Mfahamu: Jenerali Qaseem Soleimani

Mfahamu: Jenerali Qaseem Soleimani

DIDAS TUMAINI

JF-Expert Member
Joined
Nov 11, 2014
Posts
242
Reaction score
680
KAMANDA KIVULI

Qassem-Soleimani1.jpg

Leo acha nimzungumzie 'kamanda kivuli' mfanyakazi wa shirika la maji la mji wa Kermal ambaye baada ya muda wa kazi alikuwa akishinda 'gym' kunyanyua vyuma na kutunisha misuli. Akiwa na miaka 22 aliona bora aachane na kazi katika shirika la maji ili aingie jeshini kuutendea haki mwili wake pamoja na kupigania taifa lake ambalo mwaka huohuo limetoka kufanya mapinduzi na sasa ni taifa linaloongozwa kwa sharia za kiislamu. Namaanisha *'Islamic Republic of Iran'* nchi yenye jeshi imara sana pale mashariki ya kati.

Hatimaye mwaka 1979 'Kamanda Kivuli' akavaa kombati na mtutu begani tayari kulitumikia jeshi la walinzi wa mapinduzi ya kiislamu kwa kingereza tunaita 'Islamic Revolutionary Guards Cops IRGC' lakini kwa kiajemi wanaita *Sepah.*

Kama utakumbuka wakati naeleza muundo wa Jeshi la Iran nilisema kuwa Jeshi la Iran *'Iranian Armed Forces'* ilimegawanyika katika matawi matatu ambayo yote kwa pamoja yapo chini ya mkuu wa majeshi 'General staff of Armed Forces' aitwaye Meja Jenerali Mohammed Bagheri ambaye naye anaripoti kwa Amiri jeshi mkuu *Ayatollah Ali Khamenei* kiongozi mkuu wa nchi ya Iran. Hii Iranian Armed Forces imegawanyika katika matawi matatu ambayo ni:

1. *'Islamic Iranian Army IRA'* inayoongozwa na Meja Jenerali Abdolrahim Mousami. Tawi hili linajulikana kama 'Artesh' ambalo nalo limegawika katika vitengo vinne ambavyo ni •Jeshi la nchi kavu 'Army Ground Forces'.•Jeshi la majini 'Navy'• Jeshi la Anga 'Air Force' na •Jeshi la ulinzi wa anga 'Air Defense'.

2. Tawi la pili ni jeshi la walinzi wa mapinduzi ya kiislamu, *'Islamic Revolutionary Guard Corps IRGC* linaloongozwa na Meja Jenerali Hossein Salami. Tawi hili liliundwa mwaka 1979 mara tu baada ya mapinduzi ya kiislamu ya nchi ya Iran. Lengo la kuundwa kwa tawi hili 'IRGC' ni kwa ajili ya kulinda mifumo ya kiutawala na ya kisiasa katika serikali ya Iran. Kulinda mifumo hiyo ni pamoja na kuzuia mapinduzi ya kijeshi ndani ya Iran pia kuzuia nchi za nje kuingilia mambo ya ndani ya Iran. Itikadi kuu za tawi hili ni pamoja na 'Khomeinism' yaani kulinda na kutekeleza falsafa za kiongozi wao muasisi wa taifa la kiislamu la Iran, Ayatollah Khomeini. Pia IRGC imejikita katika kupambana na uzayuni(Israel) Anti Zionism, kueneza na kulinda dini ya kiislamu hususani dhehebu la shia 'Shia Islamism' pamoja na kupambana dhidi ya ubepari 'Anti imperialism'.

Tawi hili 'IRGC' likijulikana pia kwa jina la 'Sepah' nalo limegawanyika katika vitengo vitano ambavyo ni: Jeshi la ardhini 'Ground Force'. Jeshi la anga za juu 'Aerospace Force' hawa ni mahususi kwa maswala ya sayansi ya anga za juu kurusha maroketi, satelaiti. Jeshi la majini 'Navy'. Jeshi la Basij-hili ni kwa ajili ya vijana wenye umri wa 18-35 wanaojitolea kupigania nchi yao, hufanana na JKT kwa huku kwetu. Pia kitengo cha tano ni *jeshi la Quds* ambalo tangu mwaka 1998 limekuwa likiongozwa na Meja Jenerali Qaseem Soleimani aliyeuwawa jana.

3. Tawi la tatu ni Law Enforcement Force. Hili ndio jeshi la polisi la nchi ya Iran ambavyo ndani yake kuna kikosi cha usalama barabarani. Uhamiaji. Kupambana na rushwa n.k.
_____

Baada ya kufahamu muundo wa jeshi la Iran, sasa tuendelee!..Niliishia kwa kusema kwamba mwaka 1979 wakati akiwa na umri wa miaka ishirini na mbili, aliamua kujiunga na jeshi la Iran katika kikosi cha Walinzi wa mapinduzi ya kiislamu *'Islamic Revolutionary Guards Cops IRGC'.* Namzungumzia Kamanda Kivuli ambaye kwa mara ya kwanza alipangiwa kituo cha kazi huko kaskazini magharibi mwa Iran kuliookuwa na upinzani kutoka kwa jamii ya wakurdi waliokuwa wakishinikiza kujitenga ili kuanzisha nchi yao.

Mwaka mmoja baadae, 1980, Iran ilivamiwa na nchi ya Iraq chini ya Saddam Hussein. Kamanda Kivuli kwa weledi wa hali ya juu aliongoza wapiganaji wa mji wa Kerman katika kukomboa maeneo yaliyotekwa na majeshi ya Iraq. Umahiri wake ndio ulimfanya aheshimike na hata kupandishwa kuwa kamanda wa kikosi cha 41th Sarallah. Vita ya Iran-Iraq ilimfanya Kamanda Kivuli kutengeneza mahusiano ya karibu na jamii ya wakurdi waishio Iraq pamoja na wanachama cha kishia wa chama cha 'Badr Organization' waliokuwa wakipinga utawala wa Saddam.

Baada ya vita ya Iraq kumalizika mwaka 1988, miaka michache baadae Kamanda Kivuli alipandishwa kuwa kamanda wa IRGC jimbo la Kerman lililo jirani kabisa na nchi ya Afghanistan. Uwepo wa kamanda Kivuli katika Jimbo la Kerman kulisaidia kudhibiti kwa kiasi kikubwa kilimo na usafirishaji wa madawa ya kulevya yanayopitishwa kutoka Afghanistan kwenda Uturuki na nchi za ulaya. Kamanda huyu alionesha umahiri mkubwa kwenye kazi aliyopewa kiasi cha wakuu wake kumkubali na hata mwaka 1998 aliteuliwa kuwa Kamanda mkuu wa jeshi la IRGC- kitengo cha *Quds Force.*

Sasa hapo ndipo ule msemo wa 'upele umemuota mwenye kucha' ulipodhihirika. Sikia nikwambie: Jukumu kubwa la jeshi la Quds ni kufanya mikakati nje ya nchi ya Iran. Na mikakati hiyo ni pamoja na kushiriki vita vya kiwakala 'proxy wars' katika nchi za nje ya Iran lengo ni kulinda maslahi ya Iran. Proxy wars ambavyo binafsi naviita 'vita vivuli' ni ile unashiriki vita nyuma ya mgongo wa nchi fulani kupigana na nchi nyingine. Pia kuendesha operesheni za siri kwa lengo la kusaidia nchi fulani ili kulinda maslahi ya taifa lako. Sasa katika eneo hili upele ulimuota mwenye kucha kwani Kamanda ninayemzungumzia leo alikuwa ana makucha makubwa ya kukuna upele huo. Ni mtaalamu wa kuratibu proxy wars kiasi kwamba akapewa jina la 'Invisible Commander' yaani kamanda asiyeonekana. Wengine walimbabatiza jina la *'The Shadow Commander'* kwa kiswahili Kamanda Kivuli.

Hebu fikiria, ni uwezo mkubwa kiasi gani alionao kamanda huyu kiasi Cha kufananishwa na kivuli? Je ni kwakua anapigana Proxy war ambazo hajioneshi waziwazi? Au ameitwa kivuli kwakuwa ni mgumu kushindwa vita? Maana huwezi kupigana na kivuli na ukashinda. Hapo nimemkumbuka mtu mmoja wa kubuni anaitwa Lwanda Magere ambaye hakuna vita aliyoshindwa maana kila akichomwa mishale na mikuki, hafi. Kumbe nguvu na ushujaa wake upo kwenye Kivuli chake na hakuna ajuaye Siri hiyo zaidi yake mwenyewe. Lakini siku moja akiwa na mkewe baada ya kulainika na maneno matamu ya mkewe, Lwanda Magere alifanya kama alivyofanya Samsoni kwa mkewe Delilah. Akatoa Siri kwa mkewe kuwa nguvu zote alizonazo zipo kwenye Kivuli chake, hivyo ili kumshinda inabidi upambane na kivuli na sio mwili. Aaaah! baada ya kuambiwa Siri hiyo, mke wa Lwanda Magere kumbe ni shushushu aliyetumwa kupepeleza siri ya nguvu za mumewe, akakimbia kwenda kumwaga siri hiyo kwa waliomtuma ambao ni maadui wa Lwanda Magere.

Baada ya kujua Siri hiyo wakavamia Kijiji cha kina Lwanda Magere, siku zote walikuwa wakipigana Vita usiku lakini safari hii wameenda mchana jua kali wakijua fika kwamba kivuli kitaonekana. Guess What!!? Haikuchukua hata round, adui alimkaribia Lwanda Magere na kuchoma mkuki kwenye Kivuli Cha Lwanda Magere. Na huo ndio ukawa mwisho wake. Kupata stori hii Tafuta Kitabu kinaitwa Lwanda Magere. Au Kama wewe ni mwanafunzi na upo O'level, pambana ufike kidato cha tano ili uchukue somo la Fasihi ya Kingereza hapo utasoma na kuchambua Fani na maudhui ya Kitabu hiko.

Anyway, kidogo nimechomekea Story ya Lwanda Magere, sasa turudi kwenye mada yetu ya Kamanda Kivuli ambaye niliishia kueleza kwamba kuchaguliwa kuwa mkuu wa jeshi la Quds ni kama 'upele kumuota mwenye kucha' maana anajua barabara kuratibu mipango ya vita hasa proxy war kiasi Cha kuitwa 'The Shadow Commander' licha ya jina lake kamili kuwa *Meja Jenerali Qaseem Souleimani.*

Kamanda Qaseem alikuwa tishio sana pale mashariki ya kati kiasi kwamba mataifa ya magharibi yakaanza kutetemeka. Tangu ateuliwe kuwa mkuu wa jeshi la Quds, Kamanda Soleimani alisaidia sana nchi ya Iran kutengeneza mahusiano na kikundi cha Hezbollah huko Lebanon kusini ambapo tangu mwaka 1985 kumekuwa na mapigano kati ya majeshi ya Lebanon yakisaidiwa na Israel dhidi ya kikundi cha kishia cha Hezbollah. Katika Vita hiyo, nchi ya Iran kupitia jeshi la Quds chini ya Kamanda Soleimani walitoa sapoti kwa Hezbollah katika kupambana na majeshi ya kusini Lebanon SLA yanayosaidiwa na Majeshi ya Israel IDF. Kamanda Soleimani sio tu alitoa sapoti, bali alishiriki kikamilifu katika kusuka mipango yote ya Hezbollah. Mbinu zake za kivita ndizo zilipelekea majeshi ya South Lebanon Army na Israel Defensive Force kunyoosha mikono juu na kuondoka huko Kusini Lebanon mwaka 2000.

Baada ya jeshi la Quds kufanikiwa kuyaondoa majeshi ya Israel hapo Kusini Lebanon, Kamanda Qaseem Soleimani akaelekeza nguvu zote huko Afghanistan katika kupambana dhidi ya serikali ya Taliban iliyotawala tangu mwaka 1996. Nchi ya Afghanistan imekuwa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 1989 kwa kushuhudia vyama na vikundi mbalimbali vikitaka kutawala nchi hiyo ambapo kila kikundi kikipokea sapoti toka nchi za nje ikiwemo Iran ambayo kupitia jeshi la Quds ilikuwa ikitoa sapoti kwa chama cha Northern Alliance kupambana dhidi ya Taliban na Al Qaeda. Chama hiko pia kilipokea sapoti kutoka kwa Marekani ambayo nayo ilikuwa ikilenga kuuangusha utawala wa Taliban kufuatia kitendo cha Al Qaeda kulipua majengo pacha ya kituo cha biashara cha kimataifa WTC huko New York Marekani.

Kama nilivyosema hapo awali kwamba jukumu kubwa la Jeshi la IRGC-Quds ni kuendesha operesheni za kivita nje ya nchi ya Iran kwa lengo la kulinda maslahi ya Iran. Hivyo baada ya kusaidia kupunguza nguvu ya Taliban huko Afghanistan, Kamanda Qaseem Soleiman aligeukia nchini Syria kulipokuwa na machafuko ya vikundi vya watu wakitaka kumng'oa Rais Bashar Al Assad. Iran ilihakikisha Bashar Al Assad hatoki madarakani. Hebu tazama: Kuzuka kwa machafuko hayo nchini Syria kulifanya Marekani na nchi zingine za magharibi kuamini kwamba Rais Bashar Al Assad atang'oka madarakani ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita, lakini ujio wa Kamanda Soleimani pale Syria uliwaproove wrong wazungu kwani ni takribani mwaka wa tisa sasa Al Assad anakula nchi, hakuna aliyeweza kumtoa madarakani.

Sio tu Syria, hata nchini Yemen jeshi la Quds limerefusha mikono yake kusapoti wanamgambo wa kihuthi wanaopinga serikali ya Yemen inayoungwa mkono na nchi ya Saudi Arabia ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitofautiana na nchi ya Iran kiasi kwamba miaka michache iliyopita wanajeshi wa Quds chini ya Kamanda Soleimani walijaribu kumuua balozi wa Marekani nchini Saudi Arabia. Halikadharika kundi la Hamas, limekuwa likipata sapoti kubwa sana kutoka kwa jeshi la Quds kwa ajili ya kupambana dhidi ya Israel. Hiyo yote inafanyika kwa sababu ya uwepo wa kisiki imara, kamanda Qaseem Soleimani ndani ya IRGC-Quds, jeshi linalopingwa vikali na mataifa ya Marekani, Saudi Arabia, Israel, Uingereza na wengineo ambao huwachukulia kama magaidi. Kutokana na ushupavu wake katika kupigania maslahi ya Iran katika uga wa kivita, mwaka 2011 Kiongozi wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei alimpandisha cheo kamanda Qaseem kuwa Meja Jenerali. Na kutokana na kupigania uislamu na kueneza ushia, Khamenei alipata kukumuita Qaseem ni 'Living Martyr' yaani mfia dini aliye hai.

Mwaka 2014, Meja Jenerali Qaseem Soleimani hakuwa nyuma katika kuiwakilisha nchi ya Iran katika kupambana dhidi ya kundi la dola ya kiislamu la Iraq na Syria ISIS. Akiwa mkuu wa jeshi la Quds aliungana na wakurdi waishio Iraq katika kupambana na dola la kiislamu. ISIS walikuwa tayari wameshatwaa mji wa Tikrit nchini Iraq, lakini kwa uongozi wa Kamanda Qaseem Soleimani, mji huo ulirudishwa na Isis kuondoka hapo. Namkumbuka Kwenye ile operesheni ya kumuokoa rubani wa ndege ya urusi huko Syria, ambapo aliongoza kundi la Hizbola kuvamia ngome ya kundi la Daesh na kumuokoa rubani huyo mwaka 2015.

Ni mambo mengi Sana aliyoyafanya Kamanda huyu ambayo siwezi kueleza yote. Maana ni Labda kiongozi mashuhuri sana pale Iran baada ya Ayatollah Khamenei. Umashuhuri wake ndio ulipelekea kuibuka kwa uvumi kwamba huenda angewania urais wa Iran mwaka 2013 ingawa alikanusha uvumi huo.

Niweke nukta kwa kuelezea siku za mwisho za kamanda huyu aliyeuwawa kwenye uwanja wa ndege wa Baghdad huko nchini Iraq. Kuuwawa kwake kunakuja siku chache baada ya waandamaji kuvamia na kushambulia kwa mawe jengo la ubalozi wa Marekani mjini Baghdad. Baada ya marekani kumtuhumu Kamanda Soleimani katika kushiriki kupanga uvamizi huo, siku ya tarehe 3 Jan 2020 ndege zisizo na rubani zilifika katika uwanja wa ndege na kushambulia gari alilokuwemo kamanda Qaseem Soleimani. Mwili wa kamanda ulitambuliwa kwa Pete aliyoivaa kwenye kidole cha mkono wake.

Na huo ndio ukawa mwisho wa Kamanda Qaseem Soleimani aliyeuwawa akiwa na umri wa miaka 62.

___________________

Ahsanteni.


Imeandikwa na
[emoji2398]KichwaKikuu.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Inaonekana huyu mwamba angekaa miaka mitano zaidi us na washirika wake wangekuwa wamepoteza pakubwa sana.
 
U
Inaonekana huyu mwamba angekaa miaka mitano zaidi us na washirika wake wangekuwa wamepoteza pakubwa sana
Umesahau amekuwa kiongozi wa QUDS Forces kwa miaka 22 na akaishia kutegwa na kufa kama kware tu na kuiacha Marekani vile vile na utemi wake!
 
..tatizo ni kupanga mashambulizi dhidi ya ubalozi wa Marekani.

..hao jamaa ukiwagusa watakusaka hata miaka 20+ mpaka wakuue.
 
Back
Top Bottom