Joaquin "El Chapo" Guzman, mlanguzi sugu wa dawa za kulevya raia wa Mexico aliyepatikana na hatia ya kuendesha biashara ya kihalifu iliyosababisha vifo vya watu wengi na kuingiza nchini Marekani tani nyingi za dawa za kulevya, amehukumiwa kifungo cha maisha jela.
Jaji wa Marekani Brian Cogan ametangaza hukumu hiyo ya maisha pamoja na miaka 30, ambayo ni lazima chini ya sheria, katika kikao cha mahakama ya serikali kuu mjini Brooklyn. Guzman mwenye umri wa miaka 62, pia aliamriwa kulipa dola milioni 12.6.
Guzman alipatikana na hatia Februari mwaka huu kwa kusafirisha Marekani tani za cocaine, heroin na bangi na kuhusika katika njama za mauaji wakati akiwa kiongozi wa mtandao maarufu nchini Mexico wa biashara ya dawa za kulevya wa Sinaloa.