Mbunge wa zamani Jimbo la Musoma Mjini mkoani Mara, Vedasto Mathayo (CCM), ametoa kali ya mwaka baada ya kwenda kwenye vyombo vya dola, akidai arudishiwe madawati aliyotoa kwenye shule mbalimbali wakati akiwa mbunge.
Mathayo alikuwa mbunge wa Musoma Mjini kwa muhula mmoja (2005-2010) na aliangushwa na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Vincent Nyerere, katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
Mathayo alisema anataka arudishiwe zaidi ya madawati 460 anayodai aliyanunua wakati akiwa mbunge wa jimbo hilo, na hataki maelezo mengine juu ya hilo.
Madai ya mbunge huyo wa zamani, yamekuja kufuatia kile kinachoelezwa kutaka 'kuwakomoa' wananchi aliokuwa akiwatumikia, kwa kushindwa kumchagua katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Akihutubia mkutano wa hadhara hivi karibuni katika uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo, mbele ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilson Mukama, alisema tayari ameshalifikisha suala hilo kwenye vyombo vya dola kwa hatua zaidi za kisheria, akitaka apewe madawati yake ama arudishiwe fedha alizotumia kununua vifaa hivyo.
"Kweli nadai madawati niliyoyanunua wakati nikiwa mbunge wa Musoma Mjini. Ninataka warudishe madawati yangu au walipe fedha nilizotumia kununulia zaidi ya madawati 460, na kila dawati lina thamani ya Sh. 40,000, ambapo kwa madawati yote yana thamani ya Sh. milioni 18.4.
"Kwa vile nataka haki yangu, tayari suala hili nimeshalifikisha polisi kwa ajili ya kupelekwa mahakamani...warudishe mali yangu, mimi sitaki mambo mengine. Nilitumia fedha zangu binafsi kununua madawati haya ndiyo maana nazitaka," alisema Mathayo katika mkutano huo.
Wakazi wengi wa mjini Musoma, walieleza kushangazwa na hatua hiyo ya Mathayo kuanza kudai arudishiwe madawati aliyoyanunua akiwa kiongozi, na kwamba hali hiyo inatokana na kushindwa kwake kwenye uchaguzi uliopita pamoja na kukata tamaa ya kisiasa.
Mbali na hayo, walisema Mathayo hapaswi kurudishiwa madawati hayo bali yaendelee kutumika shuleni kwani aliyanunua kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo na hayakuwa dhamana ya uongozi wake.
Naye Mbunge wa sasa wa jimbo hilo la Musoma Mjini, Vincent Nyerere, aliiambia NIPASHE kwa njia ya simu kuwa yuko tayari kufungwa jela na atahakikisha madawati hayo hayachukuliwi na Mathayo.
Alisema fedha zilizotumika kununulia vifaa hivyo ni zile za maendeleo ya jimbo.
"Haiingii akilini mtu akishindwa kwenye uchaguzi halafu anaanza kudai arudishiwe mali alizotumia, kama huo ni utaratibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wananchi wa Musoma hawako tayari kwa ubabe na dharau za namna hiyo," alisema.
"Mimi niko tayari kufia jela kwa kupinga madawati haya yarudishwe kwa Mathayo. Tunafahamu madawati haya yalinunuliwa kwa fedha za umma zinazotokana na Mfuko wa Jimbo. Sasa nimemshinda anataka arudishiwe? Wapi na wapi?," Alihoji Vincent.
Aliongeza: "Kama anabisha kwamba hajatumia fedha za Mfuko wa Jimbo kununua madawati haya, basi awaeleze wananchi fedha za mfuko huo zimetumikaje wakati akiwa mbunge."
Alisema kama watu wa CCM wanataka watoto wasomee chini, wao Chadema hawataki hilo na ieleweke hivyo. Vincent kwa sasa yupo jijini Dar es Salaam kuhudhuria vikao vya Kamati za Bunge.
Baadhi ya viongozi na makada mbalimbali wa CCM mkoani Mara, walieleza kushangazwa na kitendo cha Mathayo kuanza kudai vifaa vya maendeleo alivyonunua wakati akiwa kiongozi, na kwamba hatua hiyo inakidhalilisha chama tawala na viongozi wake.