Mbinu za kukwepa kusinzia darasani, ibadani au kazini

Samahani

JF-Expert Member
Oct 29, 2018
222
335
Kwa wengi wetu tatizo la kusinzia ‘ovyo’ limekuwa ni la kawaida sana tuwapo ofisini, kwenye semina au darasani. Pamoja na ukweli kuwa walio na umri mkubwa zaidi wanateseka zaidi na hili, na mwamba pia wapo ambao imechukuliwa kuwa tabia na mazoea yao, lakini kwa namna kubwa waathirika ni wengi sana.

Kuna ambao wanapoingia tu ofisini, hasa wale ambao kazi zao zinahusisha utulivu fulani, ndani ya dakika chache sana wanaanza kusinzia au 'kudonoa'!! Kwa upande wa wanafunzi nako hakuna ahueni. Wapo ambao wanalazimika mpaka kuingiza miguu kwenye maji, kutafuna pilipili au tangawizi, kunywa kahawa au ‘energy drink’, lakini wakati mwingine, hivi vyote vinakwama na kusinzia kunabaki palepale.

Hebu tujaribu mbinu hizi, huenda zikawa ni baadhi tu ya mbinu za kupunguza tatizo.

1. Jenga utaratibu wa kulala mapema.
Hii ni mbinu ya uhakika zaidi. Tunakuwa 'wakamiaji' wa masomo na kazi mpaka tunasahau kuwa, upo ulazima wa kulala kiasi cha kutosha. Fuata ushauri wa kulala zaidi ya saa nane kabla ya kuingia darasani, kazini au kwenye semina. Weka ratiba ya kulala na kuamka na uifuate sana ili mwili uizoee.

2. Zingatia kanuni za lishe.
Kuna baadhi ya vyakula sio rafiki sana ikiwa unataka kutumia muda mrefu ukiwa macho. Mathalani, vinywaji vyenye kafeini vinaleta sana usingizi. Pia, kula vyakula vizito sana kunaulazimisha mwili kumeng’enya na matokeao yake tunajikuta tunasinzia. Wengi tunajua madhara ya uji au ugali kwa maharage ulivyotusulubu tukiwa shule za bweni. Pendelea vyakula laini na matunda ili zoezi ya usagaji wake lisiingilie sana mfumo wako wa akili.

3. Weka na heshimu ratiba ya mazoezi

Mazoezi ni mbinu nyingine nzuri sana ya kujiweka sawa. Dakika thelathini mpaka saa za mazoezi kwa siku, hasa yale mepesi yanasaidia sana kuuweka mwili kwenye msawazo. Sio tu ujipangie kuhusu mazoezi, bali iheshimu ratiba yako na iwe endelevu ili mwili pia uizoee na kuikubaki. Tembea tembea, ruka ruka na jinyooshe ili kuuchangamsha zaidi mwili.

4. Jishughulishe
Wakati mwingine tunapokuwa darasani au kazini, wengi hatupendi kujishughulisha na matukio yanayoendelea. Mtu anakuwa darasani lakini haandiki chochote, hajibu maswali wala kushiriki mijadala. Katika nyumba za ibada, wengine hata ile kuitikia tu salamu na kufuatisha vitu kama nyimbo au utani unaendelea hatutaki. Ofisini mtu unamkuta hafanyi kazi yoyote amekaa tu. Kwa namna hii kusinzia ni jambo la kawaida. Jishughulishe kwa bidii sana kwenye yote ambayo yanafanyika ili uwe makini zaidi.

5.Tumia chumba chenye hewa ya kutosha
Baadhi ya vyumba vyetu vya ofisi au shule havina hewa ya kutosha. Joto kali na upungufu mkubwa wa hewa unatulemea na kujikuta tukiwa ‘ndotoni’. Hakikisha kuwa unatumia chumba ambacho kinaruhusu mzunguko mzuri wa hewa, lazma utakuwa popo tu. Wakati mwingine inapobidi, sogea pahala penye upepo asili au hata feni kwa muda ili kuuburudisha mwili.

6. Epuka vinywaji vinavyoweza kukuchosha
Kuna ambao huzimaliza siku zao kwa ‘kujipongeza’ na pombe nyingi. Tafiti zinathibitisha kuwa, unapotumia pombe nyingi siku inayotangulia, unaamka na "hangover" ambayo ni hatari sana kuleta usingizi. Kiuhalisia, hangover inakutoa kabisa kwenye hali nzuri, kimwili, kiakili na kihisia. Ndio maana wengi katika kujaribu kuipunguza hujikuta wakitafuta tena pombe mpya ili "kuiamsha" ya siku iliyotangulia.

Thibiti kwa kiasi kikubwa utumiaji wa pombe hasa katika siku zinazotangulia ratiba yako ya kazi na elimu au ibada.

7. Kunywa maji kidogokidogo

Maji ni kinywaji cha uhakika sana katika kusaidia mwili kuondoa uchovu. Ni vema ukiwa shuleni, warsha, ibadani au kazini ukawa na chupa zako kadhaa za maji. Unapoendelea kuupa mwili wako maji ya kutosha, unausaidia zaidi kujiweka kwenye msawazo na kuondoa tatizo la usingizi.

8. Nawa uso na jimwagie maji baridi
Unapoona umezidiwa, umuhimu wa maji ni mkubwa zaidi kunawa au kama mazingira yanaruhusu, kuoga. Wakati mwingine tunasinzia kwa uchovu. Thibiti uchovu huu kwa kujimwagia maji ya baridi kwa matokeo mazuri

9. Jipe dakika chache za kusinzia
Inapotokea unahisi usingizi umekuwa mzito sana, pendelea kusinzia kwa dakika chache ikiwa mazingira ni rafiki. Dakika tano mpaka kumi za kupata usingizi kidogo (nap) zinasaidia sana kuutawanya usingizi na kukupa umakini zaidi.

10. Jongea na jichangamshe
Unapokuwa kazini, kwenye semina, darasani au eneo la ibada, pendelea kujipa vichangamsho (energizer). Usikae pahala pamoja kama gogo. Ukiweza jinyooshe, nenda msalani, toka nje kwenye hewa na zingine kama hizo. Pia, unaweza kuangalia baadhi ya picha, video au mziki unaoupenda sana ili kuiburudisha akili yako kwa dakika chache kisha ukaendelea

11. Epuka sababu za uchovu zilizo ndani ya uwezo wako
Kitaalamu, usingizi ni matokeo ya kuukosa usingizi kwa muda mrefu, uchovu, njaa au shibe iliyozidi. Pangilia vema sana mfumo wako wa maisha kuepuka yale ambayo yanakupa usingizi pale usipouhitaji.

12. Jifundishe kusema ‘inatosha kwasasa’
Wakati mwingine tunafanya mambo ya kupitiliza. Akili ya binadamu ina utaratibu wa kukulazimisha kupumzika. Kama ni shuleni, ingia kwa wakati na toka kwa wakati. Usisome kwa wakati mrefu sana mpaka akili ifikie kiwango cha kukataa kuiendelea kukupa ushirikiano. Kazini pia, weka utaratibu wa kwenda kupata kifungua kinywa, chakula cha mchana, kuongea na wengine na vingine, lakini kwa kiasi.

13. Badilisha ratiba/ masomo
Kuna kazi tu zina utaratibu wa kuchosha akili kupitiliza. Hata masomo pia, kuna ambayo ukianza tu kuyasoma unaanza kusingia. Kwenye warsha na semina, kuna watu wakianza kuzungumza tu, wanachosha. Jipe nafasi ya kuiburudisha akili yako pale unapoona inahitaji kitu cha tofauti. Kama ni ofisini, wakati mwingine anza hata kupanga panga mafaili kabla ya kuendelea na kazi ngumu zaidi.

14. Tumia vema kinywa
Ingawa hii si rahisi sehemu nyingi, lakini pale mazingira yanaporuhusu, kuwa na vitu vya kula kama pipi, karanga, kahawa, jojo na vingine. Hivi huwa vinakusaidia kuweka umakini wako katika kinywa na hivyo kuishughulisha akili pia. Zingatia sana kanuni nyingine za afya katika hili maana kula nara kwa mara kunaweza kuwa na matokeo mengine hasi.

Muhimu zaidi ni kuijua vema sana ratiba yako. Saa 24 kabla ya siku ambayo hutaki kusinzia zitumike kwa umakini mkubwa katika kuyafanya hayo

Naamini hizi pamoja na zingine nyingi watakazoongeza wadau zinaweza kuwa msaada mkubwa sana kwa wenye tatizo kama hili.

Sijasema popote na wala sikuwahi kumwambia yeyote kuwa, hayo ni mwarobaini wa matatizo yetu na eti hayo yatawasaidia wote kwa wakati wote. Lakini kwa kuwa ni njia, na zimeshawasaidia baadhi, tuzijaribu!!

Wasalaam,

Mwenye Kunoa Lubu,

ZEE LA KALE
 
Kwa wengi wetu tatizo la kusinzia ‘ovyo’ limekuwa ni la kawaida sana tuwapo ofisini, kwenye semina au darasani. Pamoja na ukweli kuwa walio na umri mkubwa zaidi wanateseka zaidi na hili, na mwamba pia wapo ambao imechukuliwa kuwa tabia na

ZEE LA KALE
Somo zuri Sana tukijaribu kufwata ushauri hapo juu naamin tutafanikiwa kuacha kusinzia
 
epuka kutumia simu ama kutizama TV lisaa limoja ama nusu saa kabla ya kulala na baada ya kuamka asubuhi
epuka vyakula vya asubuhi vyenye hamira, maharagwe etc

*morning glory nazo huchangia watu kusinzia sinziaa kazini <try to abstain>
 
Duuh wengne tunatafuta usingizi kwa gharama sana. I wish ningekua na usingizi ninge enjoy sana
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom