Mawaziri maji ya shingo majimboni

Magazetini

JF-Expert Member
Aug 16, 2014
588
1,698

JKM-21july2015.jpg

Kwa ufupi


Wasira apata wapinzani saba, Mwakyembe 9, Juma Nkamia 13, Wamo pia Kilango, Nyalandu, Nagu, Masele, Kamani.


Mawaziri kadhaa wa Rais Jakaya Kikwete wamekutana na upinzani mkali majimboni kutokana na kujitokeza kwa wanachama wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika majimbo yao kuomba uteuzi wa kugombea ubunge kupitia chama hicho.

Aidha, baadhi ya wabunge wa CCM wamekutana na upinzani mkali pia baada ya makada wenzao wengi kujitokeza majimboni kuomba kuteuliwa.

WASIRA- BUNDA MJINI (8)
Katika jimbo lililomegwa upya la Bunda mjini, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, amepata wapinzani kupitia CCM ili waweze kupimana bana ubavu kuwania fursa ya kuongoza kwa kipindi cha miaka

mitano ijayo.
Waliochukua fomu na kurejesha katika jimbo hilo ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Christopher Sanya, mfanyabiashara Robert Maboto, Magesa Julius Magesa, Simoni Odunga, Peles Magiri, Isack Maela na Exvery Rugina.

FENELA MUKANGARA
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara, atachuana na makada sita katika jimbo jipya la Kibamba. Makada hao ni George Shayo, Mashaka Sabaya, Rashid Mrisho, Issa Jumanne, Felix Mdeka na Goodvido Shayo.

DK. MWAKYEMBE
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, mkoani Mbeya, atakabiliana na ushindani kutoka kwa makada tisa wa chama hicho.

Makada hao ni Gabriel Kipija, ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, John Mwaipopo, Prof.Leonard Mwaikambo, Gwakisa Mwandembwa, Vincent Mwamakingula, George Mwakalinga, Benjamin Richard, Asajile Mwambambale na Ackim Jackson.

DK. MARY NAGU
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Mahusiano na Uratibu), Dk. Mary Nagu, anayemaliza muda wake wa kiliongoza Jimbo la Hanang’ atakutana na upinzani kutoka kwa Peter Nyalandu, Aliamani Sideyeka na Mayomba Dankani.

CHIZA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji), Cristopher Chiza, atakabiliana na makada sita waliojitokeza katika jimbo lake la Buyungu.

ANNE KILANGO
Mbunge wa Same Mashariki ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango, anakabiliwa na kibarua kugumu baada ya makada nane kuchukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kugombea ubunge.

Hao ni Michael Kadeghe, Dk. Eliji Kibacha, Semi Kiondo, Abraham Shakuri, Nyangasu Werema, Daudi Mambo na Ombeni Mfariji.

PROF. MAGHEMBE
Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Mwanga, Prof. Jumanne Maghembe, waliojitokeza kumpinga ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (Nec), Anania Thadayo, Karia Magaro, Baraka Lolila, Amani Kidali, Ramadhan Mahuna na Japhari Mghamba.

DK. KAMANI
Mbunge aliyeangushwa na ndugu yake katika kura za maoni 2010, Dk. Raphael Chegeni ni miongoni mwa watia nia saba waliojitokeza kumrithi mbunge wa Jimbo la Busega, Dk. Titus Kamani.

Licha ya Dk. Chegeni na Dk. Kamani kuchukua na kurejesha fomu, pia wapo wanachama wengine wa CCM waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ambao ni Benard Kibese, Igo Shing’oma, Dasias Sweya, Robert Nyanda, Nyangi Msemakweli na Josephat Kwamba.

JUMA NKAMIA
Naibu wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, anakabiliwa na upinzani kutoka kwa makada 13.

Makada hao ni mwanahabari mwandamizi, Khamis Mkotya, Fredi Duma, Juliana Magembe, Juliana Maghembe, Juma Ilando, Yusuph Ibrahim, Idd Kisisa, Raphael Kelesa, Francis Julius, Godfrey Mayo, Pascal Degera, Athman Hotty na Pascal Afa.

NYALANDU
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, anachuana na wagombea saba akiwamo Justine Monko, Michael Mpombo, Othman Mungwe, Amos Makiya, Yohana Eliyasini Too, Aron Mbogo na Sabasaba Manase.

MAJIMBO YA KIFO

BUKOBA MJINI
Jimbo la Bukoba Mjini lina ushindani mkali kutokana na makada nane kujitokeza wakiwamo Mbunge aliyemaliza muda wake, Balozi Khamis Kagasheki na hasimu wake mkubwa wa kisiasa, Dk. Anatory Amani.

Wengine ni Josephat Kaijage, George Rugahyuka, Filbert Katabazi, Elieth Projestus, Christina Rwezaura na aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo hilo, Mujuni Kataraiya.

MULEBA KUSINI
Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleio ya Makazi, Prof. Anne Tibaijuka, ambaye ni Mbunge anayemaliza muda wake, Prof. Anne Tibaijuka, anakabiliwa na upinzani mkali baada ya makada tisa kujitokeza kuwania nafasi yake.

Mbali na Prof. Tinaijuka, wengine waliochukua na kurejesha fomu ni Dk. Adam Nyaruhuma, Stephen Tumain, Flavius Kahyoza, Buruan Rutabanzibwa, Muhaji Bushako, Kaino Mendes, Mnawaru Amoud na Erick.

IRINGA MJINI
Makada 13 wamejitosa kuwania ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini.

Wamo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Frederick Mwakalebela na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mahamudu Madenge.

Pia wamo Dk. Yahaya Msigwa, Nuru Hepautwa, Addo November Mwasongwe, Adestino Mwilinge, Frank Kibiki, Aidani Kiponda,

Peter Mwanilwa, Fales Kibasa, Michael Mlowe na aliyetia nia ya kuwania urais, , Balozi Mstaafu Dk. Augustine Mahiga.

SHINYANGA MJINI
Mbunge wa Shinyanga Mjini na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Stephen Masele, amekutana na upinzani mkali, baada ya makada sita wa CCM kujitokeza kuomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho.

Wanaochuana na Masele ni Willy Mzanvas ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Shinyanga na Kamanda wa Vijana wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini.

Wengine ni Dk. Charles Mlingwa, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Siha; Hatibu Kazungu,Talla Mzeimana ,Abdallah Seni na Mussa Ngagara.

Wamo pia Hussein Fatu na Charles Shingino ambaye ni Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini.

JIMBO LA KONGWA
Anayeongoza Jimbo la Kongwa kwa sasa ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai. Anakabiliwa na upinzani kutoka kwa makada nane hivyo kufanya idadi ya wanaogombea nafasi ya kuwakilisha CCM katika kuwania ubunge wa jimbo hilo kufikia tisa.

Makada hao ni Samwel Chimanyi, Dk. Eliezer Chilongano, Epafra Mtango, Paschal Mahinyila, Hussein Madeni, Simon Katunga na Joseph Palingo.

DODOMA MJINI
Kwa sasa anayewakilisha Jimbo la Dodoma mjini ni Dk. David Malole.

Jumla ya wapinzani 10 wanashindana ili kupata ridhaa ya CCM kugombea nafasi ya kuliwakilisha.

Pamoja na Dk. Mallole, wengine ni Anthony Kanyama, Anthony Mavunde, Emmanuel Kamara, Haidary Gulamali, Mohammed Mgoli, Muruke Muruke, Mussa Luhamo, Robert Mtyani na Steven Masangia.

JIMBO LA MTERA
Livingiston Lusinde, almaarufu Kibajaji ndiye mwakilishi wa Jimbo la Mtera kwa sasa.

Anakabiliwa na makada tisa, akiwamo mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela, Samwel Malecela.
Wengine wanaowania kumng’oa Kibajaji ni Richard Masimba, Essan Mzuri, Lameck Lubote, Dk. Michael Msendekwa na Philip Eliezer.

SAME MAGHARIBI
Jimbo la Same Magharibi nalo lina ushindani mkali. Waziri wa zamani wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Mathayo David Mathayo, atavaana na makada wenzake 13.

Waliojitosa kutaka kumng’oa Dk. Mathayo David ni John Chaggama, Daniel Mkemi, Alfred Ngelula, David Mawa, Amon Shahidi, Gerald William, Katery Daniel, Yusuph Singo, Michael Mrindoko, Ahadi Kakore, Jordan Mmbaga na Mwalimu John Singo.

NKENGE
Katika Jimbo la Nkenge makada sita watachuana ambao ni Mbunge wa zamani, Balozi Dk. Deodorus Kamara na Mbunge anayemaliza muda wake, Asumpta Mshama. Wengine ni Julius Rugemalira, Dk. Joachim Mazima, Dk. William Nyagwa na Frolence Kyombo.

MTAMA
Katika Jimbo la Mtama lililoachwa wazi na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, makada wanne wanachuana ambao ni Selemani Mathew Luhongo, Rukia Abdallah Mandindi, Ismail Selemani Mbuni na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) wa Itikadi na Uenezi, Nape Moses Nnauye.

CHATO
Katika Jimbo la Chato lililokuwa likiongozwa na mbunge aliyemaliza muda wake ambaye pia ni mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli, limepata washindani 13 waliochukua na kurejesha fomu.

Katibu wa CCM Wilaya ya Chato, Khamis Mkaruka, aliwataja washindani hao ni Dk. Medard Kalemani, Deusdedit Katwale, Simon Bulenganija, Alexus Kagunze, Abdallah Mussa na Ismail Luge.

Wengine ni Dk. Alphonce Chandika, Ng'aranga Magai, Majura Kasika, Nassoro Yahaya, Aman Abeid, Mkinga Babuna Michael Wanjara, huku Francis Fredrick akishindwa kurejesha.

BUKOBA VIJIJINI
Kwa upande wa Jimbo la Bukoba Vijijini, waliojitokeza kurudisha fomu ni aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo hilo na waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi; Mbunge anayemaliza muda wake, Jasson Rweikiza na Nelson Sospeter.

SITTA- URAMBO
Baada ya kutochukua fomu za kutetea kiti cha ubunge Jimbo la Urambo, Samuel Sitta, ameliacha jimbo hilo huku kinyang’anyiro kikiwa kwa wanachama wanne akiwamo mkewe, Magreth Sitta.

Wengine waliochukua fomu za kulitaka jimbo hilo ni Ally Maswanya, Filbert Macheyeki na Hamis Kalaye ambao wote wamechukua na kurejesha kupitia CCM.

BARIADI MASHARIKI
Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, ni miongoni mwa watia nia wanne waliochukua fomu na kurejesha katika jimbo jipya la Bariadi.

Wengine waliochukua na kurejesha fomu hizo ni Masanja Kadogosa, Cosmas Chenya na Joram Masanja, ambao wote wanawania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, Katibu wa chama hicho mkoa wa Simiyu, Hilda Kapaya, alisema hao ni miongoni mwa wanachama 44 wa chama hicho waliochukua fomu katika majimbo yote saba ya mkoa huo, kati yao 11 kwa ajili ya viti maalum.

NYAMAGANA
Makada 17 wamejitosa kuwania Jimbo la Nyamagana, jijini Mwanza.

MGOMBEA AZIMIA
Mgombea ubunge kupitia CCM katika Jimbo la Peramiho, Lazaro Bunungu, ameanguka ghafla chooni nyumbani kwake eneo la Seedfarm, Manispaa ya Songea wakati alipokuwa ameenda kujisaidia.

Habari zilizopatikana jana mjini Songea ambazo zimedhibitishwa na mke wake Judith Mlelwa, zilisema kuwa tukio hilo lilitokea jana saa 5:00 asubuhi nyumbani kwake na kwamba baada ya kuona hali yake ni mbaya walilazimika kumkimbiza hospitali kwa matibabu.

“Leo (jana) asubuhi aliamka akiwa salama na baada ya kupata kifungua kinywa alikwenda kwenye ofisi za CCM wilaya ya Songea kuangalia ratiba ya kampeni ya uchaguzi ndani ya chama katika kata ya Maposeni Peramiho.” alisema.

Mlelwa alisema baada ya kutokea tukio hilo waliwasiliana na Katibu wa CCM wilaya ya Songea kumjulisha kuwa Bunungu hali yake ni mbaya baada ya kuanguka chooni.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Rajabu Uhonde aliiambia NIPASHE kuwa ofisi yake imepokea taarifa za tukio hilo na kwamba kwa sasa wanasubiri utaratibu wa kwenda kumuona licha ya kuwa wameambiwa alikuwa anafanyiwa mpango wa kusafirishwa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam.

Uhonde alifafanua zaidi kuwa katika jimbo la Peramiho makada watatu akiwamo aliyekuwa waziri wa wizara ya sera na uratibu Bungeni Jenista Mhagama walichukua fomu kwa ajili ya kugombea ubunge kwenye jimbo hilo lakini mmoja kati ya hao fomu yake ilikatwa kwa kuwa haikusainiwa na mgombea.

Aliwataja waliochukua fomu kwenye jimbo hilo kuwa ni Jenista Mhagama, Razalo Bunungu ambaye ni mtumishi wa Tanroads Tanga na mfanyakazi wa Bank ya NMB tawi la Tunduru Cremence Makabuli Mwinuka ambaye fomu yake ilitupiliwa mbali kwa kosa la fomu yake ya kuomba kugombea ubunge kusainiwa na mtu mwingine.

Hata hivyo Uhonde alisema kuwa licha ya kuwa mgombea Bunungu anaumwa ratiba ya kampeni inabaki kama ilivyopangwa na inatarajiwa kuanza leo asubuhi katika kata ya Maposeni Peramiho.

Imeandikwa na Daniel Limbe (Chato); Ahmed Makongo (Bunda); Anceth Nyahore (Shinyanga); Halima Ikunji (Tabora); Happy Severine (Simiyu); Shushu Joel (Busega); Rose Joseph (Mwanza)

CHANZO: NIPASHE
 
Mwaka huu ndugai amekalia kuti kavu

Challenge kubwa ni kutoka kwa kijana Dr. Joseph Elieza Chilongani ambaye ametokea kupendwa na wananchi.

Dr Joseph Elieza Chilongani (ambaye jina lake limekosewa na magazeti mengi wakimwita Dr Eliezer Chilongano )amekuwa mkweli katika kujinadi kupitia CCM na kuna uwezekano mkubwa kama haki ikitendeka atapeperusha vyema bendera ya CCM.

Nitaendelea kuwajuza yanayojiri
 
Mwaka huu ndugai amekalia kuti kavu

Challenge kubwa ni kutoka kwa kijana Dr. Joseph Elieza Chilongani ambaye ametokea kupendwa na wananchi.

Dr Joseph Elieza Chilongani (ambaye jina lake limekosewa na magazeti mengi wakimwita Dr Eliezer Chilongano )amekuwa mkweli katika kujinadi kupitia CCM na kuna uwezekano mkubwa kama haki ikitendeka atapeperusha vyema bendera ya CCM.

Nitaendelea kuwajuza yanayojiri

Kupitia ccm? Pole zakwe
 
Back
Top Bottom