Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 23,282
- 33,880
MAULIDI YA MFUNGO SITA UCHAGGANI 1950s
(KUTOKA KITABU CHA MAISHA YA RAJABU IBRAHIM KIRAMA)
(KUTOKA KITABU CHA MAISHA YA RAJABU IBRAHIM KIRAMA)
Maulid ya Mfungo Sita Moshi Uislamu ulipopata nguvu Machame na vijiji vingine Kilimanjaro kwa kuleta walimu kutoka Zanzibar kuja kufundisha dini Usangi, Ugweno na sehemu nyingine za Upare, Maulid yalibadili sura ya mji wa Moshi.
Kuanzia asubuhi mabasi yaliyobeba Waislamu yaliingia mjini kutoka milima ya Kilimanjaro na Upare yakiteremsha wake kwa waume na watoto wa madrasa waliokuja maulidini.
Hali hii ilifanya Uislamu utawale Moshi mjini ambako ndipo Waislamu walipojumuika.
Kwanza Waislamu walijumuika katika zafa, jioni wakizunguka mjini huku matari yakipigwa na kasida zikiimbwa.
Barabara zikiwa zimejaa watu na mbele zikiwa zimetangulizwa bendera za rangi ya kijana zimeandikwa ‘La Ilaha Ilallah’, yaani ‘Hapana Mungu ila Allah’.
Mji uligubikwa na hali ya furaha na msikiti miwili ya Moshi mjini, Msikiti wa Riyadha na Msikiti wa Ijumaa ilijaa waumini kuhudhuria sala.
Ilikuwa kawaida katika Maulid kama haya yaliyojaa Waislamu unatokea utambulisho kwa viongozi wa Uislamu Kilimanjaro na Upare.
Ikifika zamu ya kutambulishwa Mzee Rajabu Ibrahim Kirama, watu walimkimbilia na kumbeba juu kwa mapenzi makubwa na pia kutaka wale Waislamu ambao walikuwa wakimsikia lakini hawajamtia machoni na wao wamuone.
Jinsi miaka ilivyozidi kusonga mbele ndivyo hivyohivyo madrasa zilikuwa zikiongozeka kote Uchaggani na Upareni na ndivyo Maulid zilivyozidi ukubwa na ufanisi.
Uwanja huu wa Maulid ukawa uwanja wa mashindano ya wasomaji Qur’an na watoaji hotuba za kusisimua na kunyanyua imani za waumini.
Uislamu uliingia mwanzo Moshi lakini haukuweza kupanda mlima kwenda Uchaggani.
Katika muda mfupi wa kuingia Uislamu Machame na kuenea sehemu nyingine, Waislamu kutoka mlimani, wake kwa waume na watoto wa madrasa walikuwa sasa wanashuka kutoka mlimani makundi kwa makundi wakiingia Moshi mjini kwa vishindo kila Mfungo Sita huku wamebeba bendera za kijani zilizokuwa na maandishi ya kumpwekesha Allah.
Kila miaka ilivyozidi kusonga mbele Uislamu ulizidi kupata nguvu na maulidi ya mwaka huu yakawa makubwa na yenye kutia fora kuliko ya mwaka uliopita. Maulidi ya mwaka 1952 yaliishi katika kumbukumbu za Waislamu wa Moshi kwa miaka mingi sana kwani mwezi Oktoba 1951 Thomas Marealle II alichaguliwa kuwa Mangi Mkuu na katika maulidi yale alipangiwa kuzungumza na Waislamu waliohudhuria hadhira ile.
Pamoja wa Mangi Mkuu maulid haya alialikwa pia Mwitori Abdiel Shangali, District Commissioner Mr. B.J.J. Stubbings, Sheikh Abdallah Saleh Farsy kutoka Zanzibar alihudhuria maulidi haya.
Mwanazuoni maarufu wa Moshi Shariff Muhdhar Hussein usiku ule ndiye aliyesoma mlango wa kwanza wa Barzanj.
Shariff Muhdhar alikuwa mmoja wa viongozi wa Msikiti wa Riyadha ambao ndiyo msikiti wa kwanza kujengwa Moshi mwaka wa 1899.
Maulidi haya yalihudhuriwa na Waislamu kutoka Ugweno, Usangi, Gonja, Himo, Moshi Mjini na West Machame.
Maulidi ya mwaka 1956 Sayyid Omar Abdallah maarufu kwa jina la Mwinyi Baraka alihudhuria.
Mwinyibaraka alikuwa na namna ya uzungumzaji ambao iliwavutia wasikilizaji wake hasa alipokuwa anazitafisri aya za Qur’an kwa kutoka Kiarabu na akazisoma pia kwa Kiingereza.
Sayyid Omar Abdallah alikuwa mhitimu wa Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza na alitokezea kuwa mmoja wa wanazuoni wakubwa Afrika ya Mashariki. Ilikuwa kawaida baada ya maulidi Moshi, yatafanyika mengine Ugweno na Usangi na hivi ndivyo Uislamu ulivyozidi kuimarika sehemu za Kilimanjaro na Upare.
Picha mbili za mwanzo Rajabu Ibrahim Kirama, Sheikh Abdallah Saleh Farsy, Madrasa na shule ya kwanza aliyojenga Rajabu Ibrahim Kirama na mwisho kulia ni Sheikh Sayyid Omar Abdallah maarufu Mwinyibaraka.