Masai land grab --- at CNN in few minutes

Masai land grab --- at CNN in few minutes

Turbulence

Senior Member
Joined
Apr 24, 2012
Posts
153
Reaction score
30
Kwa wale wanaotazama TV, sasahivi CNN wanaonyesha special report on masai land grab! Siilewi hii ishu vizuri, lakini ni mbayasana kwa image yanchi.
 
Ngoja tuliombali na mang'amzi tuangalie kwenye mtandao tu.
 
Ikulu ya Tanzania imekaa UCHI mbele ya jamii ya kimataifa kuhusu hili swala la kupokonya ardhi ya wamaasai na kuwauzia watu wa dubai.

I stand with Maasai.

Sent from my BlackBerry 9700 using JamiiForums
 
Du!

Jana Peter Msigwa, akiwasilisha maonj ya Kambi ya Upinzani Bungeni kama Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, alisema;

LOLIONDO, WAARABU NA CCM

Mheshimiwa Spika,

Mgogoro wa ardhi katika eneo la Loliondo ni taswira nyingine ya jinsi ambavyo Serikali ya CCM imekiuka haki za wafugaji wa Kimaasai kwa manufaa ya wawekezaji wa kigeni katika sekta ya uwindaji wa kitalii. Kama tulivyoeleza mwanzoni, kufuatia Wamaasai kuondolewa Serengeti mwaka 1959, baadhi yao walihamishiwa katika Tarafa za Loliondo na Sale na wengine walihamishiwa katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Licha ya ahadi za Serikali ya kikoloni kwamba haki za ardhi za Wamaasai zitaendelea kulindwa katika maeneo hayo, miaka ya uhuru ilishuhudia Serikali ya Tanzania ikianza kuhujumu haki hizo. Hivyo basi, mwaka 1975 Serikali iliwaondoa kwa nguvu wafugaji waliokuwa wakiishi ndani ya eneo la Kreta ya Ngorongoro. Miaka tisa baadaye, kati ya 1983/84, Serikali ilitwaa eneo la Sukenya lenye ukubwa wa ekari 10,716 na kuligawa kwa Kampuni ya Bia Tanzania (Tanzania Breweries Ltd.)

Aidha, mwaka 1990 Serikali ilipima vijiji vyote vya Tarafa ya Loliondo na Sale na kuvipatia hati milki ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuvitambua kisheria. Hata hivyo, mwaka huo huo Serikali hiyo hiyo ilitwaa sehemu ya ardhi ya vijiji hivyo na kuimilikisha kwa Kampuni ya Orthello Business Corporation (OBC) inayomiliwa na Brigadia Mohamed Abdulrahim al-Ali anayesemekana kutoka katika familia ya kifalme ya Oman. Mwaka 1992 Serikali hii ya CCM ilipanua “… wigo wa umiliki wa ardhi wa kampuni ya OBC na kuiruhusu kampuni hiyo kuwinda katika vijiji vyote 19 vya Tarafa ya Sale na Loliondo.” Ilipofika mwaka 2003, “mkataba wa OBC na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa niaba ya vijiji ukaisha lakini OBC ikaendelea na uwindaji mpaka sasa.” Licha ya kampuni hiyo kutokuwa na mkataba halali na wananchi wa Loliondo, mwaka 2009 “operation kubwa ilifanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kuwaondoa wafugaji katika maeneo ya Sale na Loliondo na kupelekea wananchi kuchomewa nyumba zao.”

Na mwaka 2011 Serikali ya CCM “ikavitangazia vijiji vyote kurudisha hati miliki za ardhi na pia vijiji vyenye vyeti vya usajili vikaamriwa vivirudishe.” Inaelekea kwamba amri hii ilikuwa ni sehemu ya mwisho ya maandalizi ya kuwanyang’anya wananchi wa Loliondo na Sale ardhi zao kwani mnamo tarehe 26 Machi, 2013 Waziri wa Maliasili na Utalii aliitembelea Wilaya ya Ngornognoro na kuwatangazia wananchi na wakazi wa Loliondo kwamba “ameagizwa na Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, kugawa eneo la Loliondo Game Controlled Area ya zamani katika sehemu mbili: Yaani km2 2500 zimeachwa kwa ajili ya matumizi ya watu kwa kilimo, ufugaji, makazi, etc.; km2 zimechukuliwa na Serikali … ili eneo hilo liwe Game Control (sic!) mpya ya Loliondo.”

Mheshimiwa Spika,

Maelezo yote haya yanatoka katika Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba. Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, Serikali hii ya CCM “… imeamua kumega … eneo la Loliondo Game Control (sic!) Area ya zamani na kulifanya Game Control (sic!) Area mpya, na kwamba eneo hilo sasa litakuwa mali ya mwekezaji OBC kwani analimiliki kisheria.” Aidha, kwa mujibu wa Taarifa hiyo, endapo eneo hilo litamegwa kama ilivyotangazwa na Waziri Kagasheki, “… wakazi wa Tarafa (ya Loliondo) watakuwa wamebakiwa na eneo la km2 265 tu. Eneo hili ni dogo sana kwa wakazi 60,000 wa Tarafa hii.”

Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba inasema wazi kwamba kauli ya Waziri Kagasheki kuhusu unyang’anyi huu wa wazi wazi wa ardhi ya wananchi ndiyo ‘iliamsha hasira za wananchi.’ Hii ni kwa sababu, “… eneo … wanalonyang’anywa ndilo eneo pekee wanalolitegemea kwa maji ya mifugo na matumizi ya kibinadamu. Kuwaondoa ndani ya eneo hilo ni sawa na kuwauwa. Hivyo wako tayari kufa wakipiginia eneo hilo.” Aidha, “… eneo hilo … ndilo eneo pekee walilolitenga kwa ajili ya malisho ya mifugo hasa wakati wa kiangazi panapokuwa na uhaba wa malisho. Kuwaondoa hapa ni sawa na kuiuwa mifugo yao, jambo ambalo hawako tayari kulishuhudia, bora wafe.”

Mheshimiwa Spika,

Mgogoro kati ya wananchi wa Loliondo na Sale kwa upande mmoja na Serikali na OBC kwa upande mwingine umekuwa ukitokota kichini chini kwa zaidi ya miaka ishirini na tatu. Mgogoro huu ni mali binafsi ya CCM na Serikali zake za awamu ya pili, ya tatu nay a nne ya Dokta Kikwete. Ni mtoto wa ndoa haramu ya CCM na wawekezaji wa kigeni katika sekta ya uwindaji wa kitalii. Mtoto alizaliwa na Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi, akalelewa na baba wa kufikia Rais Benjamin Mkapa na sasa amefikisha umri wa mtu mzima chini ya baba wa kambo Dokta Jakaya Mrisho Kikwete!

Licha ya Serikali ya CCM kuwatukana wananchi wa Loliondo kwa kuwaita Wakenya, ni wazi – kama inavyothibitishwa na Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba - kwamba waathirika wa landgrab hii ni Watanzania wapatao 59,536 wanaoishi katika vijiji vya Ololosokwan, Soit Sambu, Oloipiri, Oloirien/Magaiduru, Arash, Losoito/Maaloni na Piyaya. Vijiji hivi vina shule za msingi na za sekondari zenye wanafunzi 2,302; zahanati nne na nyumba kadhaa za wahudumu wa afya; mashine za maji tatu; na mabwawa ya maji mawili. Maelfu ya wananchi hawa na miundo mbinu iliyojengwa kwa nguvu zao na kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania inatakiwa kutolewa kafara katika hekalu la urafiki wa Serikali ya CCM na mwekezaji huyu wa Kiarabu! Huu ndio uso halisi wa Serikali hii sikivu na inayotaka ‘maisha bora kwa kila Mtanzania’!

Mheshimiwa Spika,

Kutokana na hoja na ushahidi ambao tumeueleza hapa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu juu ya mambo yafuatayo:

1. Kama kampuni ya OBC ina haki zozote za ardhi katika maeneo ya Kata za Loliondo na Sale licha ya ukweli kwamba maeneo hayo yalikwishapimwa na wananchi kumilikishwa kihalali, na vijiji vyao kupatiwa usajili halali kwa mujibu wa sheria za nchi yetu;

2. Kama ni halali kwa kampuni ya OBC kuendesha shughuli za uwindaji wa kitalii katika vijiji vyote 19 vya Tarafa ya Loliondo na Sale wakati eneo ililopewa kwa ajili mwaka 1990 lilihusu sehemu ndogo tu ya maeneo ya vijiji hivyo;

3. Kama kampuni ya OBC inaendesha shughuli za uwindaji wa kitalii katika maeneo ya Loliondo kihalali licha ya ukweli kwamba mkataba wake na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa niaba ya wananchi wa Loliondo ulikwisha muda tangu mwaka 2003;

4. Kama ilikuwa halali kwa Serikali kuwahamisha wananchi wa Loliondo kwa nguvu na kuwachomea nyumba zao moto mwaka 2009, na baadaye kudai wananchi hao ni raia wa Kenya. Kama Serikali hii ya CCM itakiri kwamba vitendo hivyo vya kinyama havikuwa halali, basi itoe kauli kama iko tayari kuwaomba radhi na kuwalipa fidia kwa mujibu wa sheria za nchi yetu wananchi wote wa Loliondo na Sale waliodhalilishwa kwa kuitwa raia wa Kenya na kuathirika na unyama huo;

5. Kama Serikali hii ya CCM iko tayari kuwachukulia hatua za kisheria, au kiutendaji au kinidhamu wale wote walioamuru na au kushiriki katika vitendo vya kuwaondoa kwa nguvu wananchi wa Loliondo na Sale na kuwachomea nyumba zao moto pamoja na kuwatendea vitendo vya udhalilishaji au ukiukaji wa haki zao za kibinadamu;

6. Kama ni kweli kwamba kitendo cha hivi karibuni cha Waziri Kagasheki kutoa amri ya wananchi wa Loliondo na Sale kunyang’anywa maeneo yao mengine na maeneo hayo kukabidhiwa kwa kampuni ya OBC kilitokana na maagizo au maelekezo ya Mh. Rais Dokta Jakaya Mrisho Kikwete au yalikuwa na Baraka zake kama inavyodaiwa na Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba;

7. Kama huu sio wakati muafaka kwa Waziri Kagasheki kuwajibika kwa kujiuzulu kwa hiari yake au, kama atashindwa kufanya hivyo, kuwajibishwa kwa kufukuzwa kazi kwa kusababisha mgogoro wa sasa katika maeneo ya Loliondo na Sale;

8. Kama, licha ya ushahidi wote ulioibuliwa na Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba na licha ya upinzani mkubwa wa wananchi, bado kuna sababu ya kuendelea kuiruhusu kampuni ya OBC kuendesha shughuli zake katika maeneo ya Loliondo na Sale;

9. Kama, licha ya ushahidi wote ulioibuliwa na Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba kwamba chanzo cha migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro ni sera za Serikali hii ya CCM, ni halali kwa Serikali na CCM yenyewe kuendelea kuyalaumu mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ya kutetea haki za binadamu na za wafugaji wa Kimaasai kuwa yanachochea vurugu za wananchi wa Loliondo na Ngorongoro;

10. Kama, baada ya mambo yote yaliyoeleza hapa, Serikali hii ya CCM iko tayari kusitisha uamuzi wake wa kuwanyang’anya wananchi wa Loliondo na Sale maeneo yao na kuyamilikisha kwa kampuni ya OBC au kampuni nyingine yoyote katika siku za mbeleni;

Kama alivyopata kusema Dalai Lama: “Lengo letu kuu katika maisha haya ni kuwasaidia watu wengine. Na kama hatuwezi kuwasaidia, basi angalau tusiwaumize.” Serikali hii ya CCM ilikuwa na bado ina wajibu kisheria kuwasaidia Wamaasai wa Wilaya ya Ngorongoro kwa kuwaendeleza kiuchumi na kijamii. Kama imeshindwa kufanya hivyo, kama ilivyoonyeshwa katika Maoni haya, basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM angalau iache kuwaumiza wananchi hawa kwa kuwaachia ardhi zao!
 
Awali Msigwa akinukuu taarifa mbalimbali na historia, alikuwa amesema hivi juu ya haki za Wamasai huko Ngorongoro;


UKIUKWAJI WA HAKI ZA WAMAASAI

HIFADHI YA ENEO LA NGORONGORO

Mheshimiwa Spika,

Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na Loliondo ni moja ya maeneo ya asili ya jamii za Wamaasai. Kwa mujibu wa taarifa za kitafiti za ekolojia ya maeneo haya, Wamaasai wameishi katika maeneo hayo tangu karne ya kumi na nane. Kabla ya mwaka 1959 eneo hili lilikuwa ni sehemu ya maeneo ya Serengeti-Ngorongoro ambayo yalikuwa yakikaliwa na wafugaji wa Kimaasai. Mwaka 1959 Serikali ya kikoloni iliigawanya Serengeti-Ngorongoro baada ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti upande wa magharibi, na Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro upande wa milima ya mashariki ya eneo la ekolojia la Serengeti-Ngorongoro.

Wafugaji wa Kimaasai waliokuwa wakiishi katika maeneo ya Seronera, Moru na Sironet katika upande wa magharibi waliondolewa katika maeneo hayo na kuhamishiwa Hifadhi ya Eneo la Ngoroongoro na Loliondo. Hata hivyo, Serikali ya kikoloni iliahidi kwamba haki za Wamaasai juu ya ardhi za maeneo walikohamishiwa zitapewa kipaumbele na kulindwa na Serikali. Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya kikao cha Baraza la Kutunga la Sheria (LEGCO) cha siku ya Jumatatu ya tarehe 17, Novemba 1953, Gavana wa Tanganyika wa wakati huo alisema yafuatayo: “Wakati eneo hili lilipotangazwa kuwa hifadhi ya taifa, ilitambuliwa kwamba kulikuwa na watu waliokuwa na haki za asili za machungio ya mifugo na maji ndani ya mipaka yake na kwamba haitawezekana kuwaondoa watu hawa kwa nguvu.”

Kauli hii ya Serikali ilitiliwa nguvu na Waraka wa Serikali Na. 1 wa 1956 (Government Sessional Paper No. 1 of 1956) uliochapishwa kufuatia kuongezeka kwa shinikizo la mashirika ya uhifadhi ya kimataifa yaliyokuwa yanataka Wamaasai wafukuzwe katika maeneo ya Serengeti-Ngorongoro: “Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti chini ya Sheria ya Wanyamapori na baadaye kuundwa kwake upya chini ya Sheria ya Hifadhi za Taifa hakukuathiri kwa namna yoyote haki zilizokuwepo za mtu yeyote ndani au juu ya ardhi za Hifadhi. Badala yake, haki hizo sio tu kwamba zililindwa wazi wazi, bali pia Wamaasai waliokuwa tayari wanaishi ndani ya eneo la Hifadhi walipewa ahadi chanya na Serikali kwamba haki zao hazitavurugwa bila ridhaa yao.”

Kufuatia kuchapishwa kwa Taarifa ya Tume ya Uchunguzi juu ya Ngorongoro iliyoongozwa na Sir Barclay Nihill aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki, iliyopendekeza Wamaasai wafukuzwe Serengeti na pia katika maeneo ya Kreta za Ngorongoro na Empakaai, Serikali ya kikoloni ilirudia msimamo wake kuhusu haki za Wamaasai wa Serengeti-Ngorongoro katika Waraka wa Serikali Na. 6 wa 1956 (Government Sessional Paper No. 6 of 1956): “Mapendekezo ya kuwa na maeneo tengefu katika Kreta hizo mbili hayakukubalika. Yanaashiria kuondolewa kwa Wamaasai kutoka kwenye maeneo haya mawili. Haikuonekana sawa sawa kuomba ridhaa ya Wamaasai kuachia haki zao ndani ya Kreta hizo mbili wakati huo huo wakiwa wanaachia haki zao ndani ya Hifadhi yenyewe.”

Mheshimiwa Spika,

Ahadi za kulinda haki za ardhi za Wamaasai wa Serengeti-Ngorongoro ziliendelea kutolewa kwa nyakati tofauti na viongozi wa ngazi za juu wa Serikali ya kikoloni ya Tanganyika. Hivyo basi, katika kikao cha Baraza la Kutunga Sheria cha tarehe 25 Aprili 1956, Gavana Sir Richard Turnbull aliliambia Baraza hilo kwamba: “Wakati Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ilipoanzishwa mwaka 1940, ahadi rasmi zilitolewa na Serikali hii kwa Wamaasai. Hii haimaanishi kwa kabila lote la Wamaasai bali wale waliokuwa na haki za kisheria au za asili katika eneo hilo. Nina uhakika kabisa kwamba hakuna mtu yeyote anayeweza kutegemea Serikali hii, au Serikali yoyote ya Kiingereza kuvunja ahadi zake rasmi. Imekuwa ni lazima, kwa hiyo, kupata ridhaa ya Wamaasai kwa ajili ya mabadiliko yanayopendekezwa.”

Miaka miwili baadae Gavana Turnbull alirejea kauli yake hiyo wakati akifungua Mkutano wa 34 wa Baraza la Kutunga Sheria tarehe 14 Oktoba, 1958: “Nadhani ni lazima nichukue fursa hii kusisitiza kwamba kwa misingi yote ya haki na nia njema hakuna Serikali itakayofikiria kuwaondoa Wamasai kutoka maeneo yote ya hifadhi za wanyama za Serengeti na Nyanda za juu za Kreta.” Kama inavyojulikana, baadae Serikali ya kikoloni iliingia mkataba na Wamaasai ambapo Wamaasai walikubali kuhama kutoka maeneo yao ya Sironet, Moru na Seronera ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuhamia kwa eneo jipya la Hifadhi ya Ngorongoro. Kwa maneno ya Gavana Turnbull, “… uhifadhi wa eneo la Ngorongoro utajengwa kuzunguka nguzo ya maslahi ya wenyeji wa eneo hilo.”

Na katika mwaka ambao Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ilianzishwa, yaani 1959, Gavana Turnbull alisisitiza msimamo wa Serikali yake juu uhifadhi wa Ngorongoro kujengwa kwa kuzingatia maslahi ya wakazi wake katika hotuba aliyoitoa mbele ya Halmashauri ya Wilaya ya Maasai mwezi Agosti 1959: “Nataka kuweka wazi kwenu wote kwamba ni nia ya Serikali kuendeleza Crater kwa maslahi ya watu na matumizi yake, wakati huo huo Serikali inakusudia kulinda hifadhi ya wanyama katika eneo hilo, pamoja na kuwepo kwa mgongano wa jamii na serikali bado serikali inathamini na kuheshimu shughuli za jamii na haitaingilia shughuli za wafugaji wa Kimaasai.”

Mheshimiwa Spika,

Makubaliano kati ya Serikali ya kikoloni na Wamaasai wa Serengeti-Ngorongoro yalikuwa ndio msingi wa kutungwa kwa Sheria ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ya 1959. Sheria hiyo iliweka msingi kwamba eneo hilo litakuwa ni eneo la matumizi mseto wa rasilmali ambako Wamaasai wataruhusiwa kuishi na kutumia maeneo ya Ngorongoro kwa ajili ya malisho ya mifugo yao. Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NGorongoro Conservation Area Authority, NCAA) ilipewa majukumu ya kisheria ya kuhifadhi maliasili za eneo hilo na pia kuwaendeleza Wamaasai kiuchumi.

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, kwa mingi Serikali ya Tanzania imeshiriki katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu za Wamaasai wa Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na Loliondo katika Wilaya ya Ngorongoro. Serikali pia imekiuka wajibu wake wa kuwaendeleza Wamaasai wa Ngorongoro kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 1995 na Shirika la Misaada la Denmark (DANIDA), licha ya NCAA kupokea mamilioni ya fedha za kigeni kutokana na utalii unaoendeshwa katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, umaskini katika familia za Kimaasai ulifikia hatua ambayo 50% ya kaya zao zilikuwa na chini ya mifugo saba kwa kaya – ambacho kinachukuliwa kuwa chini ya kiwango cha kujikimu kiuchumi – wakati 40% ya kaya hizo zilichukuliwa kuwa ni fukara kwa maana ya kuwa na chini ya mifugo miwili kwa kaya.

Miaka karibu ishirini baadaye, hali ya kiuchumi na kijamii ya Wamaasai wa Ngorongoro imekuwa ni mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa wakati wa utafiti huo wa DANIDA. Ushahidi wa suala hili ni Taarifa ya Tume ya Uchunguzi ya CCM iliyoundwa na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana na kuongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Tanzania Bara, Mh. Mwigulu Nchemba iliyosambazwa jana tarehe 29 Aprili 2013.

Wajumbe wengine wa Tume hiyo ni pamoja na Mbunge wa Longido Mh. Lekule Laizer, Mbunge wa Simanjiro Mh. Christopher ole Sendeka na Mbunge wa Viti Maalum na Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha Mh. Mary Chatanda. Ukimwacha Mh. Chatanda, wajumbe wengine wa Tume hiyo ni wajumbe wa NEC ya CCM. Kwa vyovyote vile, taarifa ya Tume hiyo ya uchunguzi inahitaji kupewa uzito na umuhimu wa kipekee kutokana na uzito kichama wa wajumbe walioiandaa.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba: “Kutokana na ukosefu wa ardhi ya kuendeshea shughuli za kiuchumi, umaskini umekithiri miongoni mwa wakazi wa Ngorongoro kiasi cha kupelekea wakuu wa familia kukimbia familia zao.” Ukosefu wa ardhi unaopelekea umaskini kukithiri ni wa kutengeneza na Serikali hii ya CCM kwani kati ya km2 14,036 ambazo ndio eneo lote la Wilaya ya Ngorongoro, km2 8281 au 59% zimechukuliwa na Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wakati km2 870 au 6% zimechukuliwa na Hifadhi ya Misitu ya Nyanda za Juu Kaskazini. Maeneo ya wanyamapori na malisho ya mifugo ni km2 3916 au 30%, wakati maeneo ya kilimo ni km2 435 au 3% ya eneo lote la Wilaya hiyo.

Katika miaka ya mwanzo 2000, NCAA ilipiga marufuku kilimo cha mazao ya chakula katika maeneo ya Nainokanoka na Endulen ambayo yako ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Matokeo ya sera hizi za kuwanyang’anya wananchi wa Ngorongoro ardhi kwa ajili ya mifugo yao na kupiga marufuku kilimo yamekuwa, kwa mujibu wa Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba, ni “... tatizo ... sugu la njaa isiyoisha katika Tarafa ya Ngorongoro.”

Taarifa hiyo inafafanua zaidi: “Wananchi wa Ngorongoro wana njaa ya muda mrefu ambayo haijapatiwa ufumbuzi. Wananchi hawa hawaruhusiwi kulima ndani ya Hifadhi hivyo hutegemea mgawo wa chakula toka Mamlaka ya Hifadhi.” Ahadi ya Rais Dokta Kikwete kuwa Serikali ya CCM itashughulikia suala la kilimo cha kujikimu ambacho kingewasaidia Wamaasai kujipatia chakula, ahadi hiyo haijatekelezwa licha ya ukweli kwamba “... Mamlaka ya Hifadhi imeshindwa kuwapatia chakula.”

Hivyo, kama walivyosema Profesa Issa G. Shivji na Dr. Wilbert Kapinga katika kitabu chao The Maasai Rights in Ngorongoro, Tanzania, Serikali ya Tanzania, kwa kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, imekiuka sio tu haki za binadamu za Wamaasai wa Ngorongoro, bali pia imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuwaendeleza Wamaasai hao kama inavyotakiwa na sheria. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, hiki ndio chanzo cha migogoro ya ardhi ya muda mrefu na isiyomalizika kati ya Wamaasai na Serikali ya CCM na mashirika yake ya uhifadhi wa wanyamapori.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba njia pekee ya kutatua matatizo ya kiuchumi na kijamii ya Wamaasai na migogoro juu ya haki zao za ardhi na rasilmali, ni sharti Serikali iweke utaratibu mpya utakaoruhusu Wamaasai kufaidika na rasilmali za wanyamapori katika maeneo yao kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko ilivyo sasa. Kama inavyosema Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba, kuwapatia wananchi wa Ngorongoro mgawo wa shilingi bilioni moja wakati mapato ya Mamlaka ya Hifadhi ni zaidi ya shilingi bilioni 51 kwa mwaka ni ‘dhihaka na kuwapuuza.’

Aidha, utaratibu wa uhifadhi unaosisitiza binadamu na mifugo yao kuondolewa katika maeneo ambayo wameishi pamoja na wanyamapori kwa karne nyingi hauna msingi wowote kisayansi na umepitwa na wakati. Kama walivyowahi kusema watafiti Homewood na Rodgers katika kitabu chao The Maasailand Ecology: Pastoralist Development and Wildlife Conservation in Ngorongoro, Tanzania, hakujawahi kuwa na sababu za msingi za kisayansi za kuwakataza wafugaji wa Kimaasai kutumia rasilmali asili za Serengeti-Ngorongoro kwa ajili ya mifugo yao.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama bado kuna sababu zozote za kuendelea kuwazuia wafugaji wa Kimaasai wa Ngorongoro na Loliondo kutumia maeneo ya malisho ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na maeneo ya Kreta za Ngorongoro, Olmoti na Empakaai na vile vile katika Hifadhi ya Msitu wa Nyanda za Juu za Kaskazini ili kukabiliana na matatizo ya ukosefu wa malisho na maji ya mifugo hasa hasa wakati wa kiangazi.
 
Kwa jinsi wabunge wa CHADEMA wanavyofanya utafiti kabla ya kuwashilisha lolote bungeni inatisha sana jamani. Ukisoma huo hutuba kota kwa Mch Msigwa, daaahhh!!!!!!!!!!

Kumbe ndio maana wabunge wa kijani siku zote huishi tu katika kutukana maana wanaishia kuona giza tu??????
 
Back
Top Bottom