Mamia wazuiwa kuhitimu ualimu

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,041
Mamia wazuiwa kuhitimu ualimu
www.ippmedia.com/sw/habari/mamia-wazuiwa-kuhitimu-ualimu-0

Kuondolewa kwa wahitimu hao kunatokana na madai kwamba hawajalipiwa ada ya muhula wa mwisho na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Madai hayo yaliibuliwa jana na wawakilishi wa wahitimu hao, wakiongozwa na Naibu Waziri wa Mikopo wa Serikali ya Wanafunzi chuoni hapo (Mwecauso), Gerald Simon, mbele ya Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (Chadema).

"Tatizo ni hiyo ada tu, tumefanya mitihani yetu vizuri na kufuzu, hakuna tatizo jingine. Wahitimu zaidi ya 400 wa kozi ya BEDs waliofanya mitihani ya mwisho Julai, mwaka huu, hawatashiriki mahafali ya tisa yatakayofanyika Alhamisi ya Desemba 29, kwa sababu hawajakamilisha ada," alisema Simon.

Japhet Madenda, mwakilishi wa wahitimu hao, alisema tangazo la kuondolewa kwa majina yao katika orodha ya wahitimu waliliona chuoni hapo Desemba 24, mwaka huu.

"Chonde chonde, tunaiomba Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na Waziri wa Elimu, Prof. Joyce Ndalichako walitazame jambo hili kwa sababu hatuwezi kupoteza mwaka mwingine. Hebu wasikie kilio chetu na watoe tamko ili tupate haki yetu," alisema Madenda.

Akizungumza muda mfupi baada ya wahitimu hao kumweleza kilio chao, Mbunge Komu alisema kuwa baada ya kufanya tathmini, amebaini wahitimu hao kila mmoja alipaswa kulipiwa ada ya Sh. 650,000.

"Mimi kama mbunge na wahitimu wako kwenye jimbo langu, nimeona niseme kwamba huu ni mzigo mkubwa kwao. Nakumbuka Rais John Magufuli wakati wa kampeni zake alisema hakuna mtoto yeyote wa maskini atakayeshindwa kusoma kwa sababu ya kukosa ada.

Namuomba kwa dhati kabisa Waziri Ndalichako aliangalie jambo hili. Kushindwa kuhitimu maana yake ni mzigo mkubwa kiuchumi," alisema Komu.

Simu ya Mkuu wa chuo hicho, Dk. Philibert Vumilia, ilikuwa ikiita bila kupokewa alipotafutwa na Nipashe jana kuzungumzia suala hilo.
Hata hivyo, Ofisa Mahusiano wa chuo hicho, Athanas Sing’ambi, alithibitisha kubandikwa kwa orodha hiyo ya wanafunzi kwenye mbao za matangazo chuoni hapo.

"Ni kweli tumebandika tangazo, lakini kama watalipa au kulipiwa ada zao, watajumuishwa tena katika orodha ya wahitimu, bado wanao muda," alisema Sing'ambi na kufafanua zaidi:

"Kuna waliohamia chuoni hapa wakitokea Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Arusha na wale waliosoma hapa. Wamo pia wanufaika na wasio wanufaika wa Bodi ya Mikopo."


Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru, akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu kuhusu suala hilo alisema:

"Inawezekana wako wanafunzi wachache ambao hawajalipiwa ada kwa sababu kuna waliohama na kuhamia, lakini pia suala la kulipa linatokana na uwasilishaji wa matokeo yao Bodi na kama yatathibitishwa yako vizuri.

Ungeniuliza kesho (leo Jumanne), ningekuwa na jibu zuri zaidi, lakini nafanya mawasiliano na chuo ili kujiridhisha kweli kama hao ni wanufaika wa mikopo. Hata hivyo, suala la kutunuku shahada na kuhudhurisha wahitimu ni la chuo husika."

Kwa mujibu wa Badru, bodi hiyo ya mikopo inashughulika na vyuo zaidi ya 100 na kwamba utaratibu wa malipo ya ada kwa wanufaika wa mikopo hiyo hufanyika mara nne kila mwaka.

Katika mwaka huu wa masomo, upangaji wa mikopo umezingatia bajeti ya Sh. bilioni 483 iliyopitishwa na Bunge kwa ajili ya wanafunzi 119,012. Kati yao, 25,717 wakiwa ni wa mwaka wa kwanza na 93,295 wanaoendelea na masomo yao.
 
Back
Top Bottom