Matarajio ya Waguinea Bissau kwa Rais mpya aliyeipa mgongo PAIGC

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
NA MOHAMMED ABDULRAHMAN

Guinea Bissau taifa la Afrika magharibi lenye idadi ya wakaazi milioni moja na laki sita ni dogo, lakini limekuwa likigonga vichwa vya habari tangu lilipojinyakulia uhuru kutoka Ureno 1974, baada ya vita virefu vya ukombozi. Katika kipindi cha miaka 45 ya Uhuru, Guinea Bissau imeshuhudia mapinduzi manne na majaribio kadhaa ya mapinduzi, mauaji ya rais, uasi na vitisho vya mara kadhaa vya wanajeshi kutaka kutwaa madaraka, misukosuko ya kisiasa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mnamo miaka ya 1990 . Chanzo hasa ni uchu wa madaraka na tafauti za kikabila. Kwa mfano mwaka 2009 tafauti zilizozuka kati ya Rais Joao Bernado Viera “Nino,” na Mkuu wa zamani wa majeshi Baptista Tagme Na Waie, zilisababisha watu hao wawili waliokuwa wote maveterani wa vita vya ukombozi kuuwawa wakipishana kwa saa chache baina ya mmoja na mwengine. Viera alipinduliwa mara ya kwanza 199 na kukimbilia uhamishoni kabla ya kurejea na kushinda uchaguzi 2005 wa Rais.

Kuuwawa Viera na wanajeshi kulionekana kama ni kulipiza kisasi kufuatia kifo cha Jenerali Na Waie na kikosi cha ulinzi wa Rais katika shambulio kwenye makao makuu ya jeshi mjini Bissau. Uhusiano kati ya Viera kutoka kabila dogo la Papel ulikuwa wa msuguano tangu mwanzoni na maafisa wa jeshi ambao wengi ni wa kabila kubwa la Balanta.Wa-Bissau wengi wanaamini matatizo nchini mwao yalianza baada ya Viera kumuangusha Rais wa kwanza Luiz de Almeida Cabral mdogo wake muasisi wa vita vya ukombozi na chama cha PAIGC mwanamapinduzi Amilcar Cabral ambaye hakujaaliwa kuishuhudia siku ya Uhuru. Cabral aliuwawa Januari 1979 katika mji mkuu wa Guinea Conakry kulikuwa makao makuu harakati za PAIGC na mpiganaji mmoja aliyetumiwa na utawala wa kifashisti wa kikoloni wa Ureno.

Sasa kumeibuka fursa ya kuwepo matumaini, baada ya kupatikana Rais mpya katika uchaguzi uliomalizika kwa duru ya pili mwezi uliopita wa Desemba siku tatu kabla ya kuingia mwaka mpya. Duru hiyo iliyofuatia ile ya kwanza Novemba iliwakutanisha wanasiasa wawili, Waziri mkuu wa zamani Umaru Sissoko Embalo aliyeibuka mshindi kwa asilimia 54 dhidi ya mpinzani wake Domingos Simoes Pereira, mgombea aliyeungwa mkono na PAIGC.

Pereira aliongoza duru ya kwanza dhidi ya wapinzani wake 11, lakini asilimia 40 hazikutosha kumpa ushindi wa moja kwa moja. Wote wawili Embalo na Pereira walikuwa mawaziri wakuu kwa vipindi vifupi. Tayari katika kipindi cha miaka minnne iliopita Guinea Bissau imekuwa na mawaziri wakuu saba .

Uchaguzi ulifanyika kukiwa na tukio la kipekee, nalo ni kwamba kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 25 Rais aliyekuwa madarakani Jose Mario Vaz aliweza kumaliza muhula kamili wa miaka mitano madarakani.Vaz aliangushwa katika duru ya kwanza katika kile wachambuzi walichoashiria alishindwa kuchaguliwa muhula wa pili kumetokana kutoelewana na bunge, kutofanikiwa kwake katika vita dhidi ya rushwa na ufisadi, tatizo sugu sio tu nchini humo bali katika mataifa mengi barani Afrika.

Aliamua kumuunga mkono Embalo katika duru ya pili. Wakati akilihutubia taifa kuukaribisha mwaka mpya 2020 na kuaga baada ya ushind wa Embalo, Vaz alishindwa kujizuwia na kubugujikwa machozi. Alisema anaondoka akiicha Guinea Bissau yenye utulivu na kuahidi popote atakapokuweko atakuwa tayari kushikamana na kiongozi yeyote anayeamini juu ya kuijenga nchi hiyo kwa ari na uaminifu.

Kuwepo kwa kikundi cha wanajeshi wa kulinda amani kutoka Jumuiya ya uchumi ya Afrika Magharibi-ECOWAS na Angola tokea miaka saba iliopita, kumesaidia kulizuwia jeshi kujaribu kutwaa madaraka, ingawa kumekuweko na changamoto.

Guinea Bissau ni mwanachama wa ECOWAS inayozijumuisha nchi 15. Wakosoaji wa Rais mteule Sissoko Embalo wanamuangalia kwa jicho la tahadhari wakiwa na shaka shaka kama kweli ni mwanamageuzi.Wanadai alikuwa sehemu ya mfumo serikalini na katika jeshi la taifa na wanahoji kupanda kwake haraka na kufikia cheo cha Brigedia Jenerali wa kikosi cha akiba wakati sio tu ana miaka 47, kuna utata. Baadaye alistaafu kabla ya kujihusisha na siasa .

Kwa umri wake Embalo bila shaka hakuwa miongoni mwa wapiganaji wa vita vya ukombozi . Alikuwa na umri wa miaka miwili wakati Guinea Bissau ilipojinyakulia Uhuru 1974. Embalo aliyehitimu shahada ya uzamivu katika siasa mjini Lisbon Ureno, alikuwa mwanachama wa PAIGC lakini akakiacha mkono pamoja na wanachama wengine 14 alipofukuzwa uwaziri mkuu na kuunda chama cha upinzani-Chama Mbadala cha Demokrasia-MADEM .

Vyovyote iwavyo Waguinea Bissau wameamua wanataka mabadiliko. Miongoni mwa changamoto kubwa atakazokabiliana nazo kiongozi wao mpya ni pamoja na kuepusha hali yoyote ya mvutano itakayosababisha mgogoro na Waziri mkuu atakayemteuwa kutoka chama chenye wingi bungeni cha PAIGC na kuyapa mtihani mgumu madaraka yake kama kiongozi wa taifa.

Chama hicho kilifanikiwa kunyakuwa viti vingi vingi katika uchaguzi wa bunge Machi mwaka jana, ingawa kinahitaji kushirikiana na vyama vyengine kuweza kuwa na wingi bungeni.
Mengine ni kupambana na umasikini na rushwa , kuvunja ushawishi wa jeshi katika siasa na hatua za kuzuwia na kudhibiti kivitendo biashara ya madawa ya kulevya ambapo Guinea Bissau iligeuka kuwa kituo cha kupitishia madawa hayo kutoka Amerika Kusini kuelekea Ulaya. Baadhi ya maafisa wa ngazi ya juu jeshini wamehusishwa na kadhia hiyo.

Rais mteule ana kibarua kigumu pia cha ujenzi mpya wa taifa hilo lenye maendeleo duni. Wadadisi wanaashiria uwezekano wa Umaru anayependelea vazi la kanzu na kilemba kuzigeukia nchi za kiarabu akisemekana amekuwa na uhusiano nazo wa karibu na pia Nigeria na Senegal,mataifa jirani yenye ushawishi mkubwa wa kisiasa na kiuchumi katika ukanda wa Afrika magharibi na yalioshika mpini kuwa wasimamizi wa demokrasia.

Itakumbukwa nchi hizo mbili zilimshinikiza Rais wa zamani wa Gambia Yahaya Jammeh kukabidhi madaraka au awe tayari kukabiliana na hatua ya kijeshi, alipokaidi kukabidhi madaraka kwa mpinzani wake Adama Barrow aliposhindwa uchaguzi 2016.

Senegal inapakana sio tu na Gambia lakini pia na Guinea Bissau na utulivu wa kisiasa katika nchi hizo mbili ni muhimu kwa Senegal inayopigiwa upatu kuwa mfano mzuri wa demokrasia barani Afrika . Haikushangaza kwa hivyo kuona ziara ya kwanza ya Embalo nchi za nje baada ya kuchaguliwa ilikuwa Dakar Senegal na Abuja Nigeria alikokuwa na mazungumzo na Rais Macky Sall na Muhamadu Buhari.

Lakini si hayo tu Rais huyo mteule anaonekana kuwa ana nia ya kutanua mahusiano ya nchi ya nje ya ukanda wa Afrika magharibi na Jumuiya ya mataifa yazozungumza Kireno (Lusophone) Ureno, Angola, Msumbiji, Guinea-Bissau, Cape Verde, Sao tome na Principle na Brazil (nchi pekee inayozungumzwa lugha hiyo katika Amerika kusini). Embalo ameizuru Kenya taifa lenye nguvu kiuchumi katika ukanda wa Mashariki wa bara hili na kuwa na mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta. Ni mabadiliko katika sera ya kigeni, ukilinganisha na wenzake waliotangulia.

Kwa hivyo wananchi wa Guinea wanatarajia Embalo hatokuwa sawa na ule usemi, "chupa mpya lakini kinywaji ni kile kile." wanatarajia atakuwa tafauti na kufunga ukurasa mpya wa matumaini

Matokeo ya uchaguzi wa Rais nchini Guinea Bissau yanamaanisha kugawana madaraka ya ngazi mbili za juu za uongozi wa taifa,huku Rais akitoka upinzani na Waziri mkuu kutoka chama kikongwe kilichopigania uhuru na kilichoyadhibiti madaraka yote tokea uhuru.

Ni mabadiliko makubwa katika historia ya siasa ya nchi hiyo tangu uhuru. Umaru Sissoko Embalo anatarajia kuapishwa February 15



Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom