Mfuko huo sasa una utaratibu mpya ulioanza jana Machi 13, kundi hilo linalazimika kulipiwa malipo yao kupitia uanachama wa wazazi au walezi wao ambao ni wanachama kupitia vifurushi vya mfuko kulingana na ukubwa wa familia.
Vifurushi hivyo ni vilivyopewa majina ya Najali Afya, Timiza Afya na Wekeza Afya.
Januari mwaka huu, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisema atasimama kidete kuhakikisha kila Mtanzania anafahamu umuhimu wa kuwekeza na kuweka kipaumbele kwenye afya na hakutakuwa na msamaha wowote.
Waziri Ummy alisema ajenda kuu iliyopo mbele ya sekta hiyo ni huduma bora na Bima ya Afya kwa Wote, ambayo kwa sasa kiwango kinachotazamiwa ni kuwa kati ya Sh. 340,000 hadi 360,000 kwa mwaka, ili kuhudumia watu sita kwa huduma za rufani, kanda na kibingwa.
UTARATIBU MPYA
Meneja Uhusiano wa NHIF, Angela Mziray, jana aliiambia Nipashe iliyotaka kufahamu utaratibu mpya kuhusu huduma hizo, kwamba utaratibu huo ulianza rasmi jana na bei za vifurushi kulingana na familia wachangiaji kuanzia umri wa miaka 18 hadi 35, ni kuanzia Sh. 192,000 kwa huduma za kifurushi cha Najali Afya; Sh. 384,000 (Wekeza Afya) na Sh. 516,000 kwa Timiza Afya.
Aidha, kifurushi kama hicho yaani mtu mmoja, bila wategemezi, kwa wachangiaji kuanzia umri wa miaka 35 hadi 59 gharama ni Sh. 240,000 kwa huduma za kifurushi cha Najali Afya; Sh. 444,000 (Wekeza Afya) na Sh. 612,000 kwa Timiza Afya.
Kadhalika, vifurushi kwa ajili ya wanandoa pamoja na mtoto mmoja kwa wachangiaji kuanzia umri wa miaka 18 hadi 35, ni Sh. 504,000 kwa kifurushi cha Najali Afya; Sh. 924,000 (Wekeza Afya) na Sh. 1,272,000 kwa kifurushi cha Timiza Afya.
Pia kifurushi kwa ajili ya wachangiaji kuanzia umri wa miaka 36 hadi 59 wakijumuishwa watoto wawili, gharama ni Sh. 696,000 (Najali Afya); Sh. 1,248,000 (Wekeza Afya); Sh. 1,728,000 (Timiza Afya) kwa mwaka.