Maudhui ya hotuba ya Maalim Seif, fundisho kwa wanademokrasia wetu

KISHADA

JF-Expert Member
Oct 18, 2012
2,226
3,290
HOTUBA YA KATIBU MKUU WA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – CHAMA CHA WANANCHI), MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KATIKA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI KUZUNGUMZIA HUJUMA ZA DOLA KWA KUMTUMIA KIBARAKA IBRAHIM LIPUMBA DHIDI YA CUF NA MWELEKEO WA HARAKATI ZETU
RAMADA ENCORE DAR CITY CENTRE – 09 APRILI, 2017

Ndugu zangu Wahariri na Waandishi wa Habari,
Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima na kutuwezesha kukutana hapa asubuhi hii kwa lengo la kufichua njama na mbinu chafu za Dola kwa kumtumia kibaraka Ibrahim Lipumba dhidi ya chama chetu, THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi), baada ya kuishiwa na mikakati ya kisiasa ya kukisaidia Chama Cha Mapinduzi ambacho sasa kinaelekea kwenye kukata roho. Nitayaeleza hayo kwa kina muda mfupi ujao.

Pili, nawashukuru na nyinyi Wahariri na Waandishi wa Habari kwa kuupokea mwaliko wetu na kuhudhuria mkutano huu. Siku zote mmetupa mashirikiano makubwa katika kuhudhuria shughuli zetu na kuufikisha ujumbe wetu kwa Watanzania na kwa ulimwengu kwa jumla. Kwa hayo yote, nasema Ahsanteni sana.

KWA NINI TUMEWAITA LEO?
Kwa takriban wiki moja sasa nimekuwa na ziara ya kuimarisha Chama kisiwani Unguja baada ya kumaliza ziara kama hiyo kisiwani Pemba. Hata hivyo, nimeamua kukatisha ziara hiyo kwa siku ya leo ili kuja kuzungumza nanyi, na kupitia kwenu kuzungumza na Watanzania na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla, kutokana na hali tuliyofikia, ambapo tusipochukua hatua za tahadhari kama Watanzania, inaweza ikaiingiza nchi yetu katika mgogoro mkubwa sana kuwahi kushuhudiwa katika historia yetu.
Si siri tena sasa kwamba kile kinachoitwa ‘mgogoro wa uongozi’ ndani ya CUF si chochote bali ni hujuma zilizopangwa na zinazoendeshwa na Dola kupitia njama ovu na mbinu chafu kwa lengo la kuua Upinzani makini hapa nchini ikiwa ni sehemu ya kile kinachoonekana ni mkakati mpana wa kunyamazisha kila sauti inayothubutu kuwakosoa watawala.

Nataka ifahamike kwamba lengo la njama ovu na mbinu chafu hizi siyo CUF; lengo ni Upinzani na hasa UKAWA na lengo pana zaidi ni kuua demokrasia Tanzania kwa kuhujumu na kuziua taasisi zote zinazoonekana kuwa ni nguzo za demokrasia yetu. CUF ni taasisi moja tu katika mapambano ya Dola dhidi ya taasisi za kidemokrasia zinazoonekana kuwaamsha Watanzania na ambazo zinaonekana kama kikwazo kikubwa dhidi ya watawala walioingia madarakani mwaka 2015 na ambao wana hofu kubwa ya kuendelea kubakia madarakani kutokana na mwamko mkubwa ulioonyeshwa na Watanzania kuanzia kwenye uchaguzi mkuu wa 2015. Ndiyo maana hujuma hizi zimeelekezwa kwa Bunge, vyama vya siasa, taasisi na jumuiya za kijamii na kiraia hususan zile zinazosimamia Haki za Binadamu na uhuru wa kujieleza, watumiaji wa mitandao ya kijamii hasa wakosoaji wa watawala, wasanii hasa wale wanaotumia vipaji vyao kukosoa watawala na kuwazindua Watanzania, vyombo vya habari na waandishi wa habari na sasa inaonekana hata kwa wanasiasa wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi wanaoonekana kuwa na uthubutu wa kusimamia wanachokiamini na kutofautiana na watawala walioingia madarakani 2015.

Kuthibitisha ninayoyasema, tuangalie mtiririko wa utekelezaji wa njama ovu na mbinu chafu hizi za kutaka kuua demokrasia kwa kunyamazisha taasisi zote zinazothubutu kutoa mawazo tofauti na yale ya watawala walioingia madarakani 2015. Tumeshuhudia mambo mengi lakini hapa nitataja mifano kumi (10):-

1. Kupiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa nchi nzima.

2. Kuzuia matangazo ya moja kwa moja (live broadcasting) ya mikutano ya Bunge ili kuwaziba macho na masikio Watanzania wasisikie mijadala ya Bunge na kuona jinsi Serikali inavyowajibika na kuwajibishwa na Wabunge ambao ndiyo wawakilishi wa wananchi waliochaguliwa kwa lengo la kuwasemea wananchi kutoka katika majimbo yao.

3. Kufinya bajeti ya shughuli za Bunge na hasa Kamati za Bunge ili zisiweze kufanya kazi ya kuisimamia Serikali, kuchunguza mapungufu ya viongozi na watendaji wa Serikali na ili zishindwe kufuatilia ahadi za watawala walizozitoa kwenye kampeni na kupitia mipango ya bajeti.

4. Kuwakamata, kuwabughudhi, kuwalaza ndani na kuwafungulia mashtaka Wabunge wa Upinzani hasa wale wanaoonekana kuwa mwiba mkali kwa watawala ili kuwatisha na kuwanyamazisha wasifanye kazi yao ya kuwakosoa watawala.

5. Kuzipa Mahakama maagizo hadharani ya jinsi ya kuamua kesi na hata kufikia kusema hadharani kwamba Serikali itawapa fedha wanazozihitaji kwa uendeshaji wa Mahakama ikiwa na Mahakama nazo zitaihakikishia Serikali kupata mapato kiasi fulani kupitia hukumu za faini na fidia.

6. Kuwakamata, kuwaweka ndani na kuwafungulia mashtaka watumiaji wa mitandao ya kijamii, wengi wao wakiwa ni vijana, wanaoandika maoni yao kuwakosoa watawala kwa kutumia Sheria ya Makosa ya Mtandao (Cybercrimes Act), sheria ambayo tokea awali ilipingwa kwa kuwa ni sheria kandamizi.

7. Kuwatisha waandishi wa habari na vyombo vya habari hadharani na kufikia hatua ya kuyafungia magazeti yanayoongoza kwa kuandika habari zinazokosoa watawala na kuwakamata na kuwashtaki wahariri na waandishi wa habari. Tumeshuhudia watawala wakivamia vituo vya radio wakiwa na walinzi na kutoa vitisho kwa wafanyakazi wa radio hizo kwa sababu tu radio hizo zilikataa kurusha vipindi vyao.

8. Kuwatisha na kuwakamata wasanii hasa wale wanaotumia vipaji vyao katika kuwakosoa watawala na kuwazindua Watanzania juu ya mwenendo wa Serikali.

9. Kuzitisha Jumuiya za kiraia zinazojishughulisha na masuala ya haki za binadamu, sheria na utawala bora kwa lengo la kuzinyamazisha ili zisitimize wajibu wao kwa jamii. Mfano wa karibuni kabisa ukiwa ni wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) ambapo Waziri alifikia hatua ya kutishia kukifuta iwapo wanasheria wangetumia uhuru wao kuchagua mtu asiyetakiwa na Dola kuwa Rais wao. Papo hapo, watawala wamewatisha Mawakili kwa kuwapa maagizo Polisi hadharani kwamba Mawakili watakaowatetea au watakaowaombea dhamana watuhumiwa wa aina fulani basi na wao wawekwe ndani.

10. Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kujipa mamlaka wasiyokuwa nayo kisheria ya kuita watu Polisi, kutoa amri wakamatwe na kuwekwa ndan, jambo ambalo limelalamikiwa hata na Mkurugenzi mstaafu wa Makosa ya Jinai, Mhe. Adadi Rajabu kwamba ni kinyume na sharia.

Hatua hizi za ukandamizaji wa demokrasia zimeharibu kabisa taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani na nje ya nchi, taswira ambayo ilijengwa kwa miaka mingi na waasisi wa Taifa letu. Leo hii tumefikia hadi vyombo vya habari vya kimataifa vinavyoheshimika vinaiandika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama nchi inayoshuhudia kutekwa nyara na kupotea kwa raia wake wanaojulikana kwa kukosoa watawala waliopo. Jumuiya za Kimataifa zimeanza kuinyooshea kidole Tanzania kwa ukiukwaji na uvunjwaji wa haki za binadamu. Ripoti ya kila mwaka ya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu Duniani (Amnesty International) ya mwaka 2016 imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazokandamiza haki za binadamu kwa kiasi kikubwa katika Afrika Mashariki.

HUJUMA DHIDI YA CUF
Ndugu zangu Wahariri na Waandishi wa Habari,
Njama na hujuma hizi za Dola dhidi ya taasisi za kidemokrassia hazikuviacha vyama vya siasa vilivyo makini. Niligusia hapo awali matamko ya watawala ya kuzuia maandamano na mikutano ya hadhara ya kisiasa, baadhi ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kubambikiziwa na wengine kufungwa, viongozi wengi wa vyama vya siasa kutakiwa kuripoti Polisi, kutishwa, kukamatwa na kuwekwa ndani, wengine wamefunguliwa kesi na wengine bila hata kufunguliwa kesi.

Kwa upande mwengine, kama nilivyotangulia kusema hapo awali, katika njama za kudhoofisha upinzani imara na hatimaye kuua kabisa demokrasia nchini, Chama Cha Wananchi – CUF kimepandikiziwa kile kinachoitwa ‘mgogoro wa uongozi’ kwa kumtumia kibaraka Ibrahim Haruna Lipumba. Wengi mnaweza kujiuliza kwa nini iwe CUF?

Sababu kubwa ni kwamba CUF imekuwa ni taasisi imara isiyoyumba katika kuifikia dhamira na malengo iliyojiwekea. Tokea mwaka 1992 pale mfumo wa vyama vingi vya siasa uliporuhusiwa tena katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, CUF kimejipambanua na kimeonyesha uwezo wa kujipanga katika kuwatumikia wananchi na wananchi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wakakikubali na kukiunga mkono. Kwa upande wa Zanzibar, kila mtu anajua kwamba asilimia kubwa sana inayopita zaidi ya nusu ya Wazanzibari wanakiunga mkono.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ulikuwa ni kilele cha mafanikio na ushahidi wa wazi wa kuithibitishia dunia kuwa CUF ndio chaguo la wananchi wa Zanzibar. Matokeo haya hayakuwaridhisha watawala hata kidogo. Licha ya kutumia nguvu kubwa ikiwemo ile ya kijeshi na kwa kumtumia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kuiminya demokrasia isikuchukue mkondo wake kwa kuyapindua maamuzi halali ya wananchi wa Zanzibar, bado wananchi wa Zanzibar wanaendelea kuungana na kuwakataa vibaraka waliowekwa madarakani kwa nguvu. Khofu hii ndio iliyojengeka katika mioyo ya watawala. Wanatishwa na kivuli chao kila uchao. Kwa misingi hii, ndio mpango wa kumtumia kibaraka Ibrahim Haruna Lipumba ulipopangwa na kufuatiwa na njama na hujuma chafu mbali mbali zinazofanywa dhidi ya CUF. Dalili zinaonyesha kuwa njama hizi zilianza mara baada ya kibaraka Ibrahim Haruna Lipumba kukaribishwa Ikulu mapema mwaka jana.

Sikusudii kurudia tena kwa urefu mtiririko wa matukio yaliyoanzia wakati huo lakini kwa ufupi niseme nyote mnakumbuka sinema ya Lipumba, iliyoanza mara baada ya ziara yake ya Ikulu. Kwanza alitumiwa kutushawishi kushiriki uchaguzi haramu wa marudio wa Machi 20, mwaka jana huku akinambia mimi kuwa nikubali kwani angalau nitaweza kuendelea kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kisha akadai ametengua barua yake ya kujiuzulu, akavamia Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama na kuuvuruga huku akilindwa na Polisi, na hatimaye akatumiwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye alijipa mamlaka asiyokuwa nayo eti kubatilisha maamuzi halali ya vikao halali vya Chama na kulazimisha Lipumba atambuliwe kuwa Mwenyekiti.

Baada ya hapo, sinema ikaendelea kwa kuvamia Ofisi Kuu ya Chama Dar es Salaam kwa msaada wa Polisi, kutangaza eti kawatengua viongozi halali wa Chama wakati yeye akiwa si mwanachama tena baada ya kufukuzwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama, na hatimaye kiroja cha mwisho kuokota watu barabarani na kuwapachika jina la eti ni wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na kufanya maamuzi aliyoyaita ya Chama.

Tokea Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa kujipa mamlaka asiyokuwa nayo ya kutangaza kumtambua kibaraka Ibrahim Lipumba eti kuwa Mwenyekiti wa CUF hadi hivi sasa kuna hujuma zilizoambatana na mbinu chafu zilizofanywa dhidi ya CUF na nyengine zinaendelea kufanyika. Baadhi ya hujuma hizo ni pamoja na:-

1. Kwa kutumia vyombo vya dola kumzuia Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, kufanya shughuli zake za kisiasa kwa upande wa Tanzania Bara na huku vyombo hivyo hivyo vikimlinda kwa nguvu kubwa kibaraka Ibrahim Haruna Lipumba kukihujumu chama.

2. Kwa mashirikiano na vyombo vya dola, kibaraka Ibrahim Haruna Lipumba ameteka na kuvamia kwa nguvu ofisi za Chama za Wilaya mbali mbali nchini chini ya ulinzi wa vyombo vya dola.

3. Wizi wa fedha za ruzuku za chama kiasi cha TSh. 369 milioni uliofanikishwa kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, Hazina, Lipumba na Benki ya NMB.

4. Njama za kujaribu kumuengua Katibu Mkuu wa CUF kama zilivyobainishwa katika mawasiliano ya siri kati ya Msajili wa Vyama vya Siasa na kibaraka Ibrahim Haruna Lipumba.

5. Bunge kupokea wagombea feki waliopitishwa na Baraza Kuu feki la watu wasio wajumbe ambao waliokotwa barabarani na kumchagua Mohamed Habib Mnyaa kama mwakilishi wa CUF katika Bunge la Afrika Mashariki, mtu ambaye si tu kuwa hakupitishwa na Chama, wala jina lake kuwasilishwa katika Ofisi za Katibu wa Bunge na Katibu Mkuu wa Chama kama ambavyo Kanuni za Bunge zinataka, lakini pia mtu huyu si mwanachama wa Chama Cha Wananchi – CUF kwani alikwishafukuzwa uanachama na tawi lake la Mkanyageni, kisiwani Pemba.

Ndugu zangu Wahiriri na Waandishi wa Habari,
Uchafu huu wote uliofanywa kwa mashirikiano makubwa na Dola (kupitia mamlaka za umma kama Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, Polisi, Hazina, na hivi karibuni Ofisi ya Bunge) unaonekana bado haujafikia lengo kuu ambalo ni kuisambaratisha CUF.

Tunaelezwa kuwa lengo kuu hasa ni Maalim Seif Sharif Hamad ambaye anaonekana kuwa mwiba mkali kwa CCM, dhambi yake kuu ikiwa ni kushinda kwa asilimia kubwa uchaguzi mkuu wa Urais wa Zanzibar mwaka 2015, na pia kule kubakia kwake kuwa nguzo kuu ya CUF katika kuuendeleza umoja wa wapinzani (UKAWA) ambao unahatarisha nafasi ya CCM katika siasa za Tanzania. Haya tuliarifiwa mapema na tuliyatolea taarifa kwa Watanzania ili wayajue na yamethibitishwa na matamko ya kipuuzi ya kibaraka Ibrahim Haruna Lipumba aliyoyatoa wiki iliopita.

NJAMA ZA KUITUMIA RITA KUHITIMISHA MPANGO WAO:
Baada ya kuona hawajafanikiwa na CUF imesimama imara kujilinda kupitia hatua za kisheria, sasa Dola imeamua kukamilisha mpango wake mchafu kwa kutumia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

Tokea kuanza kwa njama ovu na mbinu chafu hizi, moja ya vinavyoonekana vikwazo vikubwa vinavyokwamisha kufanikiwa malengo yake imekuwa ni Bodi ya Wadhamini ya The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) ambayo imechukua hatua madhubuti za kukilinda Chama kupitia Mahakama na taratibu nyingine za kiutawala na kisheria. Sasa njama mpya zinazofanywa ni kukiondosha hiki kinachoonekana kuwa ni kikwazo kwao.

Tunazo taarifa zisizo na shaka kuwa, kuna shindikizo kubwa la kumtaka Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA kusajili wajumbe feki wa Bodi ya Wadhamini ya CUF kwa kutumia majina yaliyowasilishwa na kibaraka Ibrahim Haruna Lipumba ili kuhujumu majina halali yaliyowasilishwa na kikao halali cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kilichofanyika makao makuu ya Chama, mjini Zanzibar tarehe 19 Machi, 2017.

Nitoe maelezo mafupi kuhusiana na hili ili lieleweke vizuri. Kimsingi, Bodi ya Wadhamini ya CUF ilikwisha sajiliwa tokea 1993, kwa kufuata taratibu zote zilizoelekezwa na Sheria ya Wadhamini (The Trustees’ Incorporation Act – Cap 318) na Hati ya Usajili tunayo. Kinachofanyika kila baada ya kipindi fulani ni kuweka sawa kumbukumbu za bodi hiyo kwa kuwalipia wadhamini na kuingiza kwenye kumbukumbu mabadiliko ya wajumbe kadiri yanavyofanyika kwa mujibu wa Katiba ya CUF.
CUF, kupitia Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lililochaguliwa kihalali katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa mwaka 2014, na kwa kufuata masharti ya Ibara ya 98 ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992 (Toleo la 2014) imefanya mabadiliko machache ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini na kuyawasilisha RITA, ambapo yalipokelewa na kupatiwa stakbadhi ya malipo yake.

Hata hivyo, mara baada ya kuwasilisha mabadiliko hayo machache, kibaraka Ibrahim Haruna Lipumba na yeye akatakiwa haraka aandae majina yake na kuyafikisha RITA huku akihakikishiwa kwamba RITA itapewa maelekezo ya nini cha kufanya. Lengo la njama hizi ni kumuwezesha kibaraka Lipumba kuwa na ‘Bodi ya Wadhamini’ ambayo itatumika, kwanza, kufuta kesi zote zinazomkabili yeye na genge lake na Msajili wa Vyama Vya Siasa ambaye yuko katikati kwenye hujuma hizi zote.
Lengo la pili ni kufungua akaunti mpya ya benki na kuwezesha kupatikana kwa fedha za ruzuku za Chama na mwisho Bodi hiyo mpya kudhibiti Ofisi za Makao Makuu ya Chama zilizopo Mtendeni, Zanzibar na kumuondoa Katibu Mkuu wa Chama.

Kufikia hatua hiyo watawala wanadhani watakuwa wamejiridhisha kuwa wameweza kuidhibiti CUF na khofu yao kwa CUF itakuwa imeondoka. Wanavyojidanganya ni kwamba madai ya Wazanzibari juu ya haki yao ya ushindi ulioporwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 yatakuwa yameishia hapo na hatua zote zilizofanyika zitakuwa zimekwamishwa. Na mwisho, wanajiaminisha kwamba kufikia hapo Watanzania walioiamini CUF kama taasisi imara ya kuwaletea mabadiliko ya kweli watasambaratika.

Tunajua kwamba Msajili amekuwa akiwasiliana na RITA kutia shinikizo wajumbe feki ndiyo wasajiliwe. Ni wazi Msajili ana maslahi ya ziada katika hili kwa sababu anahitaji RITA isajili wajumbe feki wa Bodi watakaokwenda kumfutia kesi zinazomkabili zilizofunguliwa na Bodi halali ya Wadhamini wa Chama. Tunayasubiri maamuzi ya RITA tuone kama na wao watageuka kama Msajili wa Vyama vya Siasa na kukubali kutumika katika kusajili wajumbe feki wa Bodi ya Wadhamini.

UJUMBE WETU NA MWELEKEO WETU:
CUF ni taasisi imara na imepita katika misukosuko mingi tokea kuasisiwa kwake. Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, tumevuka salama kote huko tulikotoka. Nawaambia watawala walio nyuma ya hujuma hizi kwamba kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na msukosuko huu wa kumtumia kibaraka wenu Ibrahim Haruna Lipumba nao tutauvuka salama na tutaushinda.

Katika majaribu tunayoyapitia ya kutaka kuiua demokrasia kwa kuzikandamiza na kuziua taasisi za kidemokrasia Tanzania tokea 2015, nimetiwa moyo sana na ujasiri unaooneshwa na Watanzania katika kukabiliana na njama hizo na kuwapelekea ujumbe wa wazi watawala, tena pasina woga, kwamba zile zama za watawala kusema peke yao, kuwatisha na kuwanyamazisha Watanzania na kutaka matakwa ya mtu mmoja tu ndiyo yasimame, zimeshapita na hazitarudi tena. Huu ni wakati wa wapenda demokrasia wote na wapenda amani ya Tanzania kusimama pamoja na kuilinda demokrasia yetu na kuzilinda taasisi zetu zinazoisimamisha demokrasia yetu. Kinachotafutwa hapa siyo CUF; kinachotafutwa hapa ni kuua taasisi zetu zinazosimamisha demokrasia yetu moja baada ya nyengine. Tukiruhusu kufanikiwa kwa hili, hatutaweza kuzuia mengine. If we don’t hang together, we will be hanged separately! Tusiposimama pamoja, tutamalizwa mmoja mmoja. Tusitoe mwanya huo!

Binafsi nimetumia umri wangu wote kupigania demokrasia na haki za binadamu Zanzibar na Tanzania kwa ujumla na wananchi ni mashahidi wa hilo. Nimepatishwa tabu na misukosuko mingi na kupangiwa uovu mwingi huku wale walio nyuma ya mipango hiyo wakidhani wataweza kunitisha au kunikatisha tamaa. Wengi walionipangia njama hizo wameondoka na mimi wameniwacha pale pale. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunilinda na kunipa uthabiti wa kukabiliana na yote yaliyonikuta. Moja kubwa linalonitia nguvu wakati wote ni imani yangu kwa Mwenyezi Mungu na, pili ni imani isiyotetereka wanayoionyesha wananchi kwangu.

Nilichukua ahadi inayofanana na kiapo kwa wananchi walioniamini kuwa nitawatumikia katika uhai wangu wote. Na hapa tulipofikia hakuna tena cha kunitisha wala kunikatisha tamaa. USHINDI WETU UKO KARIBU, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Baada ya maelezo hayo, nihitimishe hotuba yangu kwa ujumbe mfupi ambao ndiyo lengo hasa la mkutano wetu huu leo hapa. Nawaambia watawala walio nyuma ya njama na hujuma hizi chafu dhidi ya CUF kuwa msitulazimishe kutusukuma kwenye ukuta. Tumevumilia kiasi cha kutosha, sasa basi! Nawahakikishia kwamba tutailinda CUF kwa gharama yoyote ile. Na nyinyi mlio nyuma ya hujuma hizi mtabeba dhamana ya mnayoyaandaa. Natoa wito kwa Wazanzibari na Watanzania wote wanaoiunga mkono CUF na wapenda demokrasia ya kweli kusimama imara kulinda haki yetu; ni wakati wa kulinda demokrasia ya kweli katika nchi yetu.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
 
Muhtasari.

- Njama za dola kunyamazisha sauti ya kila anaekosoa utawala wa awamu ya tano.
-Kuuwa demokrasia Tanzania.
-Hujuma za dola kwa vyama vya siasa, taasisisi za kijamii, watumiaji wa mitandao ya kijamii, vyombo vya habari na waandishi na wanasiasa ndani ya CCM wanaosimamia hoja wanazoziamini.
- Kupandikizwa mgogoro ndani ya CUF.

- Taasisi za Umma kutumika kudhoofisha CUF ( Msajili wa vyama, Hazina, Polisi na hata muhimili wa BUNGE.


Own Take

Hili ni somo la demokrasia kwa watanzania Maalim katoa na kuwakumbusha adui mpya aliyep[o hapa Tanzania.

Ni wajibu wa vyama vyote vya siasa, taasisi za kijamii na kiraia, taasisisi za kisheria na wadau wa maendeleo kupinga huu uonevu, na kusimama pamopja sasa kabla athari hazijazidi.
 
CCM inatia aibu sana , kwa sasa hawana hata uwezo wa kunadi sera zao , lakini watatumia dola hadi lini ?
 
"Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunilinda na kunipa uthabiti wa kukabiliana na yote yaliyonikuta. Moja kubwa linalonitia nguvu wakati wote ni imani yangu kwa Mwenyezi Mungu"

maneno kuntu
Hii hutuba inaweza kuwa ya " MWAKA"

Inahuzunisha na inaleta hisia kali sana. Watawala wajuwe huyu mzee ni lulu kwa amani yetu.

Nakumbuka namna alivyotumia busara kuwatuliza wafuasi wake katika taharuki ile ya uchaguzi wa 2010 pale bwawani. Watu walikuwa wakilia kwa hasira yeye katuliza kutokana na kusikilizwa.

Hutuba inagusa sana.
 
Matumizi ya dola ni ya muda tu.....
ccm WAJUE KUWA MBELE YA SAFARI MAKABURI YATAFUKULIWA TU....Hadi wale walioahidi dunia kuwa watafanya kila namna wapige goli la mkono kitu ambacho sio cha kidemokrasia watafukuliwa tu.....
TUPO PAMOJA
 
"Nawaambia watawala walio nyuma ya hujuma hizi kwamba kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na msukosuko huu wa kumtumia kibaraka wenu Ibrahim Haruna Lipumba nao tutauvuka salama na tutaushinda."

"If we don’t hang together, we will be hanged separately! Tusiposimama pamoja, tutamalizwa mmoja mmoja. Tusitoe mwanya huo!"
 
Wanademokrasia zingatieni haya maneno.

"If we don’t hang together, we will be hanged separately! Tusiposimama pamoja, tutamalizwa mmoja mmoja. Tusitoe mwanya huo!"


Ole wetu. Watanzania '....
 
Uprofesa tz sio sifa tena bora ufaulu form 4 hata usipoendelea, upate heshima nchi nzima kuwa ulifaulu form 4
 
Sasa huyo katibu wa kudumu na mgombea wa urais wa kudumu atafundisha demokrasia gani? Let's be realistic, charity begins at home.
 
Back
Top Bottom