Maziko ya Bi. Safia bint Juma Makasara - Mama yake Balozi Dr. Dau

Ukipata muda na kama hautajali naomba utuwekee hiki kisa hapa.
Fsami,
Hii makala ni ya mwaka wa 2017 niliiweka hapa katika kueleza historia ya TANU wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika:

''Kwa kuwa umependa kumbukumbu hizi za nyumbani kwetu Gerezani basi
nataka nikupe kisa kilicholeta taharuki kubwa ambayo naelezwa haijapata
kutokea katika historia ya TANU na Nyerere labda hadi Baba wa Taifa
anaaga dunia.

Siku za mwanzo za TANU viongozi wake walikuwa wakiwa na jambo zito
la kujadili walikuwa wakikutana nyumbani kwa Abdul Sykes Mtaa wa
Stanley na Sikukuu.

Walikuwa wakimaliza shughuli basi inakuwa chakula na vinywaji kujipongeza.
Siku hiyo baada ya kikao wakala chakula cha mchana.

Baada ya kula ghafla Nyerere akaanza kulalamika kuwa tumbo linamkata.
Nyerere akawa anajipindua huku na huku kwa maumivu.

Siku zote TANU walikuwa wakiishi chini ya hofu ya Nyerere kudhuriwa na
maadui wa TANU lakini katika chakula kile cha nyumbani kwake hapakuwa
na hofu kwani chakula chake kilikuwa kinatoka Kariakoo na kwa watu maalum
ambao Market Master, Abdul Sykes akiwafahamu na Mzee Mshume na ndiye
akikinunua, mpelekaji wa chakula hicho kwa Mama Maria alikuwa dereva wa
TANU, Said Kamtawa maarufu kwa jina Said TANU.

Nyerere kalala kwenye kochi anaugulia na taharuki ikazuka na minong'ono
haikuweza kukwepeka.

Nyerere kalishwa sumu!

Sumu Nyerere alishwe nyumbani kwa Abdul Sykes?

Uani jikoni walikuwa mama yake Nyerere Bi. Mgaya, Mama Maria, mama
yake Abdul Sykes Bi. Mruguru bint Mussa,
mkewe Abdul Sykes, Mama
Daisy.

Bi. Mgaya
hakuweza kustahamili alipoona wanaume ingia toka kule ndani.

Aliposikia kuwa Nyerere anaumwa baada ya kula chakula kitu cha kwanza
kilichomjia ni kuwa mwanae kalishwa sumu akawa sasa mikono kichwani
analia na kutembea ua mzima.

Bi. Mgaya anasema Kizanaki na anachanganya na Kiswahili.
Ikawa patashika nguo kuchanika kumtuliza.

Wote waliokula chakula kile walikuwa salama na hawa ni watu waliokuwa
wakijuana vizuri na wakiaminiana mwisho wa imani.

Nani anaweza kupenya nyumbani kwa Abdul akampa sumu Nyerere?
Nani?

Mama Daisy ndiye alikua akinihadithia alipomaliza aliinamisha kichwa
akasema, ''Mwanangu Mohamed, Abdul na Nyerere wametoka mbali
sana na walikuwa zaidi ya ndugu.''

Iko siku nitakileta hapa kisa cha sanduku la fedha la Abdul Sykes.''
 
Sasa mkuu wewe Tozo hazijakukumba huko ulipo ? Nimekuomba tu vigezo vya ukubwa na udogo kama hautojali kwa sentensi chache wewe unaniambia nikatumie MB zangu chache za kudunduliza nikaangalie video..., Kweli tunatakiana Heri sisi kama Watanzania ?
Key...
Pole sana ndugu yangu.

Maziko ya Abdul Sykes ni kama vile Kariakoo na Gerezani ilikutanishwa mahali pamoja.
 
Shukrani kubwa kwako!

Nasubiri pia cha "sanduku la fedha", au kama tayari uliweka hapa naomba link.
Fsami,
Vuta subra nitakufungulia hilo sanduku ambalo chanzo cha fedha hizo ilikuwa kituo cha mafuta cha Mobil Oil alichokuwa akimiliki Abdul Sykes pale Ilala Boma.

Huu ulikuwa mwaka wa 1950 na Abdul alikuwa na umri wa miaka 26.

Kituo hiki bado kipo pale na ni kituo cha mafuta chenye historia kubwa katika uhuru wa Tanganyika.
 
MAZIKO YA BI SAFIA BINT JUMA MAKASARA MAMA YAKE BALOZI DR. RAMADHANI KITWANA DAU YAMEVUNJA REKODI YA MAZIKO YOTE

Mji wa Dar es Salaam una historia ndefu ya mazishi makubwa yaliyopata kutokea.

Mimi nakua katika miaka ya 1960 nikiwasikia wazee wetu wakihadithia maziko ya Sheikh Idrissa bin Salad Khalifa wa Tariqa Askariyya.

Wanasema maziko yake hayakuwa na mfano.

Nimeanza na Sheikh Idrissa bin Saad kwa sababu wazee wakipenda kuanza historia hii na yeye.

Lakini historia hii ya maziko inakwenda nyuma kiasi cha zaidi ya miaka takriban 100 kabla yao kwa hesabu ya wakati ule.

Kwa ajili hii maziko makubwa ya kwanza ni ya Sheikh Mwinyikheri Akida, sheikh aliyeasisi Msikiti wa Mwinyikheri Akida ulioko Kisutu.

Kisha yanafuatia maziko ya Sheikh Idrissa bin Saad.

Yanafuatia maziko ya Sheikh Kaluta Amri Abeid mwaka wa 1963.

Halafu maziko ya Abdulwahid Kleist Sykes mwaka wa 1968.

Kisha maziko ya Sheikh Kassim bin Juma 1994.

Halafu maziko ya Prof. Kighoma Ali Malima mwaka wa 1995.

Maziko ya Prof. Malima yalikuwa ya aina yake kwani kwa mara ya kwanza sala ya jeneza ilisaliwa kwenye kiwanja cha wazi kwani hapakuwa na msikiti Dar es Salaam ambao ungeweza kuenea ule umma uliokuja mazikoni.

Watu wasingeweza.kuenea katika msikiti wowote. Jeneza la Prof. Malima lilisaliwa katika Viwanja Vya Mnazi Mmoja.

Yakaja maziko ya Mzee Kitwana Dau baba yake Balozi Dk. Ramadhani Dau.

Yakafuata maziko ya Sheikh Ilunga Hassan Kapungu.

Aliuliza muulizaji, ''Umma huu wote wa nani hapa mazikoni?

Umma huu wa Ramadhani au wa Mzee Kitwana?

Mtu akajibu, ''Umma huu wamegawana baba na mwananae kwani wote hawa ni watu wa watu.''

Wakati haya yakisemwa kulikuwa na kundi kubwa sana la masheikh na wote katika kanzu nyeupe kama vile wameaagana wanadhikiri.

Hawa walikuwa Qadiriyya.

Kwa miaka ile maziko kama haya ya Mzee Dau yalikuwa hayajapata kuonekana.

Ilikuwa jioni na mwili uikuwa bado haujawasili kutoka Uingereza.

Kila dakika zinavyosogea na ndivyo watu walivyokuwa wanamiminika nyumbani kwa Dr. Dau Kinondoni.

Maziko ya mama yetu Bi. Safia bint Juma Makasara hayajapata kutokea.

Alifariki siku ya Jumatano usiku nyumbani kwa mwanae Balozi Dau na kufikia Alkhamis mchana mahema yaliyokuwa yamefungwa nje ya nyumba yalimstaajabisha kila aliyefika msibani.

Mahema pembeni mwa barabara ubavu kwa ubavu nje ya lango kuu.

Hii si kawaida.

Ndani ya nyumba mahema mengine kwenye uwanja wa mbele na si mdogo.

Nyumba za jirani zote nje yameenea mahema.

Mama yetu kawakusanya watu hawajaonana miaka mingi sana wamekutanishwa na msiba wake.

Toka asubuhi ni visomo na nasaa kutoka kwa masheikh maarufu wa Dar es Salaam.

Sala ya adhuhuri imesaliwa hapo hapo nyumbani halikadhalika sala ya jeneza kwani msikiti wa jirani usingetosha kupokea umma wote ule.

Sala hii ya mama yetu ilinikumbusha sala ya jeneza ya Prof. Malima mwaka wa 1995 katika Viwanja Vya Mnazi Mmoja.

Safari ya kwenda kumzika mama yetu Mkuranga kijijini kwake Mbezi magari yalikuwa yamefunga ''convoy,'' gari moja nyuma ya lingine yalishangaza kila mtu katika vijiji tulivyopita Kilwa Road kimulimuli kikiwa mbele yetu kutusafisha njia.

Bi. Safia mimi ni mama yangu mara ya mwisho kumuona ni miaka mingi kidogo imepita.

Nilikuwa nyumbani kwa Balozi nikapita uani kwenda kumuamkia na nakumbuka nilikuwa nimefikwa na mtihani katika maisha mama akawa ananipa maneno ya kunifariji kisha akaniombea dua.

Zamani sana wakati huo yuko nyumbani kwake Mtaa wa Mvumi, Magomeni na baba yetu Mzee Dau yu hai.

Ilikuwa kila tukienda kumwamkia mimi na Dr. Dau pale nyumbani yeye bila ya kutuuliza tukikaa tu utaona mkeka unatandikwa tunatengewa chakula.

Wakati mwingine tuko katika suti zetu tumetoka katika mikutano ambayo tukihudhuria na mimi nikiwa afisa mdogo Idara ya Marketing Bandarini Ramadhani yeye akiwa Mkurugenzi wa Masoko.

Basi mama atatuangalia na ile misuti yatu tumekaa chini katika mkeka na atatabasamu tu hatiii neno labda kusema, ''Huyo samaki ndiyo kakushindeni?''

Ninachokumbuka ni kuwa kitoweo alichokuwa anatuwekea siku zote ni samaki tena samaki mwenye jina aliyeletwa nyumbani ndani ya kikapu kilichotakata.

Hii misemo ya ''samaki mwenye jina'' na ''samaki asiye na jina'' na ''kikapu kilichotaka,'' yote nimeipata kwa Balozi miaka mingi iliyopita.

Balozi kwao Mafia.
Mtu wa kisiwani.

Tabu kushidananae katika elimu ya bahari na misemo inayohusu samaki.

Wengi naamini watashangaa nikiwaambia kuwa Balozi ni mvuvi tena wa sifa.

Najua ni kwa kiasi gani ndugu yangu Ramadhani msiba huu ulivyompiga kwani natambua yale mapenzi aliyokuwanayo kwa mama yake.

Nakumbuka siku alipopokea simu kuwa bibi yake kafariki tulikuwa sote ndani ya gari yake usiku.

''Mohamed bibi yangu amefariki huyu ndiye aliyenilea mimi,'' Dr. Dau alinieleza akiwa na majonzi makubwa.

Niliongozana na Dr. Dau hijja mwaka wa 1998 na katika msafara wetu alikuwapo bibi yake wakati huo mtu mzima sana lakini alikuwa hataki kubebewa chochote chake kila kitu anataka afanye mwenyewe na Ramadhani muda wote akiwepo bibi yake yuko pembeni yake ingawa alikuwapo mama yetu mdogo kumtazama bibi.

Mume wa kweli mwenye mapenzi ya dhati na mkewe bibi yetu.

Mimi nikimuonea wivu sana Ramadhani.

Allah tunamuomba amrehemu mama yetu na amtie katika pepo Firdaus.

Amin.

View attachment 2019899
Alla amjaze kheir mama yetu na ndugu zetu sote walotangulia mbele ya haki mazishi ya ilunga nilihudhuria ukweli cjapata ona kwa miaka hii ya karibuni
 
Kipuyo,
Naam.

Dunia yangu ilikuwa hiyo.

Wala sikudhani kuwa iko siku nitaiona dunia na miguu yangu itakanyaga ardhi za mbali sana.

Kuwa nitasimama kwenye vyuo vikuu mbali na mitaa ya vumbi ya Gerezani ya 1950s na watu watakuja kunisikiliza nikizungumza.

Iko siku usiku nimesimama Broadway New York Manhattan naangalia magari yanavyopita mengi, mengi, mengi, nikajiuliza hivi huyu ni mie kweli?

Mtoto wa Gerezani na Kariakoo.

Sasa mimi niko katika uzee Gerezani ile haipo tena wala soko lile la Kariakoo Nyerere alipokuwa anakwenda ofisini kwa Market Master Abdulwahid Kleist Sykes halipo.

Nashukuru nimeweza kuihifadhi historia hii.
Kila mtafiti nikimfikisha pale sokoni ananiuliza, "Ilikuwaje hapa miaka hiyo?"

Wanashangaa wananiuliza mbona hatujaweka, "plaque," kueleza umuhimu wa sehemu hii?"
Huyu Ramadan Dau.ni mtu haswa. Kule kilindoni mafia akifika kuingia kila nyumba nakusalimia kwa adabu kabisa.licha ya kuwa anakuja na ndege bnafsi au ya abiria lakini ukishuka hujichanganya na watu wa kawaida waliovaa malapa.
Nakumbuka kijijini kwao kule BWENI aliwajengra watu wake shule yenye hadhi kubwa kabisa.
Alijenga msikiti ambao ulizia sokomoko toka kwa Wazee wahafidhina wengine wakijiapiza kutokuswali pale . Asante mungu yamekwosha.
Dau aliipigania ardhi ya kwao isiporwe na kabisa kwa hila .
Naukumbuka mgogoro wa ardhi pale nyumbani kwake TELENI. Dr. Dau akitumia hekima na kuweza kushinda mgogoro ule. Sasa teleni ipo mikono salama ya wana wa mafia.
Dr. Dau ni mtu haswa. Kazi niliyokuwa naifanya ilinifanya nizijue hila na ghiriba nyingi juu ya mtu huyu.
Sikushangaa ila nilisikitika juu ya mtu huyu aliyeijenga NSSF alipoondolewa kwa matusi na manyanyaso pale ofisini wapo waliomuita mdini ati kila chumba cha ofisi alikigeuza msikiti . Nilishangazwa sana.
Ipo siku wema wanalipwa kwa wema wao.
Dr . Dau anastahili heshima na siyo bezo wala kebehi.
Asante mzee mohamedi saidi
Mungu akujalie sina na maisha marefu.
 
Huyu Ramadan Dau.ni mtu haswa. Kule kilindoni mafia akifika kuingia kila nyumba nakusalimia kwa adabu kabisa.licha ya kuwa anakuja na ndege bnafsi au ya abiria ila
Kwa hiyo Ramadhani Dau anamiliki private jet kwa mizunguko yake ndani ya Tanzania, halafu tukisema amefanya ujangili NSSF mpaka mfuko umefilisika mnasema tuna roho ya korosho.
 
Kwa hiyo Ramadhani Dau anamiliki private jet kwa mizunguko yake ndani ya Tanzania, halafu tukisema amefanya ujangili NSSF mpaka mfuko umefilisika mnasema tuna roho ya korosho.
Dau hajawahi kumiliki private jet acha kupotosha.alichokuwa anafanya ni kukodi ndege.
Gharama ya kukodi ndege toka dar hadi mafia kwa wakati ule haikuzidi ml 1. Kwa cheo na hadhi yake halikuwa jambo kubwa.
Usichokijua ni kwamba mafia kwao na kina dau ndege ni kitu cha kawaida sana
Tuambieni kabla ya dau NSSF ILIKUAJE alipokuwepo na sasa ipoje?
Nani aliifilisi kama siyo yule aliyeunganisha mitsuko?
Tuseme na LAPF Ilifiliwa na Dau? Mbona majengo amebaki magufu pale millennium towers na kwinginepo??
Siyo kila jambo ni siasa
 
Huyu Ramadan Dau.ni mtu haswa. Kule kilindoni mafia akifika kuingia kila nyumba nakusalimia kwa adabu kabisa.licha ya kuwa anakuja na ndege bnafsi au ya abiria lakini ukishuka hujichanganya na watu wa kawaida waliovaa malapa.
Nakumbuka kijijini kwao kule BWENI aliwajengra watu wake shule yenye hadhi kubwa kabisa.
Alijenga msikiti ambao ulizia sokomoko toka kwa Wazee wahafidhina wengine wakijiapiza kutokuswali pale . Asante mungu yamekwosha.
Dau aliipigania ardhi ya kwao isiporwe na kabisa kwa hila .
Naukumbuka mgogoro wa ardhi pale nyumbani kwake TELENI. Dr. Dau akitumia hekima na kuweza kushinda mgogoro ule. Sasa teleni ipo mikono salama ya wana wa mafia.
Dr. Dau ni mtu haswa. Kazi niliyokuwa naifanya ilinifanya nizijue hila na ghiriba nyingi juu ya mtu huyu.
Sikushangaa ila nilisikitika juu ya mtu huyu aliyeijenga NSSF alipoondolewa kwa matusi na manyanyaso pale ofisini wapo waliomuita mdini ati kila chumba cha ofisi alikigeuza msikiti . Nilishangazwa sana.
Ipo siku wema wanalipwa kwa wema wao.
Dr . Dau anastahili heshima na siyo bezo wala kebehi.
Asante mzee mohamedi saidi
Mungu akujalie sina na maisha marefu.
Kinoa...
Amin kwa sote ndugu yetu.
 
Kinoa...
Amin kwa sote ndugu yetu.
1644084913701.png

Dr. Ramadhani Kitwana Dau kabeba picha ya ''Kalima'' katika chakula cha jioni New Africa Hotel kuchangisha fedha kwa ujenzi wa shule ya Kiislam, Nujum Tabora, Mgeni wa Heshima alikuwa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, 1997.

Niliandika makala kuhusu mazishi ya Bi. Safia bint Juma Makasara mama yetu, mama yake Balozi Ramadhani Kitwana Dau nikaiweka Jamii Forums.

Sababu ya kuandika ni kuwa hayakuwa mazishi ya kawaida nikaona niandike kitu katika Jukwaa la Historia ili ibaki kama kumbukumbu kwa watu wa Dar es Salaam wataokuja baada yetu.

Ukapita muda.

Juzi kuna mtu anajiita ‘’Kinoamiguu,’’ akaandika kumweleza Dr. Dau ni nani na kuwa si ajabu kuwa umma wa watu wa Dar es Salaam walijitokeza kwa wingi katika maziko ya mama yake.

Nimeona niweke hiyo makala nanyi wasomaji wangu muisome.

Kaandika Kinoamiguu anasema:
‘’Huyu Ramadhani Dau ni mtu haswa.

Kule Kilindoni Mafia akifika huingia kila nyumba na kusalimia kwa adabu kabisa licha ya kuwa anakuja na ndege binafsi au ya abiria lakini ukishuka hujichanganya na watu wa kawaida waliovaa malapa.

Nakumbuka kijijini kwao kule Bweni aliwajengea watu wake shule yenye hadhi kubwa kabisa.

Alijenga msikiti ambao ulizua sokomoko toka kwa wazee wahafidhina wengine wakijiapiza kutokuswali pale.

Asante Mungu yamekwIsha.

Dau aliipigania ardhi ya kwao isiporwe kwa hila.
Naukumbuka mgogoro wa ardhi pale nyumbani kwake Teleni.

Dr. Dau akitumia hekima na kuweza kushinda mgogoro ule.
Sasa Teleni ipo mikono salama ya wana wa Mafia.

Dr. Dau ni mtu haswa.
Kazi niliyokuwa naifanya ilinifanya nizijue hila na ghilba nyingi juu ya mtu huyu.

Sikushangaa ila nilisikitika juu ya mtu huyu aliyeijenga NSSF alipoondolewa kwa matusi na manyanyaso pale ofisini wapo waliomuita ‘’mdini’’ ati kila chumba cha ofisi alikigeuza msikiti.

Nilishangazwa sana.
Ipo siku wema wanalipwa kwa wema wao.

Dr. Dau anastahili heshima na siyo bezo wala kebehi.
Ahsante Mzee Mohamed Said.

Mungu akujalie siha na maisha marefu.’’
 
View attachment 2109328
Dr. Ramadhani Kitwana Dau kabeba picha ya ''Kalima'' katika chakula cha jioni New Africa Hotel kuchangisha fedha kwa ujenzi wa shule ya Kiislam, Nujum Tabora, Mgeni wa Heshima alikuwa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, 1997.

Niliandika makala kuhusu mazishi ya Bi. Safia bint Juma Makasara mama yetu, mama yake Balozi Ramadhani Kitwana Dau nikaiweka Jamii Forums.

Sababu ya kuandika ni kuwa hayakuwa mazishi ya kawaida nikaona niandike kitu katika Jukwaa la Historia ili ibaki kama kumbukumbu kwa watu wa Dar es Salaam wataokuja baada yetu.

Ukapita muda.

Juzi kuna mtu anajiita ‘’Kinoamiguu,’’ akaandika kumweleza Dr. Dau ni nani na kuwa si ajabu kuwa umma wa watu wa Dar es Salaam walijitokeza kwa wingi katika maziko ya mama yake.

Nimeona niweke hiyo makala nanyi wasomaji wangu muisome.

Kaandika Kinoamiguu anasema:
‘’Huyu Ramadhani Dau ni mtu haswa.

Kule Kilindoni Mafia akifika huingia kila nyumba na kusalimia kwa adabu kabisa licha ya kuwa anakuja na ndege binafsi au ya abiria lakini ukishuka hujichanganya na watu wa kawaida waliovaa malapa.

Nakumbuka kijijini kwao kule Bweni aliwajengea watu wake shule yenye hadhi kubwa kabisa.

Alijenga msikiti ambao ulizua sokomoko toka kwa wazee wahafidhina wengine wakijiapiza kutokuswali pale.

Asante Mungu yamekwIsha.

Dau aliipigania ardhi ya kwao isiporwe kwa hila.
Naukumbuka mgogoro wa ardhi pale nyumbani kwake Teleni.

Dr. Dau akitumia hekima na kuweza kushinda mgogoro ule.
Sasa Teleni ipo mikono salama ya wana wa Mafia.

Dr. Dau ni mtu haswa.
Kazi niliyokuwa naifanya ilinifanya nizijue hila na ghilba nyingi juu ya mtu huyu.

Sikushangaa ila nilisikitika juu ya mtu huyu aliyeijenga NSSF alipoondolewa kwa matusi na manyanyaso pale ofisini wapo waliomuita ‘’mdini’’ ati kila chumba cha ofisi alikigeuza msikiti.

Nilishangazwa sana.
Ipo siku wema wanalipwa kwa wema wao.

Dr. Dau anastahili heshima na siyo bezo wala kebehi.
Ahsante Mzee Mohamed Said.

Mungu akujalie siha na maisha marefu.’’
Namkubali sana dau yuko kibepari sana

Ova
 
Namkubali sana dau yuko kibepari sana

Ova
Mrangi,
Humjui Balozi Ramadhani Kitwana Dau.
Sifa kubwa ya Dr. Dau ni ucha Mungu.

Ubepari si katika sifa zake.
Ukitaka kumjua niulize mimi.

Mimi ni kati ya watu ambao wako karibu na yeye sana tena kwa miaka mingi.
Hiyo picha niliyoweka hapo nimempiga mimi na ukimtazama utamuoana kanyoa kipara.

Wiki hiyo tulikuwa tumetoka Makka na Madina kufanya Umra na ndiyo sababu ya kunyoa kipara.
 
...Timiza hii ahadi sheikh Mohamed..
Proved,
Ahadi ni deni na kesho kiyama Allah atatuuliza katika yale tuliyoahidi hatukutimiza.
Mniwie radhi kwani nilisahau.

Ili tupate picha ya Abdul Sykes niruhusini hapa niweke kipande kutoka kwa binti yake Aisha ''Daisy'' Sykes,'' kutoka makala aliyoandika mwaka wa 2018 katika kumbukumbu ya miaka 50 ya kifo cha baba yake.

Makala hii ilichapwa matoleo matatu katika Raia Mwema.
Naweka hapo chini utangulizi:

Aisha ‘’Daisy’’ Sykes Buruku ni binti ya Abdulwahid Sykes mmoja kati ya wazalendo 17 waliounda chama cha TANU kilichopigania uhuru wa Tanganyika.

Kadi yake ya TANU ni no. 3, Ally Sykes no. 2 na Julius Nyerere ni no. 1.

Daisy kama anavyofahamika zaidi kwa jina hili, ni msichana wa kwanza Mwafrika kusoma Shule ya Wasichana ya Aga Khan mwanzoni mwa miaka ya 1950 na msichana wa pili kuingia Chuo Kikuu Cha Afrika ya Mashariki, Dar es Salaam mwishoni mwa miaka ya 1960.

Daisy amefahamiana na wazalendo wengi mmoja wapo akiwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na machifu mashuhuri kama Mangi Mkuu Thomas Marealle waliokuwa wakifika nyumbani kwa baba yake wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.

Katika kuadhimisha miaka 50 ya kifo cha baba yake, Daisy ameandika makala haya kukumbuka siku zile zilizojenga haiba ya baba yake na ya wazalendo walioshiriki katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Kwa miaka mingi Daisy amekuwa akiishi na kufanya kazi nje ya Tanzania.


''Wageni hawa mashuhuri waliokuwa wakija nyumbani ni pamoja na Mangi Mkuu Thomas Marealle, Machifu Abdiel Shangali, John Maruma kutoka Moshi, Adam Sapi Mkwawa kutoka Iringa, Kidaha Makwaia kutoka Usukuma, Abdallah Fundikira, Harun Lugusha kutoka Tabora, Humbi Ziota kutoka Nzega, Michael Lukumbuzya kutoka Ukerewe na Patrick Kunambi kutoka Morogoro na wengine wengi.

Hawa machifu kwa kawaida walikuwa wakija na wake zao, wanawake warembo ambao hawakuacha kunifanya mimi kuwashangalia.

Nakumbuka katika machifu wale, alikuwapo chifu mmoja na wa pekee mwanamke - Mwami Theresa Ntare kutoka Kasulu Kibondo.

Lakini aliyeshika nafasi ya juu kabisa katika fikra zangu nikiwa mtoto alikuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na ni kupitia kwake ndipo tukapata kujua kwa mara ya kwanza kuwa kuna kabila linaitwa, ‘’Wazanaki.’’

Kila alipokuwa anakuja nyumbani kwetu kuja kwake kulikuwa jambo maalum kulikosababisha minong’ono watu wakizungumza kwa sauti za chini wakipeana taarifa kuwa, ‘’Nyerere anakuja au keshafika.”

Kwangu mimi hii ilikuwa ishara ya kutimiza kazi yangu kwani siku zote nilikuwa nikiambiwa kutengeneza kifungua kinywa cha chai na mayai kila alipokuja nyumbani akitokea Shule ya Mt. Francis, Pugu alipokuwa akisomesha.

Nakumbuka katika akili yangu ya kitoto kumuona Mwalimu Nyerere akiishi nyumbani kwetu kwa muda katika nyumba yetu ya Mtaa wa Stanley baada ya kuacha kazi wakati marafiki zake wa karibu baba na Dossa Aziz walikuwa wanamtafutia nyumba ya kuishi.

Ilikuwa katika kipindi hiki cha mimi kuanza kupata akili katika kukua kwangu ndipo nilipokutana na wanawake wazalendo waliokuwa wanaochipukia katika uongozi wa Tanganyika, wanawake kama Bi. Lucy Lameck kutoka Moshi, Mary Ibrahim na akina mama wa Kiislam kama Bi. Titi Mohamed, Bi. Tatu bint Mzee, Bi. Hawa bint Maftah, hawa kutoka Dar es Salaam, wote hawa kwangu mimi walikuwa bibi zangu.

Kitu cha kufurahisha ni kuwa hawa akina mama wa Kiislam wote walivutwa katika siasa na Bibi Chiku bint Kisusa, maarufu akijulikana kama Mama Sakina.

Alikuwa Mama Sakina ndiye aliyewapa hawa wanawake wa Kiislam niliowataja hapo juu utambulisho na wakaja kuwa watu maarufu.

Baba yeye ndiye alikuwa kiongozi wa mikakati hii yote kwa sababu bila yeye kuwatia hima kwa kutumia ushawishi wake ingekuwa vigumu kuweza kuwatia hawa wanawake katika kuwahamasisha wanawake wenzao wa Kiislam na wao watoke majumbani kuja mstari wa mbele katika mikutano wakiimba na kutoa vibwagizo vya kuunga mkono TANU na kudai uhuru.

Hili jambo lilikuwa jipya, jambo ambalo katika utamaduni wetu kwa wakati ule halikutarajiwa na ni kinyume katika utamaduni wetu kwa wanawake wa Kiislam kulifanya katika siku zile.

Prince Karim Aga Khan alipokuja kutembelea shule yetu mwaka wa 1956, wakati ule alikuwa kijana mdogo na akakagua dafatari langu.

Jambo hili halijanitoka kamwe.

Lakini zaidi ya haya uhusiano wa baba yangu na jamii ya Ismailiyya ulikuja kujitokeza kwa nguvu sana kwa uamuzi wao mwaka wa 1960 kumuuzia baba Mercedes Benz 280S, DSQ 666, ambayo ilinunuliwa makhsusi kwa matumizi ya Prince Karim Aga Khan pale alipozuru Tanganyika mwaka ule wa 1956.

Kwa siku zile hili lilikuwa jambo adhim na kubwa sana, sisi tukiwa watoto wadogo tukipakiwa na baba ndani ya gari hii nzuri na ya kifahari iliyokuwa rangi ya kijivu, hili lilikuwa jambo lisilo na mfano wake.

Baba alijikita sana katika suala la elimu. Akiwa mjumbe katika bodi ya Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika taasisi iliyoasisiwa na babu yangu, Abdallah Kleist Sykes mwaka wa 1933, pamoja na wenzake kama Ali Jumbe Kiro, Mzee bin Sudi na wengineo ambao hawa wote walikuwa vile vile katika African Association, alijishughulisha katika kuwaelimisha watoto wa kike.

Shule hii ya Al Jamiatulul Islamiyya iliyokuwa New Street (sasa Lumumba Avenue) jengo lake lipo hadi leo kama kielelezo cha Waislam katika kujiendeleza katika elimu.

Uhusiano wa baba yangu na shule ya Al Jamiatul Islamiyya unakwenda nyuma wakati wa utoto wake yeye akiwa mwanafunzi katika shule hii iliyojengwa na baba yake.

Mwaka wa 1936 akiwa na umri wa miaka 12 na mwanafunzi hapo shuleni alichaguliwa kusoma risala mbele ya Aga Khan, Sultan Mohamed Shah, baba yake Prince Karim Aga Khan huyu kiongozi wa Ismailiya aliepo sasa, alipoitembelea shule ya Al Jamiatul Islamiyya.

Ikatokea kuwa katika jengo hili la shule hii ya Al Jamiatul Islamiyya ndipo nilipoingizwa na baba kuanza chekechea na nikaanza kusoma Qur’an hapo nyakati za asubuhi na mchana nakwenda kusoma shule Aga Khan.

Uhuru ulipokuwa dhahiri sasa unapatikana na ulipopatikana ulikuja na changamoto nyingi ambazo naamini baba hakuzitegemea.

Haitakuwa sawasawa ikiwa sitaeleza upeo wa juu wa baba yangu katika wema, huruma na unyofu aliokuwanao.

Hata nilipokuwa mtoto nilipata kushuhudia na kuona chokochoko na chuki dhidi yake bila shaka kwa ajili ya hasad kwani baba kwa kiwango chochote kile alikuwa mtu aliyefanikiwa na kwenye ngazi nyingi wengi hawakuthubutu hata kuota kukanyaga, lakini sikumuona baba kukasirika wala kutaka kulipiza kisasi.

Katika unyofu wa hali ya juu aliendelea na maisha yake.''

Ndugu zanguni,
Huyo hapo juu ndiye Abdulwahid Kleist Sykes.

Naamini mmemwelewa alikuwa kiongozi wa namna gani katika TAA hadi TANU.
Sasa tuje kwenye lile sanduku la fedha.

Kitabu kilikuwa kimetoka na siku hiyo nilikwenda nyumbani kwa Mama Daisy kumpa nakala yake ya kitabu.

Tulikuwa tumekaa kwenye varanda yake nyumba yake Barabara ya Ali Hassan Mwinyi iliyokuwa mkabala na Hellenic Club.

Alikipokea kitabu akawa anatazama picha ya mumewe kwenye jalada na akawa kimya kwa muda mrefu.

Bila shaka alikuwa anawaza maisha aliyoishi na baba yetu wakati wa kuigania uhuru wa Tanganyika katika miaka ya 1950.

Mama Daisy alikuwa shoga wa marehemu mama yangu Bi. Baya bint Mohamed na nyumba zao hazikuwa mbali kwani sisi tulikuwa Mtaa wa Kipata na si mbali na Mtaa wa Aggrey.

Naamini kuwa ile mimi mtoto wa shoga yake kuwa ndiye niliyekuja kuandika kitabu cha Abdul Sykes, mtu ambae historia ilikuwa imemfuta bila shaka fikra hii ilikuwa ikizunguka katika kichwa chake.

''Mwanangu Mohamed, baba yako alijitolea sana katika kupigania uhuru wa Tanganyika,'' Mama Daisy alianza kusema.

Alikuwa na sanduku lake akiweka fedha zake na kila TANU wakija hapa kutaka kile au hiki yeye alikuwa anaingia ndani analifungua lile sanduku anatoa fedha kuwapa alikuwa hawarudishi mikono mitupu.

Mimi nikawa namwambia, Bwana Abdul taratibu lakini hakunisikia, hakuacha kutoa fedha kwa ajili ya chama chake.

Bwana Abdul alikuwa mtu karimu sana.''

1644346474419.png

Bwana na Bibi Abdulwahid Sykes katika miaka ya 1950 wakiwa Government House (Ikulu)
katika dhifa ya serikali.

Nimeweka picha zaidi katika hiyo link hapo chini:

 
Huyu Ramadan Dau.ni mtu haswa. Kule kilindoni mafia akifika kuingia kila nyumba nakusalimia kwa adabu kabisa.licha ya kuwa anakuja na ndege bnafsi au ya abiria lakini ukishuka hujichanganya na watu wa kawaida waliovaa malapa.
Nakumbuka kijijini kwao kule BWENI aliwajengra watu wake shule yenye hadhi kubwa kabisa.
Alijenga msikiti ambao ulizia sokomoko toka kwa Wazee wahafidhina wengine wakijiapiza kutokuswali pale . Asante mungu yamekwosha.
Dau aliipigania ardhi ya kwao isiporwe na kabisa kwa hila .
Naukumbuka mgogoro wa ardhi pale nyumbani kwake TELENI. Dr. Dau akitumia hekima na kuweza kushinda mgogoro ule. Sasa teleni ipo mikono salama ya wana wa mafia.
Dr. Dau ni mtu haswa. Kazi niliyokuwa naifanya ilinifanya nizijue hila na ghiriba nyingi juu ya mtu huyu.
Sikushangaa ila nilisikitika juu ya mtu huyu aliyeijenga NSSF alipoondolewa kwa matusi na manyanyaso pale ofisini wapo waliomuita mdini ati kila chumba cha ofisi alikigeuza msikiti . Nilishangazwa sana.
Ipo siku wema wanalipwa kwa wema wao.
Dr . Dau anastahili heshima na siyo bezo wala kebehi.
Asante mzee mohamedi saidi
Mungu akujalie sina na maisha marefu.
acha kabis enz zile upo enes eff ilikua hali nzur ukiwakuta wanawaka waka sijui iliemda wap ile hali

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom