Mbele ya mali, haki yakaa mbali | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mbele ya mali, haki yakaa mbali

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Msindima, Sep 23, 2009.

 1. M

  Msindima JF-Expert Member

  #1
  Sep 23, 2009
  Joined: Mar 30, 2009
  Messages: 1,018
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 135
  MARA nyingine huwa najiuliza uchaguzi unatusaidia nini wakati ambapo walio nacho wadanganya waziwazi na wasio nacho wadanganyika bila wasiwasi.


  Lakini baada ya mjadala mkali wa sebuleni, nilitambua kwa mara nyingine tena kwamba, kama kawaida, ukiwasikiliza watu waishiwa badala ya kuwashinikiza wajifunza mengi utajifunza mengi.

  Alianza mwishiwa kijana, maana sisi waishiwa hatuna ukiritimba wa wazee hata kidogo. Vijana wanakaribishwa sana kwa ujana wao, si kwa kugeuzwa jeshi la chama hiki au kile. Basi yule kijana alianza kwa kutushangaza.

  “Mwishiwa Supu, nataka kutoa pendekezo kwamba, sisi waishiwa tuanzishe chama chetu”.

  Hapo waishiwa walianza kupiga kelele kwa nguvu maana kama kuna kitu ambacho ni sumu kwa waishiwa ni chama chochote kile.

  “We kijana kama umetumwa na walewale wa Cheo Changu Mali, toka hapa”.

  “Tutakushtaki kwa uhaini na kukufukuza kwenye sebule hii, kama si kukunyima siku mwezi mzima”

  “We Bwana kwa mawazo hayo nyie vijana si taifa la leo, wala kesho, labda taifa la mtondogoo”.

  Kijana hakuonekana kufadhaika. Alikuwa anacheka tu lakini Mwishiwa Supu aliingilia kati.

  “He, jamani mbona na nyinyi mmeanza kuonyesha tabia ya haohao mnaowapinga? Hujangoja kumsikiliza hata kidogo na mmesahau kwamba, daima mawazo mapya yanatokana na mtu asiyekubaliana na wewe”.

  Waishiwa walitulia na mwishiwa kijana aliweza kuendelea.

  “Namshukuru Mwishiwa Supu kwa kunitetea. Mara nyingine tunagonga kichwa mlangoni hadi tunakipasua. Kumbe tukitafuta ufunguo mwingine mlango unafunguka. Chukua suala la wagombea binafsi. Sote tunajua ni haki yetu. Misahafu yote ya demokrasia inahubiri kwamba, ni haki yetu hata mahakama yetu inatamka kuwa ni haki yetu, lakini kwa kuwa watu wa Cheo Changu Mali wanaogopa kupoteza mali hatutapata kamwe katika mfumo uliopo.”

  “Haya, kijana sema,” mmoja wao.

  “Sasa kwa nini tusiige mfano mzuri wa wenzetu wa Kenya na kuanzisha Chama cha Wagombea Binafsi. Kule kwao kinaitwa Party of Independent Candidates Kenya (PICK) na kweli unapick, unachagua mgombea unayemtaka si kwa sababu ya chama chake, lakini ni kwa sababu unaona kweli anakufaa. Kwa njia hiyo unakuwa ndani ya chama kama inavyong’ang’aniwa na waoga wa demokrasia, lakini bado wanabaki na akili zao timamu bila kupigwa pasi na chama chochote”.

  Lo! Waishiwa walewale waliokuwa wanapinga na kukashifu wakabadilika ghafla na kuanza kumshabikia yule kijana.

  “Adumu mwishiwa kijana. Hili ni wazo la maana sana”.

  Wengine walitaka kuondoka papohapo na kuanza kusajili chama hiki. Chama cha Kugombea Uhuru (CHAGU) lakini yule kijana aliendelea.

  “Waishiwa wenzangu, sijamaliza. Napenda pia kutoa mawazo kuhusu sera za chama chetu kipya.”

  “Ohoo, unaanza mambo ya sera tena. Nilifikiri kila mmoja anaruhusiwa kutumia akili.”

  “Ndiyo lakini bila mijadala tutanoaje akili zetu? Kwanza kila mwanachama lazima akubali kwamba, hana habari na biashara ya kwenda ikulu.”

  Waishiwa walicheka na wengine waligonga meza hadi bia zao ziliruka. Ilibidi wazishike haraka kabla mambo hayajaharibika.

  “We Bwana, kwa nini uachane na biashara hii?”

  “Huoni ilivyowatokea walioweka kipaumbele kwa Ikulu … au kupita juu kwa juu ndani ya helikopta? Demokrasia haijengwi angani. Inajengwa ardhini. Bila hivyo ukitokea upepo kidogo demokrasia inaanguka kama tembo aliyejeruhiwa na sisi manyasi tunaumia tena.”

  “Haya endelea.”

  “Tena hata kugombea ubunge iwe ni kwa nadra sana. Maana kila anayetaka kujiunga na chama lazima aonyeshe kwamba, ni mkereketwa kweli kweli wa eneo lake. Si mkereketwa wa Cheo Changu Mali au chama chochote kingine. Mkereketwa wa eneo lake. Hatapumzika hadi kata yake ipate maendeleo, si kwa kulazimisha au kuhonga, bali kwa kuweka mipango madhubuti na wananchi wake.”

  Waishiwa walitaka kuingilia tena lakini Mwishiwa Supu alawatupia jicho kali hivyo waliendelea kushika chupa zao huku kijana anaendelea.

  “Tatu, baada ya kuangalia mwenendo wa uchaguzi nimegundua kwamba haidhuru kabisa tunamchagua nani. Tunataka mwakilishi tunapata mwajilishi tu. Anapotea miaka mitatu hadi minne kisha mwaka wa mwisho anarudi na kuanza kusimamia maendeleo aliyotakiwa kusimamia tangu mwanzo.”

  “Ndiyo! Lazima tuwaondoe hawa!”

  “Sasa unajuaje kwamba hautaweka mjilishi mwingine badala ya mwakilishi? Mfumo unaruhusu wajilishi tu. Na katika hali ya sasa anajua kwamba anatulisha kidogo ili ajilishe zaidi baadaye. Hata kama unajua ni mjilishi utafanya nini?”

  “Sema basi.”

  “Nimetembelea miji mitatu kwa wiki moja. Kila mahali ghafla barabara zinakwanguliwa.”

  “Wanadanganya tu, ili tuwachague.”

  “Si ndiyo! Tena nyingi zinakwanguliwa tu bila hata wazo la kuweka muram au kitu kingine kwa hiyo nasikia wanasiasa wengine wanaenda kwa waganga kuomba mvua isinyeshe kabla ya uchaguzi, maana ikinyesha tu wamekwisha.”

  “Kwa hiyo inatusaidia nini?”

  “Kwa nini tungoje miaka mitano kabla ya kukwanguliwa barabara. Kwa nini zisikwanguliwe mara nyingine zaidi. Ndiyo maana chama cha CHAGU kitapendekeza kwamba uchaguzi ufanyike kila miaka mitatu baada ya miaka mitano.”

  Waishiwa wengine walicheka.

  “Kweli Bwana. Watatuhonga kila miaka mitatu badala ya miaka mitano. Kwa hiyo tutafaidi mara nyingi zaidi kabla ya kujiondokea kwao kujilisha tena.”

  “Ndiyo lengo langu. Wananchi wafaidi mara nyingi zaidi.”

  Lakini mwishiwa mwingine akasimama.

  “Pamoja na mawazo mazuri ya mwishiwa aliyetangulia …”

  “We Bwana toka hapo na lugha hiyo ya kirasimu. Sema unalotaka kusema …”

  “Ngoja basi. Upande wa wananchi kufaidi, naungana na mwishiwa. Lakini tusisahau kwamba uchaguzi ni uchafuzi, tena uchafuzi wa kuchefua kabisa, hadi wengi tunatapika kila uchafuzi ukikaribia.”

  “Makubwa. Wajilishi watulishia kisha watutapikisha.”

  “Hapo sasa. Katika kutapatapa wanatutapikisha. Angalia hata uandikishaji wa kura mahali ambapo wana wasiwasi juu ya upinzani Kisha matumizi ya nguvu. Nikiangalia baadhi ya hao wakienda kwenye michezo na kuhubiri kwamba asiyekubali kushindwa si mshindani, natapika hata kabla ya wakati. Kweli tuna uongozi ambao unakubali kushindwa?”

  “Hakuna! Wakiona watashindwa, watatumia hila zote ili washinde. Barabara iliyokwanguliwa ni kitu kidogo tu. Tukikataa kudanganywa na kukwanguliwa kwa barabara, tunakwanguliwa sisi na matumaini yetu yote yanamwagwa mchanga kama vile sisi ni barabara.”

  Kijana akaingilia kati tena.

  “Ni kweli si ni barabara. Wanatuona barabara ya kuwafikisha kwenye mji wa kujilisha. Sikatai uchaguzi ni uchafuzi. Sikatai pia kwamba wengi wa Cheo Changu Mali hawako tayari kukubali demokrasia. Mbele ya mali, haki yakaa mbali. Angalia Wamaasai. Sasa wanafukuzwa hata katika nchi yao, si boma lao tu. Ndiyo maana nataka tuwe na chama cha wakereketwa wa maendeleo. Tukikusanyika hivyo na kulazimisha uchaguzi mara nyingi zaidi mwisho watakoma.”

  “Wachaaa!”

  “Kweli. Wao wanaona siasa kama uwekezaji. Unawekeza kwanza kisha unatumia miaka mitano kurudisha mtaji wa kuwekeza na kupata faida. Kwa miaka mitano si vigumu, lakini kwa miaka mitatu itakuwa vigumu zaidi.”

  “Si watatukamua zaidi hadi kutukomoa.”

  “Na katika kukomolewa tutajua njia ya kukombolewa pia. Lazima tupate wapiga kura ambao wako tayari kuhongwa na mtu mwenye mikono mitupu.”

  “Unaongelea nini tena?”

  “Ni wazi sana. Kwa sasa tunawachagua watu wenye mikono iliyojaa na utupu wa mawazo. Bora tuwachague watu wenye mikono mitupu lakini akili iliyojaa na azma ya kuendeleza wananchi wenzao. Kama alivyosema mwishiwa Makengeza hapa ‘kula kwa huyu, kura kwa yule.’ Hapa ndipo tutabadilisha mfumo.”

  “Lakini kijana hayo yatawezekana wapi wakati tunajua kwamba wakionekana kushindwa watashinda kwa nguvu tu?”

  “Wakati umefika kwa vijana kusimama imara. Ukiwaangalia wanawake bado wanadai umoja wao ni wa kitaifa, lakini vijana bado ni mali ya chama kimoja. Tukisimama na kusimamia wenye nia ya kutumia nguvu watashindwa.”

  Baada ya mazungumzo marefu, waishiwi wakasimama na kusema kwa nguvu moja.
  ‘CHAGU idumu! Hatudanganyiki! Hatudanganyiki na barabara zilizokwanguliwa dakika za mwisho, wala ahadi za uongo. Angalieni kama mtawaweza kutukwangua na sisi.”

  NIMEISOMA HII KWENYE MAONI YA WAHARIRI KATIKA GAZETI LA MWANANCHI NIKAIFURAHIA
   
Loading...