Meya wa Jiji la Dar aapishwa...

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,903
ISAYA Mwita, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, ameapishwa leo, akiwa meya wa 17 tangu mwaka 1949.

Mwita, Diwani wa Kata ya Vijibweni (Chadema), Kigamboni, ni meya wa kwanza wa jiji la Dar es Salaam asiyetokana na chama kinachotawala.

Kumbukumbu za Jiji zinaonesha orodha ya mameya waliomtangulia Mwita, huku baadhi yao wakiwa wameandikwa kwa jina moja tu au kwa vifupi vya majina yao ya kwanza.

Wengine wanaonekana walishika ofisi kwa muda mfupi; na wakati mwingine kulikuwa na mameya zaidi ya mmoja ndani ya mwaka mmoja.

Watangulizi 16 wa Mwita ni Pevirett Obi (1949-1952), Aya Kareemjee (1953-1955), T.W. Tyrrell (1955-1956), S.D Owarth (1957-1958), na. S.M.M. Devani (1959).

Wengine ni Ramadhan Nyamka (1978-1982), Kitwana Kondo (1983, 1995), A.A Abed (1991), M. Mfaume (1992-1993), R.O Kirundu (1994-1996), O.O Nondo (1997), A. Sambuso (1997), na Abuu Juma (1996-2000), Kleist A. Sykes (2000-2005), Adam O. Kimbisa (2005-2010), na Didas Massaburi (2010-2015).

Aziza Kalli, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Sokoine Drive, Dar es Salaam ndiye aliyemwapisha Mwita ili aanze majukumu yake rasmi.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria hafla ya kuapishwa kwa meya ni Wilson Kabwe, Mkurugenzi Mkuu wa Jiji; Sarah Yohana, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji; Charles Kuyeko, Meya wa Manispaa ya Ilala, na Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo.

Baada ya kuapishwa Mwita amezungumza na vyombo vya habari akasema anadhamiria kuwa kiongozi muunganishi bila kujali tofauti za kiitikadi.

Isaya Mwita, Meya wa Jiji la Dar es Salaam akiapishwa

Amesema hatarajii kipindi chake cha uongozi kiwe na vurugu au machafuko katika Jiji la Dar es Salaam.

‘’Viongozi wangu wa chini wajisikie amani, kwani mimi nitakuwa kiongozi bora kwa watu wote. Wala sikuja kwa ajili ya kuleta machafuko na ugomvi, bali nahitaji amani ili tutafute maendeleo,’’ amesema.

Mwita amesisitiza ushirikiano kwa viongozi wote ili washughulikie changamoto za muda mrefu katika jiji hilo – usafiri, miundombinu, afya, elimu, na huduma nyingine za jamii.

Naye Kubenea amesema wajumbe wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wamefurahishwa na kukamilika mchakato wa umeya ambao ulicheleweshwa na mizengwe ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kwa miezi minne mfululizo kilikwamisha uchaguzi wa meya, kikitafuta fursa ya kung’ang’ania madaraka ya uongozi wa jiji.

“Sasa ni wakati wetu wa kutumikia wananchi, na kusahihisha makosa na maovu yote yaliyofanywa na watangulizi wetu huko nyuma.

“Ni muda sasa wa kuanika mali za umma hadharani ili kila mwananchi azijue, kwani kuna mambo yalikuwa yakifanyika, ikiwemo kusaini mikataba feki gizani. Sasa yatawekwa hadharani. Wakwapuaji wa mali za umma wajiandae,’’ amesema Kubenea

Meya wa Manispaa ya Ilala ameahidi kushirikiana na Mwita katika kuleta maendeleo, hasa katika kusimamia ukusanyaji kodi. Amesema, “tumeahidi mengi kwa wananchi ambayo yote yanahitaji pesa, ambazo zipo kwa wananchi. Hivyo, ni ombi langu kwa wananchi wajitume kulipa kodi.”

Tukio hilo limehitimisha sekeseke la umeya lililodumu kwa miezi mitano mfululizo.

Uchaguzi wa Meya wa Jiji ulifanyika tarehe 22 Machi 2016,Mwita aliibuka mshindi kwa kura 84 dhidi ya Yusuph Omar wa CCM aliyepata kura 67.
CezjKjFXIAQ-1bU-150x150.jpeg
 
Hiyo listi ya mameya imekaa ovyo ovyo,naona wengine walikuwa na nafasi nyingine lakini si umeya na wengine hawajahudumu kwa muda uliyoelezwa mfano Abuu jumaa hakumaliza miaka mitano kwani halmashauri ya jiji ilivunjwa kabla mwaka 2000 na kuundwa tume ya keenja,na hapo kuanzia 1983 - 1995 alikuwepo kitwana kondo sasa hao wengine wanaoonekana kwenye listi ndani ya muda huo sijui vipi.
 
Wakuu hii Mahakama ya Sokoine Drive ipo jengo gani?

Kama unatokea Central Police/Railway Station kuelekea Posta ya Zamani along Sokoine Drive just before St. Joseph Cathedral, upande huo huo wa kanisa kuna mahakama pale. Imejificha kidogo lakini ndio hiyo; watu wanakatiwa vifungo vya maisha pale.
 
‘’Viongozi wangu wa chini wajisikie amani, kwani mimi nitakuwa kiongozi bora kwa watu wote. Wala sikuja kwa ajili ya kuleta machafuko na ugomvi, bali nahitaji amani ili tutafute maendeleo,’’ amesema.
.

Nakala ya tamko hili imfikie Kubenea kule ubungo,Mnyika kule Kibamba,Mbunge Godbless Lema kule Arusha,Halima mdee kule kawe,mchungaji msigwa kule Iringa na Sugu kule Mbeya ambao ni vinara wa kutunga machafuko,migomo,maandamano na vurugu
 
Kama unatokea Central Police/Railway Station kuelekea Posta ya Zamani along Sokoine Drive just before St. Joseph Cathedral, upande huo huo wa kanisa kuna mahakama pale. Imejificha kidogo lakini ndio hiyo; watu wanakatiwa vifungo vya maisha pale.

Ahsante sana.
 
Nakala ya tamko hili imfikie Kubenea kule ubungo,Mnyika kule Kibamba,Mbunge Godbless Lema kule Arusha,Halima mdee kule kawe,mchungaji msigwa kule Iringa na Sugu kule Mbeya ambao ni vinara wa kutunga machafuko,migomo,maandamano na vurugu
Umesahau nakala ya mwisho iwafikie waigizaji wote wa mazingaombwe ccm
 
Back
Top Bottom