Mfuko wa Obama wazindua mradi wa tohara kwa wanaume Mwanza

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani, Barack Obama, chini ya mpango wa kudhibiti magonjwa ya zinaa (CDC), imezindua mradi wa tohara kwa wanaume mkoani Mwanza.

Mradi huo umelenga kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na unatekelezwa katika mikoa inayozunguka Ziwa Victoria.

Katika Mkoa wa Mwanza mradi huo unatekelezwa kwenye baadhi ya visiwa vya wilaya za Sengerema na Ukerewe ambavyo vina mwingiliano mkubwa wa watu kutokana na shughuli za uvuvi.

Akizindua mradi huo mwishoni mwa wiki kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Ndikilo, Mkuu wa Wilaya Sengerema, Elnass Pallangyo, alisema mradi huo unapunguza maambukizi kwa asilimia 60.

Aliwataka wanaume wa kisiwa cha Kome kujitokeza kwa wingi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo.

Pallangyo alisema Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa minane inayokabiliwa kwa kasi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa asilimia 5.6 na kwamba hali ni mbaya zaidi kwa jamii zenye shughuli za uchimbaji wa madini na uvuvi.

Mkurugenzi wa CDC kwa niaba ya watu wa Marekani, Dk. Michelle Roland, alisema mradi wa tohara kwa wanaume barani Afrika unatekelezwa katika nchi mbili za Kenya na Tanzania.

Alisema ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Marekani, unalenga kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutokana na utafiti uliofanyika na kubaini kuwa mwanaume ambaye hajafanyiwa tohara ni rahisi kuambukizwa na kuambukiza ugonjwa huo.

Dk. Roland alisema tangu kuanza kwa kampeni hiyo, wananume 2,600 wa kuanzia umri wa miaka 10 wamepatiwa tohara hapa nchini katika mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera ambapo mkoani Mwanza kampeni hiyo inasimamiwa na huduma ya kuzuia maambukizi ya Ukimwi Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Akisoma taarifa ya hali ya maambukizi ya Ukimwi wilayani Sengerema, Mganga Mkuu, Dk. Boniventure Ndaki, alisema katika kipindi cha mwaka jana, watu 22,850 kati yao wanaume 8,262 na wanawake 14,588 walijitokeza kupima virusi vya ungojwa huo na waliobainika kuwa na maambukizi ni 1,308 ambapo kati yao wanaume ni 428 na wanawake 880.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom