Mbaya wa jerry muro matatani

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,956
22,149
Mbaya wa Jerry Muro matatani

na Mwandishi Wetu


amka2.gif
HATIMAYE mlalamikaji aliyemwekea mtego mwanahabari wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), Jerry Muro, na wenzake wawili, Michael Wage Karoli, ameanza kuchunguzwa kwa tuhuma zake za ufisadi.
Wage ambaye alikuwa mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo na baadaye kusimamishwa kazi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameanza kuchunguzwa na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata zinasema kuwa Wage anachunguzwa na TAKUKURU Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na wenzao wa jijini Dar es Salaam.
Habari hizo zinasema uchunguzi dhidi ya Wage ulianza baada ya kusimamishwa kazi na Waziri Mkuu Pinda na hata wakati alipokuwa akifuatwa na watu waliojifanya kuwa ni maofisa wa TAKUKURU, tayari alishakuwa chini ya uchunguzi.
“Wage yuko kwenye uchunguzi dhidi ya tuhuma za ufisadi zinazomkabili. TAKUKURU wamefuatilia taarifa zake mbalimbali na wakati wowote kuanzia sasa atafikishwa mahakamani,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Kwa mujibu wa habari hizo, mara ya mwisho Wage alihojiwa na TAKUKURU juzi na bado anaendelea kuhojiwa na kuchunguzwa zaidi akiwa nje kwa dhamana.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano kuhusiana na uchunguzi huo, Ofisa Uhusiano wa TAKUKURU jijini Dar es Salaam, Doreen Kapwani, alisema hana taarifa za uchunguzi dhidi ya mtuhumiwa huyo, kwani yuko chini ya TAKUKURU mkoani Pwani.
“Hapa makao makuu sina taarifa hizi, inawezekana hazijatufikia, lakini hata kama anachunguzwa katika hatua hii si rahisi kujua taarifa zake hadi hapo atakapopanda kizimbani,” alisema Kapwani.
Wage anadaiwa kuweka mtego dhidi ya Muro wa sh milioni 10 anazodaiwa kuziomba ili asirushe kipindi kinachoonyesha mali anazomiliki kifisadi, yakiwamo majumba na mahoteli yaliyopo mkoani Morogoro.
Tayari Muro amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, akikabiliwa na mashitaka ya kuomba rushwa ya sh milioni 10 kutoka Wage.
Mbali na mwanahabari huyo anayetetewa na wakili wa kujitegemea, Pascal Kamala, washitakiwa wengine katika kesi hiyo inayovuta hisia za watu ni Edmund Kapama na Deogratius Mgasa.
Kesi hiyo ambayo iko mbele ya Hakimu Mkazi, Gabriel Milumbe wa Mahakama ya Kisutu, washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matatu.
Shitaka la kwanza ni la kula njama kwa mujibu wa kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.
Inadaiwa kuwa Januari mwaka huu, jijini Dar es Salaam, Muro na wenzake walikula njama kwa nia ya kutenda kosa linalohusiana na rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.
Katika shitaka la pili, inadaiwa kuwa Januari 29 mwaka huu, wakiwa katika Hoteli ya Sea Cliff, washitakiwa waliomba rushwa ya sh milioni 10 kutoka kwa Wage ili habari zake kuhusu ufisadi zisitangazwe kwenye kituo cha televisheni cha TBC1.
Aidha, shitaka la tatu ambalo linawahusu Kapama na Mgasa ni la kujipachika wadhifa wa uongo.
Ilidaiwa kuwa Januari 29 mwaka huu, katika Hoteli ya Sea Cliff, jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao wakiwa na lengo la kumlaghai Wage, walijitambulisha kuwa ni waajiriwa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), huku wakijua si kweli.
Muro na Kapama walitimiza masharti ya dhamana lakini Mgasa alishindwa, hivyo kupelekwa rumande hadi Februari 12 kesi hiyo itakapotajwa tena.
Mwandishi huyo alikamatwa Januari 31 majira ya saa 5 asubuhi katika Hoteli ya City Garden iliyoko katikati ya Jiji la Dar es Salaam baada kuwekewa mtego na polisi.
Muro ambaye amejipatia umaarufu kutokana na kuandika habari za uchunguzi kuhusu rushwa, alikutwa na pingu katika gari alilokuwa akilitumia, akidaiwa kutaka fedha kwa njia ya vitisho kwa Wage, ambaye hivi karibuni alifukuzwa kazi na Waziri Mkuu, Pinda.
Hadi sasa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP), Said Mwema, ameunda kikosi kazi kuchunguza uhalali wa raia kumiliki pingu, kutokana na utata wa sheria ulioibuka hivi karibuni.
Mwaka jana Muro alishinda tuzo ya mwandishi bora wa mwaka na kipindi cha ITV ambacho kilisababisha askari kadhaa walioonekana wakipokea rushwa kufukuzwa kazi, ndicho kilimpandisha ngazi.
Kadhalika kipindi cha TBC1 nacho kimepeleka kilio kwa askari waliomulikwa, na sasa wanachunguzwa kabla ya kufukuzwa kazi kwa kula rushwa.
 
Tusubiri Ijumaa hii mambo yatakuwaje kwa Muro na wenzake,
 
Back
Top Bottom