Mfanyabiashara Makambako anunua kijiji

Mfanyabiashara Makambako anunua kijiji

sulphadoxine

JF-Expert Member
Joined
Nov 1, 2010
Posts
2,257
Reaction score
649
Wananchi wote kutimuliwa kupisha mradi wa miti

Aonya watakaogoma kuondoka kufunguliwa kesi polisi



MFANYABIASHARA mmoja katika Mji Makambako wilaya ya Njombe, mkoani Njombe, Ben Muyamba, amelalamikiwa na wananchi wa kijiji cha Usetule kutumia vibaya fedha zake, hila na ubabe kujimilikisha eneo la kijiji hicho, katika Kata ya Mahongole.



Hata hivyo, wananchi hao wamedai malalamiko hayo kwa mfanyabiashara huyo, yanakwenda sanjari na aliyekuwa Mwenyekiti wa serikali ya kijiji chao James Gadau, anayedaiwa kuwa mshiriki wa Muyamba kujitwalia eneo hilo kwa njia za hila.

Habari za uhakika zilizopatikana mjini Makambako zinasema kuwa hatua ya kiongozi huyo wa kijiji kushiriki hila za kuliuza eneo hilo kwa Muyamba, zilipangwa kwa muda mrefu japo zilikutana na pingamizi kutoka kwa wananchi.

Hata hivyo, habari zinasema kuwa wananchi walitishiwa kuwa wanaweza kujikuta wakishtakiwa mahakamani kwa kosa la kuzuia mwekezaji kuendelea na shughuli zake katika kijiji hicho, hatua iliyowafanya kuingiwa na woga.

Wakati wananchi wakijirusha hatua kadhaa nyuma kuhofia kauli hizo za mkono wa sheria, Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Chesan Katundu, hakuhofia suala hilo, badala yake alisimama imara kupinga mradi huo hewa katika kijiji chao na kusema kuna mazingira mabaya ya matumizi ya sheria ya ardhi.

Inaelezwa kuwa Muyamba, alitoa agizo tayari kupitia kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho Patrick Kigola, kuwa wananchi wote wanatakiwa kuanza mkakati wa kujiondoa kwenye eneo hilo ili kumruhusu mwekezaji huyo aweze kuanza kutekeleza jukumu lake la kupanda miti.

Hata hivyo, habari zinaeleza kuwa wananchi wanaoonesha nia ya kupingana na na agizo hilo la mwekezaji huyo feki, wanafunguliwa mashtaka polisi kwa kile kinachodaiwa kuwa walizuia shughuli halali zake za uwekezaji.

Inaelezwa kwamba Gadau kabla hajaondoka madarakani, aliahidi kumwekea ulinzi Muyamba, ili asisumbuliwe na watu wakati wa utekelezaji wa mradi wake kwenye maeneo ya kijiji hicho.

Inaelezwa kwamba maeneo yaliyonunuliwa kwa hila na mfanyabiashara Muyamba, hutumiwa na wananchi hao kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji, hivyo hatua ya kuuzwa kienyeji inaweza kuathiri maendeleo yao .

Athari hizo kwa mujibu wa wananchi hao ni pamoja na kuvunjiwa nyumba za makazi ya kudumu walizojenga katika maeneo hayo pamoja na kuendeleza sekta ya kilimo na ufugaji.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa Gadau aliyeonesha nia ya kupinga uamuzi wa kutaka kuhamisha kwa nguvu wananchi katika eneo hilo kwa nia ya kupisha shughuli za ‘mwekezaji’ huyo.

“Alitafutiwa sababu ikiwa ni pamoja na kufunguliwa kesi ya uongo kuanzia katika ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho Patrick Kigola na baadaye, kufikishwa kituo cha polisi Makambako,” alisema mmoja wa wanakijiji hao kwa uchungu.

Inaelezwa kuwa pamoja na kuwepo kwa vitisho hivyo vilivyoonekana kuwa ni jeuri ya fedha, Mwenyekiti wa kamati ya Ardhi ya kijiji hicho Katundu (47), akiungwa mkono na mwananchi mwingine aliyetajwa kwa jina la Sisto Lutumo (44) na Anitha Kaduma walishtakiwa kwa kuhamasisha wananchi wa kijiji hicho kuupinga mpango wa kuuzwa kwa kijiji hicho.

Inaelezwa kuwa Katundu alifanikiwa kupata ushawishi mkubwa na hivyo kuungwa na wananchi, na hivyo kujikuta akijiweka katika uadui mkubwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji hicho Gadau, Afisa Mtendaji wake Kigola na mfanyabiashara Muyamba.

Katika moja ya vikao vilivyofanyika kando ya ofisi ya serikali ya kijiji hicho, kiitishwa na kuratibiwa na kamati hiyo ya ardhi na mazingira ya kijiji cha Usetule mbele ya Tume ya Haki na Amani ya Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe, ikiongozwa na Afisa wake Boneventure Fuime, wananchi waliitaka serikali kuu kuingilia kati.

Wananchi haoo walimlalamikia Muyamba na Kigola, kwa kutumia vibaya uwezo wao wa fedha kutaka kuyumbisha haki za wananchi na kuendesha mambo kwa ubabe, huku wakijua wazi kwamba jamii haitaki suala hilo .

Pia walimlalamikia vikali Diwani wa Kata ya Mahongole John Mwandoloma, kuwa ameshindwa kukemea tabia ya mtendaji huyo wa kijiji, kuanzisha mradi wa kuuza maeneo makubwa ya ardhi bila kufuata sheria.

Lakini walilalamikia hatua ya uuzaji huo kuhusisha eneo lote linalozunguka ofisi ya serikali ya kijiji chao, ikiwa na maana kwamba hata eneo la ofisi hiyo limeuzwa na inatakiwa kuondolewa mara moja kupisha upandaji miti ya mwekezaji.

Hata hivyo, Diwani Mwandoloma alisema hakuwa na taarifa kuhusu kilichotokea kijijini hapo, badala yake malalamiko yao amekuwa akiyasikia kupitia vyombo vya habari, lakini babadaye alionyesha nia ya kuanza kufuatilia ili kujua kilichokuwa kikifanyika.

Diwani Mwandoloma, alisema kuwa hajui ni kwa nini madai hayo yameanza kutolewa hivi sasa, badala yake akamtaka mwandishi wa habari hizi kufanya uchunguzi zaidi kuhusu suala hilo .

Kwa upande wake Gadau, aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji hicho na baadaye kuondolewa kutokana na kushamiri kwa kashfa hizo za uuzaji wa maeneo katika kijiji, alikiri wazi kwamba Muyamba amekuwa akinunua mashamba kijijini hapo.

“Ni kweli Ben Muyamba ninamfahamu vizuri sana , alikuja na kujitambulisha kuwa ni mfanyabishara wa Makambako, anahitaji mashamba kwa ajili ya shughuli za upandaji miti na kilimo,” alisema Gadau.

Hata hivyo, Gadau alisikitishwa na hatua ya kamati ya Ardhi na mazingira chini ya uongozi wa Katundu na wajumbe wake kumlalamikia yeye kila mahali,(akimaanisha ofisi za mamlaka za serikali, DC, Polisi na Takukuru) akisema hawakumtendea haki.

“Unajua mimi nikiwa mwenyekiti na kwa mujibu wa madaraka niliyonayo naweza kufanya maamuzi yeyote bila kukiuka sheria, lakini pia nimekuwa nikishirikisha kamati mbalimbali za maendeleo ya kijiji kwa ajili ya kuhakikisha uongozi unaokidhi mahitaji ya umma na wala sio ubabe,” alisema Gadau.

Muyamba alikiri na kuthibitisha kununua kiasi kikubwa cha maeneo ya mashamba katika kijiji cha Usetule na vya jirani, kwa ajili ya shughuli zake za kilimo na ufugaji na kusema watu wanaomlalamikia ni wanaomuonea wivu kwa vile amepata maeneo makubwa.

“Mimi nimefuata taratibu zote muhimu na yale mashamba kule sio kuwa nimevamia, bali nimeuziwa na serikali ya kijiji chini ya uongozi wa mzee Gadau, lakini pia suala hili lilifikishwa kwa Diwani Mwandoloma na idara ya Ardhi,” alisema Muyamba kwa kujiamini.

Lakini baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wamekuwa na madai kwamba kuna harufu mbaya ya rushwa kwenye suala hilo na ndio maana kuna watu wamekuwa wakikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uongo kwenye kituo cha polisi Makambako, na kuachiwa baadaye.

“Tumekuwa wageni wa kituo cha polisi makambako kila siku, wanafuata watu na kuwaweka ndani, yote hiyo ni nguvu ya fedha za ndugu Muyamba, lakini kwa hakika ni kwa sababu viongozi waandamizi serikalini hawajui mambo yanayoendelea huku,” walisema wananchi hao.

Hata hivyo, wananchi wa mji wa Makambako na vitongoji jirani na eneo hilo , wameelezea hali hiyo kuwa mbaya na inayohitaji msimamo wa serikali ya wilaya ama ya Mkoa, kwani haitokani na utawala bora.

Source gazeti la kulikoni la leo tarehe 31/05/2013
 
aisee ila anavoamua kuwatimua raia sio kabisa kwa uwekezaji si katai ila kuwekeza sehemu kwa nia ya kuwaumiza wananchi watatoana roho bure..

komaeni tu wanakijiji..
 
Back
Top Bottom