Mbona tunaitazama tu nchi inakwenda kombo?

Semanao

JF-Expert Member
Jul 25, 2007
208
16
Na Kiganja wa Mkono

WATANZANIA tumekuwa na tabia ya kungoja mpaka viongozi wetu wanapoondoka madarakani, ndiyo tunakua mahodari wa kuwakosoa. Tabia hii hutoa mwanya mkubwa wa kutokuyabainisha na kuyashughulikia matatizo na maovu yanayowakabili wananchi katika wakati muafaka. Tabia hii inachangia kwa kiasi kikubwa kiongozi aliye madarakani kujisahau na kutokuona umuhimu wa kujirekebisha.

Wakati mwingi tumekua tukipindisha lawama zetu zisimfikie kiongozi aliye madarakani kwa visingizio kwamba wenye makosa ni washauri wake na kwamba wamemshauri vibaya na bwana mkubwa ni mtu safi!

Baada ya utawala wa awamu ya kwanza kashfa kama za Pasiyansi,Mwanza, uhujumu uchumi, ununuzi wa meli ya M.V Bukoba; Vitendo vya dhuluma vilivyotokea wakati wa operesheni vijiji na nyigine nyingi zilianza kujitokeza.

Mambo mengi kama haya ya dhuluma hayakuzungumzwa wala kukemewa wakati wahusika walipokuwa madarakani, jambo ambalo naamini kama ligefanyika na viogozi kulikubali, madhara ya makosa mengi ya viongozi kwa wananchi kwa wakati ule yangekuwa madogo hasa ukizingatia kwamba makosa mengine yaliendelea kutendeka kwa kipindi kirefu, kwa mfano, operesheni vijiji na biashara za ukiritimba.

Tukigusia jambo moja la operesheni vijij, wengi tunakumbuka madhara yaliyowafika wananchi wasio na hatia kwa kudhulumiwa utu, asili na mali zao kwa jina la ujamaa.

Badala ya kulaumiwa kinara wa suala lenyewe - hayati Mwalimu Julius Nyerere, watu wakamtupia lawama, Bw. Rashidi Kawawa kwamba eti hakufuata maelekezo ya bosi wake!

Sidhani kama wale waliokua hodari wa kumlaumu Bw. Kawawa walikuwa na ushahidi wowote kwamba alichokua anafanya sicho alichokuwa ameagizwa na kama hivyo ndivyo kwa nini basi bosi wake hakumuwajibisha au kumuadhibu?

Swali ni kwamba, wakati Kawawa anafanya kazi ya operesheni vijiji, iliyokuwa na mateso makubwa kwa wananchi, bosi wake alikuwa wapi? Hakuyajua mateso na dhuluma waliyokuwa wakipata wananchi anaowaongoza?

Si lengo la makala haya kuzugumzia mambo ya awamu ya kwanza, najiwekea taratibu za kujitahidi kutokuyataja mambo ya awamu ya kwanza ila tu pale ambako yatasaidia kueleza hoja, ama mfano wa mapitio wa jambo ninalolizungumzia. Hii si kwa sababu ya kuogopa au kwamba hakuna walilokosea, la hasha! bali ni katika kuheshimu wosia wa wazee kwamba “muwataje maiti wenu kwa wema.”

Hivi karibuni tumeshuhudia viogozi waandamizi wa siku nyingi wakimsakama Rais mstaafu, Bw. Benjamin Mkapa kwa tuhuma mbali mbali zinazomkabili na wakimshinikiza atoke hadharani azijibu tuhuma hizo. Hili ni jambo zuri sana kwa taifa letu, kama tuna dhamira ya kweli ya kujenga jamii ya ukweli, usawa na uwazi kama alivyokuwa Bw Mkapa akiinadi awamu ya uongozi wake.

Pamoja na kuunga mkono kwa dhati viongozi, waandishi na wananchi wote waliojitokeza kutaka rais mstaafu Bw. Mkapa ajibu tuhuma za ubadhirifu na ufisadi zinazomkabili, nadhani huu pia ni wakati muafaka kujaribu kuiangalia vizuri awamu ya nne iliyo madarakani ili isije ikatuingiza katika shimo kubwa kuliko tulilomo; alimotuacha Bw. Mkapa.

Ujanja wa kuambiwa kuwa ni mapema mno kuufanyia tathmini utawala uliopo madarakani umepitwa na wakati, siku njema huonekana asubuhi. Pia biashara ni asubuhi, jioni ni mahesabu.

Kutokana na maneno ya busara ya wahenga niliyoyataja hapo juu watanzania tatubidi tuwe makini mapema, twende nao sambaba viongozi waliopo madarakani wakati huu wakiwa wameshikilia mnofu wetu kiganjani mwao, maana baada ya hapo watakuja na hoja kama aliyoitoa, Bw. Mkapa hivi karibuni kwamba ‘ameshastaafu.' Sidhani kwamba kustaafu kunaondoa hoja ya mstaafu kuwajibika kwa matendo yake aliyoyafanya akiwa madarakani.
Maana kama hivyo ndiyo basi wakina, Kaunda, Chiluba, Cesescu Noriega na wegine wengi wasingeshurutishwa kubeba misalaba yao waliyoichonga walipokuwa madarakani.

Nadhani kuna haja ya kujenga mwamko wa dhati kwa wananchi wote kwamba taifa hili la Tanzania ni letu wote Watanzania na hakuna raia rasmi sote tuna haki sawa na viogozi wetu wote tokea Rais, Waziri Mkuu, Wabunge na nata Majaji wote ni raia wa kawaida tuliowapa heshima ya majukumu ya kututumikia.

Sisi wananchi ndiyo wenye heshima kubwa ndiyo maana tumeweza kuwapa sehemu ndogo tu ya heshima yetu viongozi wetu ili watutumikie. Nalisema hili kwa sababu imefikia wakati baadhi ya viongozi wetu wamelewa ukubwa kiasi kwamba kama utamsalimu kwa kumtaja Bwana au Bibi fulani basi hata kukuitikia inakua shida, kisa hukutanguliza neno "Mheshimiwa,” kana kwamba wao tu ndiyo wanaostahili heshima wengine wamefikia hata kutaka kuitwa ”Watukufu,” Nani kasema kwamba tumewapa heshima zetu zote nasi wananchi tumepaki mufilisi wa heshima?

Tukirudi katika mada yetu ya kutadhmini awamu tuliyonao, naona kuna mkangayiko mkubwa kati ya vinara wawili wa juu tulio nao huku mwenendo wa mmoja wapo ukionekana anataka kuonekana yeye ndiye 'dume' katika zizi.

Kumeibuka pia mtindop ninaoweza kuuita 'BORA MIMI,' ambapo baadhi ya viongozi wamefikia hatua ya kujionesha mbele ya jamii kuwa wao ni bora ni 'vichwa' zaidi kuliko wengine.

Kwa maono yangu mtindo huu wa 'BORA MIMI' ni hatari sana kwa taifa, kwani kwa mtazamo wangu nauona kwamba una ajenda ya siri, hivyo ni vizuri tukautathmini na kuchukua tahadhari kabla haujaleta madhara makubwa kwa taifa letu.

Kuna hisia nyingi kutoka kwa wananchi kadhaa kwamba badala ya kumsaidia kazi bosi wao baadhi ya watendaji waandamizi, wamekuwa wakitumia muda mwingi kujiandalia wao wenyewe, siku zao za baadaye.

Tumeanza kuona na hata wachunguzi wa mambo wanasema sasa kwamba yeyote anayeonekana kuwa anaweza kuwa tishio mwaka 2015, amekuwa akiitwa si mchapakazi, haimudu kasi, ari na nguvu mpya, hatekelezi ilani ya CCM na tunaona vitimbi vingi wanavyofanyiana wakubwa hawa.

Wachuguzi hawaishii hapo tu wanasema hata wale walio katika kundi la vigogo ambao hawana matarajio makubwa ya kuwa katika kinyang'anyiro cha 2015 lakini kwa namna moja au nyingine kama hawawakubali wakubwa hawa pia hutafutiwa hila za TAKUKURU na kudhalilishwa kwa nia ya kuwapuguza nguvu za kisiasa.

Wakati umefika sasa kwa wananchi kutoka katika gome la mti wa woga tulimofunikwa kwa miaka mingi na kuanza kulalama, kutetea haki na raslimali zetu, utu na heshima ya taifa letu kwani dalili zote zinaonyesha kwamba watu tuliowaamini na kuwapa dhamana ya uongozi wengi wana walakini mkubwa kiasi cha wananchi wengi kuona kwamba si tu tunaporwa nchi yetu lakini hata haki yetu ya kulalama pia inaporwa!

Natumaini wengi watakubaliana nami kwamba unapoonewa na mkubwa wako, haki ya kulalama ndiyo njia pekee ya amani ya kumuumbua mkubwa huyo na hatua ya kwanza ya kukomesha udhalimu anaokufanyia. Sasa basi, iwapo kama kuna kiongozi ambaye hata haki hii ya kulalama anataka kutunyag'anya kwa hila, kiongozi huyo kwa maneno ya hayati Mwalimu Nyerere ni wa kuogopwa kama ukoma.

Nalisema hili baada ya kufuatilia vizuri jinsi haki yetu ya kulalamika inavyouawa kiana. Kuna habari zilizozagaa mjini Dar es Salaam kwamba, ndugu yangu Kipanya amenya’ganywa penseli ya kuchorea vikatuni vinavyo beza mkangayiko wa uongozi. huku ndugu yangu Jenerali Ulimwengu naye amebakia akisubiri lifti ya kupelekwa ama kualikwa katika pango linapojikokeza la makongamano au warsha ili huko walau akaendeleze kutoa RAI zake zilizo huru zaidi kutoka moyoni mwake.

Katika nchi nyingi wasomi hasa wa vyoo vikuu ndiyo tegemeo, dira na ngao ya kukimbilia kwa wananchi kupata muongozo na msimamo thabiti wakati utawala wao ikiyumba au kujisahau.

Hivi karibuni Mzee Butiku alisema sana pale aliposema kwamba alishuhudia vitendo na kupokea habari za rushwa katika uchaguzi wa CCM wa mwaka 2005 huku akiwa mbele ya mtu aliyemtaja kuwa ni Profesa Mukandala.

Karibuni pia kumezuka uvumi kwamba kuna habari za kutaka kumsulubu Mzee Butibu katika vikao vya CCM, naomba tusali kwa Mungu na kumuombea mzee wetu yasije yakamkuta yaliyomkuta hayati Kolimba, Bwana ahimidiwe.

Naomba nikomee hapa mpaka wiki ijayo kutoa nafasi kwa wegine wanaolitakia mema taifa letu nao watoe tathmini zao ili kuliokoa taifa letu lisiendelee kwenda kombo. Mungu ibariki Tanzania.

*Mwandishi wa makala haya amejitambulisha kuwa anaishi mjini Dododma. Anapatikana kupitia barua pepe; kiganjam@hotmail.com.

Source-Majira 26/10/2007
 
Je ni kweli Kipanya Kanyang'anywa penseli yake? na Mzee Butiku anataka kusulubiwa na SISIEM?

Na kama mtu kama Prof. Mkandala na ile NGO cover yake ya REDET wanaendesha utafiti wa upimaji wa viongozi ambao yeye mwenyewe alishuudia mambo ya RUSHWA yakiwaweka madarakani, je tunaweza kuwa na imani na matokea ambayo yatatolewa?

Politics za Tanzania hazina mfano duniani kwani ni kichekesho.
 
swali zuri lakini sidhani kwa watu waliokuwepo hapa wapo tayari kuona rais anasaksidi ! umegusa mengi mazuri, nitarudi bidae kuongeza !
 
Uwezo wa kumfanyia mbaya Butiku hawana hata kidogo,kama unabisha kamuulize Warioba na Salim,yaani litakua kosa kubwa la kiufundi,hata Mkapa na Kikwete wanalijua hilo,.
 
Back
Top Bottom