Mimi sioni ujinga wa mtoa mada, sioni ujinga wa Mhe. Msigwa kama mwakilishi wa watu wa jiji la Iringa. Tofauti ya upinzani na Rais Dr. John Joseph Pombe Magufuli ni moja tu; kubinya uhuru wa watu na hasa vyama vya upinzani. Kwa kilichokuwa kinajadiliwa Iringa, Mchungaji Mhe. Peter Msingwa angeonekana kituko kama angesema kinyume na alichokisema. Mchungugaji ni mtu wa Mungu na kwa hilo la kumsifu Mhe. Magufuli ulikuwa ni upatanishi, dhamira ya kujenga madaraja na sio kuta. Ni ustaarabu wa hali ya juu. Mlitaka asemeje? Na kwa taarifa yako, wanaoleta matatizo kwa nchi hii ni wale wasiojulikana, ambao kwa kiwango kikubwa hawatumwi na mfumo rasmi wa serikali. Hao ndio tunatakiwa kujihadhari nao. Hilo amelifanya vizuri Mchungaji.
Ninamshauri jambo moja Mchungaji Peter Msigwa, aimarishe chama cha CHADEMA katika eneo lake la kazi na mkoa wa Iringa kwa ujumla. Mchungaji anatuhumiwa kujenga kuta kwa wapinzani wake ndani ya chama cha chadema. Kila mwenye maoni tofauti anasema ametumwa, amenunuliwa na CCM. Ameongeza mpasuko ndani ya chama. Hilo ndilo hatari zaidi kwa ustawi wa CHADEMA kuliko kumsifu Rais kwa mazuri yanayoonekana.
Kumkashifu hadharani au kutoa lugha za kejeli kwa kiongozi mkuu wa nchi, ni laana na ni ushenzi. Mchungaji anayo "forum inayokubalika kisheria" ya kuelezea mapungufu ya serikali na hata mapungufu ya kiongozi mkuu wa serikali; bungeni na kwenye mikutano yake ya hadhara. Lakini hata katika mikutano hiyo hawezi kupinga kila kitu mwanzo mwisho.
Nitoe wito kwa wanamageuzi wa nchi hii hasa vijana na viogozi wa vyama hivi; tukiwa na chuki dhidi ya watawala tutakwama zaidi. Tuwakosoe bila kuwatukana, tuwasifu wanapostahili na tuwaonyeshe njia iliyobora ya kuongoza nchi. Tuwafundishe namna ya kuwa na mijadala yenye tija.