Mambo ni mazito Baraza la Mitihani | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mambo ni mazito Baraza la Mitihani

Discussion in 'Jukwaa la Elimu (Education Forum)' started by BAK, Dec 12, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Dec 12, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,496
  Likes Received: 81,820
  Trophy Points: 280
  Mambo ni mazito Baraza la Mitihani

  Mwandishi Wetu Disemba 3, 2008
  Raia Mwema~Muungwana ni Viyendo

  HALI bado tete ndani ya Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) huku taarifa zikisema sasa vyombo vya dola vimepiga kambi ndani ya baraza hilo kukusanya ushahidi kabla ya kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya wahusika wanaotuhumiwa kuvuruga mambo, Raia Mwema imeambiwa.

  Habari za ndani ya Serikali zimethibitisha kuwapo kwa uchunguzi wa kina ndani ya baraza hilo nyeti baada ya uvujaji wa mitihani ya kidato cha nne kuibua matatizo mengi yaliyokuwa yakifukuta kwa miezi kadhaa ya nyuma.

  Sambamba na uchunguzi na hatua mbalimbali kuhusiana na udhibiti na usalama wa mitihani na vyeti, NECTA imekuwa ikichunguzwa kuhusiana na mambo mengine ya kiutawala ambayo yameelezwa kwenda kombo.

  Imefahamika kwamba makachero wa Serikali wameweka kambi katika ofisi za NECTA zilizopo Kijitonyama, Dar es Salaam na watendaji kadhaa wa ngazi ya juu wamekuwa katika uangalizi maalumu baada ya baadhi yao kuhojiwa kwa saa kadhaa wiki iliyopita.

  Mbali ya kuchunguzwa kwa watendaji hao, habari zilizothibitishwa na Ofisa Mwandamizi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, zinaeleza kwamba kumekuwa na uchunguzi kuhusiana na suala la ukiukwaji wa sheria ya manunuzi katika ukarabati wa majengo ya NECTA.

  "Wanachunguza kuona ilikuwaje zabuni ya Sh milioni 350 mkandarasi akawa analipwa fedha taslimu mara kwa mara na mlipaji anakuwa mtu ambaye hana uzoefu na masuala ya fedha. Wahusika wanachunguzwa jinsi walivyojipatia baadhi ya mali," anaeleza Ofisa huyo wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa sharti la kutotajwa jina.

  Vyanzo kadhaa vya habari vinasema tayari picha za baadhi ya wafanyakazi na mali zao watumishi watatu wa NECTA zimechukuliwa baada ya wahusika kuhojiwa na kuandika maelezo ya walivyozipata mali hizo, baadhi zikiwa katika maeneo mbalimbali pembezoni mwa Dar es Salaam.

  Habari zaidi zinaeleza kwamba tayari Serikali imekwisha kufanya maamuzi mazito kuhusiana na NECTA, maamuzi ambayo yanatarajiwa kutekelezwa wakati wowote ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

  Wakati huo huo, uvujaji wa mitihani na upatikanaji wa vyeti bandia, umeelezwa kuendelea kuisumbua NECTA na sasa imebainika kwamba vyeti vilivyodaiwa kuwa ni bandia vilivyopelekwa Sekondari ya Azania vilirudishwa Baraza la Mitihani lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kwa waliohusika na uzembe huo.

  "Kwa kutochukua hatua yoyote kwa wale waliohusika inamaanisha kuwa uongozi wa juu wa Baraza unalea wafanyakazi wanaochezea vyeti. Kwa upande mwingine, makaratasi maalum (result slips) yanayotumika kutolea taarifa ya matokeo kiasi cha 170 yalipotea katika mazingira ya kutatanisha.

  "Ilipogundulika upotevu huo wafanyakazi wawili waliohusishwa waliandikiwa barua wajieleze kuhusu upotevu wa nyaraka hizo maalum. Baadaye ilifahamika kuwa wafanyakazi hao hawahusiki baada ya kugundulika kuwa upekuzi uliofanywa chini ya usimamizi wa Naibu Katibu Mtendaji, Tobias L. Oseno uligundua kuwa ofisa mmoja alikuwa amezificha ofisini kwake," kinaeleza chanzo chetu cha habari.

  Imeelezwa kwamba hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa kwa madai kwamba aliyebainika kuficha nyaraka hizo analindwa.

  Baada ya gazeti hili kuchapisha taarifa kuhusiana na matatizo ndani ya NECTA, habari za ndani ya baraza hilo zimeeleza kwamba uongozi umeamua kuanza kukarabati chumba maalumu ambacho hakikuwa na dosari zozote.

  "Kwa kukifanyia ukarabati huu, uongozi wa Baraza unataka kuaminisha umma wa Watanzania kuwa mitihani ya kidato cha nne haikuchapwa hapo kwa sababu chumba chenyewe kilikuwa kibovu wakati si kweli. Umma wa Watanzania utambue kuwa hii ni hujuma kwa elimu yetu. Serikali ichukue hatua za dharura kuokoa baraza la mitihani na hujuma hii," anaeleza Ofisa Mwandamizi wa Serikali .

  Matatizo mengine yanayofanyiwa uchunguzi na vyombo vya dola ni ajira kwa watumishi wapya bila kufanyiwa uchambuzi wa kina kama kawaida ya chombo hicho nyeti na pia baadhi ya watumishi ambao hawana elimu kulingana na kazi wanazopewa.

  "Zoezi la kuwahamisha watendaji wakuu wenye ujuzi na taaluma ya uchapaji na kuweka wasio wataalam na kazi hiyo ni kuihujumu fani ya uchapaji. Kwani walihakikisha hakuna anayebaki mwenye elimu ya juu kuhusu uchapaji ili waingizwe watu wao. Kuna siri nzito sana imejificha juu ya mabadiliko haya," anaeleza mtumishi mmoja wa NECTA akizungumzia mabadiliko yaliyofanywa katika kitengo cha uchapaji.

  Imeelezwa kwamba NECTA imeandika barua kwenda kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, ikielezea mabadiliko ya mfumo wa mtandao wa baraza kwa kuondoa wa zamani na kujenga mpya. Mtandao huo unahusika na usajili, utoaji matokeo na uchapaji wa results slips lakini sasa umeanza kuleta matatizo katika utendaji kazi.

  "Kimsingi mtandao huu ni muhimu ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Cha kushangaza ni kwamba haujafanya kazi yoyote na wanataka kuujaribu kwenye matokeo ya mitihani ya kidato cha nne 2008. Kuna taarifa kwamba mtandao unawagomea hasa ukizingatia kwamba mwaka huu mitihani imefanyika katika makundi mawili hivyo maandalizi ya matokeo yanafanywa katika makundi hayo mawili na uwezekano wa matokeo ya makundi hayo mawili yanaweza kutokuwa sahihi," anaeleza mtaalamu mmoja wa mambo ya usalama wa mitihani.

  Tayari kuna wataalamu walipelekwa katika vituo vya usahihishaji wa mitihani akiwamo mmoja ambaye anaelezwa kwamba si mtumishi wa NECTA, jambo ambalo haliruhusiwi katika taratibu za mitihani.

  Waliopelekwa ni Mkuu wa Idara ya Takwimu na Huduma za Kompyuta, mtaalam wa Takwimu Idara ya Takwimu na Huduma za Kompyuta, mtaalam wa Kompyuta kutoka Idara ya Usalama wa Taifa na mtaalamu wa kompyuta kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye si mtumishi wa NECTA.

  Baada ya Serikali kukiri kuvuja kwa mtihani wa hisabati, ililazimika kuufuta na kutunga mwingine uliofanywa Oktoba 27, huku kukiwa na taarifa za kuvuja tena kwa mtihani huo na baadhi ya wanafunzi kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

  Imebainika kwamba mitihani yote ya kidato cha nne iliandaliwa mkoani Morogoro ilikovuja kabla ya kuchapwa jijini Dar es Salaam, kazi iliyofanywa bila ya kuwapo uangalizi na ulinzi makini.

  Hata hivyo, serikali imekuwa ikikanusha kuvuja kwa mitihani yote, kwa madai kwamba iliyokamatwa ni mitihani bandia.

  Iimefahamika kwamba, watahiniwa wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Morogoro, walibadilishiwa mitihani karibu yote muhimu na kujikuta wakifanya mitihani tofauti na wenzao wa mikoa mingine, baada ya kubainika kuwapo kwa kiwango kikubwa cha uvujaji katika mikoa hiyo.

  Tatizo la baadhi ya watumishi kutofanyiwa uchambuzi wa kina kabla ya kuajiriwa limeelezwa kuathiri hata baadhi ya idara nyeti ndani ya baraza ikiwa ni pamoja na maeneo zinakotunzwa nyaraka kama vile nakala za matokeo kiasi cha kusababisha usumbufu mkubwa kwa wahitimu kutokana na kupotea au kuibiwa kwa matokeo hayo.

  Hivi karibuni ziliibwa nakala 4,000 za nakala hizo zikiwa katika makasha mawili ya nakala 2,000 kila moja na hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.

  Pamoja na kulalamikiwa kuwa na malengo ya kuwatoa baadhi ya watumishi wa baraza kafara, tume iliyoundwa na Serikali imekwisha kuwahoji watumishi kadhaa wa baraza akiwamo mmoja ambaye juzi alipelekwa mkoani Morogoro kwa uchunguzi zaidi.

  Serikali iliunda timu ya uchunguzi ikiongozwa na Profesa Makenya Maboko wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na kujumuisha baadhi ya wajumbe kutoka vyombo vya dola.

  Hata hivyo, imeelezwa kwamba baadhi ya wajumbe walikuwamo katika tume nyingine iliyoundwa na Baraza Februari mwaka huu, na kuwasilisha ripoti ambayo hata hivyo ilipingwa na Bodi ya NECTA inayoongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandara.

  Tayari kuna taarifa za kufanyika mabadiliko makubwa ndani ya NECTA kufuatia uvujaji wa mitihani ambao kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania yametokea mikononi mwa baraza hilo, mabadiliko ambayo yameelezwa kuweza kutumika kuwakomoa baadhi ya watumishi wanaohofiwa kuhujumu uongozi mpya wa NECTA chini ya Katibu Mtendaji wake, Joyce Ndalichako.
   
 2. Madela Wa- Madilu

  Madela Wa- Madilu JF-Expert Member

  #2
  Dec 12, 2008
  Joined: Mar 24, 2007
  Messages: 3,074
  Likes Received: 35
  Trophy Points: 135
  Huo ni mwangwi wa ufisadi.

  Wenzetu wazungu wanaita After effect.
   
Loading...