Elias Msuya
Senior Member
- Dec 23, 2011
- 173
- 671
Ukipita mitandaoni utakutana na ujumbe (hashtag) #MaragaForPresident #Maraga2027 #RutoMustGo.
Hivyo ndivyo vijana wa Kenya wamekuwa wakiandika kuonyesha kuwa wanamkubali Jaji Mkuu mstaafu wa Kenya, David Kenani Maraga, wakimwona kama sura mpya ya uongozi ambao wanahisi taifa lao linaukosa.
Maraga ndiye anayeonakana kama asiye mwanasiasa na mwenye mvuto katika orodha ya wanaotaka kumuomdoa Rais Ruto madarakani ifikiapo 2027.
Hata hivyo, wachambuzi wanasema Maraga atakuwana kibarua kigumu kutoka kwa kundi la upinzani linaojumuisha wanasiasa wakongwe kama Kalonzo Musyoka, Martha Karua, aliyekuwa naibu rais Rigath Gachagua na aliyekuwa waziri wa usalama wa ndani Fred Matiangi'.
Alipotangaza rasmi nia yake ya kuwania kiti cha Urais wa Kenya mnamo Juni 19, Maraga alieleza kwamba hali ya kisiasa na kiuchumi nchini humo imemlazimu kujitosa katika utumishi wa umma kwa mara nyingine na kuweka kando mipango mingine aliyokuwa nayo kwa sasa baada ya kustaafu.
"Uamuzi huu umefanywa kutokana na jinsi mambo yamekuwa yakifanyika nchini. Kuwaona vijana wetu wakihangaishwa jinsi wanavyofanyiwa kwa sasa ni jambo ambalo linanipa wasiwasi mkubwa," alisema Maraga akinukuliwa na BBC.
Tamko hili lilinokena kuwa kama mwamko mpya kwa wengi ambao mara moja walionyesha hamu ya kumtaka kujitosa ulingoni na kupambana vikali kumrithi Rais wa sasa William Ruto kwenye uchaguzi wa 2027.
Katika ujumbe wao kwenye kurasa mbali mbali za mitandao ya kijami, vijana wemeonekana kumuunga mkono Maraga.
Harun Kimathi aliandika kwamba, "Sijali ikiwa nitasilia peke yangu, ila mimi na familia yangu tutampigia kura Maraga."
Carolyne Muthini naye akasema kwamba, "Pindi tu Maraga alipotangaza kwamba atawania Urais, nilijawa na matumaini kwamba nchi yetu itapata mkombozi na kuokolewa hivi karibuni. Bila shaka nitampigia kura."
Juck Tumwa naye amesema kwamba, "Jaji Mkuu, umeonyesha kwamba unafuata sheria za nchi na wewe ni mwaminifu na mtiifu wa katiba. Utaikomboa taifa hili. Endeleza mipango yako tutasimama na wewe."
Kwa sasa Maraga anasema kwamba anajiandaa kwa ajii ya kutengeneza ilani yake ya uchaguzi, ambayo ana amini itamuweka Mkenya wa kawaida katikati ya maono yake.
Ila kulingana na Daktari Peter Mwencha ambaye ni mhadhiri na mtaalamu wa uongozi na masuala ya kidiplomasia, Maraga anapaswa kuwa na ujumbe maalum atakaowapa raia ili kumuwezesha kuanza kuuza sera zake.
"Kwa kweli ni sura mpya ambayo taifa halijakuwa nalo hapo awali. Ni mgeni katika siasa na hana tabia ambazo zimeshuhudiwa awali na wanasiasa waliomtangulia. Lakini kwa sasa kilicho muhimu ni yeye kuwa na ujumbe utakaoafikiana na mahitaji ya wengi katika jamii na sio tu vijana na kuwa na suluhisho la kuboresha hali ya maisha ya wakenya," alisema Dk Mwencha kwenye mahojiano na BBC.
Maraga ni nani?
David Kenani Maraga alihudumu kama Jaji Mkuu wa pili nchini Kenya chini ya katiba mpya iliyoasisiwa Agosti 2010. Aliteuliwa katika tume ya kusimamia idara ya mahakama (JSC) mwaka 2016 kufuatia kustaafu mapema kwa mtangulizi wake Willy Mutunga aliyehudumu katika wadhifa huo kwa miaka minne chini ya muongozo wa katiba mpya ya Kenya.
Kabla ya hapo Maraga aliyezaliwa Januari 12, katika kaunti ya Nyamira alihudumu kama Jaji wa Mahakama ya juu na ya rufaa kwa jumla ya miaka 13 ambapo alihudumu katika vituo mbali mbali nchini Kenya.
Japo alikuwa Jaji ambaye alipenda sana kufuata sheria na hakutaka kujihusisha na masuala ya ufisadi, alijikuta akipishana na watu kadhaa kutokana na uamuzi wake alioutoa mahakamani.
Tamko la aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta la ''We shall Revisit'' lilionekana kuwa wimbi jeusi kwake Maraga hasa baada ya uamuzi wa Mahakama ya juu zaidi nchini Kenya mwezi Septemba 2017 kubatilisha ushindi wa Uhuru Kenyatta.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Barack Muluka anasema kwamba, ''wakati wa uamuzi huo uliokubaliana na ombi la upande wa NASA ulioongozwa na Raila Odinga kwamba kulikuwa na dosari kwenye usimamizi wa uchaguzi huo.
“Baada ya hapo, alionekana kukinzanana na uongozi wa nchi wakati huo na kuonekana mara kwa mara akilalamikia hatua zilizochukuliwa na serikali ya Kenyatta aliyotaja kama njia ya kuikata miguu Idara ya Mahakama.”
Maraga alilalamikia hatua ya kupunguzwa kwa bajeti ya Idara ya Mahakama. huku pia akitaja hatua ya Rais Kenyatta kukataa kuidhinisha majina ya majaji sita walioteuliwa kuhudumu kwenye Mahakama ya rufaa kama ukiukwaji wa sheria.
Hata hivyo, Maraga alitumia kila fursa kuzungumzia kile alichohisi ni mambo kwenda mrama Serikalini na kukashifu bunge kwa kutofuata masuala ya kikatiba.
Bunge lilipinga hatua hiyo na mamlaka za nchi pia hazikuonekana kulipa kipaumbele suala hilo wakati huo, ambapo kulingana na Muluka, Maraga alitekeleza jukumu lake kikatiba.
Mtazamo wa sasa wa Maraga
Akihojiwa kwenye vyombo vya habari nchini Kenya, katika siku chache zilizopita, Maraga amesisitiza kwamba yeye ndiye suluhu ambayo taifa inahitaji kwa sasa.
Na japo anatetea hoja zake kwa misingi ya kupambana na ufisadi na kuboresha hali ya uchumi, kwa wengi ambao wanakabiliwa na mzigo mkubwa wa kodi zinazotozwa wafanyakazi, suala hilo ni jambo ambalo wangelipenda kulisikia kutoka kwake.
Daktari Mwencha anasema kwamba, 'Maraga anapaswa kuwa na ujumbe ambao atauuza kwa vijana na taifa zima kwa jumla. Ni sharti atambue kinachowabana raia na kisha kuuza sera zake zilizozingira suala hilo mara moja.'
Maraga mwenyewe amesema kwamba anafanya mazungumzo ya kina na wataalamu ambao watampa ushauri unaofaa kuweza kujiandaa vilivyo kwa kile ambacho wengi wanahisi ni mapambano makubwa katika maisha yake.
Vijana wenyewe wanahisi kwamba msimamo wake wa kusimama nao kwenye maandamano na kutetea haki za kimsingi za raia wote ni mwanzo mwema kwao.
Maraga alikuwa miongoni mwa kundi la mawakili wakuu waliofika Mahakamani wiki hii kusikiliza kesi inayowakabili watu 71 ambao wanakabiliwa na shitaka la ugaidi na uhaini kwa kuhusia kwenye ghasia zilizoshuhudiwa katika Taaisisi kadhaa za kiserikali mnamo Juni 25 na Julai 7 mwaka huu.
Don Kitheka alimpongeza Maraga akisema kwamba, 'Huyu hapa Rais wangu katika Mahakama ya kahawa akisimama kidete na vijana. Maraga anahitaji kupongezwa na kupata likes elfu moja.'
Maraga mwenyewe amewasuta wanao mkejeli kwa kuandaa video na mwanamuziki mashuhuri nchini Kenya mwenye jina la Charisma. Katika maandishi aliyoandika kwa Kiingereza, Maraga anaoenekana kuzungumza katika lugha wanayaoitambua vijana almaarufu Gen Z kwa kusema, 'Who said that I dont have charisma?' Kisha msaanii huyo anajitokeza na wawili hao wanacheka wakisalimiana.
Mara kwa mara amesisitiza kwamba, “Watu wananiuliza ni kwa nini, ninajitosa kwenye ulingo wa kisiasa nikiwa na umri huu? Nilipatwa na wasiwasi kwa kuwa ninaamini sote tukisusia kujitolea kuliongoza taifa, huenda tukakosa taifa ambalo watoto na wajukuu wetu watalirithi. Ninajitolea kujukumika binafsi kama Maraga, na nikipata fusra ya kuliongoza taifa, basi nitajitahidi.”
Sera za Maraga za kimataifa ni zipi?
Huku wimbi la kumtaa Maraga kama kiongozi likivuma ndani ya nchi, wengi wangependa kujuwa mtazamo wake kidiplomasia ni upi.
Ana sera zipi za kimataifa mbali na utetezi wa haki za kibinadamu – kama alivyoonyesha kwa kusimama na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Tanzania (CHADEMA), Tundu Lissu alipokuwa mahakamani kuhudhuria kesi yake ya uhaini.
Ili kushawishi jamii ya kimataifa, itampasa Maraga kuwazia kwa undani sera yake na jinsi atakavyojiandaa kama mwanasiasa aliyetosha kubadili mkondo wa taifa ambao kwa sasa wengi wanahisi umekwenda kombo.
Lakini huku Maraga mwenyewe akilivalia njuga suala hilo, machapisho kama 'Maraga is my next President' yataendelea kushuhudiwa mitandaoni, huku wengi wakiwa na matumaini kwamba maneno hayo yataandamana na vitendo kwenye sanduku la kura.
Chanzo: BBC