Mchango wa Wakenya katika siasa za Tanzania

WilsonKaisary

JF-Expert Member
Apr 4, 2017
392
947
Tanzania ni Nchi ambayo husifika mno kwa ukombozi wa Nchi mbalimbali za Afrika, hasa zile zilizo Kusini mwa Bara hili Masikini zaidi Duniani. Uthibitisho juu ya Ukindakindaki wa Nchi yetu juu ya Ukombozi wa Nchi za Afrika ni Hotuba Maridhwawa iliyotolewa naye Rais Jakaya Kikwete wakati wa Mazishi ya Rais wa Kwanza Mweusi wa Afrika ya Kusini, Komredi Nelson Mandela, hotuba ambayo kwa undani ilijikita katika kueleza namna Tanganyika na kisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilivyojikita katika kutoa msaada kwa Wanaharakati mbalimbali wa Ukombozi wa Afrika, akiwemo Komredi Mandela.

Jambo moja ambalo halisemwi sana juu ya Tanzania ni namna Wakenya wawili Mashuhuri walivyochangia katika harakati za Ustawishaji Umoja wa Zanzibar na harakati za kudai Uhuru za Tanganyika, mchango ambao kwa kiasi kikubwa ndio umetupatia Tanzania tuliyonayo sasa. Watanzania Mashuhuri tumeona ni muhimu leo, wakati Rais John Magufuli akifanya ziara yake ya kwanza nchini Kenya, kuelezeka kwa undani juu ya mchango wa Wakenya wawili hao katika kuijenga Tanzania.

Wakenya wawili hao ni aliyekuwa Mwenyekiti wa PAFMECA (Pan-African Freedom Movement for East and Central Afrika) - Umoja wa Vyama vya Kupigania Uhuru wa Nchi za Afrika Mashariki na Kati, Komredi Francis Khamis na ndugu Dome Okochi Budohi.

FRANCIS KHAMIS na MUAFAKA wa KWANZA wa ZANZIBAR

Novemba 28, 1958 ulifanyika Mkutano wa PAFMECA Jijini Mwanza Nchini Tanganyika, Katika Mkutano huo Komredi Francis Khamis aliwakilisha nchi yake ya Kenya. Mkutano huo ulijikita katika kujadili namna ya kuendeleza kwa ufanisi harakati za kudai Uhuru kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati, huku Yeye Francis Khamis akiwa ndiye Mwenyekiti wa PAFMECA.

Katika Mkutano huo kwa kirefu vyama vya Ukombozi wa nchi za Afrika Mashariki na Kati vilieleza kwa undani changamoto mbalimbali vinazokabiliana nazo ili kuepeana uzoefu na mbinu imara zaidi za kuharakisha Uhuru wa nchi zao. Suala ambalo lilijadiliwa kwa kirefu ni kuhusu hali ya Zanzibar, hasa mpasuko wa Kisiasa uliokuwepo kati ya vyama vya ASP (Afro-Shiraz Party) cha ndugu Abeid Amani Karume na ZNP (Zanzibar Nationalist Party) mashuhuri kama Hizbu cha ndugu Ali Muhsin Barwany.

Mpasuko husika uliwagawa Wazanzibari katika Makundi Mawili ya Ufuasi kati ya Vyama hivyo, ufuasi ambao ulichochea chuki za kitabaka, rangi na kabila. Chuki ambayo iliondoa Umoja wa Kizanzibari na kuwa kikwazo cha kupatikana kwa haraka kwa Uhuru wake. Chuki hizo ndio msingi mkuu wa Mapinduzi ya Zanzibar na hata mgawanyiko wa kisiasa na kijamii ulioko Zanzibar mpaka leo.

Chini ya ndugu Francis Khamis wa Kenya na ndugu William Murray Kanyama Chiume wa Nyasaland (sasa Malawi), Viongozi wa ZNP na ASP waliwekwa chini na kupatanishwa na pamoja wakatoa tamko la kuonyesha Umoja wa Kizanzibari katika kudai Uhuru wa Taifa lao. Tamko hilo hujulikana kama "Muafaka wa Kwanza wa Zanzibar".

Tamko la "Muafaka wa Kwanza wa Zanzibar" lilisainiwa na Sheikh Abeid Amani Karume (Mwenyekiti wa ASP), Sheikh Thabit Kombo Jecha (Katibu Mkuu wa ASP) na Sheikh Mohammad Hamad Shamte kwa niaba ya Chama cha ASP. Na kwa niaba ya Chama cha ZNP waliosaini ni Sheikh Ali Muhsin Barwany (Mwenyekiti wa ZNP), Komredi Abdulrahman Mohammed Babu (Katibu Mkuu wa ZNP) Miiraj Sheylab.

DOME OKOCHI BUDOHI

Kulikuwepo na wazalendo kutoka nchi jirani ya Kenya kama vile Dome Okochi Budohi na Patrick Aoko ambao walikuwa wanajua vyema siasa za walowezi za kupora ardhi za wananchi Nchini. Wazalendo hawa kutoka Kenya kwa kiasi kikubwa walisaidia harakati za Ukombozi wa Tanganyika kwa kuwa ni kutoka kwa wazalendo kama hawa, Abdulwahid Sykes alipata usikivu wa mawazo yake ya kuigeuza TAA kuwa chama cha siasa chenye nguvu.

Katika wale walioasisi TANU, ni wale tu waliokuwa makao makuu ya TAA ndiyo wanaoweza kueleza historia ya kweli ya chama hiki. Hawa ni John Rupia, Dossa Aziz, Tewa Said Tewa, Julius Nyerere, Dome Budohi, Abdulwahid na Ally Sykes.

Mwezi Juni 1953, makao makuu ya TAA (Tanganyika African Association) walitangaza kamati yake ya utendaji, wafuatao walishika nafasi mbalimbali:

• Mwalimu Julius Kambarage Nyerere - Rais
• Ndugu Abdulwahid Kleist Sykes Mbuwane - Makamu wa Rais.
• Ndugu J. P. Kasella Bantu - Katibu Mkuu
• Ndugu Alexander M. Tobias - Naibu Katibu
• Ndugu Waziri Dossa Aziz - Katibu Muhtasi
• Dkt. Michael Lugazia - Mjumbe
• Ndugu Hamisi Diwani - Mjumbe
• Ndugu Tewa Said Tewa - Mjumbe
• Ndugu Denis Phombeah
• Ndugu Z. James - Mjumbe
• Ndugu Dome Okochi - Mjumbe
• Ndugu C. Ongalo - Mjumbe
• Ndugu Patrick Aoko - Mjumbe

Muundo wa uongozi katika TAA unaonyesha ule mshikamano wa Afrika ya Mashariki uliokuweko wakati wa harakati za uhuru. Wazalendo wa Kenya walichaguliwa kama viongozi wa TAA bega kwa bega na Watanganyika.

Kadi nambari 1 ya ilitolewa na Ally Sykes kwa rais wa TANU, Julius Kambarage Nyerere na Ally aliweka sahihi yake kama afisa aliyeitoa. Ilipendekezwa kwamba kadi chache za mwanzo lazima zipigwe mnada na fedha zitakazokusanywa zitiwe kwenye hazina ya chama. Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz, Rupia na wengine walipanda dau kununua kadi hizo. Ally alimshinda kaka yake Abdulwahid kwa bei akapata kadi ya TANU nambari 2, Abdulwahid alipewa kadi nambari 3, Dossa Aziz kadi nambari 4, Phombeah kadi nambari 5, Dome Okochi, mmoja wa wale wazalendo kutoka Kenya katika TANU alipata kadi nambari 6 na Rupia kadi nambari 7. Bibi Titi kadi nambari 16, Iddi Tosiri kadi nambari 25.

Lakini mara tu baada ya kuundwa kwa TANU wazalendo hawa wa Kenya wakakamatwa na serikali. Kwa miezi sita walihojiwa na kuwekwa rumande Kituo cha Polisi cha Kati (Central Police Station) huku wamefungwa minyororo. Budohi na Aoko walikuwa wakifuatiliwa na makachero (Special Branch) toka mwaka wa 1952 baada ya hali ya hatari kutangazwa Kenya.

Minongíono ilikuwa ikisikika kutoka kanda ya ziwa kuwa kiongozi wa wapiganaji wa Mau Mau, Dedan Kimathi alikuwa anaonekana mjini Mwanza. Wakati ule pale Mwanza kulikuwa na Wakikuyu wengi wakifanya biashara sokoni. Ilivumishwa kuwa Dedan Kimathi alikuwa akiwasiliana na Wakikuyu wenzake na wao walikuwa wakimkusanyia fremu za baiskeli za zamani ili zitumike kutengenezea magobole ili zitumiwe misituni dhidi ya majeshi ya Waingereza.

Mapigano yalipoanza kati ya Mau Mau na Waingereza kulikuwa na Wakikuyu kama elfu kumi na sita wakiishi na kufanya kazi kaskazini mwa Tanganyika. Kama tahadhari, Wakikuyu wachache walioonekana kuunga mkono Mau Mau, walikamatwa na kupelekwa Kenya ambako waliwekwa kizuizini katika kambi mbalimbali.

Inasemekana Dome Budohi aliponzwa na barua iliyotoka Kenya ambayo ilikamatwa na makachero. Barua hii ilikuwa inamuhusisha Budohi na Mau Mau. Inasemekana Budohi alisalitiwa na Mkenya mwenzake aliyeitwa Martin ambaye alikuwa pamoja naye katika bendi ya Blackbirds. Martin alikuwa akipuliza tarumbeta.

Askari waliokuwa wakiwalinda kule rumande walitoa habari kwa TANU kuwa kulikuwa na mpango wa kuwapa sumu wafungwa wale, Budohi na mwenzake Aoko. Baadaye wafungwa hawa walihamishiwa Handeni ambako kulikuwa na kambi ya kuwafunga watuhumiwa wa Mau Mau. Ndugu Rashid Mfaume Kawawa alikuwa amehamishiwa hapo Handeni kutoka Dar es Salaam.

Baadhi ya wafungwa walikuwa wananachama wa TAA na baada ya kuundwa TANU wakawa wanachama wa TANU. Kawawa alikuwa akifahamiana na wengi kati ya wafungwa wale. Budohi na Aoko waliwahi kuwa viongozi wa TAA. Kawawa aliwaangalia wafungwa hawa kwa moyo wa huruma akijaribu kupunguza shida zao pale kambini kila alipopata mwanya wa kufanya hivyo.

Kawawa na Budohi walijuana kitambo tu, Budohi aliwahi kucheza sinema ya Kiswahili na Kawawa iliyoitwa Mgeni Mwema iliyokuwa imetayarishwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii (Community Development Department). Idara hii ilitengeneza filamu kadhaa ambazo Kawawa alicheza kama nyota wa mchezo. Katika sinema zote alizocheza, iliyopata umaarufu na kupendwa zaidi ilikuwa Muhogo Mchungu ambalo ndiyo lilikuwa jina la Kawawa katika filamu hiyo.

Wakati Budohi na Wakenya wengine walipopita Korogwe wakati wakirudishwa Kenya kupitia Taveta, Ally Sykes, ambaye alikuwa amehamishiwa Korogwe, alikwenda hadi stesheni ya reli kuwaaga. Watuhumiwa hawa wa Mau Mau walikuwa wametiwa katika mabehewa ya kubebea ng'ombe huku wamefungwa minyororo. Dome Budohi na wazalendo wengine waliwekwa kizuizini kwa miaka saba.

Mola awalaze pema Wazalendo hao kutoka Kenya waliochangia Harakati za Ukombozi wa Tanganyika na Zanzibar na hatimaye kupatikana Tanzania tuliyonayo.

Pichani ni Komredi Dome Okochi Budohi. Ukurasa wa Watanzania Mashuhuri unatoa SHUKRAN za DHATI kwa Ndugu Nathan Chiume kwa kutupatia Tamko la Pamoja la Vyama vya ASP na ZNP la Mwaka 1958, Tamko ambalo ni hifadha ya Baba yake Komredi William Murray Kanyama Chiume, na pia Ukurasa unamshukuru Mwandishi Mohammed Said kwa kutupatia Picha ya Komredi Dome Okochi Budohi.

Kwa Picha na Maelezo Juu ya Kumbukumbu mbalimbali za Historia ya Tanzania, Like Ukurasa wa Watanzania Mashuhuri Ili kujifunza Zaidi. Unaweza Kutag Watu Wengi zaidi na Kushare Habari hii Ili kupanua wigo wa Ukurasa kuwafikia Watu Wengi zaidi.

"Watanzania Mashuhuri: Mashujaa wa Jamii, ni Kielelezo cha Jamii Husika".

 

Similar Discussions

Back
Top Bottom