Mapenzi yako ni kina gani? (How deep is your love?)

SteveMollel

JF-Expert Member
Jul 12, 2015
8,451
23,780
Awali ya yote niwashukuru wale wote wafuatiliao makala zangu. Mwanipa moyo. Kila ntakapokuwa napata wasaa basi nitashiriki nanyi kwa moyo wote.

Ebu tuanze...

Mwaka ni 1876 huko mji wa Poiters magharibi ya Ufaransa, katika mtaa ujulikanao kwa jina la ‘21 Rue de la Visitation’.

Huko alikuwa anaishi msicha mrembo ajulikanaye kwa jina la Blanche Monnier. Msichana mwenye macho makubwa rangi ya bluu na nywele zake ndefu za kuvutia. Alikuwa msichana mzuri haswa mwenye kaliba ya ukakamavu na kupendeka. Mcheshi na mtulivu.

Yeye alikuwa akiishi nyumbani pamoja na kaka na mama yake. Kaka yake na Blanche, kwa jina Marcel, alikuwa ni mhitimu toka shule ya sheria. Mama yake alifahamika kwa jina maarufu la Madame Monnier. Mama huyu alikuwa maarufu katika jiji la Poiters kwasababu ya uchapakazi wake hodari ambao ulimpelekea mpaka kupata tuzo kwa mchango wake mkubwa ndani ya jiji.

Lakini sifa yake nyingine kubwa ni kwamba, mama huyu alikuwa anaiendesha familia yake kwa mkono wa chuma.

Pengine Madam Monnier aliathirika na kitendo cha kulelea familia mwenyewe kama ‘single mother’ kwa kudhani kama angelikuwa legelege basi watoto wangempanda kichwani.

Mume wake, bwana Emile, ambaye alikuwa kiongozi mkuu wa ‘faculty’ ya sanaa, alifariki mnamo mwaka 1879, lakini uzuri alikuwa ameachia familia yake mali za kutosha kuishi maisha mazuri. Hawakuwa na shida ndogondogo.

Blanche alipofikisha miaka 25 akawa ana hamu ya kupata mchumba kabla mng’ao wa ujana wake haujamtupa mkono. Basi kama bahati akakutana na mwanaume ambaye kidogo alikuwa mtu mzima lakini alimpenda haswa.

Bwana huyo alikuwa ni mwanasheria, lakini akiwa bado hajafanikiwa. Blanche kwa kuhofu mama yake hatomkubali mwanaume huyo ambaye ni chaguo la moyo wake kwasababu ya ufukara wake, akaamua kufanya mahusiano yao yawe ya siri. Alihofia pia na ukali wa mama yake.

Lakini siri hii itaenda mpaka lini? Mapenzi ni kikohozi, unakibanaje daima ya milele? …

Basi inasemekana Blanche akaja kubeba mimba ya bwana huyo mwanasheria, na mwishowe maneno maneno haya yakaja kumfikia mama yake. Mama yake akabanwa na hasira kali hata kumkataza Blanche kumwona tena huyo mwanaume fukara!

Lakini Blanche angewezaje na alikuwa anampenda sana yule mwanaume wake? Akalumbana sana na mama. Mama yake akafoka na hata hatimaye akamwomba mwanaye lakini hakufanikiwa. Blanche akawa anatoroka usiku na kwenda kuonana na mpenzi wake.

Basi baada ya mama yake kugundua, akasuka mpango na mwanaye wa kiume kuwa wamfungie Blanche ndani ya chumba cha paa (attic room), chumba ambacho huwa kinatumiwa kama stoo, ili wamkomeshe kwa kuwa mkaidi lakini pia kumshinikiza abadili maamuzi yake.

Na mama ampe sharti moja tu, kwamba akae humo mpaka pale atakapoahidi kukatisha mahusiano yake na yule bwana, huku akitumai kuwa mwanaye atakubali shauri hilo mapema kutokana na adhabu hiyo.

Baada ya Blanche kurudi nyumbani akiwa amekawia ikiwa ni usiku mzito, taratibu akapanda ngazi akijaribu kutomwamsha mama na kaka yake. Hakuwa anatambua kuwa mama na kaka yake, Marcel, walikuwa wanamngojea juu kabisa ya ngazi.

Alipofika akatahamaki kuwaona, na wao wakamkamata na kumpeleka kwenye chumba cha paa, wakamfungia na kumwacha humo.

Baada ya kuzoezana na giza la mule chumbani, Blanche akawa mkali mno kwa mama yake na akaapa kwamba kamwe hatotengua shauri lake la kuwa na mpenzi anayempenda. Hata kama atafungiwa humo kwa muda gani.

Baada ya kukagua chumba alichofungiwa, Blanche akagundua kutoroka kutoka chumba hicho kilikuwa ni kitu kisichowezekana kabisa. Basi na atangoja mpaka pale mama yake atakapokuja kujifunza kuwa kweli alikuwa anampenda bwana wake.

Pasi na kujali atakuja kuligundua lini hilo.

Ajabu miaka na miaka ikapita. Pasipo kuzania kabisa, miaka 25 ikaenda huku Blanche akiwa kifungoni ndani ya nyumba yao. Miaka ya tabu, upweke, kutengwa na kuvunjika moyo. Miaka yote hiyo akiwa anaomba Mungu pasi na kuchoka amwokoe toka kwenye tabu hizo na ukatili wa mama yake mzazi na kaka yake wa damu.

Basi mnamo mwaka 1901, mwanasheria mkuu wa Paris, akapokea barua kutoka kwa mtu asiyejulikana ikisema kuwa kuna mwanamke alikuwa amefungwa kifungo ndani ya nyumba inayopatikana kwenye mtaa wa watu wenye uwezo, mtaa wa ‘21 rue de la Visitation’.

Barua ilikuwa inasomeka kama ifuatavyo,

“Bwana mwanasheria mku. Ni heshima kwangu kukuhabarisha juu ya jambo kubwa sana kumhusu mwanamke ambaye amefungiwa kwenye nyumba ya Madame Monnier.

Mwanamke huyo amekuwa akiishi nusu njaa, na kwa miaka ishirini na tano kwenye kinyesi chake mwenyewe.”

Polisi wakashangazwa sana na habari hii kwani Madam Monnier alikuwa ni nguzo kubwa inayoheshimiwa kwenye jamii yake, lakini kwa kutimiza wajibu wao wakawa hawana budi kwenda kufuatilia.

Baada ya kufika na kugonga mlango mara kadhaa, tena wakiwa wanasikia vitu vikisogea ndani, wakafungua mlango kwa nguvu na kuzama.

Humo ndipo wakaenda kumkuta Blanche akiwa amelala kwenye dimbwi la kinyesi na mabaki ya chakula kitandani. Kichwa chake kimefunikwa. Mwanamke huyo alikuwa uchi wa mnyama, mwoga na mwenye kutetereka. Hakuwa ameona mwanga wa jua kwa miaka ishirini na minne!

Shuhuda aliyekuwepo kwenye tukio hilo asema, “Haraka tuliamuru dirisha lifunguliwe lakini hilo likafanyika kwa ugumu sana. Pazia lilikuwa jeusi na zito. Milango ya madirisha nayo ilikuwa migumu sana kufunguka ikalazimu ibanduliwe kabisa kwenye vishikizo vyake.”

Shuhuda anaendelea kusema,

“Punde baada ya mwanga kuingia, tukatambua kuwa mwanamke huyo alikuwa amefunika kichwa chake na blanketi lenye kujawa na mabaki ya kinyesi. Mwanamke huyo tukamtambua ni Blanche Monnier. Mwanamke huyo alikuwa amelala uchi kabisa kwenye godoro lililooza.”

Shuhuda akaendelea kuteta,

“Vitu vilivyokuwa vimemzunguka ni kinyesi, mabaki ya nyama, mboga za majani, samaki na mikate iliyooza. Pia tuliwaona wadudu wakiwa wanakimbia kwenye kitanda cha Blanche Monnier.

Hewa ilikuwa ni chafu mno. Harufu iliyokuwa inatoka ndani ilikuwa kali kiasi kwamba ilikuwa haiwezekani kwa sisi kukaa humo na kuendelea na upelelezi zaidi.”

Blanche aliyekuwa amekonda mno, akafunikwa blanketi upesi na kisha akawahishwa hospitali haraka, Paris, ambapo mwanzoni madaktari wakadhani atakuwa ni wa kufa tu.

(ona picha yake hapo juu inavyomwonyesha alivyokutwa)

LAKINI VIPI KUMHUSU MAMA YAKE?

Akiwa ni mtulivu kabisa ameketi kitini nyumbani, Mama yake Blanche akakutwa na polisi ambapo walimshikilia yeye na kaka yake Blanche, Marcel, kwa ajili ya kuhojiwa.

Kule hospitali, wafanyakazi wakasema kuwa Blanche alifurahi sana kuogeshwa na pia kupata fursa nyingine ya kuvuta hewa safi. Alipayuka, “Ona namna inavyopendeza!” waligundua alikuwa anapenda sana mwanga kwasababu aliukosa kwa muda mrefu.

Japokuwa kaka yake Blanche, Marcel, alisema kuwa dada yake ni mkaidi, mwenye hasira na kiburi, madaktari walitambua kuwa Blanche hakuwa mtu wa tabia hizo kwa muda wote waliokuwa naye.

Alionekana ni mtulivu na si mtu wa kubebwa sana na hisia za mishangao.

Muda ukapita na Blanche hakuwa mdogo tena. Mwanasheria aliyekuwa anampenda alikuwa ameshafariki mwaka 1885.

Kwa mujibu wa mashuhuda kadhaa mahakamani, walikuwa wanasikia sauti ya Blanche ikiwa inapiga kelele, kuomba na hata kupayuka maneno kama vile, polisi, polisi, huruma na uhuru!

Mama yake na Blanche akatiwa kifungoni, lakini akaja kufariki siku kumi na tano baadae akiwa hospitali. Kaka yake naye alitiwa kifungoni lakini baadae akakata rufaa na kuachwa huru.

Ingawa Blanche alifanikiwa kuongeza uzito na kurudi kwenye hali yake ya usafi, bado hakurudi kwenye hali yake ya kawaida. Alikuja kufariki mnamo 1913, miaka kumi na miwili baada ya kuokolewa toka kifungoni.

Je, walimwambia Blanche na hata yeye angeelewa kuwa mpenzi wake alikufa miaka tisa baada ya yeye kutiwa kiifungoni akiwa afahamu nini kimemtokea mwanamke wake?

Je, Blanche angeweza kumsamehe mama yake ambaye mpaka anafungwa na kufa hakuwa ameona kama amefanya makosa?

Pengine si kila mama duniani ni malaika kama tudhaniavyo. Wawezaje kumtenda mwanao kiasi hiki?

Mapenzi yako yana kina kirefu kama cha Blanche?


***






Sent using Jamii Forums mobile app
 
Blanche akiwa yu mzima wa afya na akiwa vile alivyokutwa baada ya kufungiwa miaka kadha wa kadha ili abadili msimamo wake.
images-3.jpg


Sent using Jamii Forums mobile app
 
KWELI DUNIA INA MAMBO MENGI BINADAM HAISHI KUIBUA MAMBO KILA SIKU MAPYA...AHSANTE KWA KISA ICHI MKUU
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom