Mapotopoto:matunda pori yenye sifa tatu

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,299
33,080
*Utamu wake wamithilishwa na asali

*Miti yake yadaiwa kutibu malaria

*Magamba yake ni mbolea maridhawa

Na Jacob Malihoja

RUVUMA ni mkoa uliojaliwa neema nyingi. Una aina mbalimbali za madini na inaelezwa kwamba utafiti wa kina ukifanyika unaweza kuwa na migodi mikubwa hivyo kuinua uchumi na ajira.

Katika sekta nyingine, Ruvuma ina misitu mikubwa iliyosheheni miti ya aina mbalimbali. Pia una Ziwa Nyasa lenye samaki watamu na dagaa wazuri kuliko dagaa wowote nchini.

Vile vile Mkoa wa Ruvuma una mito mingi, Mngaka, Ruhuhu na Ruvuma, kutaja michache, inavutia na inatoa samaki watamu kama mbasa, mbufu, mbelele na wengineo. Ruvuma ni moja ya mito mikubwa nchini na ambao unatenganisha Tanzania na Msumbiji.

Mkoa huo una milima ya kuvutia ambayo kama ikifanyiwa kazi inaweza kuwa moja ya vivutio vya kitalii na kuliingizia taifa na vijiji vinavyoizunguka kipato.

Milima Mara kwa mfano, uliopo Kata ya Magagura, unaweza kuwa kivutio kutokana na urefu na mandhari yake. Pia ipo Milima ya Litenga iliyotegwa na maji ambayo inalisha vijiji zaidi ya saba kwa miaka zaidi ya 30 sasa. Kuna safu ya Milima ya Livingstone, kuna Jiwe la Mungu huko Mbinga.

Pamoja na sifa hizo nilizotangulia kuzitaja, Mkoa wa Ruvuma una sifa nyingine kubwa inayotambulika zaidi hata kwa wanafunzi wa shule ya msingi, kilimo.

Mkoa huu ni moja ya mikoa minne 'the Big four' inayolisha chakula Tanzania na nchi za jirani. Pamoja na kuwa kilimo cha mahindi kinacholimwa zaidi Wilaya ya Songea, Ruvuma inazalisha kwa wingi mpunga, ulezi, ufuta, mtama, mihogo na soya.

Mbali ya mazao hayo ya chakula, kuna mazao ya biashara kama vile kahawa inayolimwa na kustawi zaidi wilayani Mbinga, na korosho inayolimwa zaidi Tunduru.

Sambamba na mazao ya chakula na biasharaRuvuma pia ina aina mbalimbali za matunda, ya kupandwa na yapo pia ya asili yanayopatikana kwa wingi misituni. Matunda pori haya yanajulikana kama mapotopoto, pia huitwa masuku.

Matunda mengine yanayostawi kwa wingi katika hasa katika Wilaya za Songea na Mbinga ni yake yanayojulikana kama Matunda Mungu.

Katika matunda yote hayo, mapotopoto yanaongoza kwa sifa. Wenyewe wanayafananisha na asali kwa utamu. Tunda lake lina mbegu nne ndani yake zinazozungukwa na utando wenye rojorojo ambao ndio hasa unaonywewa. Msimu wake wa mavuno ni kila robo ya mwisho wa mwaka.

Matunda haya yamekuwa chanzo kizuri cha ajira kwa akina mama wengi kwani wakati wa msimu, huenda porini na kwenda kuyauza katika maeneo mbalimbali kama vile kwenye vituo vya mabasi, sokoni, na wengine wakitembeza mitaani.

MMoja wa wachuuzi wa matunda hayo, Flora Mhagama anasema wakati mwingine huuza ndoo nzima kwa siku lakini kutokana na wingi wake porini, watu wengi huyafuata hivyo kufanya bei yake kuwa ndogo.

Anasema kwa ndoo hiyo moja anaweza kuingiza kati ya Sh1,000 na 1,500. Anauza kwa kupanga mafungu na kila fungu huuza kwa Sh50... “Yanatusaidia kupata fedha ya chumvi na sabuni.”

Wenyeji pia wanaamini kwamba miti inayotoa matunda hayo huweza kutoa dawa ya kutibu malaria inapokuwa michanga. Hii ni changamoto kwa watafiti wa dawa za tiba kubainisha ukweli huo.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Wilaya ya Songea Vijijini Rogatus Haule anasema amewahi kusikia fununu hizo.

“Nimewahi kusikia kuwa miti michanga huweza kuwa dawa ya malaria ila siwezi kuthibitisha kama ni kweli au la. Ni ni wakati muafaka kwa taasisi za serikali na binafsi zinazojihusisha na utafiti wa dawa kutopuuzia fununu hizi na kuifanyia utafiti mimea hiyo,” anasema.

Inaelezwa pia kwamba masalia ya maganda ya matunda hayo ni rutuba nzuri kwa zao la uyoga. Hiyo inathibitishwa na ukweli kwamba katika misitu ambayo mapotopoto huzaliana kwa wingi, uyoga pia huota na kustawi.

Tatizo lililopo katika biashara ya matunda hayo kama ilivyo kwa mazao mengi mengine ni soko. Kwa mfano, Mkoa wa Dar es Salaam ambao hauna msimu wa matunda haujawahi kupelekewa mapotopoto.

Tatizo la kutopanua soko na kuangalia uwezakano wa kuyasindika matunda hayo ni moja ya changamoto ambazo zinawakabiliwa wadau wa kilimo wa Mkoa wa Ruvuma.
 
Back
Top Bottom