Mawsali Magumu: CCM itapona kwa kuiga CHADEMA?

Bramo

JF-Expert Member
Oct 21, 2009
13,160
10,007
SINA ugomvi na kaulimbiu ya zamani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) – “zidumu fikra za mwenyekiti.”
Katika maisha ya sasa ya CCM hii inayoporomoka, inayotapatapa, inayojivua gamba na inayoishi kwenye kivuli cha kauli ya hayati Horace Kolimba kwamba “haina dira wala mwelekeo,” kaulimbiu ile ina maana sana.
CCM ya sasa imeishiwa fikra. Haina tanuri la kuzalisha mawazo mapya. Lakini imeweza kuzalisha na kutunza mitambo ya makombora ya fitina za kisiasa.
CCM hii legelege, iliyozaa serikali goigoi, kwa muda sasa imejigeuza chama cha wanachama wanaokulana wao kwa wao.
Kama alivyowahi kusema mtu mmoja mahali fulani, CCM hii imekuwa mithili ya dume zee la ng’ombe linalopenda kupanda madume badala ya majike.
Wafugaji wanaelewa dume la namna hiyo linapokataa jike, na likakosa dume la kupanda, hujigeukia na kujifanyia mzaha gani!
CCM isiyo na mawazo mapya, inashindwa hata kunakili au kuboresha fikra ilizoachiwa na waasisi wake. Kwanza imeziua, na sasa imeanza kurukia na kudandia fikra na mipango ya wapinzani wake. Hii ni CCM inayojimaliza.
Si hilo tu. Hata vile inavyoviiga kwa wapinzani, inavitekeleza kwa kubabia, bila umakini na weredi wa kuviboresha.
Nitatoa mifano michache. Baada ya kusikia Rais Jakaya Kikwete anazindua Bodi ya Taasisi ya Uongozi, wiki hii kwenye Hoteli ya Movenpick, Dar es Salaam, kumbukumbu zangu zilinipeleka hadi Desemba 10, 2010.
Siku hiyo, katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempiski, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kwa niaba ya uongozi wa CHADEMA, alitangaza nia yao ya kujenga Chuo cha Mafunzo ya Uongozi, kama njia ya utekelezaji wa azima yao ya kuondoa ombwe la uongozi nchini. Si chuo cha viongozi wa CHADEMA, bali cha kitaifa. CHADEMA walikuwa waasisi tu wa wazo, ambalo walilitangaza siku hiyo.
Katika kuenzi mchango wa mwana CCM mmoja ambaye amejipambanua kwa kuchangia ukuaji wa upinzani, kupitia CHADEMA, Mustafa Sabodo, wakaamua kuita chuo hicho The Mustafa Sabodo Academy of Leadership and Excellence.
Mustafa Sabodo mwenyewe alikuwapo. Alikubali jina lake litumiwe, na alichanga kianzio cha sh milioni 150 papo hapo kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho.
Nia ya CHADEMA, kama ilivyotangazwa na Mbowe, ni kukabiliana na ombwe la uongozi kwa kuandaa viongozi werevu na waadilifu kwa ajili ya uongozi wa taifa hili na taasisi nyingine za kitaifa na kimataifa.
Siku hiyo hiyo, CHADEMA walimtunuku Sabodo medali ya ujasiri na nia njema; maana si kawaida kwa mwana CCM kuchangia upinzani. Sabodo alikuwa ameichangia CHADEMA sh milioni 200 wakati wa kampeni za mwaka jana.
Walimshukuru na kumpongeza kwa kuunga mkono harakati za mabadiliko chanya katika siasa za Tanzania, na kwa ujasiri wa kujitokeza, tofauti na wafanyabiashara wengi wanaotumika kuhujumu harakati za mabadiliko.
Miezi mitano baadaye, Mei 18, 2011, Rais Jakaya Kikwete amezindua Bodi ya Taasisi ya Uongozi, inayotarajiwa kuwa kituo cha maendeleo ya uongozi.
Ni wazo zuri, lakini nani anaamini uwezo wa serikali hii katika kuanzisha na kusimamia taasisi makini ya viwango hivi, kama watawala wale wale wameua, na wameshindwa kusimamia taasisi ndogo ndogo zilizokuwapo?
Inawezekana wameibuka upya kwa sababu ya wazo la CHADEMA? Je, kwa kuiga huku wataweza kulitekeleza kwa ufanisi? Nguvu hii ya rais na serikali isingefaa kuunganishwa na walioasisi wazo la awali ili kuleta ufanisi mkubwa zaidi katika chuo kimoja chenye hadhi na umakini?
Wasiwasi wangu ni huu: watawala wale wale walioasisi ombwe lile lile, wakiachiwa peke yako kujenga vyuo vya namna hii, wanaweza wakatumia fursa hii kujenga misingi ya kusimika na kutaasisisha ombwe la uongozi. Maana walioshindwa uongozi hawawezi kusimamia taasisi ya uongozi.
Kuiga si kosa, kama wanaoiga wanaweza kulikuza na kuliboresha wazo la awali. Je, hawa wana uwezo huo? Kama wameanzisha taasisi hii kwa nia njema, si kuipiku CHADEMA, basi, waifanye taasisi ya taifa, si ya serikali, si ya CCM. Na waijenge pole pole, isije kuwa mithili ya shule za kata zinazojivunia wingi wa watoto na idadi kubwa ya sifuri katika mitihani ya taifa.
Upo mfano mwingine. Katika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010, ilani ya CHADEMA ilisema wazi kwamba kama kingepata ridhaa ya kuunda serikali, kingefumua mfumo wa uongozi na kuufuma upya.
Kwa kuanzia, ndani ya siku 100 za kwanza, kingeanzisha mchakato wa mabadiliko ya katiba, ili ipatikane katiba inayoendana na matakwa ya sasa kisiasa, kijamii na kiuchumi, hasa kwa kuzingatia kuwa mabadiliko ya mfumo yanajikita katika muundo wa katiba.
CCM ilikejeli azimio hilo la kuunda katiba mpya. Hata baada ya uchaguzi, CHADEMA iliposhinikiza serikali ianzishe mchakato wa kuandika katiba mpya, serikali ilisema hakuna haja.
Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani, alikataa katakata, akaisifia katiba iliyopo; akawakejeli wanaodai katiba mpya, akasisitiza haiwezekani. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, naye akaunga mkono hoja ya Kombani, kwamba hakuna haja ya katiba mpya.
Baada ya shinikizo la umma kutaka katiba mpya, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, na Rais Jakaya Kikwete wakaamua kutekeleza madai ya wanamageuzi.
Rais Kikwete akakiri kwamba baada ya miaka 50, Tanzania inastahili kuwa na katiba mpya. Akaamuru serikali ianzishe na kusimamia mchakato huo.
Matokeo ya kuiga bila kujipa muda wa kujifunza tumeyaona. Mchakato wenyewe umeanza vibaya kwa serikali kuandaa muswada wa sheria wenye kasoro zile zile zinazosababisha madai ya katiba mpya.
Wasiwasi wangu ni huu: CCM inaiga mipango ya wapinzani bila kujiandaa vema. Na kuiga huku kunaanza kuwafanya wananchi wahoji: kama CHADEMA wana mawazo mazuri hivi hadi CCM inayaiga, hata kuacha kutekeleza ilani yake ya awali, ni nani anaongoza nchi hii?
Tusisahau kwamba CHADEMA ndicho kiliasisi mpango uitwao ‘Operesheni Sangara’ kwa ajili ya kujijenga na kuinua hamasa ya siasa za upinzani vijijini. Mkakati huo umekiwezesha kukua kwa asilimia 400 kwa muda mfupi.
Matunda ya awali ya Operesheni Sangara yalionekana kwenye uchaguzi mdogo wa Busanda, Biharamulo na Tarime. Uchaguzi Mkuu uliopita ni ushahidi mwingine wa matokeo ya Operesheni Sangara.
Nguvu hiyo ya Operesheni Sangara ndiyo ilivifanya vyama vingine navyo viige mkakati kama huo na kuupa majina yanayoshabihiana nao.
Kwa mfano, CUF waliibuka na Operesheni Zinduka. CCM nao wakaiga, wakatengeneza kitu kinachoitwa Operesheni Chakaza! Kama CCM imekosa ubunifu kwa viwango hivi, si ni dhahiri kwamba hawakuwa na makosa kuimba zidumu fikra za mwenyekiti? Maana sasa tumegundua kwamba ndiye pekee aliyekuwa anasumbua kichwa chake kufikiri na kuweka dira na mipango mkakati ya chama.
Mwaka 2005, CHADEMA walibuni utaratibu mpya wa kufanya kampeni kwa kutumia helikopta. CCM wakadhihaki, wakasema ni matumizi mabaya ya pesa.
Lakini CCM walilazimika kulamba matapishi yao wenyewe katika uchaguzi mdogo wa Tarime, na baadaye katika uchaguzi mkuu wa 2010.
Badala ya helikopta moja, wakakodi tatu na kubwa kuliko za CHADEMA. Kumbe CHADEMA waliona mbali?
Tukumbushane pia, kwamba hata Chuo Kikuu cha Dodoma, kimetokana na wazo la CHADEMA. Mwaka 2005, mgombea urais kupitia CHADEMA, Mbowe, alitoa matamko mawili makubwa yaliyonakiliwa na CCM baada ya uchaguzi.
Akiwa katika mji wa Merererani (Mkoa wa Arusha wakati huo), Mbowe alisema kama CHADEMA kingeingia madarakani, kingepitia upya mikataba ya madini nchini, ili kuondoa unyonyaji unaofanywa na serikali na wawekezaji dhidi ya wananchi maskini.
Mwaka 2008, serikali ilipobanwa vilivyo, ikaamua kuunda Tume ya Bomani kwa lengo lile lile la kupitia sheria na sera ya madini. CCM ikaanza kujitapa kwamba ni sehemu ya ilani yake.
Lakini hakuna popote katika ilani yake paliposema kwamba wangepitia upya mikataba ya madini. Waliiga wazo la CHADEMA ili kuwanyamazisha kisiasa, lakini hawakuwa wamejifunza kwao jinsi walivyodhamiria kulitekeleza.
Tamko jingine muhimu la CHADEMA lilitolewa na Mbowe katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma. Akasema CCM inawahadaa wananchi kuhusu serikali kuhamisha makao makuu kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Akasema CHADEMA haina sababu ya kudanganya wananchi. Akasema sera ya CHADEMA si kuufanya makao makuu ya serikali, bali kuufanya Dodoma uwe mji wa wasomi – kwa kujenga vyuo vingi vya elimu ya juu. Akatoa faida nyingi za kuufanya mji wa wasomi; mojawapo ikiwa ni ongezeko la mzunguko wa pesa, hivyo kuinua uchumi wa Dodoma.
Mara baada ya uchaguzi, Rais Kikwete akanakili wazo hilo; akatangaza uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha Dodoma, ambacho kilianzishwa rasmi Machi 2007, bila maandalizi ya kutosha.
Katika mkutano wao wa mwaka 2010, CHADEMA walitangaza ubinifu wao wa kuchangisha wananchi kwa kupitia ujumbe mfupi wa simu za mkononi.
Katika hali iliyodhihirisha wivu na fitina za kisiasa, CCM, kupitia serikali, ilitisha makampuni ya simu yasiwezeshe mfumo huu kwa CHADEMA hadi wao watakapokuwa wameutumia.
Nilishuhudia viongozi na maofisa wa CHADEMA wakivutana na watendaji wa makampuni hayo kuhusu utekelezaji wa mpango huo.
Baada ya miezi kadhaa, CCM nayo ikazindua kwa kishindo mpango huo huo kwa kutumia makampuni yale yale. Woga, wivu, fitina!
Haya ni maeneo machache ambayo CCM imeiga waziwazi kutoka CHADEMA. Na huu ni ushahidi mwingine kuwa CCM inaanza kupoteza taratibu uhalali wa kutawala.
Ni kielelezo cha kauli iliyomponza aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, hayati Horace Kolimba, kwamba: “CCM haina dira wala mwelekeo,” iliyosisitizwa upya na mzee Joseph Butiku, wiki chache zilizopita.
Hii ndiyo CCM inayojitahidi kujitambua, ingawa haipo tayari kujikubali; CCM inayojivunia miaka 50 madarakani, lakini inadhani njia pekee ya kudumu madarakani ni kuiga mikakati na mipango ya CHADEMA. Kwa mbinu hii, itapona?
 
Back
Top Bottom