CCM tu lakini si kwenye upinzani?
  Angalau wapinzani wanaweza kukaa meza moja na angalau wao walikuwa na uwezo hata wa kutimuana na kufikishana mahakamani! CCM kufukuzana hawafukuzani, kukaa pamoja hawataki, kumeguka hawameguki, yaani wapo wapo tu! Hii ni aibu!
  Aibu ya familia zao
  Hili hata sitaki kuingia kwa undani kwani hawa jamani ni wazazi, wengine ni wajukuu na wana vitukuu! Leo watu wazima na akili zao na wengine wahenga wangeweza kusema “wamekula chumvi nyingi” lakini wanavyozungumza kimipasho na kigangwe wanashindana na wachuuzi Kariakoo na waimba taarabu wa enzi zile!
  Sijui watoto wao huko waliko wanajisikiaje ati “mama apelekwe Mirembe”! Jamani, hata kama hamjiheshimu nyinyi wenyewe angalau kumbukeni familia zenu.
  Watu wazima wanaitana waongo, wazushi, sijui madubwasha gani kweli jamani CCM mmefika hapa na hamsikii aibu yoyote wala soni? Mmevipoteza wapi vitu hivi? Au ndo mmelewa madaraka hadi hamuoni aibu; maana walevi hawana haya!
  Aibu ya Rais Kikwete
  Kati ya yote ambayo yananigusa sana ni kuwa yanayotokea ndani ya CCM leo hii na serikali yake anayeaibika zaidi ni Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho. Leo hii amegeuzwa kuwa hana umuhimu ndani ya chama. Angalia kile kilichomshinda Zanzibar katika muafaka Wazanzibari wameamua kufanya wenyewe na sasa Maalim na Karume wamepatana huku Kikwete akihangaika na wawekezaji wake!
  Ni aibu ya Kikwete kwa sababu tayari ana matatizo chungu nzima kwenye baraza lake. Mawaziri wenye digrii feki, mawaziri wanaodai serikalini kuna wabinafsi na wezi (utadhani wao hawako serikalini!); mawaziri wenye kutumia madaraka vibaya. Yaani, ukiangalia baadhi ya teuzi zake hadi unajiuliza hivi kweli yupo au kuna mtu mwingine anafanya teuzi hizi.
  Kilichonikata mimi maini ni pale alipoamua kumrudisha Andrew Chenge kwenye baraza lake kiasi kwamba hata Chenge mwenyewe ilibidi aseme “muulizeni Rais” alipoulizwa na mwandishi mmoja kwa nini anafikiri amerudishwa madarakani licha ya tuhuma dhidi yake. Wiki chache baadaye akajikuta analazimishwa kujiuzulu katika sakata lile la “vijisenti”.
  Leo, Mwenyekiti wa Chama hana ujiko (clout) ndani ya Chama chake mwenyewe. Inapofikia aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama anahoji uwezo wa Rais kuteua Waziri ujue tumefikia pabaya. Malecela anapomtuhumu Sofia Simba kuwa ana matatizo kichwani moja kwa moja anahoji utimamu wa yule aliyemteua! Haiwezekani aliyeteuliwa awe fyatu na aendelee na nafasi yake bila ya kuhoji uwezo wa aliyemteua kupima wateuliwa wake! Hii ni aibu!
  Ninamuonea huruma Rais Kikwete kwa sababu sidhani kama alitarajia kuwa urais unakuja na mambo haya yote. Wakati mwingine nafikiria (sijui kama ni fikra au imani) kuwa yawezekana Rais Kikwete aliutaka urais ili atimize ndoto yake tu na siyo urais kama jukumu la uongozi.
  Leo hii Rais hatoi uongozi unaotakikana kwa nchi wala kwa chama chake na badala yake anafuata. Viongozi wenzake wanagongana, kuumbuana na kutoboana macho yeye huyo katimka kwenda Misri katika safari zile za ki-Vasco da Gama nilizosimulia wakati ule.
  Sasa, tusipoangalia tutajikuta matatizo makubwa endapo Rais hatoamua kuleta nidhamu kwenye serikali yake kwanza na pili kwenye chama chake. Hatuwezi kuwa na watendaji serikalini ambao wanatenda bila kuonesha uungwana, weledi, utaalamu, nidhamu na wito wa kazi ya Watanzania. Kama kila Waziri anajisema kivyake vyake na kama kila mmoja anatumia nafasi yake kujipatia taarifa za wabaya wake, basi tumekwisha.
  [​IMG]

  Rais Kikwete
  Nina pendekezo hata hivyo. Kama Rais Kikwete anaona mzigo wa serikali na wa chama ni mzito mno kwake, na kuwa haya yanayotokea kwa kweli yamemzidi, basi anaweza akafuata kile ambacho Katiba imeweka; yaani ajiuzulu nafasi yake na Dk. Shein atapanda ngazi na labda yeye atajaribu kuleta nidhamu.
  Kama wote wawili wanaona mambo haya ni mazito kwao, na hawana njia; basi Rais aamue kuitisha Uchaguzi Mkuu mapema (labda Machi mwakani) na yeye asigombee ili hawa walioko CCM wanaogombana kila kukicha watoane ngeu hadi mmoja wao ashinde na tuanze naye upya!
  Vinginevyo, chonde Rais Kikwete onesha uongozi kwa taifa lako; kwani mzigo huu uliupigia magoti wewe mwenyewe. Kama unaona tunakukera na kukusumbua, basi, unaweza kuamkua kujipumzisha mapema. Hiyo nayo ni sehemu ya demokrasia.
  Vinginevyo, aibu yenu CCM mmeifanya kuwa ni aibu ya Taifa zima. Lakini itabakia yenu peke yenu kama vile yale ya wapinzani yalikuwa ni ya kwao na haya ya kwenu mtayabeba wenyewe!
  [​IMG]
   
 2. Freetown

  Freetown JF-Expert Member

  #2
  Nov 14, 2009
  Joined: Apr 6, 2008
  Messages: 887
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 35
  Mgogoro CCM ni mzuri kwa Taifa, ili chama kigawanyike, kuwepo na CCM Mageuzi na CCM Asilia. nani wakuwepo katika hivyo vyama viwili kila mtu anajua
   
Loading...